SoC01 Mimi, UKIMWI na tiba binafsi ya Uchanya

Stories of Change - 2021 Competition

NJUBER

Member
May 22, 2015
11
31
UKIMWI ulikuwapo, upo na bado utaendelea kuwepo mpaka hapo mkono wa heri utakapofanyika tiba ili kukomesha janga hili. Kiufupi Ukimwi bado unayachukua maisha ya ndugu zetu makundi kwa makundi. Kwa ndugu zangu ambao ni waraibu wa ngono nakuaseni kwamba pindi tunapofanya basi tufanye kwa kinga na kuzingatia tahadhari.

MWANZO WANGU NA VIRUSI VYA UKIMWI
Naamini nilizaliwa na Virusi vya Ukimwi tangu utotoni japo nimekuja kujigundua rasmi kwamba mimi ni mwathirika mwaka 2009 pindi nikiwa kidato cha pili.

Nilizaliwa siku ya mapumziko ya Muungano Jumanne ya tarehe 26/04/1994 huko mkoani Iringa katika Hospitali ya serikali ya mkoa Goverment Hospital (Sasa ni hospitali ya rufaa) Nilimpoteza Mama yangu miezi mitatu tu baada ya kuzaliwa kwangu.

Nililelewa na Bibi mzaa baba ilihali baba akisimama nafasi ya kuhakikisha napata matunzo kupitia kipato chake cha ngama alichokivuna kwenye kazi mbalimbali alizokuwa anazifanya. Nilichelewa sana kujua kwamba niliyekuwa namwita Mama hakuwa Mama ila ni bibi yangu hiyo yote ni kutokana na kuwa pembeni yake tangu nilipoliona jua na kujitambua. Niliondoka nyumbani na kuwa mbali na Bibi baada ya kuamua kuanza kujitegemea na kuhamia mkoani Njombe. Hicho ni kipindi ambacho nilikuwa na miaka ishirini.

Sikuwa na historia nzuri sana utotoni. Kiufupi nimekua nikiwa mgonjwa mgonjwa mpaka umri wa miaka 17. Historia hiyo ya kuugua mara kwa mara ndiyo iliyopelekea niamini kwamba maambukizi ya virusi vya ukimwi nilikuwa nayo tangu utotoni. Nilikuwa dhaifu sana kiasi cha kutabiriwa umauti na kila aliyenitazama pindi walipomtembelea bibi. Yaani nilikuwa tia maji tia maji kutokana na kukonda sana kiasi cha kuiumiza mifupa ikiwa nitatengwa kuketi bila ya kutanguliziwa kitu chochote chini.

Eneo jingine lililopelekea niamini wazi kwamba nilizaliwa na virusi vya ukimwi ni baada ya kuugua kifua kikuu nikiwa darasa la pili. Kifua kikuu kilipelekea nisitishe masomo ili nihamishie umakini kwenye dozi. Miaka ya 2002 - 2003 dozi ya kifua kikuu ilipaswa kunywewa hospitali tu na sio mtu apewe ili aende kunywea nyumbani. Na hicho ndicho kipindi ambacho kifua kikuu kiliua maelfu ya watu ndio maana watu walipaswa kusimamiwa na wahudumu wa afya pindi wanapomeza dawa zao. Nililazimika kusitishiwa masomo kwa muda kwasababu nilipaswa kuhudhuria hospitali kwa ajili ya unywaji wa dawa kila siku.

Baada ya kifua kikuu nilirejea shuleni na hapo nilihesabiwa mwanafunzi mdhaifu kwa kuwekewa nembo nyekundu begani. Nilipaswa kuwa na nembo hiyo kwenye mashati na masweta yangu kutokea darasa la pili mpaka darasa la saba.

WASAA NILIPOJUA NIMEATHIRIKA, BAADA YA VUGUVUGU LA UPOFU.

Sikuwahi kufikiria kwamba na mimi ni miongoni mwa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi. Naam! nilijihakikishia ushindi na niliamini mimi ni mzima wa afya wakati wote. Nililelewa kwa kuchungwa sana na kuchukuliwa tahadhari muda mwingi na wala sikuwahi kuhisi lolote zaidi ya kuamini kwamba kwasababu niliwahi kuugua kifuu kikuu kikali.

