Tutaisaidia Serikali kupitia mikataba Wanasheria
na Amana Nyembo
Tanzania Daima
WANASHERIA wa Tanganyika tawi la Arusha, wamedai kuwa, wapo tayari kuisaidia serikali kupitia mikataba yote yenye utata na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuiboresha ili kulinda maslahi ya taifa kwa mujibu wa katiba.
Hayo yalibainishwa jana katika taarifa iliyotolewa na Katibu wa chama cha wanasheria hao, Eliakunda Makange, kuhusu mikataba ya ubinafsishaji na uvunaji wa rasilimali za taifa, hususani madini.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa, katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, serikali inawajibika kuchukua hatua za kuweka wazi mikataba inayohusu ubinafsishaji wa mali za mashirika na taasisi za umma na mikataba inayohusu uchimbaji wa madini na vito vya thamani na uvunaji wa aina yoyote ya maliasili ya nchi.
Ilifafanua kuwa, kuwekwa wazi kwa mikataba hiyo, lengo ni kuwawezesha wananchi kujiridhisha iwapo inakidhi masharti ya katiba na kulinda maslahi ya taifa, badala ya usiri uliopo sasa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni jukumu la chama cha wanasheria hao kutetea na kuisaidia jamii juu ya masuala yanayogusa sheria na kutekeleza wajibu chini ya kifungu 3(e).
Aidha, waliielekeza serikali na wananchi kuwa, vifungu vya nane, tisa na 27 vya Katiba ya Muungano, vinatamka kuwa Tanzania ni nchi inayofuata misingi na demokrasia na haki ya kijamii, kwa hiyo serikali itawajibika kwa wananchi.
Taarifa hiyo, ilieleza lengo la katiba hiyo ni kuwezesha ujenzi wa Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, au chochote kati ya vyombo vyake, na kufuata siasa ya ujamaa na kujitegemea, inayosisitiza utekelezaji wa misingi ya kijamaa kwa kuzingatia mazingira.
Iliendelea kudai kuwa, shughuli za serikali zinatekelezwa kwa kuhakikisha kuwa utajiri wa taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi, na kuzuia mtu mmoja kumnyonya mwingine.
Matumizi ya utajiri wa taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi hasa yanaelekezwa kwenye jitihada ya kuondoa umaskini, ujinga na maradhi
Kila mtu ana wajibu wa kulinda maliasili ya Jamhuri ya Muungano, mali ya mamlaka ya nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, pia kuheshimu mali ya mtu mwingine, ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Ilieleza kuwa waliohusika kwa namna moja au nyingine katika kutia sahihi mikataba yenye utata hawana uwezo wala uhalali wa kuifanyia mapitio mikataba hiyo.
Hata hivyo, waliitaka serikali kuanzisha daftari maalum la kusajili mikataba yote inayohusu ubinafsishaji na uvunaji wa rasilimali za umma, ili mwananchi afanye upekuzi kwa lengo la kujiridhisha kuwa mikataba hiyo inalinda maslahi ya taifa kwa mujibu wa katiba.