MBUNGE wa Jimbo la Rombo, mkoani Kilimanjaro, Basili Mramba ambaye aanakabiliwa na mashtaka ya kutumia vibaya madaraka yake akiwa Waziri wa Fedha, jana aliingia katika ukumbi wa Bunge kwa huku wabunge wakionekana kumpa pole na kumkumbatia.
Mramba aliingia katika ukumbi wa Bunge saa 2:46 asubuhi akiongozana na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo huku baadhi ya wabunge wakimfuata na kukumbatiana katika hali iliyoonyesha kuwa walikuwa wakimpa pole kwa matatizo yaliyomkuta.
Alipoingia katika ukumbi huo, alisimama kwa muda mrefu mlangoni kwa ndani, akizungumza na Benedicti Ole-Nangoro ambaye ni mbunge wa Kiteto (CCM) huku, baadhi ya wabunge wa CCM wakipita na kusalimiana naye kwa kukumbatiana.
Katika hali hiyo haikuweza kufahamika mara moja Mramba na Ole-Nangoro walikuwa wakizungumza kitu gani, kwa muda mrefu mlangoni hapo hadi mazungumzo yao yalipokatizwa na sauti iliyoashiria kuwa Spika wa Bunge alikuwa anaingia katika ukumbi huo.
Ole-Nangoro ni mmoja wa wabunge walioingia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuziba nafasi za wazi baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo la Kiteto Benedict Losulutya mwishoni mwa mwaka 2007, hivyo sio mbunge wa siku nyingi katika bunge hilo.
Mbunge huyo wa Rombo alipewa kibali na Mahakama kwa kutembelea jimbo lake na hata kuhudhuria vikao vya bunge akiwa bado ni mbunge halali wa jimbo hilo, ingawa kesi yake bado iko katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Haikuweza kufahamika mara moja ni kwa nini mbunge huyo, alifuatwa na wabunge wengi kutoka katika chama chake (CCM na kusalimiana naye, ingawa dalili zilionyesha kuwa walikuwa wakimfariji kesi inayomsumbua.
Wakati wa mchana mbunge huyo, alitoka katika ukumbi wa bunge mnamo saa 7:03 akiwa amefuatana na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anna Makinda, wabunge walindelea kumfuata na kusalimiana naye kama ilivyokuwa asubuhi.
Mramba anatuhumiwa kutumia vibaya madaraka yake akiwa Waziri wa Fedha wakati wa utawala wa awamu ya tatu chini ya Rais mstaafu Benjamini Mkapa na alifikishwa mahakamani pamoja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini kwa wakati huo Daniel Yona na baadaye kufuatia na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Gray Mgonja, ambaye pia alipandishwa kizimbani kwa tuhuma za aina hiyo.
Hivi sasa yuko nje kwa dhamana na mahakama ilimpa ruhusa ya siku 29 kuanzia Januari 3 hadi Februari 2, mwaka huu kwa ajili ya kwenda kusalimia ndugu, kutembelea jimbo lake na kuhudhuria mkutano wa bunge.
Pia Yona na Mgonja na wako nje kwa dhamana na walishapewa ruhsua ya kwenda kuwatembelea ndugu zao nje ya Dar es Salaam.