Mtwara: TAKUKURU yarejesha Milioni 600 za Korosho za Mwaka 2018. 2019 kutoka kwa Wabadhirifu

TAKUKURU MKOA WA MTWARA YACHUNGUZA UBADHIRIFU WA FEDHA ZA MALIPO YA KOROSHO ZA MSIMU WA 2018/2019: YAFANIKIWA KUREJESHA SHILINGI MILIONI 600 KUTOKA KWA WATUHUMIWA

Ndugu Waandishi wa Habari,

Nimewaita kwa mara nyingine tena ili kupitia kwenu, tuujulishe umma kazi ya uchunguzi iliyofanywa na TAKUKURU Mkoa wa Mtwara kuhusu taarifa tuliyopokea tarehe 14 Machi 2020 kutoka chanzo cha siri kwamba kuna wizi na ubadhirifu mkubwa wa fedha za Serikali uliodaiwa kufanywa katika malipo ya korosho za msimu wa 2018/2019 ambao Serikali ilinunua korosho kwa wakulima. Taarifa ilieleza kuwa kuna fedha za Serikali zilizotolewa kwa ajili ya malipo ya wakulima wa korosho lakini sehemu ya fedha hizo zilifanyiwa ubadhilifu na watu wasio waaminifu na kusababisha wakulima kutopata fedha zao.

Ndugu Waandishi wa Habari,

Uchunguzi wa awali dhidi ya tuhuma hii ulifanyika na kubaini kwamba baadhi ya watumishi wa Serikali walioaminiwa na kupewa jukumu la kuwa kwenye timu ya uhakiki na timu ya malipo ya korosho katika msimu wa 2018/2019 walikula njama na kufanya wizi na ubadhirifu wa fedha za Serikali kwa kuingiza katika nyaraka za malipo majina na akaunti za watu ambao hawakuuza korosho kwenye msimu huo na kisha kulipa fedha na wengine wakulima halali kwa kuwazidishia fedha ambazo baadae ziliwarudia watumishi hao.

TAKUKURU mkoa wa Mtwara ilifanya uchunguzi wa kina kwa kuishirikisha Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania (CPB) iliyokuwa na jukumu la kusimamia malipo hayo. Hadi sasa uchunguzi umebaini yafuatayo:-

  • Kiasi cha fedha shilingi 922,702,132.65 zililipwa kwa watu ambao hawakuuza korosho
  • Kiasi cha fedha shilingi 533,809,490.01 zililipwa zidifu kwa wakulima waliouza korosho

  • Hivyo jumla ya fedha za Serikali zilizolipwa kwa wasio stahili ni shilingi 1,456,511,622.67
Katika uchunguzi huu tulibaini kuwa fedha zilizolipwa kwa watu ambao hawakustahili zilikwenda kuwanufaisha baadhi ya watumishi wa Serikali waliohusika katika timu za uhakiki wa malipo hayo, baadhi ya wafanyabiashara, baadhi ya wakulima na baadhi ya Maafisa wa Benki waliohusika kuchakata malipo ya msimu huo.

Ndugu Waandishi wa Habari,

Kufuatia yaliyobainika katika uchunguzi huu, zoezi la kuwatafuta watuhumiwa, kuwahoji kwa kina na kuwabana ili warejeshe fedha hizo Serikalini lilifanyika na linaendelea kufanyika. Hadi sasa takwimu za fedha zilizookolewa ni kama ifuatavyo:-

  • Kiasi cha fedha zilizookolewa kupitia TAKUKURU mkoa wa Mtwara ni shilingi 600,000,000
  • Kiasi cha fedha zilizookolewa kupitia CPB ni shilingi 147,941,718.99
  • Hivyo jumla ya fedha za Serikali zilizookolewa ni shilingi 747,941,718.99
Zoezi linaloendelea kwa sasa ni kufuatilia miamala katika baadhi ya akaunti za kwenye tuhuma hii, kuwatafuta watuhumiwa walionufaika na fedha hizo, kuwahoji kwa kina na kuwabana ili warejeshe fedha hizo Serikalini ili zikatumike kuwalipa wakulima ambao bado wanaidai Serikali.

Ndugu Waandishi wa Habari,

Wizi na ubadhirifu huo wa fedha za Serikali ulisababisha madhara makubwa kwa wakulima halali waliostahili fedha hizo na wengi wameshindwa kukidhi kuhudumia mashamba yao, kutatua shida zao za kifamilia na kupelekea kuilaumu Serikali yao kwamba imewadhulumu korosho zao.

Tunapenda wananchi wa mkoa wa Mtwara wafahamu kwamba, Serikali ililipa fedha zote za kununulia korosho za msimu wa 2018/2019 lakini baadhi ya watumishi na watu wasio waaminifu ndio waliokwamisha malipo hayo kwa manufaa yao binafsi.

TAKUKURU mkoa wa Mtwara ipo imara kuwafuatilia wale wote waliojihusisha na ubadhirifu huu ili warejeshe fedha walizoiba. Hatua kali dhidi ya wote ambao watakaidi agizo la kurejesha fedha walizochukua zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kutaifisha mali za watuhumiwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka.

