‘Mwanaharakati’: Msamiati uliopewa mtazamo hasi - Tunahitaji mgongano wa kimawazo ili Nchi iweze kusonga mbele

BigTall

JF-Expert Member
Mar 9, 2022
422
1,049
‘Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.

‘(2) Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na Duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.” - (Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977)’


Siku ya leo tuchukue muda kidogo na tufanye tafakuri ya kina juu ya dhana nzima ya ‘Mwanaharakati’ (Activist) au “Uhanaharakati” (Activism).

Kwanza kabisa, ni vyema tukajiuliza maana ya mwanaharakati ni nini? Sehemu ya kwanza, inayoweza kutusaidia kuelewa dhana hii ni kamusi zetu.

Kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili, Toleo la 2, Mwanaharakati; “Ni mtu anayejishughulisha na utetezi na uelimishaji wa umma katika masuala mbalimbali ya kijamii k.v. siasa, uchumi, sharia au haki za binadamu.”

Pia kwa mujibu wa ‘Oxford Dictionary,’ neno “Activist” maana yake: ‘a person who takes action to cause political or social change, usually as a member of a group.’ Aidha pia inasema ‘a person who campaigns to bring about political or social change.’

Mtu ambaye anachukua hatua kuleta badiliko la kisiasa au kijamii mara nyingi kama sehemu ya mwanakikundi. Pia, mtu ambaye anayefanya kampeni kuleta badiliko la kisiasa au kijamii.

Hizo ndio tafsiri za dhana hii ya mwanaharakati. Ni vyema pia tukajiuliza kinyume cha Uanaharakati ni nini?

Kinyume ni neno la Kiingereza ‘passive’ au ‘submissive’, au ‘inactive’.

Mtu ambaye ni passive au submissive. Kuwa passive ni kutoshiriki, kutochukua hatua yoyote, kutokuonyesha msimamo au maslahi yoyote, kutotoa mchango wowote wa mawazo. Ni ile hali ya kukaa na kusubiri, hapa nimejaribu tu kueleza maana ya mwanaharakati.

Labda hapa kwa kuchambua maana ya dhana hii, ni wazi kuwa Uanaharakati ni jambo jema na zuri. Ili nchi iweze kusonga mbele inahitaji wanaharakati ambao watakuwa wakifanya shughuli zao kama maana ya dhana yenyewe inavyojieleza hapo juu.

Baada ya kujadili maana za dhana hii, hebu sasa kwa upana mkubwa, ndani ya nchi yetu na nje mipaka yetu, tuangalie mifano michache ya Wanaharakati kwa mujibu wa maana tulizozianisha hapo awali.

Nitataja mifano michache ya wanaharakati ambao walijishugulisha na utetezi na uelimishaji wa umma katika masuala mbalimbali ya kijamii, kisiasa, uchumi, sheria, haki za binadamu n.k.

Mfano wa kwanza, ni Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Sote tunayajua aliyoyafanya. Alijishughulisha na utetezi katika masuala si tu ya kisiasa bali pia kilimo, haki, usawa wa binadamu, ukombozi wa Afrika, alipinga ubaguzi wa rangi, kabila na dini. Alikuwa mstari wa mbele katika kuboresha sekta za elimu, afya n.k.

Martin Luther King, Malcolm X, Fidel Castro, Che Guevara, Bibi Titi Mohammed, Sofia Kawawa, Frantz Fanon, Mahatma Ghandi, Nelson Mandela, Steve Biko, Ken Saro-Wiwa (huyu alikuwa mwanaharakati aliyeongoza harakati kwa njia ya amani kulinda mazingira na haki za watu wa Ogoni ambao ardhi yao iliporwa na makampuni makubwa ya mafuta huko Nigeria).

