Sugu awashambulia Mawaziri
*Awaita wapumbavu
MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi
(Chadema), maarufu kwa jina la Sugu, juzi
alilishambulia Baraza la Mawaziri akisema kuwa
limejaa wapumbavu. Tukio hilo lilitokea juzi
jioni wakati mbunge huyo akichangia hotuba ya
bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa
fedha 2013/14.
Sugu, alisema Baraza lote la Mawaziri
linaundwa na wapumbavu, kwa kuwa linashiriki
kubomoa nchi linayoiongoza.
Kabla sijaanza kuchangia, nataka ninukuu
maandiko katika biblia yanayosema kwamba:
Mwanamke mpumbavu huibomoa nyumba
yake kwa mikono yake mwenyewe vilevile
Serikali pumbavu inabomoa nchi yake yenyewe,
yaani namaanisha Baraza la Mawaziri
wapumbavu.
Mambo mengi nchi hii hayaendi kutokana na
Serikali pumbavu, juzi hapa Mbatia (James
Mbatia, Mbunge wa Kuteuliwa kupitia NCCR-
Mageuzi) alileta hoja bungeni kuhusu mitaala ya
elimu nchini, mkatumia wingi wenu
kuinyanyapaa sasa matokeo ya form four
(kidato cha nne), yamewaumbua.
Hatuwezi tukawa na Waziri wa Elimu boya,
mwenye elimu ya kuungaunga halafu tukafanya
vizuri katika elimu.
Sugu alikwenda mbali akisema jambo hilo
lilikuwa ni kazi ya Idara ya Usalama wa Taifa,
kufanya uchunguzi wa mawaziri wanaotarajiwa
kuteliuliwa na Rais ili kubaini uwezo wao.
Aliwashutumu Usalama wa Taifa kwa kuacha
kufanya mambo hayo ya msingi na kubaki na
kazi ya kuifuatilia Chadema na kungoa watu
kucha.
Mimi binafsi sijisikii kuwa sehemu ya Bunge
hili, kukaa na wabunge kama wakina Mwigulu
(Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Iramba
Magharibi kupitia CCM), huyu naye ni
mpumbavu, alisema Mbilinyi.
Kabla ya kuendelea na mjadala, Spika wa
Bunge, Anne Makinda, alimkatisha mbunge
huyo na kumtaka kutotumia neno pumbafu
wakati akiendelea kuchangia hoja yake.
Hata hivyo, Sugu aligoma kutotumia neno hilo
kwa kusema kuwa: Mheshimiwa Spika, naomba
taifa lielewe upumbafu sio tusi ndio maana lipo
hata kwenye biblia, upumabavu ni stupidity,
lucky of knowledge of understanding ambayo
mawaziri wote wanayo, alisema Sugu.
Mbali na Sugu Mbunge wa Kigoma Kusini, David
Kafulila (NCCR-Mageuzi), naye akichangia
mjadala huo, alisema Tanzania ni nchi tajiri ila
wanaosababisha umasikini wa Watanzania ni
viongozi.
Kila kitu cha utajiri tunacho, nchi yetu ni nchi
ya pili kwa vivutio vya utalii duniani, lakini
mapato yetu ni chini ya asilimia 10, kwa nini
tunashindwa kuwatajirisha Watanzania, alihoji
Kafulila.
Aliwataka pia wabunge kutokubali mkutano wa
Bunge kumalizika bila majibu ya Serikali kuhusu
taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG).
Kwa sababu mnaona CAG anaikosoa Serikali
mnaleta sheria za kuifinya ripoti yake, hii
mnafanya kwa faida ya nani? Hii nchi ni yetu
sote, hamuwezi mkasema nchi ni ya amani
wakati mnakula wenyewe, alisema.
Kafulila pia alizungumzia misafara ya viongozi
isiyo na tija ambayo inasababisha fedha nyingi
za Serikali kupotea.
Kwa upande wake, Mbunge wa Nzega, Dk.
Khamis Kigwangala (CCM) akichangia hotuba
hiyo ya bajeti yeye aliwashambulia Chadema
akisema kuwa vitendo vyao ni vya kipuuzi.
Alisema Chadema wanachezea mchakato wa
uundwaji wa Katiba mpya, kitendo alichodai
kuwa ni cha kipuuzi.
Aliishangaa Serikali kuona inawaacha watu
wachache kutaka kuharibu mchakato huo
ambao ni muhimu kwa mustakabali wa taifa.
Mbunge wa Mkanyageni, Habibu Mnyaa (CUF)
aliitaka Serikali kumaliza mgogoro wa Mtwara
ndani ya miezi minne kwa kuwa mgogoro huo
bado upo licha ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
kusema umekwisha.
Aliyataja madai ya watu hao kuwa ni uzalishaji
wa umeme wa Megawati 300 katika Mkoa wa
Mtwara, kuunganisha mkoa huo katika gridi ya
taifa na kufungua fursa za viwanda na bandari.
Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo
(UDP), alisema Serikali lazima ichukue
tahadhari kulinda amani na umoja wa kitaifa
nchini.
Alisema migogoro inayoendelea sasa kuhusiana
na udini, ardhi na maliasili nyingine kama vile
gesi idhibitiwe ili kuiepusha nchi katika
machafuko.