Wakati nikiwa darasa la sita, kuelekea darasa la saba nilianza kusumbuliwa na macho. Sikuamini kama macho yalikuwa ni tatizo, niliamini ilikuwa ni shida tu ya ukungu iliyosababishwa na ulaji wa maharage mara kwa mara. Nilijificha kusema kwakuwa nilikuwa sipendi kuvaa miwani. Nilishtukiwa mara kwa mara kutokana na kufinya macho pindi ninapokutana na mwanga mkali lakini bado nilificha. Nilijikongoja mpaka sekondari, nikaendaenda mpaka kidato cha pili.

Kwakuwa shida ilianza kuwa kubwa, baba aliamua kunichukua ili nije nifanyiwe uchunguzi CCBRT jijini Dar es Salaam. Bahati mbaya shida ya macho ilikuwa haionekani kwa vifaa vya kitaalam ilihali kwa macho ilionekana wazi kwamba nilikuwa na mtoto wa jicho wataalam wanaita Cataract.

Kutokana na usumbufu huo madaktari wakashauri nipimwe na damu yangu pia. Hapo ndipo bomu likalipuka mbele ya baba yangu ambaye alishajua undani wa afya yangu. Nilijiamini na nikawa na majibu yangu, sio siri nilikuwa na furaha tu maana kwa umri huo hata binti sikuwahi kumjua.
Majibu yalitoka nimeathirika, nikayapokea kikawaida tu na nilipoulizwa juu ya mtu niliyeambatana naye nikajibu kwamba ni baba na anapaswa aambiwe. Daktari akauliza juu ya kupima afya ya baba, mimi nikashinikiza apimwe baba akakataa kupimwa. Hapo ndipo nikatokwa na chozi na kuipoteza amani maana nilipata jibu la moja kwa moja kwamba chimbuko la shida yangu baba pia ni mhusika. Tuliambiwa mambo ya kufanya ili nianze kuhudhuria kliniki, tulifanya hivyo baada ya kurejea Iringa.

Kwa kuwa shida ya macho ilikuwa na utata na iligubikwa na taswira ya zongo, hivyo hakukuwa na lolote lililofanyika zaidi ya kupewa miadi ili nirejee wasaa mwingine. Nilirejea Iringa na kuanza kliniki lakini sikuanzishiwa dawa za kufubaza virusi vya ukimwi kutokana na kuwa na kinga nyingi. Sikwenda muda mrefu sana Kliniki, niliamua kusitisha na kuendelea na maisha yangu maana nilikuwa sijalikubali tatizo. Niliishi kwa kupotezea na sikutaka nijione mwathirika na mdhaifu japo mawazo yalipelekea niishe na kunyonyokwa nywele. Hatua mbaya zaidi ni pale nilipojiaminisha kwamba nilikuwa mzima baada ya kupata kikombe cha babu Ambilikile Mwaisapile wa Loliondo, nakumbuka tulikwenda familia nzima.

Shida ya macho haikukoma, tatizo liliendelea kukua na nakumbuka nilivuka kidato cha tatu kwa wastani mbaya sana lakini nilivushwa kwasababu kipindi hicho hakukuwako na kukariri darasa kwa sababu ya kufeli. Hali ilikuwa mbaya sana mpaka nikalazimika kusitisha shule mwezi wa nne baada ya kujiunga kidato cha tatu.

Kiufupi kukaibuka janga jingine la upofu lililopelekea niamini sina bahati, maana kuwa na Ukimwi nilihesabu ni adhabu tosha kwangu. Upofu uliniendesha kwa kipindi cha mwaka mzima mpaka hapo tatizo lilipokuja kuonekana na nikafanyiwa uchunaji wa macho na kuwa sawa. Kumbuka kwamba nilisema tatizo liligubikwa na zongo hivyo suluhu haikupatikana kirahisi ilitulazimu kukanyaga kila pahala kuanzia kwa waganga wa kienyeji, kanisani hadi kwa ndugu zangu waislamu.

Wasaa pekee nilioamini kujiua kuna faida ni wasaa niliosumbuliwa na macho. Niliwaza mara kadhaa kufanya hivyo lakini ujasiri, uthubutu, imani na kutokukata tamaa kwa bibi juu yangu kulinipigania mpaka tukayashinda yote. Baada ya mwaka mmoja nilipona na kurudi shule na kuendelea na masomo yangu kama kawaida japo nililazimika kukariri kidato.

