Mtazamo wa wazungu mambokale kuhusu maadili asilia

Mama Amon

JF-Expert Member
Mar 30, 2018
2,021
2,478
1(1).jpg

Mchoro wa mtu anayefanya udadavuzi wa fikira

Na Dkt. Ada LOVELACE, Pambazuko Toleo Na. 0031

1. Usuli


Maadili asilia ni kanuni za kuongoza tabia za watu zinazopatikana kutokana na kuangalia maumbile ya watu wenyewe yanataka wafanye nini kusudi waweze kubaki wazima na kustawi hadi ukomo wa juu kabisa, kwa kuzingatia hulka yao kama viumbehai walio katika tabaka moja la viumbehai wenye mwili ambao ni kitovu cha akili na utashi huru.

Kwa mtazamo wa wazungu wa kale, msingi wa nadharia kongwe ya maadili asilia, walioisanifu wao, ni masharti makuu mawili.

Mosi, ni sharti kwamba kila kitendo ambacho kinakubaliana na “silika asilia ya kibayolojia” iliyo katika mwili wa mtu inafaa kwa ustawi wake na ni halali kimaadili.

Na pili ni sharti kwamba kila kitendo ambacho kinakiuka “silika asilia ya kibayolojia” iliyo katika mwili wa mtu hakifai kwa ustawi wake na ni haramu kimaadili.

Kutokana na masharti haya mawili, hoja ifuatayo inazaliwa:

Kwamba, kwa mujibu wa maumbile yao, watu wanayo mielekeo asilia inayowafanya wawe na shauku ya kutunza uhai, uzazi, ukweli, urafiki, jumuiya na malengo mengine yanayohusiana na silika asilia za kibayolojia walizo nazo;

Kwamba, ni jambo jema kwa watu kuenenda katika namna ambayo inaonyesha utii kwa silika asilia za kibayolojia walizo nazo, na jambo baya kuzikiuka silika hizo;

Na kwamba, kwa hiyo, watu wanapaswa kuenenda katika namna ambayo inaonyesha utii kwa silika asilia za kibayolojia walizo nazo, na kujiuzuia kuzikiuka silika hizo.

Hata hivyo, hoja hii inazo dosari kadhaa. Dosari kubwa za hoja hii ni ukweli kwamba, japo inatwambia kuwa kwa sehemu kubwa “silika asilia za kibayolojia” ni misingi thabiti ya kimaadili, haituelezi ni kwa nini baadhi ya “silika asilia za kibayolojia” sio misingi thabiti ya kimaadili.

Haituelezi kwa nini ni kosa kimaadili kwa mtu kuitii “silika asilia ya hasira” aliyo nayo kwa kuwapiga wenzake;

Haituelezi kwa nini ni kosa kimaadili kwa mwanamume mwenye “silika asilia ya kujamiiana na mwanamke” kuitii “silika” yake kwa kufanya mapenzi na mtu asiye mke wake, wakati tendo hilo hilo ni halali kimaadili kama akilifanya pamoja na mkewe.

Haituelezi kwa nini ni kosa kimaadili kwa mwanamume mwenye “silika asilia ya kufanya ulawiti” kuitii “silika” yake kwa kumlawiti mwanaume mwenzake.

Na, haituelezi ni zipi “silika asilia za kibayolojia” zinapaswa kupewa utii na kila mtu, kila mahali na kila wakati; na zipi zinaweza kukaidiwa na kuminywa ama kwa muda, au kwa sehemu au kwa ujumla.

Kwa hiyo, makala hii inafafanua nadharia kongwe ya maadili asilia, na kubainisha urefu na upana wa udhaifu huu. Lengo ni kuonyesha jinsi ambavyo wanazuoni mamboleo wamejaribu kuondoa udhaifu huu hatua kwa hatua, kuanzia na Wamarekani na hatimaye Waafrika.

Makala hii inazo sehemu zifuatazo: (1) Utangulizi, (2) Uzio wa miundombinu ya kifikra na kinadharia, (3) jawabu kwa swali la kiteolojia, (4) jawabu kwa swali la kibayolojia, (5) jawabu kwa swali la kisaikolojia, (6) jawabu kwa swali la kiepistemolojia, (7) jawabu kwa swali la kisemiotiki, (8) jawabu kwa swali la kiakisiolojia, (9) jawabu kwa swali la kiprakisiolojia, (10) jawabu kwa swali la majukumu ya kimaadili, (11) jawabu kwa swali la kimantiki, (12) jawabu kwa swali la falsafa matumizi, (13) majumuisho ya makala, na (14) Marejeo muhimu. Endelea kujisomea.

2. Utangulizi

WAZUNGU
wa Ulaya ya kale, kama vile Plato na Aristotle wa Ugriki, Marcus Cicero na profesa Thomas Aquinas wa Italia, Hugo Grotius wa Uholanzi, Thomas Hobbes na John Locke wa Uingereza, walisisitiza “sifa asilia zinazo tambulisha usawa wa binadamu kama tabaka moja la viumbehai” na kuzitafsiri kwa kutumia misamiati ya enzi zao na kuunda nadharia kongwe ya maadili asilia.

Kwa ujumla, mawazo yao yanaunganishwa na uzi mmoja wa kifikra: kwamba, “sifa asilia zinazotambulisha usawa wa binadamu kama tabaka moja la viumbehai,” bila kujali tofauti zao wa kimwili, kihistoria na kijiografia, zinatoa mwongozo wa kimaadili ulio na kipaumbele kikubwa kuliko miongozo ya kimaadili inayotengenezwa na vikao vya watu kwa kupiga kura za wengi.

Na kama ilivyo kwa mifumo yote ya kimaadili, tafsiri ya Wazungu hawa inatoa majibu kwa maswali makubwa tisa. Nataka kufupisha majibu yao hapa chini kwa msaada wa fikra za wanazuoni wafuatao:

Marcus Cicero (1929) na kitabu chake, “On the Commonwealth”; Aristotle (1941) na vitabu vyake, “Ethica Nicomachea,” “Physica,” na “Politica”; Thomas Aquinas (1948) na kitabu chake, “Summa Theologica”; Plato (1961) na vitabu vyake, “Gorgias” na “The Republic”; Hans Jonas (1984) na kitabu chake, “The Imperative of Responsibility”; J. Budziszewski (1997) na kitabu chake, “Written on the Heart”; David Oderberg (2010) na makala yake, “The Metaphysical Foundations of Natural Law”; Edward Feser (2015) na makala yake, “In Defense of the Perverted Faculty Argument”; pamoja na Melissa Moschella na Robert George (2015) katika makala yao “Natural Law.”

