Michirizi ya Damu

Michirizi ya Damu

SEHEMU YA 152

Wakamchukua na kumpakiza ndani ya mtumbwi na kuelekea naye kwenye meli ile. Alikuwa akiugulia kwa maumivu makali, wakati mwingine aliwaambia watu hao kwamba alikuwa akifa na kitu kilichomuuma zaidi ni kwamba alikuwa akifa hata kabla hajamuua padri Luke ambaye alimbaka badala ya kumuongoza sala ya toba alipokwenda kuungama kwenye kanisa lake.

Hiyo ilikuwa meli kubwa ya wavuvi waliokuwa wakivua samaki katika eneo la kimataifa, walitokea nchini Marekani na miaka mingi kazi yao ilikuwa hiyo, walishinda kwenye meli na ni mara chache sana walikuwa wakitoka na kwenda kuzurura sehemu mbalimbali.

Hawakujua kitu chochote kuhusu Fareed, wakati dunia ikimtafuta kwa mauaji aliyokuwa ameyafanya, wao hawakuwa na habari hata kidogo. Walimkaribisha katika meli yao, wakampa dawa ya tumbo na kuondoka naye.

Kidogo dawa hiyo ikampunguzia maumivu makali. Wakati meli ikiendelea kuvua kama kawaida, alichokuwa akikifikiria ni kutoroka mara baada ya meli kufika nchi kavu.

Fareed akapata nafuu, akawa muongeaji mkubwa, alitaka kuwazoea watu hao ili wasiwe na maswali mengi.

Alipoulizwa kuhusu sababu iliyomfanya kuwa mahali pale, hakutaka kuwaambia ukweli, aliwadanganya kwa kuwaambia kwamba alikuwa akisafiri kwa meli na wezake, ghafla bahari ikachafuka, meli ikapasuka na maji kuingia, kilichoendelea ni meli hiyo kuzama.

Ilikuwa rahisi kumwamini kwa kila kitu alichokuwa akikiongea, alizungumza huku akionekana kumaanisha kile alichokuwa akikisema mbele yao. Sura yake ilivyokuwa, ilifanana na maneno aliyokuwa akizungumza hivyo kumwamini kwa asilimia mia moja.

Zoezi hilo la uvuaji liliendelea kwa siku kadhaa na ndipo wakarudi nchi kavu tayari kwa kuuza samaki wao waliokuwa wamewavua katika kipindi walichokuwemo huko.

Japokuwa walimzoea Fareed na waliahidi kumsaidia lakini baada ya meli kufika nchi kavu walishangaa kuona mtu huyo akiwa amewapotea katika mazingira ya kutatanisha.

Hawakujua alikuwa wapi, walijaribu kumtafuta kila kona, mwanaume huyo hakuwepo kitu kilichowapa maswali mengi yasiyo na majibu.
 
SEHEMU YA 153

Fareed alikuwa njiani akielekea kulipokuwa na mgahawa wa McDonald, alikuwa akitaka kula, kwa kiasi cha pesa alichokuwa nacho mfukoni mwake aliamini kingemsaidia.

Wakati akiwa kwenye mgahawa huo, akiwa ameagiza chakula ndipo macho yake yakatua katika televisheni ambapo kulikuwa na habari iliyokuwa ikizungumzia kuhusu kukamatwa kwa Bilionea Williams.

Alishangaa, alipoangalia sababu ya kukamatwa huko akaona ni kwamba alikuwa akihusika kushirikiana na magaidi katika kulipua kituo cha treni huko Pennsylvannia na pia alihusika kumtuma mtu kwenda kuwaua mabilionea wawili kwa kumtumia mtu aliyeonekana kwenye picha.

Fareed alipoangalia picha ile, alikuwa yeye, alionekana vilivyo alivyokuwa ameingia kwenye piramidi kwenda kumuua Bilionea Keith, alipoingia hotelini kumuua bilionea Bellck mpaka pale alipokuwa akikimbia katika kituo hicho cha treni.

Sura yake ikaanza kuwa maarufu, hapo mgahawani hakutaka kukaa sana, akasimama, akalipia na kisha kuondoka.

Alijua fika kwamba ilikuwa ni lazima kukamatwa, hakutaka kuona akikamatwa pasipo kumuuua Padri Luke aliyekuwa amembaka, alitaka kumaliza kila kitu ili pale atakapokuja kukamatwa na kushtakiwa kifo basi afe akiwa na amani moyoni mwake.

“Ni lazima niende kanisani!” alisema Fareed.
Hakutaka kubaki mahali hapo, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kwenda katika kanisa hilo lililokuwa umbali wa kilometa mbili kutoka hapo alipokuwa.

Akakodi teksi ambayo ikaanza kumpeleka huko.
Macho yake yalikuwa chini, aliogopa kuonekana na kugundulika, na hata alipokuwa ameongea na dereva wa teksi hiyo alikiinamisha kichwa chake chini.

Safari iliendelea mpaka alipofika kwenye kanisa hilo, akaingia. Kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma ndivyo ilivyokuwa kipindi hicho, kulikuwa na watu wachache sana kanisani humo, akaelekea mpaka katika sehemu ya kuungamia dhambi na kukaa tayari kwa kuzungumza na padri huyo ambaye ndani ya dakika chache, akaingia humo.

“Nimekuja kuungama dhambi zangu,” alisema Fareed huku akiangalia chini.
Padri Luke hakumgundua kwani alikuwa amebadilika, hakuwa kama vile alivyokuwa kipindi cha nyuma.

