Mwanzo mzuri kwenye ushirikiano kati ya China na Kenya katika Serikali mpya

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,034
sdfsfsf.png

Ni muda mfupi sasa tangu Rais William Ruto aingie madarakani, na polepole ameanza kuweka mipango ya utekelezaji wa sera atakazozipa kipaumbele katika kipindi chake cha uongozi. Wakati vumbi la uchaguzi sasa limetua, ufuatiliaji hasa kuhusu sera za uchumi na jinsi zitakavyogusa wananchi wa kawaida na hata taifa kwa ujumla umeanza kuonekana.

Katika kipindi cha kampeni za uchaguzi, Rais Ruto alisikika akisema atachukua hatua za kuhakikisha wafanyabiashara vijana wa Kenya wanakuwa na mazingira mazuri ya biashara, na watapewa uwezo wa kuwa na nguvu ya ushindani. Baadhi ya watu walitafsiri kauli hiyo kuwa ni kauli inayowalenga wafanyabiashara wachina wenye mitaji mikubwa, ambao wanaonekana kuhodhi baadhi ya sekta za uagizaji wa bidhaa kutoka China.

Bila shaka, kwa sasa ni jambo la kawaida kuona wafanyabiashara wachina katika miji mikubwa ya nchi za Afrika, na kutokana na kufahamu vizuri wazalishaji na wasafirishaji wa bidhaa wa China, nguvu yao ya ushindani katika baadhi ya sekta inakuwa kubwa. Hali hii inatumiwa na baadhi ya wanasiasa wakati wa kampeni za uchaguzi, wakitangaza kuwa watairekebisha pindi watakapoingia madarakani. Bahati mbaya ni kuwa baadhi ya vyombo vya habari vinachukulia hali hiyo kama ni kuipinga China, na kuipa vichwa vya habari kama hiyo.

Tarehe 12 Septemba, Rais William Ruto alikutana na mjumbe maalum wa China kwenye eneo la pembe ya Afrika Bw. Liu Yuxi, aliyeiwakilisha China kwenye sherehe ya kuapishwa kwa Bw. Ruto. Kwenye mazungumzo yao Rais Ruto alisema, urafiki uliopo kati ya China na Kenya ni “imara”, na serikali yake itafanya kazi kuimarisha ushirikiano huo. Zaidi ya hapo Rais Ruto alisema serikali yake itapanua ushirikiano huo, ili kuboresha miundombinu, kilimo, elimu na sekta nyingine.

Ukweli ni kwamba, ushirikiano kati ya China na Kenya umekuwa na matokeo yanaonekana wazi kwa wakenya wote. Iwe ni kwa wale wanaoishi Mombasa wanaonufaika kwa kazi za usafirishaji wa mizigo kutoka bandari ya Mombasa, wale wanaishi kandokando ya reli hiyo ya SGR ambayo reli hiyo imechangamsha biashara zao au kuwarahisishia usafiri, au wakazi wengine waliopata ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kupitia ushirikiano kati ya pande hizo mbili.

Rais Ruto ambaye kwa mara kadhaa alitaja kuwa yeye ni mjasiriamali, anatarajiwa kuleta msukumo katika sekta ya biashara. Katika miaka ya hivi karibuni ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika umekuwa na mchango chanya katika kuhimiza ujasiriamali barani Afrika, ikiwa ni pamoja na Kenya. Vijana wengi wa Kenya wakiwemo wale wa Juakali, wameweza kujiajiri kutokana ushirikiano wa kibiashara na China. Wakulima pia kupitia kuuza mazao ya kilimo kama chai, kahawa na maparachichi, pia wananufaika na ushirikiano huo. Bila shaka maeneo haya yatakuwa na msukumo mpya katika serikali mpya, kama ilivyoahidiwa wakati wa kampeni.

Tukumbuke pia kuwa Kenya ni mdau muhimu kwa maendeleo na usalama wa eneo la pembe ya Afrika. Kati ya nchi zote za eneo hilo, Kenya ni nchi ambayo ni kimbilio la wakimbizi wengi kutoka kwa majirani zake ambao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiusalama na hata hali ya hewa. China pia inaibuka na kuwa mmoja wa wadau wakubwa katika kutafuta amani ya muda mrefu na hata kuhimiza maendeleo katika eneo hilo. Rais Ruto ameahidi kuwa serikali yake itaendelea kubeba jukumu hilo kama alivyofanya mtangulizi wake Bw. Uhuru Kenyatta. Ni wazi kuwa ushirikiano wa karibu kati ya serikali mpya ya Kenya na China kuhusu eneo la pembe ya Afrika, ni muhimu katika kufanikisha jambo hilo.
 
Deni la wakenya juu ya treni ya Nairobi - Mombasa halikuzungumziwa maana ni mradi usiokuwa na faida na wenye hasara.
 
Back
Top Bottom