Mjadala unafuata, lakini baada ya kubainisha "uzio wa miundombinu ya kifikra na kinadharia" utakaoongoza uchambuzi huu.

3. Uzio wa miundombinu ya kifikra na kinadharia

Dunia yetu imejaa utitiri wa mifumo ya kimaadili. Kwa mfano, kuna mfumo wa maadili ya Kikristo, Kiislamu, Kibahai, Kikonfuchio, Kibuda, na Kiyahudi.

Katika ulimwengu wa kisekulari kuna maadili ya kikomunisti, kijamaa, kidemokrasia, kifalme, na maadili asilia.

Mifumo hii hufanana na kutofautiana kutokana na inavyojibu maswali ya kudumu kuhusu mwingiliano wenye sura ya kietiolojia, yaani sura ya sababu na matokeo, kati ya maisha ya mtu mmoja mmoja, mazingira ya kimaumbile, na mazingira ya kijamii. Napendekeza kwamba, maswali makubwa ni kumi.

Ni maswali kuhusu aina tofauti za upaswa (oughtness): Yaani, kuna upaswa wa kimaadili, upaswa wa kibayolojia, upaswa wa kiepistemolojia, upaswa wa kimantiki, upaswa wa kipraksiolojia, upaswa wa kietiolojia, na upaswa wa kiteolojia. Ufafanu wake unafuata.

Mosi, ni swali la kiteolojia na linauliza, “mango wa Mungu wa dini yetu unasema nini kuhusu maisha bora na ustawi thabiti wa kila mtu?”

Pili, swali la kibayolojia linauliza, “binadamu ni kiumbehai chenye hulka ya namna gani endapo udhati wake utatazamwa kama mti wenye matawi mbalimbali?”

Tatu, swali la kisaikolojia linalouliza, “kuna uhusiano gani kati ya fikra, maamuzi na matendo ya kibinadamu?”

Nne, swali la kiepistemolojia linauliza, “tunawezaje kupata maarifa kuhusu sifa zinazoambatana na hulka ya ubinadamu na matawi yake mbalimbali?”

Tano, swali la kisemiotikilinauliza, “tunaweza kutumia alama gani tunapowasiliana kuhusu maarifa tuliyo nayo juu ya hulka ya ubinadamu na matawi yake mbalimbali?”

Sita, swali la kiakisiolojia linauliza, “maarifa yetu kuhusu sifa zinazoambatana na hulka ya ubinadamu yanaonyesha kwamba ni tunu zipi zenye mchango chanya kwa ustawi wake na tunu gani zenye mchango hasi kwa ustawi wake?”

Saba, swali la majukumu ya kimaadili linauliza, “maarifa yetu kuhusu sifa zinazoambatana na hulka ya ubinadamu yanaonyesha kwamba ni matendo yapi zenye mchango chanya kwa ustawi wake na matendo gani zenye mchango hasi kwa ustawi wake?”

Nane, swali la kimantiki linauliza, “tunawezaje kuchuja na kupata kanuni za kimaadili kutokana na maarifa yetu kuhusu sifa zinazoambatana na hulka ya ubinadamu, lakini bila kuvunja kanuni za kimantiki?”

Tisa, swali la kiprakisiolojia linauliza, “tunawezaje kupangilia malengo, mbinu na mazingira ya utekelezaji wenye kuleta ufanisi wa matokeo tunayoyataka?”

Na kumi, swali linalohusu namna ya kutofautisha matumizi ya majawabu ya maswali haya nane katika sekta tofauti linauliza, “tunawezaje kutumia majawabu ya maswali haya nane katika sekta mbalimbali za maisha ya watu, kama vile sekta ya elimu, afya, kilimo, ufugaji, biashara, ujenzi, viwanda, siasa, mazingira, ujinsia, ndoa, na sekta baki?

Naona kuwa, maswali haya tisa yanaunda “uzio wa miundombinu ya kifikra na kinadharia,” wenye umbo la pande tisa, yaani “nonagoni.” Umbo la nonagoni ni ndugu wa maumbo kama vile pentagoni na heksagoni.

4. Jawabu kwa swali la kiteolojia

Swali la kiteolojia linalouliza, “mpango wa Mungu wa dini yetu unasema nini kuhusu maisha bora na ustawi thabiti wa kila mtu,” na majibu ya kambi ni haya:

Kwamba, inawezekana kuwa kanuni za maumbile, tunazozikubali kwa kauli moja, zilitoka kwa Mungu fulani, japo hatukubaliani kwa kauli moja ni Mungu yupi amesanifu kanuni zipi, lini na kivipi;

Kwamba, uharamu wa tabia, kama vile wizi, hautokani na tamko la kimungu kwamba "usiibe", bali tamko la kimungu kwamba "usiibe" linatokana na ukweli kwamba, tabia hiyo inapingana na kanuni ya ustawi wa watu, na hivyo tamko la kimungu ni mfereji wa taarifa tu;

Na kwamba, kwa hiyo, hata bila kujiuliza kanuni za maumbile zimetoka wapi, tunaweza kujadili na kukubaliana kuhusu kanuni za maadili asilia kutokana na kanuni za maumbile pekee bila kuongelea kanuni za ufunuo wa kimungu.

5. Jawabu kwa swali la kibayolojia

Swali la kibayolojia linalouliza, “binadamu ni kiumbehai chenye hulka ya namna gani endapo udhati wake utatazamwa kama mti wenye matawi mbalimbali,” na majibu yao ni haya:

Kwamba, hulka ya binadamu inahusisha seti ya sifa na tabia za kimaumbile zitakazojitokeza katika mwili wake baada ya kuwa amekomaa, kustawi, na kufukia ukamilifu wake; kwamba, silika asilia za kibayolojia zilizo katika viungo mbalimbali vya mwili ni dira asilia zenye kuzionyesha akili za watu hulka ya ubinadamu ikoje;

Kwamba, wanadamu ni “viumbe wenye miili” yenye kazi kuu mbili, kulinda maisha ya kiumbehai kupitia ushirikiano wa kifiziolojia uliopo kati ya viungo mbalimbali mwilini na kuendeleza ukoo wa watu kwa kuzaa watoto wapya;

Kwamba kila kiungo cha mwili wa mtu kinayo silika asilia ya kibayolojia inayokielekeza namna ya kutekeleza kazi yake;

Kwamba, wanadamu huzaliwa katika jumuiya, kukulia katika jumuiya, na kuunda jumuiya mpya, na hivyo ni “wanajamii”;

Kwa hiyo, wanaona kwamba, kwa kuwa ustawi wa binadamu unakuwepo endapo kila kiungo cha mwili kinatekeleza kazi yake kwa ufanisi, hatua ya kwanza katika kutafuta kanuni za kimaadili ni kubainisha silika asilia ya kibayolojia ambayo hutoa dira ya kiutendaji kwa kila kiungo cha mwili.

Na hatimaye, wanahitimisha kwamba, kwa kuwa, binadamu wote, isipokuwa walemavu, wanayo seti ile ile ya akili, utashi, viungo vya mwili, na silika asilia za kibayolojia, basi, inafuata kimantiki kwamba, kwa sehemu kubwa, silika asilia za kibayolojia zinaunda msingi thabiti wa kutofautisha kati ya tabia njema na tabia mbaya, bila kujali mapokeo, uzito, urefu, jinsia, dini, rangi, utaifa au kabila la mtu.

6. Jawabu kwa swali la kisaikolojia

Tatu
, kuhusu swali la kisaikolojia linalouliza, “kuna uhusiano gani kati ya fikra, maamuzi na matendo ya kibinadamu,” majibu yao ni haya:

Kwamba, wanadamu ni “viumbe wenye urazini,” yaani uwezo wa kutumia ubongo kufikiri, kukumbuka, kutambua, kuamua na kufanya matendo huru ya kimwili chini ya uongozi wa ubongo, matedo haya yakiwa ni mbinu ya kufanikisha lengo kuu la maisha binafsi na ustawi wa jamii.

7. Jawabu kwa swali la kiepistemolojia

Swali la kiepistemolojia linalouliza, “tunawezaje kupata maarifa kuhusu sifa zinazoambatana na hulka ya ubinadamu katika matawi yake anwai,” na majibu yao ni kama ifuatavyo:

Kwamba, silika asilia za kibinadamu zinagunduliwa pole pole kwa njia ya mazoea, na pia kutokana na mafunzo rasmi, kama vile, kupitia masomo ya darasani kuhusu bayolojia, kemia na fizikia.

8. Jawabu kwa swali la kisemiotiki

Swali la kisemiotiki linalouliza, “tunaweza kutumia alama gani za mawasiliano tunapobadilishana maarifa tuliyo nayo juu ya hulka ya ubinadamu,” na majibu yao ni kama ifuatavyo:

Kwamba, aina ya kwanza ya alama za mawasiliano ni alama zikiwa zinabeba maana inayozingatia mapatano ya kinasibu kati ya watu waliozibuni, kama vile maneno ya lugha ya Kiswahili, au lugha ya Kiingereza;

Kwamba, aina ya pili ya alama za mawasiliano ni alama zilizobuniwa na binadamu zikiwa zinabeba maana inayozingatia ufanano uliopo kati ya alama na kitu kinachowakilishwa na alama, mfano alama za barabarani, ramani ya eneo, au picha ya kitu;

Kwamba, aina ya tatu ya alama za mawasiliano ni alama asilia zenye kubeba maana inayozingatia hali ya utokanifu iliyopo kati ya kitu na alama yake, ambapo sababu huwa alama ya matokeo, mfano ni mawingu kuwa alama ya mvua.

Na kwamba, aina ya nne ya alama za mawasiliano ni alama asilia zenye kubeba maana inayozingatia hali ya utokanifu iliyopo kati ya kitu na alama yake, ambapo matokeo huwa alama ya sababu, mfano ni moshi kuwa alama ya moto.

Hivyo, misamiati muhimu katika kujadili maadili asilia ni: viungo vya mwili, kazi za viungi vya mwili, silika asilia za kibayolojia kama zinavyodhihirika kupitia kazi za viungo vya mwili, ustawi wa binadamu, akili na utashi.

9. Jawabu kwa swali la kiakisiolojia

Swali la kiakisiolojia linalouliza, “maarifa yetu kuhusu sifa zinazoambatana na hulka ya ubinadamu yanaonyesha kwamba ni tunu zipi zenye mchango chanya kwa ustawi watu na tunu gani zenye mchango hasi kwa ustawi watu,” na majibu yao ni kama ifuatavyo:

Kwamba, kitu chochote kinachohusiana na silika asilia ya kibayolojia kama inavyodhihirika kwenye viungo vya mwili ni tunu ya kibinadamu.

Mfano, uwezo wa kuona kwa macho, uwezo wa kisikia kwa masikio, uwezo wa kuonja kwa ulimi, uwezo wa kunusa kwa kutumia pua, uwezo wa kusukuma damu kwa moyo, uwezo wa kuvuta pumzi kwa mapafu, uwezo wa kupokea na kusaga chakula tumboni, uwezo wa kuzaa watoto kwa kutumia jenitalia, uwezo wa kupoza mwili kwa kutoa jasho kupitia vinyweleo, uwezo wa mama kumnyonyesha mtoto wake kwa kutumia matiti yake, na uweo wa kuendelea kuwa hai, na kadhalika.

10. Jawabu kwa swali la kiprakisiolojia

Swali la kiprakisiolojia linalouliza, “tunawezaje kupangilia malengo, mbinu, na mazingira ya utekelezaji ili kupata ufanisi wa matokeo yanayotakiwa,” na majibu ya kambi ni haya:

Kwamba, kila kitendo cha kibinadamu ni mbinu inayotekelezwa kwa ajili ya kufanikisha lengo fulani, na katika mazingira fulani, mazingira hayo yakiwa yanatueleza ulini, uwapi, na uvipi wa kitendo husika.

Kwamba, mtekelezaji wa kitendo cha kibinadamu hufanya uamuzi wa kuchagua mbinu, lengo na mazingira ya utekelezaji, baada ya kutathmini na kuridhika kwamba muungano wa vitu hivi vitatu utampatia matokeo anayoyataka.

Na kwamba, ili matokeo yaliyokusudiwa na mtendaji yatimie, mtendaji anapaswa kuhakikisha kuwa kuna muungano wa lazima wenye sura ya kietiolojia , yaani sura ya sababu na matokeo, kati ya mbinu, lengo na mazingira ya utekelezaji.

Mfano, huwa tunawasha moto (lengo) kwa kutumia njiti ya na kasha kavu la kiberiti (mbinu) ndani ya chumba kisicho na upepo mkali (mazingira), kwa kuwa kuna muungano wa lazima wenye sura ya kietiolojia , yaani sura ya sababu na matokeo, kati ya vitu hivi vitatu.

Yaani, kwa mujibu wa kanuni za kietiolojia, ufanisi wa matokeo unahitaji mbinu halali, lengo halali na mazingira halali, na sio vinginevyo. Kwa maneno mengine, mbinu haramu haiwezi kufanikisha lengo halali.

11. Jawabu kwa swali la kimaadili

Swali la majukumu ya kimaadili linalouliza, “maarifa yetu kuhusu sifa zinazoambatana na hulka ya ubinadamu yanaonyesha kwamba ni matendo yapi yenye mchango chanya kwa ustawi wake na matendo gani yenye mchango hasi kwa ustawi wake,” na majibu yao ni kama ifuatavyo:

Kwamba, kanuni za maadili ni miongozo kuhusu matendo yanayotakiwa kwa ajili ya kufanikisha ustawi wa kiumbehai, kama vile binadamu, kulingana na hulka yake ya kimaumbile;

Kwamba, kila kitendo cha binadamu kinaambatana na malengo ya aina mbili, lengo la mtendaji na lengo la kitendo. Mfano, kulamba asali ili kufaidi utamu wake ni lengo la mtendaji, wakati kazi asilia ya kujenga mwili baada ya asali kulambwa ni lengo la kitendo.

Kwamba, pale lengo la mtendaji linapokubaliana lengo la kitendo, basi kitendo hicho kitaleta ustawi wa mhusika, na hivyo kinakuwa kitendo kizuri kimaadili.

Na kwamba, pale lengo la mtendaji linapopingana na lengo la kitendo, basi kitendo hicho hakitaleta ustawi wa mhusika, na hivyo kibaya kimaadili.

Kutokana na masharti haya mawili, hoja ifuatayo inazaliwa:

Kwamba, kwa mujibu wa maumbile yao, watu wanayo mielekeo asilia inayowafanya wawe na shauku ya kutunza uhai, uzazi, ukweli, urafiki, jumuiya na malengo mengine yanayohusiana na silika asilia za kimwili na kiakili walizo nazo;

Kwamba, ni jambo jema kwa watu wote, kila mahali na kila wakati, kuenenda katika namna ambayo inaonyesha utii kwa kila silika asilia ya kimwili na kiakili waliyo nayo, na jambo baya kuzikiuka silika hizo;

Na kwamba, kwa hiyo, watu wote, kila mahali na kila wakati, wanapaswa kuenenda katika namna ambayo inaonyesha utii kwa kila silika asilia ya kimwili na kiakili waliyo nayo, na kujiuzuia kuzikiuka silika hizo.

Kimsingi, wanatoa hoja kwamba kuna kanuni moja kuu ya kimaadili ambayo inazaa kanuni nyingine zote. Kanuni hiyo inasema kuwa: “Tunapaswa kufanya matenda mema na kuepuka matendo maovu.”

Kwamba, tunaliyambua “tendo jema” kwa kutazama silika asilia za kimwili na kiakili. Kwa kutumia kanuni hii wanaorodhesha silika asilia sita zinazofaa. Kuna silika asilia ya kulinda uhai, kufanya ngono, kuelimisha watoto wetu, ujirani mwema, ujuzi wa Mungu, na kuishi katika jamii.

Kutokana na hizi silika asilia tunaambiwa kuwa kuna kanuni sita za daraja la kwanza katika sheria ya asili. Yaani: (1) kuhifadhi uhai wa mwanadamu, (2) kuzaa, (3) kusomesha watoto wako, (4) kuepuka ujinga, (5) kukitafuta kilele cha wema wote, na (6) kushirikiana na wengine badala ya kuwadhuru.

Kwamba, kila moja ya kanuni hizi za daraja la kwanza inajumuisha kanuni maalum zaidi za daraja la pili. Kwa mfano, kanuni isemayo kwamba “usidhuru wengine” inazalisha kanuni za daraja la pili kama vile “usiibe” na “usiue.” Kanuni za daraja la pili zinazalisha kanuni za daraja la tatu, kama vile "usiandike cheki mbaya."

Kadiri tunavyozidi kushuka chini zaidi katika madaraja ya kikanuni, vivyo hivyo kanuni zinazidi kuwa mahususi zaidi, na kuondoka kwenye uwanja wa sheria asilia na kuingia katika uwanja wa sheria za kibinadamu. Hizi hubadilika kulingana na mazingira ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Lakini, katika ngazi ya jumla, kanuni za msingi, kama vile “usiwadhuru wengine,” ni sawa katika watu wote.

Wanasema kuwa sheria ya binadamu hubeba nguvu ya sheria ya asili ikiwa imechujwa kwa usahihi kutokana na kanuni asilia. Hata hivyo, ikiwa kwa namna yoyote ile inapingana na sheria asilia, si sheria tena bali ni upotovu wa sheria, wanasema.

Hata hivyo, nadharia hii unakumbana na changamoto moja. Ingeweza kusimama imara, kama wanadamu wote, kila mahali na kila wakati, wangekuwa na silika asilia za kibindamu zile zile.

Lakini, ukweli ni kwamba, baadhi ya silika asilia za kibindamu ni silika za kisekta. Na silika za kisekta zinazalisha maadili ya kisekta.

Mfano, “silika asilia ya kunyonyesha mtoto” ni silika ya kisekta kwa kuwa inaihusu sekta ya wanawake pekee, na tena sekta ya wanawake wenye rutuba ya uzazi na wasio wanawake wagumba.

Vivyo hivyo, “silika asilia ya uheterofilia” ni silika ya kisekta kwa kuwa inaihusu sekta ya watu wenye kuvutiwa kimapenzi na watu wa jinsia tofauti.

Kwa hiyo, basi, “silika asilia ya kunyonyesha mtoto” haiwezi kutumika kutunga kanuni za maadili zinazowahusu wanawake au wanaume wasio na uwezo wa “kunyonyesha mtoto.”

Katika suala hili, sekta ya wanaume inahitaji kanuni zake za maadili asilia, na vivyo hivyo kwa sekta ya wanawake.

Kadhalika, “silika asilia ya uheterofilia” haiwezi kutumika kutunga kanuni za maadili zinazowahusu watu wenye “silika asilia ya uhomofilia.”

Katika suala hili, sekta ya “maheterofilia” inahitaji kanuni zake za maadili asilia, na vivyo hivyo kwa sekta ya “mahomofilia.”

Hii ndiyo dosari iliyo katika sheria ya makosa ya jinai, yaani Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Toleo la 2002, katika ibara ya 154, isemayo kuwa:

“Any person who has carnal knowledge of any person against the order of nature, commits an offence.”

Katika kanuni hii, maneno "any person" yanazo maana mbili. Yaani "any [heterosexual] person" na "any [homosexual] person."

Pia, maneno "the order of nature" yanazo maana mbili. Yaani, "the order of [heterosexual] nature" na "the order of [homosexual] nature"

Jamii inayotoa haki sawa kwa watu wote walio sawa, na kutoa haki tofauti kwa watu walio tofauti inapaswa kurekebisha kanuni hii kusudi isomeke tofauti kwa kila kundi.

Kwa kuzingatia "kanuni ya uheterofilia" kama kanuni yenye kipaumbele kwa sababu inawahusu watu wengi katika Taifa, yaani "heteronormative norm," napendekeza kwamba, yanahitajika marekebisho yafuatayo:

1. “Any [heterosexual] person who has carnal knowledge of any person against the order of [heterosexual human] nature, commits an offence.”
2. “Any person [who is not medically certified as having a homosexual human nature and] who has carnal knowledge of any person against the order of [heterosexual human] nature, commits an offence.”

Hivi ndivyo “kanuni za ustahili,” yaani “principles of justice” zinavyotutaka kuenenda. Kanuni hizi zinasema kwamba, tunapaswa kutoa “haki sawa kwa watu wote walio sawa, na kutoa haki tofauti kwa watu wote walio tofauti.”

Bila kuzingatia misingi hii, tunaweza kujikuta tunaunda jamii inayokiuka “kanuni za ustahili” kwa kutumia kisingizio cha kutekeleza “kanuni ya maamuzi ya kiimla,” yaani “principle of totality.”

Kanuni hii hutumika kuhalalisha maamuzi ya kitabibu katika kukata na kuondoa baadhi ya viungo vya mwili vinavyohatarisha uhai wa mwili mzima.

Kwa ufupi, katika ngazi ya mtu binafsi,” yaani "an individual person," hii “kanuni ya maamuzi ya kiimla” inasema kuwa:

Pale kiungo kimojawapo katika “mwili wa mtu mmoja” kinapohatarisha uhai wa mwili wote, uhai wa kiungo hicho unaweza kusitishwa kwa ajili ya kulinda uhai wa mwili mzima.

Katika ngazi ya kikundi kama vile familia, yaani "corporate person," basi “kanuni ya maamuzi ya kiimla,” inasema kuwa: Pale mtu mmojawapo katika “mwili wa familia” anapohatarisha uhai wa familia yote, uhai wa mtu huyo unaweza kusitishwa kwa ajili ya kulinda uhai wa mwili wa familia nzima.

Na katika ngazi ya kikundi kama vile Taifa, “kanuni ya maamuzi ya kiimla” inasema kuwa: Pale mtu mmojawapo katika “mwili wa Taifa” anapohatarisha uhai wa Taifa lote, uhai wa mtu huyo unaweza kusitishwa kwa ajili ya kulinda uhai wa mwili wa Taifa zima.

Hivyo, katika ngazi ya “mperisona mwenye sura ya kikundi” kama vile familia na Taifa, “kanuni ya maamuzi ya kiimla” inageuka kuwa “Kanuni ya Kayafa,” kwamba heri mtu mmoja afe kwa faida ya Taifa zima.

Hii ni kanuni ya umachiaveli. Inapingana na “Kanuni ya Paulo,” kwamba “malengo mema hayapaswi kuhalalisha mbinu haramu.”

Kwa hiyo, ni “ukayafa,” na hivyo “umachiaveli,” kutumia silika asilia za tabaka mojawapo la watu kama msingi wa kutunga sheria zinazowahusu watu walio katika matabaka baki yasiyo na silika hiyo.

Hivyo, katika hatua hii, nadharia kongwe ya maadili asilia inajikwaa katika kisiki cha “ukayafa” na kisha kuangukia kisiki cha “umachiaveli.”

Kwa hiyo, bado kunahitajika jitihada za ukolonuzi wa kifikra katika eneo hili. Naongelea "decolonisation of the mind." Sio kila mawazo yanayoletwa na wazungu ni mazuri.

12. Jawabu kwa swali la kimantiki

Swali la mchujo wa kimantiki linalouliza, “tunawezaje kuchuja na kupata kanuni za kimaadili kutokana na maarifa yetu kuhusu sifa zinazoambatana na hulka ya ubinadamu, lakini bila kuvunja kanuni za kimantiki,” na majibu yao ni kama ifuatavyo:

Kwamba, kanuni muhimu ya kufanya mchujo wa kimantiki kuanzia kwenye madokezo kuelekea kwenye hitimisho, inasema kuwa, taarifa zote zilizo kwenye hitimisho lazima zichujwe kutokana na taarifa zilizo kwenye madokezo;

Kwamba, kwa kuwa silika asilia za kimwili na kiakili zinazopatikana katika viungo vya mwili ni dira asilia za tunu zilizo na mchango chanya kwa ustawi wa kibinadamu;

Na kwa kuwa mfumo wa kanuni za maadili yanayoongoza ustawi wa kiumbehai, kama vile binadamu, unapaswa kuakisi, kukubaliana, na kusikilizana na taarifa za kimaumbile zilizomo kwenye silika asilia za kimwili na kiakili, ndani ya mwili wa kiumbehai, ambazo ni chimbuko la majukumu yote;

Basi, inafuata kimantiki kwamba, silika asilia za kimwili na kiakili zinapaswa kuchukuliwa kama msingi thabiti wa miongozo ya kimaadili unaopaswa kuheshimiwa na kila mtu, kila mahali na kila wakati.

Yaani, tunapaswa na tunaweza kufanya mchujo wa kimantiki moja kwa moja kuanzia kwenye silika asilia za kimwili na kiakili ili kupata kanuni za kimaadili bila kuvunja kanuni za michujo ya kimantiki.

Twende kwa njia ya mifano, na mfano wa kwanza ni huu: Watu wote wanayo silika asilia ya kibayolojia inayowaelekeza kuishi katika jamii (taarifa ya kifiziolojia);

Kama viumbe wote walioko katika tabaka moja wanapenda kustawi, mara zote na katika sehemu zote, viumbehai wote waliomo katika tabaka moja wanapaswa kuenenda katika namna ambayo inaonyesha utii kwa kila silika asilia ya kimwili na kiakili waliyo nayo (taarifa ya kipraksiolojia);

Ni kweli kwamba, viumbe wote walioko katika tabaka moja hupenda kustawi (taarifa ya kisaikolojia).

Hivyo basi, mara zote na katika sehemu zote, watu wote wanapaswa kulinda uhai wa jamii yao (taarifa ya kimaadili).

Mfano wa pili: Samaki wakubwa wanayo silika asilia ya kibayolojia inayowaelekeza kuwameza samaki wadogo (taarifa ya kifiziolojia);

Kama viumbe wote walioko katika tabaka moja wanapenda kustawi, mara zote na katika sehemu zote, viumbehai wote waliomo katika tabaka moja wanapaswa kuenenda katika namna ambayo inaonyesha utii kwa kila silika asilia ya kimwili na kiakili waliyo nayo (taarifa ya kipraksiolojia);

Ni kweli kwamba, viumbe wote walioko katika tabaka moja hupenda kustawi (taarifa ya kisaikolojia).

Hivyo basi, mara zote na katika sehemu zote, samaki wakubwa wanapaswa kuwameza samaki wadogo (taarifa ya kimaadili).

Mfano wa tatu: Hakuna mtu anayeweza kukua na kustawisha vipaji vyake bila kupata msaada wa jamii alimozaliwa kama ambavyo hakuna maslahi ya pamoja katika jamii yanayowezekana bila kuunganisha vipaji vya mtu mmoja mmoja (taarifa ya kifiziolojia);

Kama viumbe wote walioko katika tabaka moja wanapenda kustawi, mara zote na katika sehemu zote, viumbehai wote waliomo katika tabaka moja wanapaswa kuenenda katika namna ambayo inaonyesha utii kwa kila silika asilia ya kimwili na kiakili waliyo nayo (taarifa ya kipraksiolojia);

Ni kweli kwamba, viumbe wote walioko katika tabaka moja hupenda kustawi (taarifa ya kisaikolojia).

Hivyo basi, katika ngazi binafsi, kila mtu anapaswa kuwa na haki ya kutumia vipaji vyake kama vile kufikiri, kuamua na kufanya matendo huru ya kimwili, na katika ngazi ya kijamii, kila mtu anapaswa kubeba jukumu la kushirikiana na wenzake katika kufanikisha maslahi ya pamoja (taarifa ya kimaadili).

Mfano wa nne: Kazi ya matiti ya mama mwenye mtoto mchanga ni kunyonyesha mtoto wake (taarifa ya kifiziolojia);

Kama viumbe wote walioko katika tabaka moja wanapenda kustawi, mara zote na katika sehemu zote, viumbehai wote waliomo katika tabaka moja wanapaswa kuenenda katika namna ambayo inaonyesha utii kwa kila silika asilia ya kimwili na kiakili waliyo nayo (taarifa ya kipraksiolojia);

Ni kweli kwamba, viumbe wote walioko katika tabaka moja hupenda kustawi (taarifa ya kisaikolojia).

Hivyo basi, mara zote na katika sehemu zote, kila mwanamke mwenye mtoto mchanga anapaswa kumnyonyesha kwa kutumia matiti yake, na sio vinginevyo (taarifa ya kimaadili).

Mfano wa tano: Kitendo cha kunywa kemikali ya hemloki husababisha kifo cha kimwili (taarifa ya kifiziolojia). Kusema kuwa “mtu anapaswa kufanya kitendo fulani” tunamaanisha kuwa “atatimiza matamanio au malengo yake kupitia kitendo hicho” (taarifa ya kipraksiolojia). Watendaji wote huwa na matamanio ya kuepuka kifo (taarifa ya kisaikolojia). Kwa hiyo, watendaji wote wanapaswa kuepuka kunywa hemloki (taarifa ya kimaadili).

Mfano wa sita: Kitendo hiki huhatarisha ustawi wa watu (taarifa ya kifiziolojia). Kama watu wote wanataka kustawi, wanapaswa kuepuka kitendo hiki (taarifa ya kipraksiolojia). Watu wote hupenda kustawi (taarifa ya kisaikolojia). Kwa hiyo watu wote wanapaswa kuepuka kitendo hiki (taarifa ya kimaadili).

Mfano wa saba: Kitendo hiki huchangia ustawi wa watu (taarifa ya kifiziolojia). Kama watu wote wanataka kustawi, wanapaswa kufanya kitendo hiki (taarifa ya kipraksiolojia). Watu wote hupenda kustawi (taarifa ya kisaikolojia). Kwa hiyo watu wote wanapaswa kufanya kitendo hiki (taarifa ya kimaadili).

Katika mifano hii, mambo mawili yako wazi. Kwanza, mifano yote ni hoja zenye muundo wa kimantiki unaoheshimu kanuni ya uhalali wa mchujo wa kimantiki. Yaani, taarifa zilizo katika hitimisho zinatokana na taarifa zilizo katika madokezo (logical validity).

Lakini, hoja zote zinalo tatizo la kukosa uhalisia unaozifanya zikubalike kwa kila mtu, kila wakatu na kila mahali (logical plausibility).

Tatizo liko kwenye dokezo la pili, yaani maneno haya: “Mara zote na katika sehemu zote, viumbehai wote waliomo katika tabaka moja wanapaswa kuenenda katika namna ambayo inaonyesha utii kwa kila silika asilia ya kimwili na kiakili waliyo nayo.”

Kuna mifano mingi inapingana na tamko hili. Na mfano wa haraka ni kwamba, mojawapo ya “silika asilia za kimwili na kiakili walizo nazo” watu ni “kanuni ya uzito,” yaani “law of gravity.”

Kanuni hii inasema kwamba, kila kitu kilichoko angani hudondoka kwa sababu ya uzito wake kuelekea kwenye uso wa dunia kwa mwendokasi unaoongezeka kwa meta 10 kwa sekunde.

Kuna wakati “silika asilia za kimwili na kiakili walizo nazo” watu zinawaelekeza kuitii kanuni ya uzito, na kuna wakati zinawaelekeza kuikaidi kanuni ya uzito.

Mfano, tunapotaka kuhama kutoka eneo moja hadi jingine, tunatembea kwa miguu, kwa kunyanyua miguu yetu katika namna ambayo inakiuka kanuni ya uzito kwa makusudi.

Na tukiwa tunatembea tukagundua tumemkanyaga mtu tunaikaidi kanuni ya uzito kwa makusudi, kwa kunyanyua mguu wetu ili kumwondolea maumivu mtu tuliyemkanyaga.

Pia, tunaposafiri kwa ndege kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, tunakuwa tumekubaliana na rubani wa ndege kuturusha angani kwa kukiuka kanuni ya uzito kwa makusudi. Hata tunaponyanyua mizigo tunavunja kanuni ya uzito.

Lakini, kuna wakati tunaitii kanuni ya uzito. Mfano ni wakati wa kushindilia udongo pale tunakuwa tunajenga msingi wa nyumba; tunaposhindilia kokoto wkati wa kujenga barabara; na tunapomsigina nyoka wakati wa kumwua.

Kwa hiyo, kanuni kwamba, “mara zote na katika sehemu zote, viumbehai wote waliomo katika tabaka moja wanapaswa kuenenda katika namna ambayo inaonyesha utii kwa kila silika asilia ya kimwili na kiakili waliyo nayo,” haina uhalisia. Inahitaji kuwekewa mipaka.

13. Jawabu kwa swali la falsafa matumizi

Swali linalohusu falsafa matumizi, linauliza namna ya kutumia majawabu kutoka kwenye maswali tofauti hapo juu katika sekta tofauti za maisha ya watu.

Kama tukitumia mfano wa sekta ya “afya ya mama na mtoto,” majibu ya kambi hii ni kama ifuatavyo: Kwamba, ni kosa kila wakati, kila mahali, na kwa kila mama anayenyonyesha kukamua na kumwaga maziwa yaliyo katika matiti yake, hata kama hakuna uwezekano wa kumpata na kumyonyesha motto wake kwa wakati huo.

Na kama tukitumia mfano wa sekta ya “vinyweleo na kazi yake ya kupoza mwili,” majibu ya kambi hii ni kama ifuatavyo: Kwamba, ni kosa kila wakati, kila mahali, na kwa kila mhusika kutumia pafyumu zinazositisha kazi ta kutoa jasho mwilini.

Mifano hii miwili inaonyesha wazi kwamba nadharia kongwe ya maadili asilia haiendani na uhalisia wa dunia ya leo.

Hii ndio sababu mojawapo iliyoawalazimisha baadhi ya wanafalsafa wa Marekani kutilia mashaka nadharia ya maadili asilia katika mtazamo mkongwe.

14. Majumuisho ya makala

Kwa ufupi, tumeona kwamba, kwa mtazamo wa wazungu wa kale, msingi wa nadharia kongwe ya maadili asilia ni masharti mawili.

Yaani, sharti kwamba kila kitendo ambacho kinakubaliana na “silika asilia ya kibayolojia” iliyo katika mwili wa mtu inafaa kwa ustawi wake na ni halali kimaadili; na sharti kwamba kila kitendo ambacho kinakiuka “silika asilia ya kibayolojia” iliyo katika mwili wa mtu hakifai kwa ustawi wake na ni haramu kimaadili.

Kutokana na masharti haya mawili, hoja ifuatayo inazaliwa:

Kwamba, kwa mujibu wa maumbile yao, watu wanayo mielekeo asilia inayowafanya wawe na shauku ya kutunza uhai, uzazi, ukweli, urafiki, jumuiya na malengo mengine yanayohusiana na silika asilia za kibayolojia walizo nazo;

Kwamba, ni jambo jema kwa watu kuenenda katika namna ambayo inaonyesha utii kwa silika asilia za kibayolojia walizo nazo, na jambo baya kuzikiuka silika hizo;

Na kwamba, kwa hiyo, watu wanapaswa kuenenda katika namna ambayo inaonyesha utii kwa silika asilia za kibayolojia walizo nazo, na kujiuzuia kuzikiuka silika hizo.

Dosari kubwa za hoja hii ni ukweli kwamba, japo inatwambia kuwa kwa sehemu kubwa “silika asilia za kibayolojia” ni misingi thabiti ya kimaadili, haituelezi ni kwa nini baadhi ya “silika asilia za kibayolojia” sio misingi thabiti ya kimaadili.

Haituelezi kwa nini ni kosa kimaadili kwa mtu kuitii “silika asilia ya hasira” aliyo nayo kwa kuwapiga wenzake;

Haituelezi kwa nini ni kosa kimaadili kwa mwanamume mwenye “silika asilia ya kujamiiana na mwanamke” kuitii “silika” yake kwa kufanya mapenzi na mtu asiye mke wake, wakati tendo hilo hilo ni halali kimaadili kama akilifanya pamoja na mkewe.

Haituelezi kwa nini ni kosa kimaadili kwa mwanamume mwenye “silika asilia ya kufanya ulawiti” kuitii “silika” yake kwa kumlawiti mwanaume mwenzake.

Na, haituelezi ni zipi “silika asilia za kibayolojia” zinapaswa kupewa utii na kila mtu, kila mahali na kila wakati; na zipi zinaweza kukaidiwa na kuminywa ama kwa muda, au kwa sehemu au kwa ujumla.

Lakini pia, Wamarekani mamboleo wanapinga utaratibu wa kufanya mchujo wa kimantiki ili kupata kanuni za maadili kwa kuanzia katika kanuni za maumbile, yaani silika asilia za kibayolojia. Kwa maoni yao, utaratibu huu ni sawa na kujaribu kuvuna mchicha kutoka kwenye shamba ya bangi.

Hivyo, makala ifuatayo inaonyesha jinsi Wamarekani mamboleo walivyojaribu kutatua matatizo haya.

15. Marejeo muhimu
  1. Aristotle (1941), Ethica Nicomachea, trans. W. D. Ross, in McKeon (1941), 935-1126.
  2. Aristotle (1941), Physica, trans. R. P. Hardie and R. K. Gaye, in McKeon (1941), 21-397.
  3. Aristotle (1941), Politica, trans. Benjamin Jowett, in McKeon (1941), 1127-324.
  4. David Oderberg (2010), “The Metaphysical Foundations of Natural Law,” in H. Zaborowski (2010).
  5. Edward Feser (2015), “In Defense of the Perverted Faculty Argument,” in Feser (2015).
  6. Edward Feser (2015), Neo-Scholastic Essays (South Bend, IN: St. Augustine’s Press).
  7. Edith Hamilton and Huntington Cairns, (ed.) (1961). Plato: Collected Dialogues. Princeton: Princeton University Press.
  8. H. Zaborowski (2010), (ed.), Natural Law in Contemporary Society (Washington, D.C.: Catholic University of America Press).
  9. Hans Jinas (1984), The Imperative of Responsibility: In SErach of an Ethics for the Technological Age (Chicago: University of Chicago Press).
  10. J. Budziszewski (1997), Written on the Heart: The Case for Natural Law. (Westmont: InterVarsity Press).
  11. Marcus Cicero (1929), De Re Publica: On the Commonwealth, trans. George Holland Smith and Stanley Barney Smith. Indianapolis: Bobbs-Merrill.
  12. Melissa Moschella and Robert George (2015), “Natural Law,” in The International Encyclopedia of Social and Behavioral Sciences, Second Edition.
  13. Plato (1961), Gorgias, in Hamilton and Cairns (1961), 229-307.
  14. Plato (1961), The Republic, in Hamilton and Cairns (1961), 575-844.
  15. Richard Mckeon (1941), (ed.) The Basic Works ofAristotle, (New York: Random House).
  16. Thomas Aquinas (1948), Summa Theologica (Rome: Marietti).

