Michirizi ya Damu

Michirizi ya Damu

SEHEMU YA 120

Kiasi alichokitaja kilikuwa kikubwa, mkuu wa kikosi kile alijua kwamba walikuwa wakipoteza muda na mule ndani hakukuwa na mtu yeyote yule. Hakutaka kuona pesa hizo zikimpita, uchumi ulikuwa mbaya na hivyo kukubaliana na Mzee Ahmed kwamba ampe kiasi hicho na kumruhusu kuondoka.

Akawaambia vijana wake waachane na upekuzi na hivyo waondoke ndani ya meli hiyo. Vijana wale walitii na kuondoka pasipo kujua kwamba mkuu wao alikuwa amepewa mkwanja chinichini.

Hiyo ndiyo ikawa salama kwa Fareed, kule ndani ya boksi alipokuwa, baada ya kusikia watu wakiondoka akashusha pumzi nzito na kumshukuru Mungu.

Baada ya muda, meli ikawashwa na kuanza kuondoka mahali hapo.
“Asante Mungu! Ndiyo maana niliamua kuyabadilisha maisha yangu kwa ajili yako ila yule mpumbavu aliamua kuyaharibu tena,” alisema Fareed huku akionekana kuwa na furaha tele.

Mzee Ahmed alifurahi, alipoianza tena safari hakuamini kama alikuwa amefanikiwa kuondoka bandarini hapo.

Hakujua kama mtu aliyekuwa amembeba alikuwa akitafutwa kila kona hapo Misri tena huku mtu ambaye angefanikisha kukamatwa kwake angelipwa kiasi kikubwa cha pesa.

Safari ya siku nne ikaendelea majini, ilikuwa ni lazima wapite Cyprus hata kabla ya kuelekea Uturuki. Ilikuwa ni safari ndefu ya majini lakini walitakiwa kuvumilia.

Fareed aliyekuwa ndani ya chumba kile, akapewa uhuru wa kuzungukazunguka ndani ya hiyo meli kwani kusingekuwa na mtu yeyote ambaye angewababaisha kwani tayari waliondoka barani Afrika.

Baada ya siku nne kukatika, wakafika Cyprus na meli kutia nanga katika bandari kubwa ya Limmasol ambapo wangekaa hapo kwa siku mbili na kuondoka kwenda kutia nanga katika Bandari ya Latchi kabla ya kuendelea na safari yao ya kuelekea nchini Uturuki.


“Utahitaji kutembeatembea katika Mji wa Limmasol?” aliuliza Ahmed.
“Hapana! Nitakaa humuhumu. Nitatoka nikifika nchini Uturuki!” alisema Fareed.
“Hakuna tatizo! Ngoja tukale bata kwanza na warembo wa Kicyprus,” alisema Mzee Ahmed huku akionekana kuwa na furaha mno.
 
SEHEMU YA 121

Walitumia siku sita nchini Cyprus mpaka kuiacha nchi hiyo na kuelekea nchini Uturuki.

Hakukuwa na umbali mkubwa, ni ndani ya siku saba tu meli ikaanza kuingia katika Bandari ya Akdeniz iliyokuwa katika Jiji la Antalya.

“Tumefika Uturuki! Utakwenda wapi sasa?” aliuliza Mzee Ahmed huku akimwangalia mwanaume huyo.
“Popote pale.”
“Kwa hiyo utaishi hapa?”
“Kwa muda!”
“Halafu?”
“Nataka kuondoka kuelekea Marekani!”
“Unataka kwenda Marekani?”
“Ndiyo!”
“Utafikaje?”
“Kivyovyote vile,” alisema Fareed.
“Hautakiwi kuhisi.

Ngoja nitafute mtu wa kukusaidia,” alisema Mzee Ahmed na kuchukua simu yake na kuwasiliana na mtu mmoja upande wa pili.

Fareed akashukuru Mungu, hakuamini kama angepata urahisi wa kuingia nchini Marekani kama ule aliokuwa amepewa. Alimshukuru Mzee Ahmed kwani alionekana kuwa mwanaume mwema kabisa.

Mara baada ya mzee huyo kumaliza kuzungumza na mtu huyo, akamwambia Fareed asubiri ambapo baada ya saa moja, mwanaume mmoja akafika hapo bandarini ambapo kinyemela akamchukua Fareed na kuondoka naye.

Mzee huyo akajitambulisha kwa jina la Al Fakh. Alikuwa mzee mwenye ndevu nyingi mno, aliongea kitaratibu sana, hakuwa na mapepe, alikuwa mwanaume mstaarabu sana kiasi kwamba wakati mwingine Fareed alihisi kwamba mwanaume huyo alikuwa mtumishi wa Mungu hapo Uturuki.

Walizungumza mambo mengi mno, Fareed alimdanganya mzee huyo kwamba alitaka kwenda nchini Marekani kwa kuwa alikuwa mzamiaji, alitaka kwenda kutafuta maisha nchini humo.

Mzee Al Fakh alifurahi sana, akamwambia kwamba angemsaidia kwa hali na mali pasipo gharama zozote zile.
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Nashukuru sana!”

Wakachukua dakika chache wakafika nyumbani kwa mzee huyo. Ilikuwa nyumba kubwa, yenye walinzi wengi na kila kitu kwa ndani. Wakaingia ndani, akakutana na familia ya mzee huyo ambaye alimkaribishwa kwa furaha tele.

Akapelekwa katika chumba ambacho alitakiwa kukaa kwa siku zote ambazo angesubiri safari ya kwenda nchini Marekani.

Moyo wa Fareed ulikuwa na furaha tele, hakuamini kama kweli alikutana na familia ya watu waliokuwa na upendo mkubwa kama watu hao.
“Jisikie huru!” alisema mzee huyo.....
 
Back
Top Bottom