Michirizi ya Damu

Michirizi ya Damu

SEHEMU YA 114

Fareed alijifanya kuswali, watu wengine walikuwa wakimshangaa, walijua kwamba alikuwa mtu wa dini sana kumbe upande wa pili kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea. Alichukua dakika saba, alipomaliza, akarudi garini huku uso wake ukiwa umefunikwa kwa kiasi fulani.

“Twende!” alisema Fareed, dereva akawasha gari na kuondoka mahali hapo huku polisi wale wakiwa kwenye magari mengine, hawakujua kama mtu waliyeamini kwamba alikuwa ni wa dini sana, aliyependwa kuswali kumbe ndiye alikuwa mtu waliyekuwa wakimtafuta kwa udi na uvumba.

Hawakuchukua muda mwingi wakafika Fayed, Fareed alimshukuru Mungu kwa kuona kwamba sasa ilikuwa ni nafasi yake ya kutoroka nchini Misri na kwenda katika nchi yoyote ya Ulaya.

Aliamini kwamba kama angepanda ndege ndani ya nchi hiyo ilikuwa ni lazima kukamatwa, hakutaka kuona hilo likitokea na ndiyo maana aliamua kupanda meli, tena iliyokuwa ikielekea Ulaya kwa kupitia katika Mfereji wa Suez ambayo ingempeleka mpaka Cyprus na kuunganisha mpaka nchini Uturuki.

Alipofika Fayed, akateremka na kumlipa dereva kiasi cha fedha alichokihitaji na kuondoka mahali hapo. Hakutaka kuelekea hotelini, bado aliona kwamba alikuwa kwenye hatari kubwa hivyo kama angediriki kwenda huko ingekuwa ni rahisi kwake kukamatwa.

Alichokifanya ni kwenda katika ufukwe wa Ziwa Great Bitter ambapo kwa mbali aliziona meli zikiwa zimepaki huku nyingine zikipakiza mizigo ambayo ilitakiwa kupelekwa katika nchi mbalimbali barani Ulaya.

Huku akiwa mahali hapo, macho yake yakatua kwa vijana wanne waliokuwa wamekaa pembeni kabisa huku macho yao yakiangalia kule meli zilipokuwa.

Kwa ufahamu wa harakaharaka akahisi kwamba hao walikuwa Beach Boys ambao kazi zao zilikuwa ni kuwafanyia mipango watu waliokuwa wakitaka kuzamia kwenda barani Ulaya.

Akawafuata, aliposimama mbele yao, kila mmoja akayainua macho yake na kumwangalia mwanaume huyo.
 
SEHEMU YA 115

Hawakujua mwanaume huyo alikuwa akifanya nini mahali hapo kwani haikuwa rahisi kumuona mtu mweusi akiwa katika ufukwe huo.

Wakamuuliza alichokuwa akikihitaji, hakuwaficha, akawaambia kwamba alitaka kuzamia kuelekea barani Ulaya, alikuwa amesafiri kwa umbali mrefu, lengo kubwa likiwa ni kufika huko.

“Umetokea nchi gani?” aliuliza mwanaume mmoja.
“Nigeria!”
“Ooh! Sawa. Kwenda Ulaya si tatizo. Ila una pesa?” aliuliza kijana mmoja.
“Kiasi gani?”

“Kukufanyia mpango ni paundi mia tano. Ukiingia ndani ya meli, mwenyewe utatakiwa kumlipa,” alisema kijana mmoja.
“Kiasi gani?”
“Huwa anahitaji paundi elfu moja!”
“Hilo si tatizo!”
“Una passipoti?”
“Ndiyo!”

“Umegongewa viza?”
“Yeah! Ya hapa ila nilikuwa mpitaji tu!”
“Sawa.”

Hiyo ndiyo ilikuwa kazi yao kubwa, walikuwa wakiwasafirisha watu wengi katika Mfereji wa Suezi kuelekea nchini Uturuki, Hispania au Ugiriki. Walikuwa wakilipwa kiasi kikubwa cha fedha ambacho waligawana na watu wa ulinzi na kuwaruhusu watu hao kupita bila tatizo lolote lile.

