Watendaji mamlaka ya maji Arusha (AUWSA) ni kero

MMASSY

JF-Expert Member
Jan 13, 2011
290
193
Ninaitwa JEROME ERNEST MMASSY ni mkazi wa kata ya Olasiti jijini Arusha.

Wakati Mh.Rais Magufuli akizindua mradi mkubwa wa maji jijini Arusha nililazimika kuacha kazi zangu zote za siku ile na kuungana naye katika hafla ile nikijua tumepata ukombozi ndani ya jiji la Arusha.

Pamoja na kuwa sikuwahi kupata ajira yoyote rasmi tangia nihitimu chuo kikuu mwaka 2011, nikajikusanya kusanya na kuhangaika nikapata sehemu nikaweka kibanda changu.

Wakati Rais wetu Samia Suluhu alipokuja Arusha juzi juzi pia nikajitokeza kusikiliza na kuona akizindua kisima mfano kuanza rasmi matumizi ya maji yaliyoasisiwa na JPM,nilifurahi kuona namna serikali inavyopambana kuhakikisha Arusha kama ilivyo maeneo mengi nchini inaondokana na uhaba wa maji.

Lakini nikadondokwa na machozi kwa sababu,Tarehe 08/03/2021 nilifika katika ofisi za mamlaka ya maji jijini Arusha AUWSA kuchukua fomu ya kuomba kuunganishiwa maji na nikahudumiwa ipasavyo ambapo siku hiyohiyo nilijaza fomu hiyo na kuirudisha ofisini.

Nikapewa utaratibu wa kumfuata Surveyor kesho yake yaani tarehe 09/03/2021nikafanikiwa kwenda na Surveyor eneo langu akafanya survey na gharama zote za usafiri niligharamia.Kituko nilichokiona hapa ni kwamba surveyor wa mamlaka hii ya maji hapandi gari ya abiria,hapandi pikipiki wala babaji,anataka ukodi taxi au umchukue na gari private.

Ukishinda basi atakutajia kiasi cha fedha unachotakiwa kumpatia ndiyo aende nawewe kufanya survey.La sivyo hutakaa umwone surveyor kwako.Baada ya zoezi la kufanyiwa survey, akanijulisha kuwa,ningepata ujumbe wa kulipia vifaa ndani ya wiki mbili ndio niunganshiwe maji lakini ilichukua muda mrefu bila kupata ujumbe kwenye simu yangu.

Nikawasiliana naye akaniambia niendelee kusubiri.Baada ya kitambo tena,nikalazimika kufika tena ofisini kuulizia,mwezi wa sita mwaka huu 2021 nikajulishwa kuwa, fomu yangu inaonekana kwenye mfumo lakini haina taarifa za survey.

Nikaelekezwa kumwona tena Surveyor lakini hakuwa ofisini, nilipompigia akaniuliza umbali uliopo kutoka kwenye chemba za kuunganishia maji hadi kwangu nikamjulisha ni mita 55. Akaniambia atanijazia kwenye fomu nitumiwe namba za malipo(control number).

Baada ya muda tena nikalazimika kuwa nampigia kumkumbusha lakini sikufanikiwa kupata huduma hiyo.Tarehe 26/08/2021 nikalazimika kufika ofisini kwao tena kuulizia nikaambiwa bado fomu yangu haina taarifa za survey a nikaelezwa kumwona Surveyor naye alinielekeza kuchukua tena fomu mpya kujaza ili nianze mchakato upya wa maombi jambo ambalo sikukubaliana nalo.

Baada ya kuvutana sana,ikanilazimu kumtafuta meneja wa mamlaka ya AUWSA sikufanikiwa sababu kila nikifika kuomba kibali cha kuonana naye ninanyimwa.

Nimepiga sana simu ya huduma kwa wateja lakini sijafanikiwa kupata ufumbuzi wa suala langu.Ilipofika tarehe 07/10/2021 nikalazimika kuwaandikia email na nikapeleka nakala kwa katibu mkuu wizara ya maji juu ya kuzungushwa huko.

Ilipofika tarehe 11/10/2021 nikapigiwa simu na Surveyor akiniomba msamaha kuwa wakati wanahamisha mafile ofisini eti fomu yangu ilipotea ndio maana sijapata control number kwa miezi yote hiyo na akawa ananiomba nimpelekee nakala ya kitambulisho changu na passport size mbili. Lakini kesho yake yaani tarehe 12/10/2021 asubuhi sana kabla sijapeleka nikapata ujumbe wenye control number na kutakiwa kulipia, ilipofika tarehe 15/10/2021 nikawa nimelipia na kufika ofisi za mamlaka kuchukua vifaa kama nilivyoelekezwa na mtoa huduma katika simu yao namba 0800110069.

Bado sikufanikiwa kupata huduma kwa kisingizio kuwa Rais alikuwa Arusha hivyo wafanyakazi walikuwa kwenye ziara ya Rais.

Baadaye nikarudi nikapewa popythene,elbows,connectors nikaambiwa vifaa vingine nifuate baada ya wiki.Tarehe 21/10/2021 nikarudi tena nikapewa gate valve,connector poly,bib cock na kuambiwa nirudie tena vingine wiki inayofuata.Tarehe 28/10/2021 nikarudi huko nikapewa nipple hex na elbows halafu nikaambiwa nisiende tena bali nitapigiwa simu vifaa vingine vikija.

Ilipofika tarehe 01/11/2021 nikapiga simu huko nikajibiwa kuwa niendelee kusubiria vifaa havijaja.Ukienda ofisini unaambiwa endelea kusubiria.Tarehe hiyohiboy nikaandika tena email kukumbushia suala langu lakini hadi leo ni kimya kikuu.

