MBUNGE wa Arusha Mjini Kupitia Chadema, Godbless Lema, amerushiwa mawe na kundi la watu katika mji mdogo wa Sirari alipotaka kushawishi vijana katika mji huo kujiunga na maandamano ya chama hicho jana wakati wa kuchukua miili ya watu wanne ambao bado ipo mochari ya hospitali ya wilaya ya Tarime.
Kamanda Mkoa wa Tarime/Rorya, Costantine Massawe, jana alithibitisha tukio hilo la kurushiwa mawe lililofanyika saa 11 jioni wakati Mbunge huyo alipokwenda Sirari akiwa na gari lake na wafuasi wa Chadema waliokuwa na sare za chama hicho waliposhuka kutoka ndani ya gari hilo huku wakisema nguvu ya umma hadi kieleweke, na kuanza kuwakusanya vijana kwa nia ya kuwashawishi wajiunge na maandamano ya chama hicho mjini Tarime na Nyamongo.
Kamanda Massawe alisema Jeshi lake lilipata taarifa kuwapo na mkusanyiko usio halali uliokuwa unafanywa na wafuasi wa chama hicho katika mji huo wa Sirari, ambapo msafara huo wa Lema ulikumbana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kupitia CCM, Amos Sagara.
Sagara ni Diwani wa kata hiyo ya Sirari na mmoja wa watu waliopigwa mawe katika msafara wa Mbunge wa Jimbo hilo, Nyambari Nyangwine, Nyamongo, ambapo vijana wa maeneo hayo ya Sirari walikasirishwa na kitendo cha Diwani wao na Mwenyekiti wa Halmashauri kupigwa Nyamongo na wafuasi wa Chadema, ambapo nao walitaka kulipiza kisasi.
Mbunge Lema na msafara wake walipanda ndani ya gari aina ya Toyota Land Cruiser haraka huku wengine wakining'inia mlango wa nyuma huku mvua ya mawe ikiwafuata nao wakipiga mayowe hadi kituo kidogo cha Polisi katika eneo la Forodha na msafara huo kuokolewa na polisi wa kituo hicho waliojihami kwa silaha kuzuia vijana hao waliokuwa na hasira na kisha kusindikizwa na polisi kuondoka katika maeneo ya mji huo.
Hali ya kisiasa wilayani hapa si shwari kutokana na vurugu za watu watano waliouawa walipovamia mgodi wa North Mara Barrick ambapo Chadema imekuwa ikiegemea kwa familia za marehemu na kuzishawishi kususa miili hiyo.
Mkuu wa Wilaya Tarime, John Henjewele, ameonya kwa wanachama wa vyama vya siasa wanaotaka kuleta vurugu kwa kutumia maafa hayo kisiasa, Serikali itawachukulia hatua kali. Hilo ni tukio la pili la kupigwa mawe wabunge ambapo Mei 18, Nyangwine na msafara wake walishambuliwa Nyamongo walipokwenda kuwapa pole wafiwa.
Source: Habari Leo
my take:
Hili gazeti naona limegeuka kuwa la udaku, muda wanaousema wa saa 11 jioni Mh. Lema alikuwa Arusha na aliwahutubia wananchi maeneo ya hospitali ya St. Thomas.