Mkoa wa Hunan waelekea kuwa na hadhi sawa na Guangzhou kwa nchi za Afrika

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,014
1,039
193.jpg


Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na msukumo mpya kwenye ushirikiano katika sekta ya kilimo kati ya China na nchi za Afrika. Kupitia majukwaa mbalimbali ya biashara ya China, kama vile maonesho ya uagizaji wa bidhaa ya China yanavyofanyika mjini Shanghai (CIIE), maonyesho ya bidhaa za kilimo ya mji wa Changsha, Hunan, na hata kupitia majukwaa ya mtandaoni kama vile Alibaba, jd.com, Taobao.com, na shughuli mbalimbali za livestreaming, uuzaji wa bidhaa za kilimo za kutoka Afrika, umekuwa ukiingia kwenye hatua mpya.

Hapo awali ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika kwenye sekta ya kilimo, ulijikita zaidi kwenye upande wa China kutoa mafunzo ya utaalamu wa kilimo, utekelezaji wa miradi ya mfano ya kilimo, na hata kutoa msaada wa chakula kwa baadhi ya nchi zenye changamoto za usalama wa chakula. Hivi karibuni jukwaa jipya la ushirikiano katika sekta ya kilimo limejikita kwenye biashara ya mazao ya kilimo.

Ni muda mrefu sasa umepita tangu China itoe hadhi ya ushuru sifuri (zero tariff status) kwa uagizaji wa bidhaa nyingi za kilimo kutoka barani Afrika, lakini kutokana na kuwa na miundo dhaifu ya kufanikisha bidhaa za kilimo za Afrika kuingia kwenye soko la China, hakujawa na maendeleo ya kufurahisha kwenye uingizaji wa bidhaa za kilimo kutoka Afrika. Ndio maana China iliamua kufungua majukwaa mpya kushajiisha uagizaji wa bidhaa za kilimo kutoka Afrika.

Kati ya majukwaa hayo, maonyesho ya uchumi na biashara kati ya China na Afrika ya mji wa Changsha, mkoani Hunan (China-Africa Economic and Trade Expo -CAETE) ni mahsusi kwa uagizaji wa bidhaa za kilimo kutoka Afrika, yanaonekana kuleta nguvu na kasi mpya kwenye ushirikiano kwenye sekta ya biashara ya mazao ya kilimo.

Kwa sasa limekuwa ni jambo la kawaida, kusikia maofisa wa balozi wa nchi za Afrika na wafanyabiashara mazao ya kilimo kutoka nchi za Afrika wakikutana mjini Changsha na wateja wa China kutangaza bidhaa za kilimo kutoka kwenye nchi zao. Hadi sasa shughuli hiyo kubwa inayofanyika mara moja kila miaka miwili hadi sasa imefanyika mara mbili, na itakayofuata inatarajiwa kufanyika mwezi juni mwaka kesho

Kwa muda mrefu mji wa Guangzhou umekuwa ni lango la biashara kati ya China na Afrika, lakini dosari moja ambayo imekuwa ikizungumzwa mara kwa mara na wachambuzi wa mambo ya kidiplomasia na uchumi, ni kwamba mji huo ni lango la bidhaa za China kwenda Afrika na si za Afrika kuingia China. Hali hii imekuwa inatajwa kuwa ni chanzo cha kuwepo kwa urari mbaya wa biashara kati ya China na nchi za Afrika.

Kutokana na hali hii, China na nchi za Afrika wamekuwa wakitafuta njia mbalimbali za kujaribu kuleta uwiano kwenye biashara kati yao. Baadhi ya njia hizo ni pamoja na kuzialika nchi za Afrika kwenye maonesho mbalimbali ya biashara, ili kutafuta njia ya kupunguza urari mbaya wa biashara na nchi za Afrika.

Maonesho ya Changsha yanaonekana kufungua fursa mahsusi kwa nchi za Afrika, na hii itafanya mji huo kuwa na hadhi muhimu kwa nchi za Afrika. Mji wa Guangzhou ukiendelea kuwa lango la kuagiza bidhaa kutoka China, mji wa Changsha na mkoa wa Hunan, utakuwa ni lango la kuagiza bidhaa za kilimo kama vile kahawa, chai, matunda na bidhaa nyingine kuingia kwenye soko la China.

Mwanzo mzuri unaonesha kuwa kwa sasa ni bidhaa kilimo ndio zinaonekana kuingia kwenye soko la China, lakini katika siku za baadaye mkoa wa Hunan, China na nchi za Afrika watakuwa na fursa mbalimbali za ushirikiano, ikiwa ni pamoja na uvumbuzi wa teknolojia za kilimo kama vile matunda, usindikaji wa bidhaa hizo, minyororo ya usambazaji, na hata uuzaji. Pande zinazohusika zikizidisha ushirikiano na kufanya kazi pamoja, bila shaka pande zote mbili zitanufaika na fursa hizo.
 
Guangzhou ni mji wa kimafia mkuu. Unaweza kupata kitu chochote kwa bei yoyote. Vitu vingi vinavyouziwa Guangzhou havitengenezwi hapo ila hilo soko limewekwa maalumu kwa kuuzia vitu feki na og kila kitu kwa bei wezeshi ni umeme tu utaufuata Ywu na ujenz foshan lakin viwanda vyote kule fujiang soko lake ni Guangzhou.
 
Back
Top Bottom