SEHEMU YA 71
Ndani ya dakika kadhaa wanaume watatu wakafika mahali hapo, walikuwa wamejiandaa vilivyo, kwa jinsi walivyoonekana, walikuwa tayari kufanya kazi muda wowote ule. Belleck akawakaribisha huku akionekana kuwa na furaha tele, katika maisha yake yote, hakukuwa na kitu kilichokuwa kikimuingizia fedha kama biashara ya madawa ya kulevya.
Alitaka kumtumia Fareed katika biashara zake, alitaka kumpa mzigo wa madawa ya kulevya na kuyasafirisha maka nchini Ufaransa. Hilo kwake halikuwa tatizo, usiku huohuo wakamnywesha kete kumi na mbili za madawa ya kulevya na kumsubiri aamke ndipo wamwambie kuhusu safari hiyo kwani tayari walimuandalia tiketi yake.
Fareed aliamka baada ya saa moja kupita. Alijisikia uchovu, hakujua alikuwa mahali gani. Pale alipokuwa kulikuwa na kitanda kikubwa, chumba kizuri, akaamka na kuanza kuangalia huku na kule na ndipo kumbukumbu zake zikaanza kurudi na kukumbuka kwamba mara ya mwisho alikunywa pombe kali na baada ya hapo hakujua ni kitu gani kiliendelea.
“Nipo wapi? Belleck kanileta wapi?’ alijiuliza huku akisimama kutoka pale alipokuwa.
Akaelekea dirishani, akachungulia, alikuwa kwenye ghorofa ya nne, aliogopa, ile haikuwa hoteli aliyokuwa amefikia, ilikuwa nyingine kabisa. Alipoangalia kwenye kimeza kidogo akakutana na kitabu kidogo kilichoandikwa ‘King Caspian Hotel’.
“Nimefikaje King Caspian?” alijiuliza.
Aliijua hoteli hiyo, ilikuwa hapohapo Kuwait, haikuwa hoteli ile aliyofikia, alijiuliza sana lakini mwisho wa siku akajua kwamba Belleck ndiye aliyekuwa akifahamu kila kitu kilichokuwa kimetokea.
Alijaribu kutoka ndani ya chumba hicho, mlango ulikuwa umefungwa kwa nje, moyo wake ukajawa na hofu kwa kuhisi kwamba Belleck alikuwa mmoja wa wafanyakazi wa Keith ambao walijua kwamba hakuwa amekufa baharini hivyo kutaka kumuua tena.
“Mungu! Huyu Keith ananitakia nini lakini?” alijiuliza huku akionekana kuwa na hasira kali.
Akaliangalia begi lake lililokuwa pembeni, zipu ilikuwa wazi kuonyesha kwamba kulikuwa na mtu alilifungua, alipoangalia ndani, akakuta kukiwa kumepekuliwa, hakukuwa na vitambulisho vyake, hakukuwa na hati ya kusafiria.