Wangari Maathai (mwanaharakati kutoka Kenya aliyepambana kulinda mazingira na mshindi wa tuzo ya Amani ya Nobeli), Hellen Kijo-Bisimba, Ananilea Nkya, Maria Sarungi, Fatuma Karume, Getrude Mongela, Gema Akilimali, Anna Henga, Mary Rusimbi, Ussu Malya, Malala Yosafzai, Vanessa Nakate, Harriet Tubman. Hawa ni baadhi tu ya wanaharakati wachache ambao wametoa mchango mkubwa katika nchi yetu na dunia kwa ujumla.

Hoja yangu ya msingi ni kuwa hawa wote wana sifa za kuwa wanaharakati kwa mujibu wa tafsiri zote mbili kutoka katika kamusi zetu. Michango yao inatambulika na wataendelea kukumbukwa na vizazi vijavyo na kwa hakika wameingia katika vitabu vya historia kutokana na matendo yao mema kwa jamii.

Wanaharakati hawa walijitoa katika kufanya shughuli mbalimbali za kijamii katika kutetea maslahi mapana ya jamii. Si rahisi kuweza kueleza michango ya hawa wote.

Itoshe tu kusema kuwa wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa dunia yetu ina haki, usawa, inaheshimu utu, inafuata misingi ya kidemokrasia, inaheshimu haki za binadamu, inafuata utawala wa sheria, inaondoa ukoloni, unyonyaji, ubaguzi wa rangi, tunazingatia utunzaji wa mazingira, haki za wanawake, watoto, vijana, wazee na watu wenye mahitaji maalum. Haki za kisiasa zinaheshimiwa na wachache wanalindwa na sauti zao zinasikika. Hii ndio kazi adhimu za Wanaharakati, na kazi hii ni muhimu na inahitajika sana katika jamii yoyote ile.

Hebu tutafakari kwa kina iwapo katika nchi yetu na Dunia nzima kwa ujumla tusingekuwa na Wanaharakati, ingekuwaje ? Tungekuwa na jamii ya namna gani?

Tusingekuwa na mwanaharakati kama Marehemu Reginald Mengi, hivi Mlima wa Kilimanjaro, leo ungekuwa vipi ? Tusingekuwa na kina Hellen Kijo Bisimba, Ananilea Nkya na wengine, je tungekuwa na uwakilishi wa wanawake katika ngazi mbalimbali ? Je tatizo la ukeketaji lingekuwa vipi? ndoa za utotoni na ukatili wa kijinsia? Hali ingekuwa vipi kama hakuna watu wa kusimama mbele na kupaza sauti?

Wanaharakati wana mchango chanya na muhimu sana katika jamii yetu. Niendelee kutoa mifano mingine. Katika miaka takribani kumi iliyopita, tumeshuhudia utungaji wa sheria kandamizi kama Sheria ya Makosa ya Mtandaoni, Sheria ya Takwimu nk.

Wanaharakati, asasi za kiraia na mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali, yamekuwa mstari wa mbele katika kushiriki katika mijadala na kuishauri serikali kuzifanyia mapitio sheria kadhaa kandamizi.

Kumekuwa na mafanikio japo kidogo, mathalani, sheria ya Takwimu ilifanyiwa marekebisho na kuboreshwa, ingawa bado safari ni ndefu kwani bado kuna mapungufu.

Asasi za kiraia kama Twaweza, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), zilifanya uchambuzi wa sheria hii na nyinginezo kubainisha mapungufu ya sheria hizo.

Sote tunakumbuka sheria ya Takwimu ilivyokuwa hapo awali ambapo ilikuwa na vipengele kandamizi kadha wa kadha, ambavyo viliboreshwa na hatimaye kuwa na sheria ambayo angalau imeboreshwa kidogo kwa kuondoa vipengele vya jinai.

Kama nilivyosema safari bado ni ndefu katika kurekebisha mfumo wa kisheria nchini. Zipo Sheria nyingi zinahitaji mapitio na kuboreshwa:

Sheria ya vyama vya siasa, sheria ya habari, sheria ya ndoa, sheria ya makosa ya kimtandao, sheria ya asasi za kiraia n.k.

