SoC01 Muundo wa Majimbo ya Uchaguzi ya Vyuo Vikuu

Stories of Change - 2021 Competition

Filosofia ya Rorya

JF-Expert Member
Sep 20, 2021
3,214
3,587
Nyanja: Demokrasia.

Muundo wa majimbo haya uwepo kwenye nafasi za ubunge na udiwani pia ambapo watakao kuwa na uhalali wa kugombea wawe ni wanajumuiya za vyuo husika na siyo wanafunzi.

Wanafunzi wasiruhusiwe kugombea wala kuchagua wabunge na madiwani watokanao na majimbo ya uchaguzi ya taasisi za vyuo vikuu na wala wasiruhusiwe kujiandikisha kwenye majimbo haya isipokuwa tu kama mwanafunzi ni mkazi wa kudumu wa majimbo haya kupitia udugu/uhusiano wake na mwanajumuiya wa chuo husika.


Utaratibu huu usibague vyuo kwa misingi ya imani na umiliki wake bali uruhusu chuo chochote ambacho kimeanzishwa kwa mujibu wa sheria ya vyuo vikuu kutambuliwa kama jimbo halali la uchaguzi isipokuwa vyuo vikuu vya majeshi ya ulinzi na usalama. Hii itasaidia kuzuia ubaguzi kujipenyeza katika jamii yetu; dhambi ambayo taifa letu lilikwishaimaliza na wala halifurahii uwezekano wa urejeo wake.

Haki za wagombea zibaki vile vile kama zilivyoainishwa na sheria ya uchaguzi kupitia tume ya taifa ya uchaguzi na ikibidi utafiti ufanyike zaidi kuona kama kuna maboresho yake yanahitajika ili kuweka kwenye mizania sahihi namna ya kupatikana wabunge na madiwani wa majimbo ya uchaguzi ya taasisi za elimu ya juu. Wote wanataaluma na wasio wanataaluma lakini wenye sifa ya uanazuoni wawe na haki sawa ya kuchaguliwa na kuchagua.

Kigezo cha idadi ya wakazi wa kutosha kuanzishwa jimbo la uchaguzi kisiangaliwe kwa uwiano na majimbo mengine ya kawaida isipokuwa kigezo cha uanzishwaji wa majimbo ya uchaguzi ya taasisi za elimu ya juu kizingatie ukweli na umuhimu wa kuwa ni taasisi zenye watu wenye kaliba ya kipekee katika kuitumikia jamii yetu. Hiki kigezo ambacho naamini kinatumika katika kuwapata wabunge wanaoteuliwa na taasisi ya Urais nacho kitumike katika kuanzisha majimbo ya uchaguzi ya taasisi za elimu ya juu.

Kuhusu wigo wa mambo ya kuwakilishwa na wabunge na madiwani hawa, ninapendekeza kuwa wasiwe na mipaka ya kujadili mambo bali pia waruhusiwe kujadili mambo yenye sura ya kitaifa na kimataifa katika kuitumikia jamii yetu ikiwemo mambo yanayohusu majimbo yao pia.

Hii ni muhimu kutokana na ukweli kuwa wabunge na madiwani wa majimbo ya uchaguzi ya taasisi za elimu ya juu wanahesabika kama kundi maalum lenye nguvu ya kitaaluma na kitaalam ya kiushawishi [think tank] katika kuibua, kujadili, kutetea, kupitisha na kusimamia mambo ya jamii, lakini zaidi ya yote ukweli huu unafungamanishwa kwenye mwito wao na viapo vyao vya kutumikia nafasi zao za kitaaluma na kitaalam kwenye maeneo yao ya kazi kwa maslahi ya umma na kwa uadilifu mkubwa wa kutolea mfano.

Napendekeza sheria inayotaka mbunge wa jimbo awe na chama cha siasa irekebishwe ili wabunge hawa na madiwani hawa ambao kimsingi ni watumishi wa umma ambao sheria ya utumishi wa umma imeweka mipaka ya mahusiano kati ya kazi zao za kiserikali na shughuli za vyama vya siasa; waweze kugombea bila tiketi na bendera ya chama cha siasa bali wagombee kwa kigezo cha unyeti wa taasisi zao na taaluma zao ili kuyaepusha majimbo haya kutawaliwa na siasa na itikadi za kichama.

Lakini pia kigezo hiki kitawapa wabunge na madiwani hawa uhuru mkubwa wa kutofungamana na upande wowote katika kutenda kazi zao za kibunge na kiudiwani na kwamba wataunga mkono ndani ya bunge na mabaraza ya madiwani hoja zile ambazo wanaona zina maslahi kwa umma hivyo katika kujadili na kupitisha hoja hizi watakuwa na kura za turufu kutegemea maslahi ya umma yanavyohakikishwa, kwa tafsiri nyepesi watakuwa wabunge na madiwani wasio na mipaka [MPs and Councillors without borders].

Hii pia itawatofautisha kimsingi kabisa na wabunge na madiwani wasomi ambao wako bungeni kwa tiketi, bendera na itikadi za kichama ambao huanza ubunge na udiwani wao kwa ukali na bidii na mwisho humalizia kwa udhaifu na kukata tamaa ambako kumetafsiriwa mara nyingi na jamii kuwa wamedhihirisha kuwa wasomi ni butu kwa sababu wameshindwa kuchagiza mabadiliko ya msingi ya mfumo wa jamii.

