Shy !,Tumeipeleka habari hii kwenye magazeti...itaonekana kama ilivyo chini
Mike Sikawa wa BBC afariki dunia
MTANGAZAJI wa idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Mike Sikawa (55) ,amefariki dunia jana mchana baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu na ugonjwa wa kisukari.
Sikawa, ambaye pia aliwahi kufanya kazi katika Kampuni ya Tanzania Standard Newspapers (TSN) inayomiliki magazeti ya Daily News na HabariLeo, alifariki dunia juzi majira ya saa 8.47 mchana nyumbani kwake Njiro, nje kidogo ya mji wa Arusha.
Kwa mujibu wa mdogo wake marehemu, Mchungaji Charles Sikawa, ndugu yake alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari kwa muda mrefu na kutokewa na kidonda mguuni.
Mchungaji huyo alisema ndugu yake alipata matibabu katika hospitali mbalimbali hapa nchini ikiwamo AICC, KCMC, St. Thomas na Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili iliyoko Dar es Salaam lakini hakupata nafuu yoyote.
Alisema ilifika wakati nusura akatwe mguu uliokuwa na kidonda lakini madaktari walifanikiwa kukwangua nyama ya mguu wa kidonda lakini haikuweza kusaidia.
Mchungaji huyo aliendelea kusema kuwa baada ya kuhangaika kwa muda mrefu katika hospitali mbalimbali hapa nchini na kushindwa kupata nafuu, Sikawa alikuwa akipata matibabu akiwa nyumbani kwake hadi alipofikwa na mauti.
Alizaliwa Kingori wilayani Arumeru mkoani Arusha na kusoma elimu ya msingi katika eneo hilo kabla ya kufaulu na kuendelea na elimu ya sekondari katika shule ya Ilboru na Mzumbe ya mkoani Morogoro.
Katika miaka ya 1970, aliajiriwa katika kampuni ya TSN kama mwandishi wa kawaida na baadaye kujiunga na idhaa ya Kiswahili ya BBC kama mtangazaji. Ameacha mjane na watoto wawili ambao wako Amerika ya Kusini.
Mipango ya maziko inasubiri ndugu, jamaa na marafiki walioko nje ya mkoa wa Arusha na sehemu zote alizofanyia kazi.
Wakati huo huo, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro ametuma salamu za rambimbi kutokana na kifo cha mwandishi huyo na kuelezea jinsi alivyoguswa na msiba huo.
Dk. Migiro alisema alipoteuliwa kushika wadhifa huo katika UN, Sikawa alikuwa mwandishi wa kwanza kumtafuta kwa ajili ya kumhoji juu ya uteuzi huo.