Jeshi la Wananchi Tz, (JWTZ) ni chombo adhimu, angalau bado linaheshimika. Kuna sababu nyingi za kuliheshimu jeshi letu, ingawa sababu hizo zinagawanyika katika makundi makuu mawili. Moja, ni sababu zitokanazo na kazi za jeshi lenyewe. Hapo kuna nidhamu ya jeshi na wanajeshi (bila kujali wachache wanaoharibu taswira hiyo), misheni mbalimbali za ndani na nje zilizofanikishwa na jeshi letu, shughuli mbalimbali za kijamii katika kujenga taifa pamoja na kutoa huduma za kijamii (elimu, afya nk)
Pili, ni sababu zinazotokana na wananchi wenyewe. Hakuna namna wananchi wanaweza kufanya zaidi ya kuheshimu na kulienzi jeshi lao. Na kwa bahati nzuri, watanzania wamekuzwa kwa namna hiyo, ya kuliheshimu jeshi.
Natambua kuna baadhi ya watumishi wa jeshi wanaotumia 'sare' na vitambulisho vyao kujinufaisha mitaani, na wakati mwingine kufanya vitendo vya uonevu kwa raia. Hao ni wajinga wachache ambao leo sioni haja kuwajadili.
Pamoja na hayo, kuna jambo la kustua ambalo kama halitadhibitiwa, jeshi hili adhimu litageuka kuwa janga taifa; kutumiwa hovyo na serikali.
Narudia kwa msisitizo; "Kutumiwa hovyo na serikali".
Tulianza kuona jambo hili wakati Rais Magufuli akiwatunuku kamisheni wanajeshi waliohitimu mafunzo kule Arusha, Septemba mwaka 2017. Kwenye shuguli hizo za kijeshi, Rais alionekana kujadili jambo na Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, liloashiria kuwapo kwa mpango wa kufanya tukio la kisiasa.
Mpango unaoatajwa kuwapo ni ule wa kuwaita watu walioandaliwa (miongoni mwa wananchi waliohudhuria) ili wamsifie Rais kwa maneno waliopandikizwa. Baada ya Gambo kushindwa kuandaa mpango huo, Rais alisikika akimtukana mkuu huyo wa mkoa. Ilikuwa ni ishara mbaya kwa matukio hayo kufanyika kwenye shughuli za kijeshi.
Haikuwa bahati mbaya, matukio ya aina hiyo yanaendelea. Inaonekana ni kama hulka ya serikali ya awamu ya tano kulitumia jeshi, hata kwenye mambo yasio ya lazima.
Kutumia jeshi kwenye sakata la korosho, ni muendelezo wa matumizi ya hovyo ya jeshi. Pamoja na mikurupuko mingine, karibuni tutaona mpango huo ulivyoleta matokeo mabaya.
Tunaambiwa pia, jeshi limepewa kazi ya kulinda maduka ya kubadilishia fedha, eti kuna operesheni maalum ya kudhibiti wanaotakatisha fedha, inastua.
Je! Serikali haina mifumo ya kudhibiti utakatishaji fedha badala yake inatuma wanajeshi wakae kwenye milango ya maduka ya kubadilisha fedha? Natamani kujua taaluma za wanajeshi waliosimama kwenye milango ya maduka kama wana ufahamu wa masuala ya utakatishaji fedha.
Rais ana wasiwasi?
Matumizi ya jeshi, au kukimbilia kutumia jeshi katika mambo yanayoweza kufanywa na taasisi zingine, ni ishara ya nini? Wasiwasi? Hofu? Ulimbukeni wa madaraka? Au vitisho?
Ikiwa sababu ni wasiwasi na/au hofu ya kushindwa kuongoza, maana yake tayari umeshinda kuongoza. Hapa nirejee maneno ya Profesa Mkandala, kwamba kiongozi bora ni yule mwenye wafuasi wa hiari. Ikiwa Rais anatumia jeshi kwa kukosa imani na taasisi zingine, maana yake ameshindwa kuongoza taasisi hizo.
Je! Ni vitisho? Kama ni vitisho, Rais anamtishia nani? Haiwezekani kutumia jeshi kuwatisha watu mmoja mmoja ambao wanaonekana kuwa maadui (wa kisiasa). Jeshi linapotumika kwa lengo la vitisho, maana yake wanaotishiwa ni wananchi. Kuwatisha wananchi unaowaongoza ni ishara ya kushindwa kuongoza.
Bado natafuta kujua lengo la matumizi ya jeshi yasiyo ya lazima.
Mwisho, mimkumbushe Rais Magufuli na wafuasi wake, madaraka ni kama mchanga. Kadiri unavyoukumbatia mchanga kiganjani ndivyo unavyokuponyoka, na ukilegeza vidole pia unakuponyoka. Unahitaji kuwa mtu wa kiasi (gentle), mtu wa hekima na maarifa.
Ni vema kujua kwamba hakuna mahala pengine baada ya jeshi. Ikiwa matumizi haya ya jeshi yana lengo la kujitutumua, kutunisha misuli, maana yake umejitutumua hadi mwisho, na umetunisha misuli hadi mwisho, kwa kuwa jeshi ndio mahali pa mwisho. Hakuna pengine pa kukimbilia. Kutumia jeshi badala ya taasisi zingine ndio tafsiri ya kuyakumbatia madaraka (kama mchanga kiganjani) kwa nguvu zote, kifuatacho ni madaraka hayo kukuponyoka.
Ni vema hatua za haraka zikachukuliwa kudhibiti matumizi haya ya jeshi yasio ya lazima.
Nimeandika.