Fareed alipowapa kiasi hicho, wakachukua mtumbwi mmoja na kuanza safari ya kufuata meli moja kubwa ya mizigo. Kabla ya kuifikia, wakawasiliana na nahodha aliyekuwa akihusika katika meli hiyo, walimwambia kwamba walikuwa na mtu aliyetaka kuingia nchini Uturuki.

Hilo halikuwa tatizo, walipofika katika meli hiyo, wakakaribishwa kinyemela, nahodha, Mzee Ahmed akakabidhiwa kiasi chake cha dola elfu moja na kumpeleka Fareed ndani ya chumba kimoja cha siri kilichokuwa na mizigo mingi na kumwambia akae huko.

Moyo wa Fareed ukaridhika, akahisi kwamba hiyo ndiyo njia salama ya kuepuka mkono wa sheria nchini Misri. Alijifungia ndani ya chumba hicho, baada ya saa kadhaa, meli ikatoa nanga mahali hapo na kuanza safari ya kuelekea Cyprus kabla ya kuingia nchini Uturuki.
 
SEHEMU YA 116

Mfereji Wa Suez ulikuwa ni miongoni mikubwa duniani, ukiachana na mfereji wa Panama, huu ndiyo uliokuwa ukishika nafasi ya kwanza kabisa kwa urefu ambao ulikuwa na urefu wa kilometa 102 huku ukiwa na madaraja mawili makubwa ambayo yalikuwa yakitoka Cairo ambapo ni Magharibi mwa Misri kwenda Sinai ambapo ni Mashariki mwa Misri.

Safari ilikuwa ikiendelea, njiani, kulikuwa na vizuizi vingi walitakiwa kuvipitia na kote huko meli ya Mzee Ahmed ilikuwa ikiachiwa, haikuwa ikikaguliwa kwani kazi yake kubwa ya kuwavusha watu ilijulikana na alikuwa akiwapoza kiasi fulani cha pesa.

Kwake, safari haikuwa ngumu, alipita Ismailia, meli iliendelea mbele mpaka Al Firdan, kote huko alipokuwa akipita, hakuwa na hofu yoyote ila kitu kilichomfanya kuona ugumu wa kumvusha Fareed ni kwenye bandari ya Said ambayo ndiyo ilikuwa ya mwisho kuelekea nchini Cyprus.

Alimuomba Mungu kwani watu wa hapo hawakuwa wakikubali kuiona meli yoyote ikivuka na watu ambao walikuwa wakizamia Ulaya.

Kila meli ilipekuliwa vilivyo na kitu ambacho kilikuwa kikimsaidia Mzee Ahmed kutokugundulika kama alikuwa akiwavusha watu ni kwamba alikuwa akiwaweka katika chumba ambacho kilikuwa karibu na injini.

Ili kumuweka mtu humo kulitakiwa kuwa na maandalizi makubwa, ilitakiwa chumba kiandaliwe wiki moja kabla. Kwa Fareed ilikuwa vigumu kumuweka humo kwa kuwa alikuwa mteja wa ghafla ambapo hawakuwa wameandaa chumba kama kinavyotakiwa na hivyo kuepelekwa katika chumba kingine.

Hawakuchukua muda mrefu wakafika katika bandari hiyo, walipofika katika bandari hiyo, meli hiyo ikawekwa katika foleni na meli nyingine, walitakiwa kubaki mahali hapo mpaka meli walizozikuta zikaguliwe na ndipo waendelee na safari.

Wakati huo, picha za Fareed zilikuwa zimesambaa kila kona, zilibandikwa na kila mtu alitaka kumkamata mtu huyo. Mbali na kuwatafuta watu waliokuwa wakivuka kuelekea barani Ulaya lakini pia walikuwa wakimtafuta Fareed ambaye mpaka katika kipindi hicho hawakujua mahali alipokuwa.
 
Back
Top Bottom