Hali hii pia itasaidia wabunge na madiwani wa majimbo ya uchaguzi ya taasisi za elimu ya juu kuondokana na dhihaka ya kuwajibishwa kichama pale ambapo wanajaribu kutofautiana kimantiki na matakwa ya vyama vyao ndani ya bunge na mabaraza ya madiwani ambayo nayo imetafsiriwa kama ni udhalilishwaji wa unyeti wa taaluma zao kwa shinikizo za ki-itikadi na mafungamano ya kichama.

Kwa minajili ya demokrasia na uhuru wa uwajibikaji, napendekeza wabunge na madiwani hawa wa taasisi za elimu ya juu wasihusike kuchukuwa nafasi za uteuzi e.g. mawaziri, wawakilishi wa madaraka ya Rais kama wakuu wa mikoa, wilaya na mabalozi isipokuwa tu zile za kuchaguliwa e.g. umeya na uenyekiti wa halmashauri ili kuwaepusha na siasa fungamani za kichama.

Hii pia itawezekana pale ambapo taifa litakuwa limeridhia na kuanza utekelezaji wa sheria ya ugombea binafsi. Lakini waruhusiwe kukubali nafasi za kiuteuzi za watendaji wakuu wa mashirika, mamlaka, idara, wakala wa serikali, kamati za bunge, kamati za mabaraza ya madiwani nk ili waweze kutumia kaliba zao kuleta ufanisi wa vyombo hivyo katika kuihudumia jamii.

Napendekeza wabunge na madiwani hawa wa majimbo ya uchaguzi ya taasisi za elimu ya juu waruhusiwe kuwa wawakilishi wa wapiga kura wao na kwa wakati huo pia waendelee na ajira zao kwenye taasisi zao ili waendelee kusukuma gurudumu la maendeleo ya taifa kwa kofia mbili.

Ili kuepusha taasisi za elimu ya juu na siasa za itikadi za kivyama ninashauri utaratibu wa sasa wa mikoa ya kichama ya taasisi za elimu ya juu ufutwe na nafasi hiyo ichukuliwe na majimbo ya uchaguzi ya taasisi za elimu ya juu.

Utaratibu wa mikoa ya kichama ya taasisi za elimu ya juu unafaa tu katika mfumo wa demokrasia ya chama kimoja na kwamba katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi unaweza kufanya asasi hizi zisitawalike kirahisi na kwa tija na huweza kusababisha hata na tabia za kiuonevu pale ambapo uvumilivu wa hoja mbadala za kiitikadi utakavyokosekana miongoni mwa wanajumuiya na wanafunzi wa asasi hizi nyeti.

Demokrasia ya nchi yetu kama ilivyo kwa nchi zingine za Afrika bado haijakomaa kwa kiwango cha kuleta uvumilivu wa hoja na fikra mbadala zenye mwelekeo wa kiitikadi. Tumeshuhudia katika chaguzi mbalimbali nchini kwetu raia wakipoteza roho zao na wengine kumwaga damu zao kwa kukosa tu uvumilivu wa hoja mbadala, hivyo ni bora tusipandikize tabia hii kwa wanafunzi wa asasi hizi wawapo vyuoni na baadaye wakaipeleka kwenye jamii badala yake tuwaandae katika mazingira ya uvumilivu wa hoja mbadala.

Sehemu ikiishapewa hadhi ya mkoa wa kichama lazima patakuwa na harakati nyingi za kisiasa ili kufanya mkoa uwe hai, harakati ambazo zinaweza kuathiri usalama wa ajira za wafanyakazi wa taasisi hizi pia.

Kuhusu upatikanaji wa mgombea wa kiti cha ubunge na udiwani wa taasisi za elimu ya juu, napendekeza majina mawili kwa kila nafasi yapatikane kwa mchujo wa kura za maoni. Majina haya mawili yapambanishwe kwenye uchaguzi ili kupata jina moja kwa kila nafasi/kiti kwa kura zilizo nyingi [majority votes] jina ambalo ndilo litakalo tangazwa mshindi wa kiti cha ubunge na vivyo hivyo kwa kiti cha udiwani.

Demokrasia ya uchaguzi wa viongozi katika asasi hizi usiishie tu kwenye ngazi ya serikali za mitaa yaani uchaguzi wa wajumbe wa nyumba kumi kumi na wenyeviti wa serikali za mitaa kama ilivyo hivi sasa, bali demokrasia hii ipanuliwe hadi ngazi ya majimbo ya uchaguzi ya asasi hizi ili wapatikane madiwani na wabunge wanazuoni ambao wataipa jamii mawazo ya kimapinduzi ya kuharakisha maendeleo ya taifa letu.

Msomi aliyeko nje ya taasisi za elimu ya juu asiruhusiwe kisheria kwenda kugombea katika majimbo ya taasisi za elimu ya juu mpaka pale ambapo atathibitika kuwa ni mwajiriwa hai/full time employee ambaye hadi anapogombea na kushinda uchaguzi awe bado yuko katika payroll ya chuo husika na lazima awe amelipwa mshahara na posho zote stahiki kwa mwezi huo wa uchaguzi.

Hii itasaidia kumtambua kama mwanajumuiya hai wa chuo husika. Pia mikataba yao ya ajira katika vyuo hivi lazima ioane na muda wa kulitumikia bunge na mabaraza ya madiwani wa miaka mitano na kwamba waruhusiwe kuongeza mikataba ya ajira ili kumalizia vipindi vyao vya ubunge na udiwani pale ambapo itathibitika kuwa mikataba yao ya ajira inakwisha kabla ya muda wa ubunge na udiwani kufikia ukomo.

Naomba kura yako.
 
Back
Top Bottom