The Game has begun...
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown leo (Jumatano, Aprili 16, 2008), amemshutumu Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, akimwita mwizi wa kura, kuhusiana na Uchaguzi Mkuu wa Zimbabwe uliofanyika Machi 29, mwaka huu.
Shutuma hizo za Brown zimetolewa kwenye siku ambako Uingereza na Marekani, kwa pamoja, zimeongeza kasi ya shinikizo lao kwa Serikali ya Rais Mugabe kuhusiana na uchaguzi mkuu huo.
Nchi hizo mbili zimetumia nafasi ya mkutano wa viongozi wakuu ulioitishwa kujadili jinsi Umoja wa Mataifa (UN) unavyoweza kushirikiana na Umoja wa Afrika (AU), katika kutatua migogoro ya Afrika, kuishambulia Serikali ya Mugabe ya Zimbabwe.
Waziri Mkuu Brown amekuwa wa kwanza kuzungumza katika kikao hicho cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwenye Makao Makuu ya UN mjini New York, Marekani.
Uchaguzi ulioibiwa hauwezi kamwe na kwa njia yoyote ile kuwa uchaguzi wa kidemokrasia, amesema Brown katika hotuba yake ya dakika tano kwenye kikao hicho.
Zimbabwe ambayo ilifanya uchaguzi mkuu Machi 29 mpaka sasa haijatangaza matokeo ya kura ya urais, siku 18 tokea kufanyika kwa uchaguzi huo, ingawa mpaka sasa matokeo ya serikali za mitaa, ya ubunge na ya seneta yamekwishatangazwa.
Brown ambaye nchi yake itakuwa Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la UN mwezi ujao, hata hivyo, ametumia hotuba yake hiyo kutoa sifa kwa Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa juhudi zake katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo la kisiasa la Zimbabwe.
Lazima nielezee furaha yangu kwa jitihada zinazofanywa na SADC kutafuta ufumbuzi wa tatizo la Zimbabwe. Nafurahi zaidi kuwa jumuia hiyo itakutana tena mwishoni mwa wiki hii kujadili tena hali ya Zimbabwe.
Naye Mwakilishi wa Kudumu wa Marekani katika UN, Balozi Zalmay Khalilzad ameishutumu Zimbabwe kwa kusema kuwa ni dhahiri kuwa wananchi wa Zimbabwe wamenyimwa nafasi ya mabadiliko hata kama walipiga kura wakitaka kuona mabadiliko katika uongozi na mwelekeo wa nchi yao.
Ni siku 18 sasa tokea kufanyika kwa uchaguzi mkuu katika nchi hiyo, na mpaka sasa bado hakuna kauli yoyote juu ya matokeo ya kura ya urais. Ni dhahiri kuwa wananchi wa Zimbabwe wameibiwa, amesema Balozi Khalilzad.
Balozi huyo ametoa mapendekezo matano ya jinsi ya kutimiza matakwa na utashi wa mabadiliko ya wananchi wa Zimbabwe, ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa kundi la pamoja la UN na AU kutafuta njia ya kumaliza mgogoro huo.
Waziri Mkuu Brown amekuwa mmoja wa viongozi kadhaa wa serikali na nchi ambazo wamehudhuria mkutano wa leo uliotishwa na nchi ya Afrika Kusini ambayo ni mwenyekiti wa sasa wa Baraza la Usalama la UN.
Viongozi wengine ni Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Waziri Mkuu wa Italia, Romano Prodi; Rais wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo; Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Joseph Kabila; Rais wa Somalia, Abdullahi Yusuf Ahmed; Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi na Mwenyekiti wa Tume ya AU, Alpha Omar Konare.
Viongozi na wawakilishi wa nchi 42 wamezungumza katika kikao cha leo.
Mwisho.
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais na Habari
NEW YORK.
17 Aprili, 2008