Mkuu Mwanakijiji,
Hayo makaburi ya halaiki ulotuonesha katika picha yako wapi katika Zanzibar ya leo? Yaani waweza kututajia angalao jina la kijiji au mtaa au sehemu yanakopatikana makaburi hayo? Nauliza maana ninao mshangao mkubwa kuhusu jinsi jambo kama hili linavyoweza kufichika tusisikie japo tetesi miaka yote hii (kabla sijajiita "kilaza", maana nimesoma historia hadi university, na nimebahatika kutembelea maeneo rasmi na yasiyo rasmi ya kihistoria, lakini kuhusu yalipo makaburi haya sijapata kusikia japo fununu!) Nafahamu kuwa watu wengi waliuawa wakati wa mapinduzi ya Zanzibar, na hesabu zilikuwa zinatofautiana kati ya duru za Okello na zile za CIA na vyombo vya habari vya kimagharibi. "Field Marshal" John Okello alikuwa na tabia ya kutaja idadi ya kutisha kwa kila kitu alichotangaza, haieleweki ni kwa kutojua thamani halisi ya namba hizo au ni sehemu ya "mkwala" wake. Mfano alipotangaza redioni kuhusu kupinduliwa kwa sultani, alidai jeshi lake lina wapiganaji milioni 99! Hiki chenyewe kilikuwa kituko maana Tanganyika wakati huo ilikuwa na watu wasiozidi milioni 12. Duru nyingine zinakadiria wapiganaji waliofanikisha mapinduzi hawakuzidi watu 300. Kuhusu waliouawa, Okello alidai kwa usiku wa mapinduzi tu waliua watu zaidi ya elfu mia moja, na hawaoni shida kuua wengine ikibidi! Alitishia pia kwamba jeshi lake liko tayari kutoa adhabu mara 888 kwa yeyote atakayepinga mapinduzi hayo! Alikuwa na mikwala sana huyu jamaa! Lakini kumbukumbu nyingine zilizopo zinaonesha hawakuuawa wengi kiasi hicho siku ya mapinduzi, mauaji mengi yalifanywa na makundi ya watu dhidi ya waliokuwa na chuki nao (hata zisizokuwa za kisiasa), na hii ilikuwa rahisi kwa kuwa nchi haikuwa tena na vyombo vya kulinda usalama, kulikuwa na "lawlessness" au tuiite "anarchy", fujo tupu. Hapo ndipo watu walipovamiwa majumbani mwao na kukatwa vichwa mbele ya wake na watoto wao, wanawake walibakwa, na uporaji ulikuwa wa kutisha. Hakuwepo mtu mwenye uwezo au nafasi ya kuratibu mauaji ya halaiki ama hata hayo maziko ya halaiki. Okello mwenyewe alishindwa kutuliza au kudhibiti fujo hizi, na kuna wakati alitangaza kwenye radio kuwa atakayekamatwa anafanya uporaji angeuawa, lakini bado haikusaidia. Kilichosaidia kutuliza fujo zile ilikuwa ni jeshi la polisi kutoka Tanganyika ambalo lilitumwa huko, na wakafanikiwa kunyamazisha.
