Michirizi ya Damu

Michirizi ya Damu

SEHEMU YA 100

Ndani ya piramidi kulikuwa na mwanga hafifu, watu waliokuwa ndani ya piramidi hilo walikuwa wakiongozwa na watu maalum waliokuwa na kazi ya kuwatembeza watu huku na kule.

Macho ya Maria hayakutulia, muda wote alikuwa akiangalia huku na kule, alitaka kumuona mwanaume aliyeuteka moyo wake, alimwambia kwamba angekuwa mahali hapo pamoja naye lakini mpaka muda huo hakumuona na hakugundua kwamba alikuwa katika kundi la watu waliokuwa wameingia na kundi hilo.

Fareed hakutaka kuonekana, macho yake yalikuwa chini, hakutaka kukutanisha macho yake na msichana Maria. Waliendelea kusonga mbele, hakuwa akimsikiliza muongozaji aliyekuwa akiwaambia kuhusu kila kitu kilichokuwa mule ndani.

Alichokifanya Fareed ni kuchukua simu yake na kumtumia ujumbe mfupi Maria kwamba watakapofika sehemu kubwa, basi aachane na Keith na kumfuata yeye.

“Sawa. Utaniambia utakapokuwa,” alisema Maria, kidogo moyo wake ukapoa, alikuwa na hofu kubwa na alipowaangalia vizri watu wale waliokuwa katika kundi lile, akamuona mwanaume huyo japokuwa kulikuwa na mwanga hafifu.

Walikwenda mpaka walipofika sehemu kubwa, ilionekana kuwa kama uwanja fulani, sehemu ambayo Wamisri kwa zamani walitumia kama sehemu za wafalme kufanya vikao na viongozi wengine, kwa pembeni, kulikuwa na vyumba vingi ambavyo vingine vilitumika kama vyumba vya kulalia lakini vingine vilitumika kama makaburi.

“You can go to other rooms to have a look,” (mnaweza kwenda kwenye vyumba vingine kuangalia) alisema msimamizi.
Keith hakutaka kumuachia Maria, alimshikilia msichana huyo na kuanza kwenda kwenye chumba kimoja. Kwenye chumba walichokuwa wakienda, walikuwa wawili tu.

“Baby! Just wait,” (mpenzi! Subiri kwanza!) alisema Maria.

“What’s wrong?” (kuna tatizo gani?)
“I have seen my aunt?” (nimemuona shangazi yangu)
“Where is she?” (yupo wapi?)
“In that room,” (ndani ya chumba kile) alisema Maria huku akijifanya kuwa na hofu.
 
SEHEMU YA 101

Alimdanganya mwanaume huyo, aliyemuona hakuwa shangazi yake bali mwanaume ambaye alitamani sana kulala naye. Akataka kuondoka hapo kumfuata Fareed, Keith alipong’ang’ania akamwambia kwamba huo si muda mzuri wa kumuona shangazi yake kwani hakuwa akijulikana nyumbani na haikuwa mila za kiafrika.


Keith hakuwa na jinsi, kwa kuwa alimpenda sana msichana huyo, akamuacha aendele kwa huyo shangazi yake na yeye angemsubiri ndani ya chumba hicho.


Wakati hayo yote yakiendelea, Fareed alikuwa akiangalia kupitia mlangoni huku akiwa ametokeza jicho tu. Alipomuona Maria akianza kuja kule alipokuwa, kwa haraka sana akapitia mlango mwingine, wakati msichana yule akiingia ndani ya chumba kile, na yeye alikuwa akitoka kutoka katika mlango mwingine.


Alitakiwa kuwa na haraka sana, hakutakiwa kupoteza muda hata mara moja. Akatembea kwa mwendo wa haraka mpaka katika chumba alichokuwemo Keith, akaingia ndani. “Who are you?” (wewe nani?) aliuliza Keith kwani kwa jinsi Fareed alivyoingia ndani ya chumba kile, alionekana kama mtu mwenye haraka nyingi.
“Nobody!” (si mtu yeyote) alijibu Fareed,
Hiyo ndiyo ilikuwa nafasi yake aliyokuwa akiisubiri kwa hamu. Akamsogelea Keith mahali pale, alipomfikia, akamziba mdomo, hakutaka kuchelewa, akamchoma kisu mara tatu tumboni kisha kumlaza chini.


Hakukuwa na mtu aliyeona tukio hilo, kulikuwa na mwanga hafifu na kila mtu alikuwa na mpenzi wake katika vyumba vingine. Fareed alipohakikisha mwanaume huyo amekufa, akatoka ndani ya chumba kile na kuelekea katika chumba alichokuwemo.
“Ulikwenda wapi?” aliuliza Maria huku akimwangalia Fareed.
“Kwani hukuniona?”
“Hapana! Ulijificha?”
“Ndiyo! Nilidhani unakuja na bwana wako!” alisema Fareed.


Akamkumbatia Maria na hapohapo kubadilishana mate. Mwili wa Maria ukasisimka mno, hakuamini kama kweli siku hiyo alikuwa na mwanaume huyo.


Hakutaka kurudi kwa Keith, alikuwa tayari kugombana naye lakini si kumuacha mwanaume huyo ambaye kwake alikuwa mwanaume mzuri, hakuwa radhi kumuacha.

Wakaendelea kuangalia mambo ya historia mpaka walipoitwa ambapo walitakiwa kukusanyika na kuondoka. Maria aliogopa, alijua fika kwamba Keith angemuona na kumkaripia kwa kile alichokuwa amekifanya.
 
Back
Top Bottom