Ni vizuri Wanaharakati na asasi za kiraia kwa juhudi zake za ulaghabishaji, na uchechemuzi na kutoa elimu kwa wananchi ili sheria hizi zifanyiwe marekebisho, aidha, mapendekezo ya kikosi kazi yatekelezwe ili tuweze kuwa na uchaguzi unaoaminika, huru na wa haki na tuendelee kutunza tunu yetu ya amani na utulivu. Amani hupatikana pale tu penye haki.

Licha ya kazi zao hizi nzuri, ni kwa nini wanaharakati wanapewa jina hasi? Jibu la swali hili ni rahisi sana. Ukirejea maana ya dhana ya mwanaharakati yapo mambo ambayo ni dhahiri kabisa.

Mosi, shughuli hizi za wanaharakati zinagusa maslahi binafsi ya watawala. Watawala na si viongozi, hawa ni watawala ambao wanaamini mawazo yao ni sahihi na wengine wote hawana maarifa kuwazidi.

Wanaamini wao ndio wana hati miliki ya nchi, ni wao ndio wenye kuamua na katiba imewapa mamlaka ya kuamua kila kitu, ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha au kutowashirikisha ! Nchi ni kama mali yao binafsi! Hawapendi kukosolewa, hawapendi kuhojiwa, hawapendi mawazo mbadala, hawapendi mawazo kinzani. Wanapenda wananchi waendelee kuwa wakimya, ili wao wafanye wanachotaka na wakae madarakani milele.

Lakini mtazamo hasi pia unaweza kuchochewa na namna matumizi ya mbinu na mikakati ambayo inatumiwa na wanaharakati katika kupigania suala au jambo kuwa si tamu machoni mwa watawala mathalani uchaguzi wa lugha, aina ya vitendo kama maandamano. Kwa jicho la watawala matendo na mienendo ya namna hii huwakwaza.

Ni vyema kwa wanaharakati na asasi za kiraia kushiriki katika mijadala inayojenga, kufanya tafiti na kazi zao na mitazamo yao iwe inatokana na tafiti zenye ushahidi na takwimu sahihi katika kujenga hoja.

Wanaharakati na asasi za kiraia hawana budi kushirikiana, kubadilisha uzoefu na kujipanga vizuri ili waweze kuwatumikia Watanzania na kutekeleza majukumu yao.

Tunahitaji mgongano wa kimawazo ili nchi iweze kusonga mbele. Wanasiasa ni muhimu sana, wanaharakati ni muhimu pia, asasi za kiraia ni muhimu, sekta binafsi, wafanya biashara, wasomi, taasisi za Utafiti, Chama Tawala, Vyama vya Upinzani, vyombo vya habari, kila kimoja kinapaswa kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa katiba, sheria, na kanuni. Kila chombo kinatakiwa kufanya kazi zake kwa uhuru, weledi na uadilifu.

Hapo ndipo tutapata jamii jumuishi, yenye ustawi na maendeleo. Mwanasosholojia wana nadharia inayoweza kufafanua umuhimu wa kila taasisi, chombo au kundi katika jamii likitenda wajibu wake – nadharia wanayoiita; “structure functionalism”.

Kama kweli watawala wana dhamira ya dhati ya kujenga jamii iliyo na usawa, haki, utu na maendeleo, basi watafanya kazi na Wanaharakati.

Wanaharakati na serikali watakuwa ni watoto pacha, ambao lengo lao ni kuleta haki ya jamii na kuondoa umaskini. Ili watimize hilo hawana budi kushirikishana, kujadiliana na kamwe hawatakiwi kuwa ‘maadui.’ Kwa sababu wanafanya yote haya kwa ajili ya Watanzania.

Andiko la:
Selemani Rehani
na Michael Dalali
 
Back
Top Bottom