Ndugu Waandishi wa Habari,
  • Kufuatia mafanikio haya ya TAKUKURU Mkoa wa Mtwara, leo tunayo furaha kuikabidhi Serikali kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania (CPB) fedha shilingi 600,000,000/= zilizookolewa katika awamu hii ya kwanza ili zikatumike kuwalipa wakulima waliosalia.

  • TAKUKURU Mkoa wa Mtwara imeelekeza nguvu zake katika kuhakikisha fedha shilingi 708,569,903.68 zilizobaki mikononi mwa watuhumiwa hadi sasa zinarejeshwa Serikalini na hatua kali za kisheria zinachukuliwa dhidi yao.
Ndugu Waandishi wa Habari,

TAKUKURU inaendelea kuwasihi wananchi wa mkoa wa Mtwara popote pale walipo, waendelee kutupatia taarifa za wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa ili tuhakikishe kwamba hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya wale wote wasiolitakia mema Taifa letu.

Taarifa zinaweza kufikishwa kwetu kwa njia ya simu ya Dharura 113 ambayo ni BURE, pia Mwananchi anaweza kufika katika ofisi zetu zilizoko katika kila Mkoa, kila Wilaya na hata katika Vituo Maalum ambavyo vina mkusanyiko wa shughuli nyingi za kuichumi.

Ndugu Waandishi wa Habari,

TAKUKURU Mkoa wa Mtwara inatoa wito kwa Maafisa Ushirika ngazi ya Halmashauri, Viongozi Ushirika ngazi ya Mkoa, Wadau mbalimbali wa Ushirika na Bodi za Mazao kila mmoja kusimamia ipasavyo Sheria na Kanuni ili kuhakikisha ushirika unajengwa katika misingi imara na kuondoa matatizo ya rushwa na ubadhirifu wa mali unaoathiri wanachama wakiwemo wakulima wa korosho.

Aidha TAKUKURU Mkoa wa Mtwara inawaasa Wananchi wote wa Mtwara kujiepusha na vitendo vya rushwa katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka huu wa 2020 na wahakikishe wanatumia vizuri kura zao ili kuwapata viongozi bora na wenye malengo mema na Taifa letu.

Imetolewa na:

ENOCK P. NGAILO

KAMANDA WA TAKUKURU (M) MTWARA

15/09/2020
Kampeni za kitoto sana hizi
 
Nilikua nasoma nikitegemea majina ya watuhumiwa nitayaona 😀. Anyway mmejitahidi kufanya mlichofanya Ila hamueleweki bado.
Huwezi kuoana majina kwa sababu hii ni kufunga watu ''kamba''. Ilivyo ni kwamba serikali haikulipa wakulima wengi baada ya kuchukuwa korosho zao na sasa baada ya kuona uchaguzi umemkalia vibaya Magufuli wanajaribu kusahihisha makosa aliyofanya. Kweli huu uchaguzi ni mgumu kuliko wa kipindi chochote kwa CCM. Na mbaya zaidi hizi ni zile ngome ambazo CCM ilikuwa inategemea kura za bwerere leo hali ni mbaya. Bado na huko CCM kwenyewe wengi hawampendi mwenyekiti na hawatampigia kura.
 
Unaweza kuwa ubabaishaji wa funika kombe mwanaharamu apite, hela zinarudishwa watuhumiwa hawajulikani. Inaweza kuwa mbinu ya kuwalipa wakulima kiaina


Hao WEZI na WABADHILIFU watajwe kwa majina na kiasi cha pesa walizopora.

Je, huo siyo UHUJUMU?

Kama ni UHUJUMU,

SUKUMA NDANI WOTE MPAKA BAADA YA UCHAGUZI.
 
huyu huyu alieibua watymishii hewa,Leo anatuletea stori za malipo hewa ya korosho,mwizi haachi asili yake
 
Wacha walazimishe upendo maana washajichafua kila kona
Jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya kilimo alikuwa Mwanza kukutana na wawakilishi wa vyama vya ushirika kutoka Kegera, Mwanza na mikoa jirani ili kuangalia namna ya kuwalipa pesa za kahawa na pamba.
 
