MADARAKA Nyerere ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, ameibuka na kuthibitisha kuwa Mbunge wa sasa wa Musoma mjini (Chadema), Vincent Nyerere ni mdogo wao na mwanafamilia hiyo, kwani ni mtoto wa baba yao mdogo, Josephat Kiboko Nyerere.
Kauli ya Madaraka imekuja siku chache baada ya Rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa, kudai kwamba hamtambui mbunge huyo kuwa ni miongoni mwa familia ya Mwalimu Nyerere kwani katika kipindi chote alichofanya kazi na Mwalimu, hakusikia jina hilo.
Jumatatu ya wiki, akizindua kampeni za CCM katika uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki, mkoani Arusha, Mkapa aliuambia umati uliohudhuria kwamba hakuwahi kusikia kama kulikuwa na mtoto wa familia hiyo aliyekuwa akiitwa Vincent Nyerere.
Kauli hiyo ilipingwa vikali juzi na Vincent akisema si jambo la ajabu Mkapa kutomfahamu yeye kwasababu Mkapa si sehemu ya ukoo wao huku akimrushia kombora kwamba akiwa madarakani alishinikiza Mwalimu Nyerere kupelekwa Hospitali ya St Thomas, Uingereza, kinyume na matakwa ya familia yao na wakati huo huo, daktari wake Profesa David Mwakyusa alijua maradhi ya mwasisi huyo wa taifa.
Vincent alikwenda mbali zaidi na kumshambulia Mkapa kwa kuongoza ubinafsishaji holela enzi za utawala wake huku akimtuhumu kuuza viwanda na rasilimali za nchi kwa kisingizio cha ubinafasishaji.
Jana gazeti hili liliwasiliana na Madaraka kutaka kupata ukweli wa kauli hiyo ya Mkapa. Katika jibu lake fupi, Madaraka alithibitisha kuwa Vincent ambaye sasa ni Meneja Mwenza wa Chadema katika kampeni za Arumeru Mashariki, ni mmoja wanafamilia ya Mwalimu Nyerere ambayo chimbuko lao ni Kijiji cha Butiama mkoani Mara.
Katika jibu lake alilolituma kwa barua pepe Madaraka alisema; "Naomba kutoa maelezo yafuatayo kuhusu yanayozungumzwa kwenye kampeni za uchaguzi wa Arumeru; Ili kuepuka kujiingiza kwenye masuala ya kampeni, nitajibu sehemu ndogo sana ya maswali yako".
Aliongeza "Nataka kuthibitisha tu kuwa Mhe. Vincent Nyerere ni ndugu yetu, mtoto wa marehemu baba yetu mdogo, Mzee Josephat Kiboko Nyerere. Hayo maswali mengine naomba yaelekezwe kwa Mhe. Benjamin Mkapa au Mhe.Vincent Nyerere".
Maswali mengine ambayo Madaraka aliulizwa na Mwananchi ni pamoja na kwamba; Nani alishinikiza Mwalimu Nyerere kupelekwa St Thomas, Uingereza na kama familia hiyo iliridhia apelekwe Uingereza au nchi nyingine za Kijamaa.
Madaraka pia aliulizwa anamtambuaje Vincent Nyerere, Ni mmoja wa familia hiyo ama la?
Akizindua kampeni za CCM kwenye uwanja wa michezo wa Ngaresero, Usa River Jumatatu wiki hii, Mkapa alisema:
"Nimefanya kazi na Mwalimu kwa miaka 25, nikiwa mwandishi wake, Waziri na katika muda huo, nimemzika yeye, kaka yake na mama yake mzazi, sijawahi kusikia jina la mtu kama huyo katika familia ya hiyo".
Vicent alimtaka pia Mkapa kuacha kujiingiza katika masuala ya familia yasiyomuhusu na kwamba akiwa Rais mstaafu, ana kashfa nyingi zinazougusa utawala wake wa awamu ya tatu.