....Nafasi aliyonayo Mama Six yeye pia aliigombea 2005 akaangukia pua.
Notburga Maskini anaendelea kujibu hoja (nanukuu tena):
(3) Baadhi ya mambo yanayoashiria tabia na mahusiano yangu ni kama yafuatayo:-
1.0 Kukubalika katika makundi ya watu wa aina mbalimbali:
1.1 Sehemu kubwa ya maisha yangu kuanzia shuleni, utumishi na jamii nimekuwa kiongozi. Hali hii imenifanya nishindwe kujitofautisha au kuweka umbali kati yangu na watu hasa wanyonge. Ndio maana hata nikiwa na madaraka ya kuwasimamia watumishi wenzangu kiutendaji katika ngazi ya menejimenti bado waliendelea kuniamini na kunichagua kuwawakilisha. Nafarijika kusema kuwa pamoja na mafanikio niliyoonesha katika maeneo niliyosimamia; sijawahi kuonekana kama Bossna wote niliowasimamia kwa maana ya watumishi na Wananchi.
1.2 Nafasi hizo ni Dada Mkuu wa Shule, Katibu wa tawi la Vijana (TYL), Katibu wa Tawi la wafanyakazi Tume ya utumishi wa Serikali za Mitaa (TUMITAA), ujumbe katika kamati ya Ajira Serikalini; Mkurugenzi Mtendaji, kaimu mkurugenzi wa utumishi na Utawala na nafasi nyingine kama ilivyo kwenye maelezo yangu binafsi. Nilichaguliwa na wenzangu kuwa Katibu wa Tawi la chama cha Wafanyakazi(nikiwa kaimu Mkuu wa Idara ya Utumishi na Fedha). Wengi mtakubaliana nami kuwa kuna baadhi ya wakubwa wa aina hii hutumia nafasi hizi kufanya mbwembwe, kujipatia fedha kwa kuwanyima haki watumishi wenzano, kuwatisha wateja wao na kuwadhalilisha hasa watumishi au wananchi wasio na madaraka!
Nilipopangiwa kazi katika Idara ya Ajira ya Tume nilipangwa kuwahudumia wafanyakazi wa Serikali za Mitaa nchini. Katika nafasi hii nilijenga mahusiano ambayo sikuyajua mpaka mwaka 2003 nilipojiunga na Mfuko wa Akiba wa Serikali za Mitaa.
1.3 Nilipokwenda LAPF mwaka 2001 kusimamia Component ya Menejimenti wakati wa kubadilisha Mfuko huo wa Akiba kuwa wa Pensheni tulishirikiana na Chama cha wafanyakazi wa Serikali za Mitaa kuunda Tawi la chama cha Wafanyakazi na Baraza la Wafanyakazi.
1.4 Kutokana na mahusiano hayo, Baraza Kuu la Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa TALGWU, walinichagua kwa kura sabini na tatu(73) kati ya kura themanini na mbili (82) zilizopigwa kuwawakilisha katika Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la vyama vya Wafanyakazi TUCTA safari hii nilikuwa (Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utumishi na Utawala LAPF). Ningekuwa mtishaji, ninayeogopwa nisingechaguliwa. Viongozi wenzangu walishangaa sana na kuniuliza ni kwa nini nimechaguliwa kwa kura nyingi kiasi hicho. Huenda walitishika na kitendo hicho.
1.5 Miaka miwili baadae nilichaguliwa kuwa mmoja wa wagombea 9 wa kiti kimoja (1) cha wafanyakazi. Japokuwa sikupata Ubunge; nilipata kura zipatazo 33 za wajumbe ambao nilikutana nao kwa mara ya kwanza au ya pili. Aliyeshinda alipata kura 60 kati ya kura 125 zilizopigwa. Wagombea wengine walipata kura 14,4,3,3,3,3,2 na 0. Kwa upande wangu wote tisa tulifanya vizuri; tulikwenda tukijua isingewezekana wote kuwa wabunge katika nafasi moja iliyokuwepo. Si mimi wala yeyote kati yetu aliyeangukia pua kama Mzitokabwela anavyoeleza kwenye maoni yake. Tulifurahi kwa kupata uzoefu na uwezo wa kushiriki, kujitangaza na kujenga mahusiano kati yetu wagombea, wapiga kura na viongozi wengine. Nina uhakika nisingeshiriki katika uchaguzi huo nisingeweza kutangaza nia kama nilivyofanya.
1.6 August Mwaka 2006 nilichaguliwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya wafanyakazi wa Tanzania TUCTA kwa kura 163. Aliyenifuatia alipata kura 65. Japokuwa nilifika mkutanoni siku moja kabla ya Uchanguzi nikitokea kijijini kwenye msiba wa mama mzazi. Nilipokea simu kutoka kwa mmoja wa viongozi wa TUCTA akiniuliza iwapo tumekwishamzika mama. Nilipomjibu ndio, alitaka niende Arusha. Nilijisikia mchovu na nilimwomba waendelee.
1.7 Baadae nilipigiwa simu na wajumbe wengine sita kila mtu kwa wakati wake kunishawishi niende. Mmoja kati ya hawa alikuwa ni mgombea wa nafasi hiyo ambayo iligombewa na watu 11. Alinieleza kuwa ni mgombea wa nafasi hiyo; lakini alinitaka niende kwa maneno yafuatayo namnukuu:
mimi nimechukua fomu, lakini ninavyoona upepo unaelekea sana kwako. Tafadhali njoo, nitakapotolewa kwenye mchakato, mimi na kundi langu tutakuunga mkono wewe
.
1.8 Nilifika Arusha siku moja kabla ya uchaguzi na nilishinda nafasi hiyo. Ushindi wangu uliwafurahisha wengi walionifahamu hasa Watumishi wa Serikali za Mitaa na LAPF. Tawi la Wafanyakazi LAPF walinipongeza kwa barua. Menejimenti haikunipongeza lakini baadae walinitumia sana katika kuushawishi uongozi wa Chama cha Walimu ili waalimu waandikishwe kwenye Mfuko wa LAPF.
1.2 Matokeo haya ni ushahidi wa mahusiano mazuri nilio nao na wenzangu. Nimeendelea kujenga uwezo na uzoefu wa kusimamia maslahi ya umma na pia ya wafanyakazi kwa wakati mmoja.
Majibu mengine yanakuja.