SEHEMU YA 62
Maria alikichanganya kichwa cha Keith, hakutaka kukubali hata mara moja, kwake, msichana huyo alionekana kuwa na uzuri wa ajabu na alipanga kuwa naye maisha yake yote, hata kama ingemgharimu kiasi cha fedha kikubwa namna gani lakini ilikuwa ni lazima amchukue.
Walipoondoka Malaysia safari ya kwanza ilikuwa ni kwenda nchini Marekani. Hakutaka kumuacha msichana huyo, alizungumza naye sana, alimtongoza, kwa kutumia uwezo wake kifedha, akafanikiwa kumpata msichana huyo ambaye alikubaliana naye kwenda nchini Marekani kula raha kama kawaida yake.
Huko, walifanya kila kitu kilichotakiwa kufanywa kwa wapenzi, akatumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya Maria. Akamtambulisha kwa marafiki zake, kwa kuwa alikuwa kwenye makwaruzano na mkewe kwa muda mrefu, akawaambia kwamba huyo ndiye ambaye angeziba pengo la mkewe kama tu wangetengana.
Maisha yaliendelea kama kawaida, hakutaka kumkumbuka Fareed, aliamini kwamba msichana huyo alifariki dunia nchini Dubai, moyo wake ulijisikia amani tele, kuua, halikuwa jambo la kushangaza kwake, kama walivyokuwa mabilionea wengine, hata kwake kuua ilikuwa ni sawa na kumuua panzi.
Uhusiano wao haukuwa siri hata kidogo, waandishi wa habari wakazipata taarifa hizo, wakaanza kuwapiga picha na kuziweka kwenye mitandao huku wengine wakizitumia picha hizo kuziweka katika magazeti yao.
Kila mmoja alishtuka, hakukuwa na aliyeamini kama mzee huyo angemchukua msichana kama Maria. Si kwamba hakuwa mzuri bali alikuwa msichana wa Kiafrika, na mabilionea wengi nchini Marekani walipenda kuwa na Wazungu wenzao.
Safari hazikukoma, mara kwa mara walikuwa wakisafiri huku na kule wakila bata, hakutaka kuona akitulia, kwa sababu alimpenda Maria kwa mapenzi ya dhati aliamini kwamba kama angekwenda naye sehemu mbalimbali kula raha basi ingemfanya kufanikiwa kuliteka penzi la msichana huyo moja kwa moja.
Kwa kuwa alijua kwamba alikuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na bilionea mkubwa duniani, Maria hakutaka kuona mwanaume huyo akiondoka mikononi mwake, alijitahidi kumfanyai utundu mkubwa kitandani kiasi kwamba mzee wa watu alichanganyikiwa kabisa.