BILIONI 12 ZA WAKULIMA WA KAHAWA KAGERA KULIPWA: KATIBU MKUU KILIMO - KUSAYA

Serikali imesema wakulima waliokusanya kahawa yao kwenye vyama vya ushirika mkoani Kagera wataanza kulipwa madeni yao mapema wiki hii.
Kauli hiyo imetolewa leo (01.09.2020) Jijini Mwanza na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya wakati alipoongoza kikao cha viongozi wa Wizara ya Viwanda na Biashara, mikoa ya Mwanza na Kagera na vyama vikuu vya Ushirika KDCU na KCU kilichofanyika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Kusaya alisema tangu msimu wa ununuzi wa kahawa ulipofunguliwa mwezi Juni mwaka huu jumla ya shilingi Biioni 32 tayari zimelipwa kwa wakulima wa mkoa wa Kagera kutokana na kukusanya tani 62,336 za kahawa ghafi na tani 31,168 za kahawa safi kwenye vyama vikuu vya ushirika na vile vya msingi.
“Pamoja na kulipa Bilioni 32 za wakulima bado Chama Kikuu cha Ushirika KDCU kinadaiwa shilingi Bilioni 12 kutokana na kukusanya kahawa ya wakulima ,hivyo kikao chetu leo tumekubaliana KDCU waanze kulipa wakulima shilingi Bilioni 7 zilizopo tayari kuanzia kesho na zingine Bilioni 5 zitalipwa mapema wiki ijayo” alisema Kusaya
Katibu Mkuu huyo alisema deni hilo linatokana na KDCU kuendelea kukusanya kahawa ya wakulima kufuatia uwepo wa mavuno mazuri ambapo takwimu zinaonesha wanakusanya kwa siku kahawa yenye thamani ya shilingi Bilioni 1.7 kutoka kwa wakulima na tayari wamenunua kilo milioni 37.3 kati ya lengo la kilo milioni 45 za kahawa msimu huu.
Kuhusu Chama Kikuu cha Kagera ( KCU) ,Katibu Mkuu Kusaya alisema wanadaiwa na wakulima shilingi Bilioni 7.1 na kuwa wamekubaliana kuanza kulipa shilingi Bilioni 2 mapema wiki huku wakiendelea na kukusanya fedha toka kwa wanunuzi waliowauzia kahawa.
“Shilingi Bilioni 2 za wakulima waliouza kahawa KCU tumekubaliana zitaanza kulipwa wiki hii Kagera na kuwa zingine Bilioni 3 zitatolewa na mnunuzi aliyeuziwa kahawa na KCU katika muda mfupi ujao” alisisitiza Kusaya.
Kusaya aliongeza kusema serikali imejipanga kikamilifu kuona wakulima wa kahawa kote nchini wanalipwa fedha zao kwani mfumo unaotumika wa vyama vikuu na AMCOS kununulia kahawa ni wa uhakika na kuwa wakulima wawe na subira kipindi kifupi fedha zitapatikana kwani wanunuzi toka nje ya nchi wameanza kuonyesha nia ya kuja Tanzania kutokana na tatizo la korona kudhibitiwa .
“Kuchelewa kwa malipo ya wakulima wa kahawa hususan mkoa wa Kagera yametokana na vyama vikuu vya ushirika kuchelewa kuuza kahawa” alisema Kusaya na kuwa serikali ipo tayari kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kutoa mikopo kwa vyama vya ushirika kununua kahawa na kulipa wakulima.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof.Riziki Shemdoe alisema kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo wanaendelea kutafuta masoko ya uhakika ya mazao ya wakulima kama alivyoelekeza Rais Dkt.John Pombe Magufuli.
Prof. Shemdoe alisema kwa sasa wanunuzi na wafanyabiashara binafsi wanaruhusiwa kununua kahawa toka vyama vikuu vya ushirika au vyama vya msingi (AMCOS) lakini wahakikishe wanatoa bei nzuri na yenye ushindani wa soko.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Prof. Faustin Kamuzora alisema wakulima wa kahawa msimu huu wamepata bei nzuri karibu asilimia 75 ya bei ya soko la dunia na kuwa vyama vikuu vya Ushirika (KDCU) na (KCU) kwa mkoa wa Kagera wamefanya kazi nzuri kuwezesha wakulima kulipwa bei nzuri.
Prof.Kamuzora ametoa wito kwa watanzania kuwa na tabia ya kunywa kahawa ili kusaidia upatikanaji wa soko la kahawa ndani ya nchi tofauti na ilivyo sasa kahawa asilimia 93 inayozalishwa nchini inauzwa nje ya nchi.
Mrajis wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini Dkt. Benson Ndiege alisema wanunuzi binafsi wa kahawa wanaruhusiwa kununua lakini sharti waingie mikataba na vyama vya vikuu vya ushirika au AMCOS ili kuwa na uhakika wa bei nzuri kumfikia mkulima.
Dkt. Ndiege alitoa wito kwa viongozi wa vyama vya ushirika nchini hususan mkoa wa Kagera kutoa kipaumbele cha malipo ya wakulima waliouza mapema kahawa yao kutokana na fedha zilizopatikana sasa na makubaliano yaliyofikiwa kwenye kikao cha Makatibu Wakuu Kilimo na Viwanda .
Kwa mujibu wa taarifa ya Bodi ya Kahawa Tanzania imeonesha makusanyo ya kahawa msimu wa 2020/2021 yamefikia jumla ya tani 79,245 (73%) za kahawa ghafi kati ya lengo la tani 108,000 na tani 44,695 (63 %) za kahawa safi kati ya lengo la tani 70,000.
Kahawa hiyo imekusanywa toka kwenye mikoa yote 17 inayolima zao la kahawa nchini.
Aidha bei ya kahawa kwa mkulima msimu huu imekuwa ikilipwa kwa utaratibu wa malipo ya awali kupitia vyama vyao vya ushirika ambapo mkulima analipwa kwa kilo shilingi 1,200 kahawa ya Robusta maganda (dry cherry) na shilingi 1,250 na 1,500 kahawa za Arabika maganda (parchment)
Mwisho.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom