Habari wakuu.
Napenda kutoa shukrani kwa wana JF wenzangu waliojitoa kunishauri katika ombi langu nililolitoa mwezi januari mwaka huu katika uzi huu
msaada hospitali nzuri ya kansa nchini india. Wapo walionishauri kwenye thread na wengine PM. Wote asanteni.
Pamoja na shukrani, nia ya uzi huu ni kueleza changamoto nilizokumbana nazo ili walau mtu mwingine ambaye hana mwanga juu ya matibabu nchini India asije kuzipitia.
Kabla ya kuomba ushauri hapa nilikuwa nimeshatafuta mwenyewe Hospitali kadhaa na nilikuwa nimeshapokea makadirio ya gharama ya matibabu ya hospitali hizo. Hospitali nyingi zilikuwa ngeni masikioni mwangu hivyo nilizihofia ubora wake na kubaki na dhana kuwa Hospitali nzuri na kubwa India ni ile wanayopenda kwenda kutibiwa viongozi wetu.
Nilipokea pia makadirio yao ambayo hayakuwa ya kutisha sana japo tayari nilikuwa nimeshapewa angalizo hapa JF kuwa wana tabia ya kutaja kiasi kidogo halafu ukishafika kule wanabadirika. Nikiwa nawaza hilo akatokea mgonjwa anayetaka kwenda moja ya Hosp zao na alipewa makadirio ya Dollar 15,000 na yeye akabeba Dolla 20,000 ili awe na ziada. Nikaona huyo nimuache atangulie halafu then atakuwa ananipa mrejesho kama ni kweli. Basi wiki ya kwanza tu Dollar 20,000 zote zikaisha, hadi wiki ya tatu akawa katumia dollar 40,000. Ikawa ndugu wanauza vitu wanamtumia fedha. Hii ilinitisha na nikaghairi kwenda huko.
Nikiwa sijui la kufanya, akatokea msamaria mwema akanishauri niende Hospitali flani Dar Es Salaam (jina nalihifadhi) kuwa kuna daktari atanisaidia kuniunganisha na hospitali nzuri na nafuu. Nikamuona huyo Dr, akaniunganisha na hospitali hiyo huku akinihakikishia kuwa wana gharama nafuu sana na ni waaminifu sana, kwamba ni kama taasisi ya dini inayotoa msaada.
Tukaondoka kwenda India. Tukapokelewa airport na watu wa “Hospitali” hiyo. Ile kufika hospitalini kwao tukashangaa kukuta ni kama dispensary. Kuna vyumba vinne tu vya kulaza wagonjwa. Kuna mgonjwa mmoja tu tena Mtanzania aliyeelekezwa na dokta huyo huyo aliyetuelekeza sisi. Ana wiki tatu, hajatibiwa bali anasubiri majibu ya vipimo. Kumbe hako ka dispensary wanafanya udalali. Ukishawatajia ugonjwa, wanaenda hospitali kubwa kutafuta Dr wa tatizo hilo then akiandika vipimo wanakuchukua na kukupeleka Diagnostic Centre mahali kwingine then unapima halafu unarudishwa kwenye kituo chao kusubiri majibu. Siku ya operation huyo Dr anakuja kukufanyia kwenye hako kakituo then unamlipa hela yake na baada ya hapo unalipa gharama zote za kukuhudumia baada ya operation. So kama uanatakiwa kuonwa na madaktari tofauti itabidi waitwe kwa style hii hii au utibiwe nusu.
Mwenyeji wetu alitushauri tuchague chumba kati ya vitatu vilivyobaki na kila chumba ni karibu laki 2 kwa siku na kwamba haturusiwi kukaa nje ya hospitali. Tulibishana hadi usiku wa manane. Katikati ya ubishi wetu akaja Dr waliyetuandalia akatupa treatment plan yake. Ikawa ni ghali sana ukijumuisha na gharama za kukaa pale. Tulikataa.
Kufupisha habari, baada ya hekaheka zote, siku ya pili tukafanikiwa kutoroka pale japo kwa shida na ikawa ni risk sana. Nikampa address mtu wa bajaji (wanaita Auto) atupeleke Hospitali nyingine ambayo tuliwasiliana nayo kabla hatujaondoka Tanzania, ila hatukuwa na nia nayo. Tuliamua kukimbilia hapo kwa sababu ndio hospitali ilikuwa mji tuliokwenda so hatukuwa na choice. Mungu mkuu, tukakuta ni kubwa sana, Multi-specialty, wamejipanga kila idara. Gharama ni nafuu sana na tukatafutiwa nyumba ya kupanga jirani na hospitali na kila siku wanatufata na gari na kuturudisha. Gharama ya matibabu ni kwa package na ukishalipa hakuna cha ziada, unasubiri tu kukabidhiwa mgonjwa wako baada ya matibabu. Wana huduma nzuri sana. Kama bei hujaiafiki unaweza omba wakapunguza kidogo. Kwa kweli mgonjwa wangu alitibiwa vizuri, haraka na kwa gharama nafuu sana tofauti na watu walivyokuwa wananitisha habari za milioni 50 hadi 70 kabla ya kuondoka.
Nilichojifunza
1. Watu wengi hatuna taarifa sahihi juu ya matibabu India so baadhi ya madaktari hapa nchini wanageuka madalali na hata kuingiza watu matatizoni ili mradi kuna kitu wanapata.
2. Wenzetu wako juu sana kimatibabu na teknolojia na gharama wakati mwingine ni za kawaida sana japo ukiingia kichwa kichwa utaliwa.
3. Kuna hospitali nyingi na nzuri sana ila hazina majina huku kwetu. Bahati mbaya hospitali inayofahamika huku kwetu hawaaminiki tena. Gharama zao ziko juu na bado wanabambikiza bill. Wanatumia umaarufu wao vibaya.
4. Vipo vingi vinavyochangia gharama ya matibabu kuwa kubwa. Malazi huchangia sana so ni bora kuhakikisha Hospitali inakutafutia nyumba nafuu mapema kabla ya safari.
5. Dawa katika pharmacy za hosp ni ghali kuliko mtaani so ni bora unapaondikiwa dawa za gharama ukanunue pharmacy kubwa mjini coz wanatoa punguzo la bei ukiomba. Wakati mwingine hata nusu bei unauziwa.
6. Chakula ni changamoto kubwa, vyakula vyao ni tofauti kabisa. Hivyo ni vyema kusafiri na unga, mchele, na maharagwe kama mnapendelea. Vitu hivyo havipatikani kabisa. Vyakula vingine vyote bei ni kama hapa hapa Tanzania.
Narudia tena kuwashukuru wote walionichangia mawazo na mimi nimeona nitoe mrejesho ili uwe mwanga kwa wengine. Asanteni wana JF.