Kumbukumbu pekee katika picha inayoashiria kuwepo kwa mauaji yaliyoratibiwa ya halaiki ni filamu iliyotengenezwa na mtengeneza filamu wa kiitaliano, na kuanza kuoneshwa kwenye mwaka wa 1966 kama documentary. Huyo mtengenezaji alidai amepiga picha hizo akiwa kwenye helikopta wakati mapinduzi yakiwa yanaendelea, na ukiiangalia filamu hiyo utaona watu wanavyopangwa katika mstari, kupigwa risasi, kupakiwa katika malori na kupelekwa kwenye shimo kubwa lililokwisha kuchimbwa tayari kwa maziko ya jumla. Yeyote anayetazama filamu hiyo atashangaa jinsi mtengenezaji alivyoweza kuwafuatilia wauaji hao wenye bunduki kwa karibu kiasi hicho, wanayotekeleza mauaji hatua kwa hatua bila yeye kudhurika! Au labda alikuwa mmoja wao? Katika eneo jingine kwenye documentary hiyo amewafuatilia watu waliokimbilia pwani ili wakapande mitumbwi watorokee bara, kumbe wanafuatwa kwa nyuma na "wanamapinduzi", kufika pwani wakamiminiwa risasi wote, kisha wauaji wakachimba shimo mchangani na kuwafukia kwa jumla. Nilijiuliza huyu mzungu alikuwa na helikopta ngapi, na alijiaminije kuwa asingetunguliwa? Mauaji ya halaiki ya Rwanda yalifanyika katika kipindi ambacho teknolojia ilikuwa kubwa kuliko mwaka 1964, lakini hakuna documentary yoyote ya filamu inayoonesha jinsi yanavyofanyika, ziko zinazoonesha matokeo ya mauaji hayo (maiti zilizolundikana kwenye majengo, barabarani, mtoni nk) na wakimbizi wanaokimbia vita wanaosimulia yaliyowapata. Na hayo makaburi ya halaiki ukienda Rwanda hata leo utaoneshwa.
Nahisi mzee Mwanakijiji amepata picha hizo kutoka kwenye hiyo documentary ninayosema. Hebu na nyie itazameni mniambie mpigaji wa picha hizi alikuwa wapi? Je tuna uhakika hakukuwa na uhariri wa kuganga hizi picha kuleta ujumbe alioutaka huyo mtaliano? Nimeshuhudia leo Tv ya BBC wakiomba radhi kwa kuonesha picha za tsunami ya Indonesia na kudai ni kimbunga cha Burma! Tuna uhakika gani hapa panapooneshwa na huyu mzungu ni Zanzibar kweli?
Napinga mauaji, lakini napinga pia upotoshaji wa aina yoyote, na kwa mazingira yetu upo upotoshaji wa historia unaofanywa na wazungu kwa manufaa yao!
Hebu tazameni wenyewe hizi documentaries, nawawekea link hapa chini, nayi mtoe maoni yenu:
[media]http://www.youtube.com/watch?v=ZSkamXwMDYk[/media]
[media]http://www.youtube.com/watch?v=kT1LCuxXdcg&feature=related[/media]
Na hapa chini wazungu wanadai kuwa hata wakati wa maasi ya jeshi ya 1964, kulikuwa na mauaji mengi sana yaliyofanywa na waafrika dhidi ya wazungu, na anaonesha jinsi maiti walivyofurika huko Bagamoyo, na jinsi waarabu na wazungu walivyokuwa wanashambuliwa na kuuawa hadharani huko Dar es salaam! Hebu itazameni msikilize na lugha za hao wanaodaiwa kuwa ni "waasi" halafu mniambie ni lugha za Tanzania kweli hizo? Hata mwaka 1964 nadhani watanzania walikuwa wakizungumza kiswahili! Angalieni kipande kwenye link hapa chini:
[media]http://www.youtube.com/watch?v=0ZouHC9GfxY&feature=related[/media]
Huyo aliyetengeneza filamu hiyo hapo juu ndiye aliyetengeneza pia kipande hiki hapa chini, ambapo anazugumzia jinsi mwafrika alivyo mpumbavu kulinganisha na mzungu! Itazameni mniambie mtu anayezungumza mambo kama haya dhidi yenu anaweza kuwasemea mema?
[media]http://www.youtube.com/watch?v=n0KLhSwMvcs&feature=related[/media]
Angalia hapa anavyozungumzia "the new African":
[media]http://www.youtube.com/watch?v=vD3bwEI316I&feature=related[/media]
Jitahidini muangalie series yote ya "Africa Blood and Guts", inapatikana kwenye youtube, ziko parts 1-10. Halafu mrudi hapa mniambie tuna sababu gani ya kuwaamini hawa wazungu?