EMT
Platinum Member
- Jan 13, 2010
- 14,477
- 15,357
Katika thread yangu ya Mtwara: Ilipotoka, ipo wapi sasa na inaelekea wapi nilizungumzia kitabu cha Michael Longfold kiitwacho "The Flag Changed at Midnight: Tanganyika's Progress towards Independence" kilichochapishwa mwaka 2001. Katika kitabu hiki, Michael Longfold anaelezea ushuhuda wake wa macho akiwa kama mfanyakazi (District Officer - Mtwara) wakati wa utawala wa kikoloni miaka 10 ya mwisho kabla ya Tanganyika kupata uhuru.Kwenye Sura ya Nne yenye kichwa cha habari "Southern Province", mwandishi anasema (nimetafsiri kwa Kiswahili):
"Mwanzoni, mji wa Mtwara ulikuwa umepangwa kusaidia maelfu ya wakazi wake hapo baadae na pia kuvutia wakazi wapya. Waingereza walikuwa na mpango wa kujenga mji maarufu wenye vitu kama maktaba, sehemu za kuombea, shule, hospitali, kumbi za sinema, n.k. Lakini mipango yote hii iliwekwa kapuni baada ya kuanguka kwa kilimo cha karanga."
Kupata picha kamili ya Mtwara wakati wa ukoloni unaweza kusoma article ya Ronald M Munga: Makala toka Mtwara: Gesi na Maandamano; Nani haeleweki? na thread yangu ya Mtwara: Ilipotoka, ipo wapi sasa na inaelekea wapi?
Katika hotuba yake kwa taifa ya 31 Jamuary 2013, Rais Jakaya Kikwete amerudia yale yale yaliyosemwa na wakoloni zaidi ya miaka 60 iliyopita kwa kusema:
"Kupanga Mji wa Mtwara
Ndugu Wananchi;
Baada ya kutembelea bandari ya Mtwara na Chuo cha VETA, nilikaa na kuzungumza na viongozi wa Serikali na Manispaa ya Mtwara. Katika mazungumzo yangu nao niliwasisitizia umuhimu wa kuwa na mpango kabambe wa kuendeleza mji wa Mtwara – (Mtwara Masterplan) Mpango ambao utawezesha kujengwa mji mkubwa wa kisasa unaokidhi mahitaji ya mji wa uchumi wa gesi. Niliwataka wahakikishe kuwa kuna maeneo ya viwanda, biashara, makazi, mahoteli, huduma za afya, elimu, mapumziko na burudani, viwanja vya michezo na kadhalika. Kazi ya kutayarisha Masterplan hiyo imeanza na Manispaa ya Mtwara inashirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi."
Inaonekana alichosema Rais Kikweye siyo kipya. Mpango wa kujenga mji wa Mtwara kama mji mkubwa kusini mwa Tanzania ulianza tokea miaka ya 1950s. Ulikuwa ni mpango kabambe wa serikali ya kikoloni chini ya mpango mzima wa kilimo cha karanga. Mpango huu ulianzishwa na serikali ya Labour ya Uingereza iliyoingia madarakani mwaka 1945 chini wa Waziri Mkuu, Clement Attlee. Lakini madhumuni ya kuanzishwa kwa kilimo cha karanga Nachingwea ilikuwa siyo kwa ajili ya kujenga mji wa mtwara bali moja ya sehemu ya kutatua tatizo la utapiamlo nchini Uingereza; tatizo ambalo lilisababishwa na Vita Kuu ya Pili ya Dunia
Leo hii zaidi ya miaka 60 bado tunazungumzia kuujenga mji wa Mtwara. Tena hii ni baada ya gesi kugunduliwa Mtwara. Kama siyo hii gesi basi wala serikali isingekuwa na mpango wa kuuendeleza mji wa Mtwara. Kama siyo malalamiko ya watu wa kusini, gesi ungevunwa na kupelekwa Dar Es Salaam kutatua tatizo la utapiaumeme na Mtwara kubakia hivyo hivyo kama ilivyo Mwadui - Shinyanga. Sana sana Mtwara ingeachiwa mabaki ya gesi aka maganda ya karanga (kama wakoloni wangefanikiwa na kilimo chao cha karanga).
Ghafla Mtwara imekuwa tena a "Cinderella Province" kama ilivyokuwa wakati wa ukoloni. "Cinderella" maana yake ni " mtu au kitu ambacho uzuri au uwezo wake haujatambulikana" au uzuri/uwezo wake unatambuliwa ghafla baada ya muda mrefu wa kutotambuliwa. Zaidi ya miaka 60, leo ndiyo serikali inashtuka kuwa Mtwara inahitaji kujengwa?