Alizungumza naye kwa kirefu na kumwambia kwamba angerudi baadaye kwa ajili ya kuzungumza naye.
 
SEHEMU YA 154

Akaondoka kanisani hapo, kitu cha kwanza alichokitafuta kilikuwa kisu, akafanikiwa kukinunua katika supamaketi ambayo haikuwa mbali kutoka hapo alipokuwa.

Mwanaume aliyemuuzia ndani ya duka hilo alimwangalia kwa makini mno, sura yake haikuwa ngeni, ni kama aliwahi kumuona sehemu fulani.

Fareed akaogopa, akahisi kwamba mwanaume huyo aliliona tangazo la kutafutwa kwake hivyo alichokifanya ni kuondoka harakaharaka huku akiwa na kisu alichokinunua.

Alipofika kanisani, hakuingia katika mlango wa mbele, akapitia katika mlango wa nyuma, ule aliotolewa na padri yule, akafungua nati za kitas, akakitoa na kuingia ndani.

Kulikuwa na giza, akapiga hatua mpaka alipoufikia mlango mwingine ambao ulikuwa ni wa nyuma kuingia katika ofisi ya padri huyo. Akaingia na kutulia katika kochi moja. Padri hakuwepo, alikuwa katika chumba cha kuungamia dhambi akimsikiliza mtu mwingine.

Alikaa hapo kwa dakika ishirini, akamsikia padri huyo akija kule alipokuwa, haraka sana akaelekea nyuma ya mlango na kusimama, padri huyo akaingia.

Hata kabla hajafanya kitu, akamkaba kwa nyuma, padri Luke akashindwa hata kupiga kelele, akajikuta akianza kulegea. Hapohapo Fareed akamuacha.

“Do you remember this face?” (unaikumbuka sura hii?) aliuliza Fareed huku akimwangalia padri Luke.
“Please! Don’t kill me,” (usiniue tafadhali) alisema padri huku akipiga magoti.

“Do you?” (unaikumbuka?)
“I saw you a while ago,” (nilikuona muda mfupi uliopita)
“Okey! I came to kill you,” (Sawa! Nimekuja kukuua) alisema Fareed huku akimwangalia padri huyo.

“I’ve done nothing! Please! Have mercy, I have done nothing,” (sijafanya lolote! Tafadhali nihurumie! Sifanya lolote) alisema Padri huyo huku akiwa amepiga magoti.

Fareed akaanza kumkumbusha padri huyo kila kitu kilichokuwa kimetokea kuhusu wao. Alianzia mbali, jinsi alivyokuwa ameathirika kwa vitendo vya kishoga mpaka kufikia hatua ya kwenda kanisani hapo kwa ajili ya kuungama dhambi zake.

Padri Luke akakumbuka, akamwangalia vizuri Fareed, akamkumbuka. Akazidi kulia na kuomba msamaha zaidi kwamba kile alichokifanya ni shetani tu ndiye aliyempitia.
 
SEHEMU YA 155

Fareed hakutaka kumuelewa, hapohapo akamchukua na kuelekea naye ndani ya chumba kile cha kuungamia dhambi, kama alimfanyia vitendo hivyo ndani ya chumba kile basi alitaka kumuua ndani ya chumba hicho hicho.

Hakutaka kupoteza muda, hapohapo akamchoma visu vitatu tumboni na kifuani mwake, padri akaugulia kwa maumivu makali, akaanguka chini, akatoka damu nyingi na hapohapo Fareed kumburuza na kuacha michirizi ya damu pale sakafuni.

Hakuishia hapo, alitaka kuijulisha dunia kwamba yeye ndiye aliyefanya mauaji ya watu hao watatu hivyo kuchukua karatasi na kuuacha ujumbe uliosomeka C'est fait yakiwa na maana ya kukamilika kwa jambo au ‘done’ kwa Lugha ya Kiingereza. Hakutaka kupoteza muda, alipoona amekamilisha kila kitu, akaondoka mahali hapo haraka sana.

**** FBI walishindwa kujua ni kwa namna gani wangeweza kumpata muuaji wa mauaji hayo, walisambaza picha za Fareed kila kona lakini hawakuwa wamefanikiwa. Walijua kwamba kijana huyo alikuwa nchini Marekani lakini kitu cha ajabu kabisa hawakuweza kumuona.

Walichokifanya ni kuweka dau kwamba kwa mtu yeyote ambaye angefanikisha kupatikana kwake basi angezawadia zawadi nono ya dola elfu hamsini, zaidi ya milioni mia moja lakini napo zoezi hilo likaonekana kuwa gumu.

Watu ambao walionekana kufanana nja Fareed walikamatwa na kupelekwa katika vituo vya polisi, kila mmoja alikuwa na uchungu wa kupata pesa hizo ambazo zilikuwa nyingi, pesa ambazo zingeweza kuwatoa katika hali waliyokuwa nayo na kuwapeleka sehemu nyingine kimaisha.

Siku zikakatika, hakukuwa na mtu aliyejua mahali mtu huyo alipokuwa. Walitoa taarifa katika hoteli zote hapo Marekani kuhakikisha kwamba mtu huyo anakamatwa mara baada ya kuingia hotelini lakini zoezi hilo lote lilionekana kuwa gumu kwani bado mtu huyo hakuwa amepatikana mpaka muda huo.

“Where the hell is he?” (yupo wapi?) aliuliza jamaa mmoja, kama walivyokuwa wenzake, hata yeye mwenyewe alikuwa amechanganyikiwa.
 
Back
Top Bottom