Upofu ulipona lakini zimwi la Ukimwi liliendelea kuiteketeza nafsi yangu kwa kujihesabia mimi ni mfu ninayehesabia siku ya mazishi yangu. Mawazo yalinipelekea kuamini kwamba pombe na uhuni (ugumu) ndiyo suluhu ya kila kitu. Niliamua kuwa mgumu na kuanzisha genge la ulevi, utoro, na usumbufu shuleni. Tulifahamika kama UEC (UGUMU ENOUGH CREW) huku mimi nikiwa rais wa genge hilo. Tulisumbua kwa kitambo mpaka hapo tulipokuja kunasa na kusulubishwa hadi tukafukuzwa shule pindi tukiwa kidato cha nne. Tulifukuzwa shule na kuja kuruhusiwa kufanya mitihani ya mwisho baada ya baadhi ya wazazi wa watoto waliokuwa kwenye Genge kuomba radhi kwa walimu.

2013 nilihitimu rasmi kidato cha nne huku nikiwa nimebeba bango la kijana mhuni, mkorofi, na mlevi wa kutupwa. Genge halikwenda muda mrefu baadae lilikufa na kila mmoja kuelekea maeneo mbalimbali kwa ajili ya kusubiria matokeo. Kwa hiyari yangu mimi mwenyewe niliamua kuachana na ulevi na kumakinika kwenye masomo chuoni. Nilijiunga na chuo cha ualimu japo nilitamani kwenda bagamoyo ili nikanoe kipaji changu cha uchoraji. Ndoto hiyo ya kunoa kipaji iliungwa mkono na Baba lakini hakuweza kunisaidia kuitimiza kwasababu na yeye alianza kuugua kiasi cha kushindwa kuhimili hata kazi yake. Nilisomeshwa ualimu kwa ufadhili wa mjomba na nikaamua kumakinika na masomo tu hali iliyopelekea niujue uwezo wangu na kufanya vizuri chuoni.

Baba alianza kuugua mwishoni mwa mwaka 2013 na kuugua mfululizo mwaka 2014 wote mpaka kufikwa na mauti mwaka 2015 tarehe 2 mwezi wa 1. Hali ya baba ilinitisha maana aliyaishi mateso makubwa ya maradhi, kukonda na vidonda visivyopona. Ndugu bado waliendelea kuficha maradhi ya baba, nami niliendelea kuamini kilichokuwa kinamtesa ni Ukimwi.

Ilipita miezi saba tangu mazishi ya baba yafanyike, mwishoni mwa mwezi wa sita nami nikaanza kuugua. Nilibanwa haswa nakumbuka ilikuwa Taiphod na kwakuwa ilikuwa ni lazima kupima nililazimika kupima na kupokea majibu kimaigizo ilihali nilishajua kila kitu kunihusu. Tarehe 1 Julai 2015 nilianzishiwa rasmi dozi ya ARVs (antiretroviral). Sasa ni miaka sita tangu nianze dozi hiyo.

Kunywa dawa mpaka kuzizoea halikuwa zoezi jepesi kwa upande wangu. Nilikerwa na kero zake kama vile kizunguzungu, ukubwa wa vidonge na ladha yake ya uchungu. Lakini niliendelea kuzoea taratibu maana kila wasaa niliuona uzembe wa kufa kwa kujitakia kama ulivyomgharimu baba yangu. Baba alifariki kwasababu ya kupuuzia dozi nami sikutaka hilo linitokee.

Sikuamini kama ningekuwa na maisha marefu baada ya kujigundua kwamba mimi ni mwathirika. Niliutamani wasaa wa uhuru na amani kipindi nilipokuwa sijui lolote lakini hakukuwako na uwezo wa kuurejea utoto tena. Nilijifichaficha kunywa dawa na nilipata sana shida pindi nilipotembelea ugenini. Nilijishtukia kila pahala ambapo Ukimwi ulitajwa.

Nilihudhuria kliniki kwa kuvizia kwasababu dawa nilichukulia eneo la karibu kabisa na maeneo niliyokuwa naishi. Majuma yalikwenda, udhaifu ukaachia hatamu, mwili ukaanza kuzoea hali, kliniki nikazoeleka mpaka kukaririwa jina.

Kuna pahala nataka tufike, nataka niseme na waathirika, waliopo kwenye hatari ya kuathirika, nataka niseme na wote wenye maradhi sugu kwenye maisha yao. Nataka nifukue kaburi la hofu ya kifo na kumjaza ujasiri kijana wa kitanzania. Nataka niuanike ukweli ambao utafanyika dhamana ya kuwatoa wengi kwenye hofu. Nataka nifikie kilele cha hamasa ya waliooza kwa kujiogopa, kujihukumu, kujishtukia, na kujiona hawana maana tena. Nataka niamshe mioyo ya makamanda walioolemewa na vita. Usiache kuamini sisi sote ni wa thamani.