Nikiwa bado katika tafakari,najiuliza maswali yafuatayo;
  • Wale wananchi ambao hawajui haki zao,hawajui kusoma wala kuandika huwa wanazungushwa kiasi gani kama mimi angalau mwenye vimadarasa kadhaa nafanyiwa hivi?
  • Kama fomu zinapatikana bure kwenye ofisi za hii mamlaka lakini gharama za kumsafirisha surveyor ni za mteja tena kwa usafiri anaotaka yeye,Je?Hizo bajaji,pikpiki na magari yaliyozagaa huku mtaani ya mamlaka hii yanabeba watu gani na kwa kazi gani?Ni kweli serikali imeidhinisha upuuzi huu?Mbona Meneja namaafisa wengine wanatembelea VX new model kabisa na maafisa wengine ina maana sio kodi zetu?
  • Kama mamlaka hii inaweza kuwa na kiburi cha kupuuzia malalamiko yalioandikwa kwenye email (maandishi) tena nakala ikaenda kwa katibu mkuu wa wizara.Je inakuwaje kwa wale wanaoenda kulalamika kwa mdomo pale ofisini?Inakuwaje wale ambao wamekuwa wakipiga simu?Ni nani zaidi wanaweza kumheshimu kama kiongozi wao?Ni waziri?ni Rais ama nani?
  • Mkataba wa huduma kwa wateja wa mamlaka hii unaonyesha mteja anatakiwa aunganishiwe maji chini ya siku 14 tangia alipie maji.Mimi sasa inakimbilia mwezi tena ni baada ya watu kuona nimewashtaki kwa katibu mkuu.Mamlaka hii ikipelekwa mahakamani kwa kusababisha usumbufu na hasara kwa mteja watakuwa na la kujitetea?Vipi kwa wale ambao wanakaa miezi mitatu hawajaunganshiwa maji huku wakiendelea kununua maji ya visima bei ghali?
  • Juhudi anazofanya waziri Jumaa Aweso kila kukicha kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa wananchi mamlaka hii inamfanyia hujuma?Waziri anasema anatamani kati ya wizara 3 zinazotajwa kwa ubora wa huduma basi wizara ya maji iwepo.Ukija Arusha utagundua kuwa wizara yako ni ya kwanza kwa ubabaishaji kupitia watendaji wako ambao wanahujumu juhudi za serikali.
  • Mamlaka hii imekuwa na tabia za ajabu,wanatoa meter kwa mafundi wa mtaani(vishoka),halafu wale mafundi wanakupigia mteja simu kutaka kuja kukufungia maji na uwalipe fedha angalau 20,000/=Na utamaduni huu umezoeleka kila kona.Huo ndio mwongozo wa wizara?Ni kweli kuwa serikali haijui uzembe huu?
  • Inawezekanaje serikali kufanya mradi wa bilioni 520 ikakosa mafundi wa kufunga mita na kuunganishia wateja maji?Yaani ofisi nzima kuanzia getini hadi kwenye vifaa imekaa kiupigaji tu.
  • Ni kweli kwamba ofisi ya katibu mkuu wizara ya maji hawajaona email za wananchi,ama nao wanaamua kulinda uovu ulioko katika mamlaka hii ya AUWSA?
  • Kama mimi kijana ninazungushwa hivi,inakuwaje kwa wazee ambao huwa wanakuja kwenye hizi ofisi alfajiri na wanashinda hapo bila kusaidiwa shida zao?Tena saa nyingine wanakuambia njoo kesho saa nane,ukifika muda huo wanakuambia subirini angalau mfike 100 bado ni wachache,ukianza kuwauliza lengo lao ni nini wanakuambia halafu wewe una kiherehere sana.Namatani Magufuli afufuke lakini ndio hivyo tena.
  • Ni kweli kuwa hii mamlaka na wizara ya maji wana agenda tofauti katika kuwatumikia wananchi?Maji yanayotegemewa kupatikana hapa Arusha ni lita milioni mia mbili kwa siku kwa mujibu wa Rais Samia katika ziara yake Arusha, hayo maji yakishafika Arusha ni watu gani watayatumia kama kuna hizi bureaucracy kwenye kuunganishiwa?Hivi kweli mamlaka inakosa Stand pipe 3/4 inayouzwa 5000?
Binafsi naishangaa serikali huwa inakuwa wapi wakati matatizo yanafikia kiwango hiki,naishangaa serikali inakuwaje watu wanasumbuka namna hii na serikali ipo.Kama serikali ilikuwa haijui huo ndio baadhi ya uozo wa ofisi za mamlaka za maji jijini hapa.Inawezekana nikaonekana sina nia nzuri lakini serikali inaweza kufanya uchunguzi nami nitawasaidia kwa karibu sana.

Naiomba serikali iangalie malalamiko haya kwa jicho la huruma na kuona namna ambavyo wananchi anateseka na kuwasaidia.Hatufurahii sana kuona watu wanatumbuliwa lakini inatuuma zaidi pale ambapo watendaji wanabweteka na kujawa na kiburi kiasi cha kuzorotoshe utoaji wa huduma katika ofisi za umma.Naambatanisha maelezo haya na fomu yangu ambayo hadi leo ninayo na sijapewa vifaa vyote hadi sasa.Lakini pia naambatanisha namba zangu za simu kwa taarifa zaidi.

Juhudi za kupata mawasiliano ya simu ya Mwenyekiti wa bodi ya AUWSA,Katibu Mkuu wa wizara na hata waziri zimegonga mwamba sababu nikaamua kuleta hapa pengine wataliona na kulifanyia kazi zaidi.

Jerome Mmassy
Arusha
0623141643

Arusha

250803189_613808719748958_2984440796297268134_n.jpg
 
Back
Top Bottom