SEHEMU YA 119
Fareed alikuwa ndani ya meli, moyo wake ulikuwa na shauku kubwa ya kufika nchini Uturuki. Alikuwa na hofu moyoni mwake, alihisi kwamba huo ingewezekana kuwa mwisho wa maisha yake kwani kila alipoangalia, hakuamini kama angefika salama nchini humo.
Alibaki ndani ya chumba hicho huku akiwa na hofu kubwa. Meli ilipofika katika Bandari ya Said, akashtuka kuona meli ikizimwa.
Mara ya kwanza alihisi kwamba ilikuwa tayari imefika nchini Uturuki lakini alipoangalia muda waliotumia, akahisi kwamba kulikuwa na kitu, hasa msako wa kumtafuta yeye.
Hakutaka kukamatwa, hakutaka kuona kwamba huo ndiyo uwe mwisho wake, ilikuwa ni lazima ajifiche ili asiweze kuonekana na watu hao hivyo alichokifanya ni kuangalia ndani ya chumba hicho kuona kama angeweza kuona kitu chochote ambacho kingemfanya kujificha.
Humo ndani kulikuwa na maboksi mengi na kitu kilichomfurahisha zaidi ni kwamba kulikuwa na maboksi makubwa ambayo yengemfanya kuingia ndani na kujificha.
Hakutaka kuchelewa, hapohapo akalifuata boksi moja kubwa, akalisogeza pembeni kabisa kisha kulifungua, mule ndani hakukutana na vitu vingi vizito, aliona kukiwa na vitambaa vingi vya kushonea kanzu hivyo alichokifanya ni kuvitoa, akaingia, akavirudisha juu yake na kulifunga boksi hilo kwa ustadi mkubwa.
Akahisi kwamba hapo angefanikiwa kujificha na kutokugundulika. Baada ya dakika kadhaa, akasikia watu wakiongea nje ya chumba hicho na baada ya sekunde chache mlango kufunguliwa na kuingia ndani.
Wanajeshi wale walidhamiria kuyafungua maboksi yote, waliamini kwamba inawezekana humo ndani kulikuwa na mtu waliyekuwa wakimtafuta. Mkuu wa kikosi akawaagiza watu wake wayafungue maboksi yale na kuangalia ndani.
Mzee Ahmed alibaki akitetemeka, kitendo cha kumkosa Fareed ndani ya chumba kile ilionyesha kwamba mwanaume huyo alikuwa amejificha ndani ya boksi mojawapo hivyo kuona kwamba kama asingemtumia shetani mkubwa duniani, pesa basi mtu huyo angeonekana na kugundulika kwamba alikuwa akimsafirisha mzamiaji.
“Hivi kweli dola mia mbili haziwezi kuniruhusu kuondoka niwahi?” aliuliza Mzee Ahmed.
“Mia mbili?”
“Ndiyo!”
“Ongeza kidogo!”
“Basi mia tano! Ilimradi niwahi tu!”