Ukipata wasaa nakuomba tena upitie mwendelezo wa makala hii mpaka hapo tutakapofikia tamati ya shindano hili kwa ajili ya ujenzi thabiti wa taifa.

Ahsante kwa muda wako.

Kwa majina halisi, Naitwa Victor Ramadhan Kalinga. +255 620 433 048 victorramadhankalinga@yahoo.com
 
Hongera sana mkuu
emoji120.png
. Ni ujasiri mkubwa sana kuandika jambo kama hili. Ni upendo mkuu Sana kutumia changamoto zako kwa ajili ya kutahadharisha wengine wasipate yakukutayo wewe. Mungu akujaalie afya njema na maisha ya furaha. Pole kwa kuwapoteza wazazi kwa janga la ukimwi
 
Hongera sana mkuu . Ni ujasiri mkubwa sana kuandika jambo kama hili. Ni upendo mkuu Sana kutumia changamoto zako kwa ajili ya kutahadharisha wengine wasipate yakukutayo wewe. Mungu akujaalie afya njema na maisha ya furaha. Pole kwa kuwapoteza wazazi kwa janga la ukimwi
Ahsante kwa yote.
Shukrani sana mkuu
 
Ujaniambia he umesha ajiriwa jeTendo unafanya au umeogopa kabisa?
Nilipita kwenye ajira baadaye nikaacha, nikarudi kupambana mtaani na sasa nipo kwenye biashara kama mshirika wa kibiashara (Business Partner) na nimewahi kushiriki tendo mara kadhaa na nina mchumba ambaye nitamuoa mwakani kwa kadri ambavyo Mwenyezi Mungu atajalia.
Ujaniambia he umesha ajiriwa jeTendo unafanya au umeogopa kabisa?
 
Usisahau kugusa neno VOTE pindi ukikamilisha kusoma andiko hili.
Neno VOTE linapatikana chini ya makala.

Ahsante kwa ushirikiano wako.
 
Baadhi ya nchi zitaacha kutumia ARV’s kuanzia mwaka huu. Wagonjwa watachomwa sindano inayoingia kwenye immune system na inadumu kwa miezi sita. Maana yake mgonjwa anachomwa sindano mbili kwa mwaka
Naam njia ya sindano ipo, sijui ni lini ilianza kutumika ila ipo na niliwahi kukutana na shuhuda kutokea South Africa anatumia njia hiyo. Nadhani bajeti za wizara zikikaa sawa, siku sio nyingi sindano pia itaingizwa nchini.
Baadhi ya nchi zitaacha kutumia ARV’s kuanzia mwaka huu. Wagonjwa watachomwa sindano inayoingia kwenye immune system na inadumu kwa miezi sita. Maana yake mgonjwa anachomwa sindano mbili kwa mwaka.
 
Naam njia ya sindano ipo, sijui ni lini ilianza kutumika ila ipo na niliwahi kukutana na shuhuda kutokea South Africa anatumia njia hiyo. Nadhani bajeti za wizara zikikaa sawa, siku sio nyingi sindano pia itaingizwa nchini.
Hii ni dawa mpya iko katika majaribio Imperial Collage. ARV za sindano zilitolewa kwa wenye magonjwa ya akili wasiokumbuka kunywa dawa kila siku, lakini gharama yake ni kubwa.
 
Hii ni dawa mpya iko katika majaribio Imperial Collage. ARV za sindano zilitolewa kwa wenye magonjwa ya akili wasiokumbuka kunywa dawa kila siku, lakini gharama yake ni kubwa.
Oh sawa muungwana sikulijua hilo. Ahsante kwa kuniongezea hili.
 
Kuishi kwa matumaini kunataka moyo...

Umeweza hili bila shuruti...mshukuru Mungu sana...

Mzae na watoto ...furaha ya roho...
 
Bro uko vyema japo Ibada sijaona ukiipa nafasi kwakuwa Mungu pekee ndie mwenye funguo ya maisha yako.

Mtolee sadaka akulinde na azidi kukutunzaaa.

Asante sana kijana mwenzangu songa mbelee usirudi nyuma.
Mungu wetu mpendwa akupiganie azidi kukulinda daimaa.



Sent from my SM-A125F using JamiiForums mobile app
 
Back
Top Bottom