Imewasilishwa na:

Mama Amon,
Sumbawanga Mjini,
S.L.P P/Bag
Sumbawanga.

Dated: 21 March 2023

Updated: 24 March 2023.
 

Attachments

  • 1679412393050.jpeg
    1679412393050.jpeg
    11.6 KB · Views: 4
Nane, kuhusu swali la kiprakisiolojia linalouliza, “tunawezaje kupangilia malengo, mbinu, na mazingira ya utekelezaji ili kupata ufanisi wa matokeo yanayotakiwa,” majibu ya kambi ni haya:

Kwamba, kila kitendo cha kibinadamu ni mbinu inayotekelezwa kwa ajili ya kufanikisha lengo fulani, na katika mazingira fulani, mazingira hayo yakiwa yanatueleza ulini, uwapi, na uvipi wa kitendo husika.

Makala ya kisomi na ndiyo maana tunaona ktk jamii zilizo tofauti na zetu zimepanga na zina mfumo wa kila kitu kifanyikaje wakati ya jamii yetu ya 'kiswahili' vitu hivyo vya kujiuliza kwa kina kila sabuseti hatuna na jamii yetu kukosa mpangilio, kipi kipewe kipau mbele na kiwe endelevu kwa vizazi vijavyo n.k

Maadili Asilia ya ulipoanzia ujenzi wa mji mkongwe wa ngome (castle) uliozungukwa na maji (castle moat) kuilinda jamii husika hadi kuwa na makazi ya wazi yenye kuilinda jamii bila ujenzi za ngome mfano kuchora ramani ya mpangilio wa miji, mitaa na vijiji vyetu ktk namna itakayoweza kutufanya kuishi kwa raha bila karaha ya kukosa huduma ya haraka toka Polisi, barabara za kupitisha mabomba ya maji, mifereji ya maji taka au uzuiaji wa mafuriko n.k
1679416817230.png

Naendelea kuisoma makala hii, pongezi kwa Mama Amon kutupia makala hii muhimu ikiwa tunataka kuendelea ktk nyanja zote kama jamii ndani ya ulimwengu huu mpana .
 
Makala ya kisomi na ndiyo maana tunaona ktk jamii zilizo tofauti na zetu zimepanga na zina mfumo wa kila kitu kifanyikaje wakati ya jamii yetu ya 'kiswahili' vitu hivyo vya kujiuliza kwa kina kila sabuseti hatuna na jamii yetu kukosa mpangilio, kipi kipewe kipau mbele na kiwe endelevu kwa vizazi vijavyo n.k

Maadili Asilia ya ulipoanzia ujenzi wa mji mkongwe wa ngome (castle) uliozungukwa na maji (castle moat) kuilinda jamii husika hadi kuwa na makazi ya wazi yenye kuilinda jamii bila ujenzi za ngome mfano kuchora ramani ya mpangilio wa miji, mitaa na vijiji vyetu ktk namna itakayoweza kutufanya kuishi kwa raha bila karaha ya kukosa huduma ya haraka toka Polisi, barabara za kupitisha mabomba ya maji, mifereji ya maji taka au uzuiaji wa mafuriko n.k
View attachment 2560796
Naendelea kuisoma makala hii, pongezi kwa Mama Amon kutupia makala hii muhimu ikiwa tunataka kuendelea ktk nyanja zote kama jamii ndani ya ulimwengu huu mpana .
Bro, Msalimie Vladimir Ilyich Lenin ...
 
Nimesoma wewe uko confused not educated unachambua concept common in à complicated way.
Ushauri
Get à psychlogist
 
Nimesoma wewe uko confused not educated unachambua concept common in à complicated way.
Ushauri
Get à psychlogist
Badala ya kufurahi kwamba kuna mtu anaweza kuandika mambi haya kwa Kiswahil unashambulia mleta hoja!

Hata hivyo, kwani wewe ni SI unit ya maarifa yote hapa duniani?

Na kinachokufanya uache hoja na kumshambulia mleta hoja ni nini?

Lakini pia, hujui kuwa ninayo haki ya kutumia ubongo wangu kufikiri juu ya kitu chochote, na kwamba hapa duniani hakuna mtu mwenye mamlaka ya kunizuia kufanya hivyo?

Ni kana kwamba, huelewi historia ya vita chungu ya kupigania uhuru wa kufikiri na jinsi ushindi wake ulivyopatikana!

Ni vivyo hivyo kuhusu uhuru wa kujieleza.

Jielekeze kwenye hoja.

Fanya utafiti, leta hoja mbadala.

Vinginevyo kaa kimya.
 
Badala ya kufurahi kwamba kuna mtu anaweza kuandika mambi haya kwa Kiswahil unashambulia mleta hoja!

Hata hivyo, kwani wewe ni SI unit ya maarifa yote hapa duniani?

Na kinachokufanya uache hoja na kumshambulia mleta hoja ni nini?

Lakini pia, hujui kuwa ninayo haki ya kutumia ubongo wangu kufikiri juu ya kitu chochote, na kwamba hapa duniani hakuna mtu mwenye mamlaka ya kunizuia kufanya hivyo?

Ni kana kwamba, huelewi historia ya vita chungu ya kupigania uhuru wa kufikiri na jinsi ushindi wake ulivyopatikana!

Ni vivyo hivyo kuhusu uhuru wa kujieleza.

Jielekeze kwenye hoja.

Fanya utafiti, leta hoja mbadala.

Vinginevyo kaa kimya.
Wakati tunalinda haki zako ,usisahau nina haki ya kuita utumbo maoni yako
 
Wakati tunalinda haki zako ,usisahau nina haki ya kuita utumbo maoni yako
Ungefanya hivyo nisingehoji.
Hakika, "haki ya kuita utumbo maoni yangu" unayo, but with critical evidence provided.
Lakini wewe unashambulia mleta maoni.
Kidole kinakuonyesha mwezi, wewe huoni mwezi, unabaki kukodolea kidole!
Hiyo inaweza kuwa ni hatua ya kwanza ya safari yako ya kuelekea Milembe, Dodoma.
 
Ungefanya hivyo nisingehoji.
Hakika, "haki ya kuita utumbo maoni yangu" unayo, but with critical evidence provided.
Lakini wewe unashambulia mleta maoni.
Kidole kinakuonyesha mwezi, wewe huoni mwezi, unabaki kukodolea kidole!
Hiyo inaweza kuwa ni hatua ya kwanza ya safari ya kuelekea Milembe, Dodoma.
pole
 
Back
Top Bottom