Mgao wa umeme: Hospitali ya KCMC yasitisha baadhi ya huduma

Kinuju

JF-Expert Member
Mar 20, 2021
2,390
5,310
Mgao wa maji na umeme unaoendelea hapa nchini umeitikisa hospitali ya KCMC inayotegemewa na zaidi ya watu millioni 15 nchini na imelazimika kusitisha baadhi ya huduma kama vile upasuaji, uzalishaji wa mitungi ya Oxygen n.k.

=======

Moshi. Makali ya uhaba wa maji na umeme usipime. Hivi ndivyo unavyoweza kuelezea adha wanayopitia wananchi huku Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC ikieleza athari inazopata kutokana na mgawo wa umeme.

Kukosekana kwa umeme kunaifanya KCMC, inayohudumia wananchi zaidi ya milioni 15, kusitisha baadhi ya huduma kwa muda, ikiwamo upasuaji, uzalishaji mitungi ya oksijeni, maji tiba na vipimo vya MRI na Digital Xray.

Wakati hali ikiwa hivyo KCMC, mikoa mbalimbali nchini nako kuna kilio kama hicho, huku wananchi wakidai maji na umeme ni kama watoto pacha.

Kukosekana kwa umeme kumesababisha baadhi ya maeneo yanayotumia pampu kukosa huduma ya maji.

Katika mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mbeya, Morogoro na Arusha, shughuli nyingi za kiuchumi zinazotumia umeme zimetatizika, hasa saluni, wachomea vyuma (welding), wauza samaki, mashine za kusaga, hoteli na baa.

Tatizo la upungufu wa maji linaelezwa linatokana na ukame na mabadiliko ya tabianchi.

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (Muwsa), imewajulisha wateja wake kuwa kukatika kwa umeme mara kwa mara kumeathiri uzalishaji na usambazaji maji ya kutosha kutoka kwenye visima vinavyotumia pampu.

Visima hivyo vya Mawenzi na KCMC vimesababisha maeneo ya Shanty Town, CCP, Kitandu, Rau, Kiborlon, Ngurumo ya Upako, Sango na Mdawi Manispaa ya Moshi kuwa na upungufu wa maji kwa wateja wake.

Hali ilivyo hospitali ya KCMC
Ofisa Habari wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Gabriel Chisseo alisema maji kwa sasa ni changamoto kubwa kwa kuwa kisima chao kinategemea mitambo ya umeme kusukuma maji, lakini umeme nao ni changamoto.

“Kwa hiyo kama umeme ukiwa hakuna, hiyo sio athari ya kwanza. Kuna wagonjwa wako ICU, kuna mashine zinazotumia umeme, kuna vyumba vya upasuaji ambavyo upasuaji unaendelea na tunafanya kazi saa 24,” alisema Chisseo.

“Wakati mwingine inaweza kusababisha kifo kwa sababu mtu anatakiwa kufanyiwa upasuaji, kama ajali imetokea majeruhi wamekuja wanataka kufanya upasuaji, vyombo vinavyotumia umeme lakini umeme hakuna.

“Lingine Watanzania tunaendesha hospitali kwa kuchangia huduma, sasa unakuta umeme unapokuwa umekatika tunatakiwa tununue mafuta, sasa hela tuliyokuwa tupeleke kwenye dawa na vitenganishi inabidi tukanunue umeme,” alisema Chisseo.

“Kwa mfano mtambo wa kuzalisha oksijeni hauna uwezo wa kutumia jenereta, ni lazima tuache kuzalisha mitungi kwa sababu ni lazima tuwe na umeme mkubwa. Ina maana kile kiwanda cha kuzalisha kinasimama na ile mashine haitaki mgawo.

“Ukiiwasha umeiwasha mpaka inapomaliza procedure (utaratibu) wake wa kuzalisha gesi. Sasa ukishaipelekea umeme wa mgawo au wa kukatikakatika kwanza unaiua mashine, huzalishi inavyopaswa na wagonjwa wanakosa mitungi,” alisema.

Pia, alisema hata kwenye maji tiba mitambo yao inahitaji umeme mkubwa, hivyo hawazalishi.

Dar es Salaam ni mtafutano
Kama ilivyo katika mikoa mingi nchini, hali si shwari katika jiji la Dar es Salaam, huku mkazi wa Sinza, Hanifa Athumani akisema kutokana na changamoto ya ukosefu wa maji inamlazimu kutumia gharama kuyanunua.

“Yani kwa jana (juzi) nimetumia kama Sh6,000 kwa ajili ya kununua maji kutokana na dumu moja la lita 20 kuuzwa hadi Sh700, inaumiza kwa kweli,” alisema Hanifa, akitaka Serikali ije na mipango ya kutatua adha hiyo. Mjasiriamali mwenye saluni ya kike eneo hilo, Mariam Sultani alisema upungufu wa maji umewahi kumkosesha wateja kadhaa waliokuwa wakihitaji huduma ya kuosha nywele saluni hapo.

“Napata changamoto kwenye biashara kutokana na kukosa maji na gharama ya kununua kwa madumu ni kubwa, hivyo wateja wanaohitaji kuosha nywele wanashindwa kupata huduma hiyo na siwezi kupandisha bei,” alisema Mariam.

Edward Nombo ambaye ni mkazi wa Tabata Magenge, alisema kutokana na ugumu wa kupata huduma ya maji kwa matumizi ya nyumbani, anatumia muda mwingi kutafuta maji kwa watu wenye visima.

“Ukienda kwa wanaomiliki matanki unakuta foleni kubwa, ili upate madumu mengi unatakiwa uwahi foleni,” alisema.

Pia, alisema kutokana na uhaba huo, wanaomiliki matanki wamepandisha bei kutoka Sh200 hadi 400 kwa dumu la lita 20.

Mshikemshike
Wakazi wa Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro wamedai kukatika kwa umeme na maji kunakoendelea kunasababisha baadhi ya biashara kusimama, huku wakidai kuna wakati umeme hukatika kwa siku nzima hadi usiku.

Mmiliki wa saluni iliyopo mjini Moshi, Happy Tarimo alisema juzi umeme na maji vilikatika kwa siku nzima na kurejeshwa usiku, hali iliyosababisha shughuli za saluni kusimama kwa kuwa aina ya biashara yake hutumia maji na umeme.

“Biashara yangu inatumia umeme na maji, vyote vinakatwa kwa siku nzima nashindwa kufanya kazi, nilikopa fedha marejesho yanahitajika, naomba Serikali itusaidie hili suala maana sasa limekuwa ni janga,” alisema Tarimo.

Muuzaji wa samaki, Neema Mbuya alisema wafanyabiashara wengi wameingia kwenye mikopo na taasisi za fedha, hivyo kukatika kwa umeme kunasababisha samaki kuharibika na kupata hasara.

Huko Arusha, inaelezwa kuwa changamoto ya mgawo wa umeme na maji imekuwa adha kwa wananchi, huku Mkuu wa Chuo cha Uandishi wa Habari Arusha Fanikiwa, Andrea Ngobole akisema kukosekana kwa umeme kunasababisha kudorora mazoezi ya vitendo.

Mkoani Morogoro hali ni hivyo hivyo, inaelezwa imeathiri shughuli za kiuchumi huku Catherine Bombwe anayemiliki saluni akisema kukatika kwa maji na umeme kumesababisha kipato chake kushuka.

Katika hatua nyingine, wakazi wa Jiji la Mbeya wamedai kwa sasa wanalazimika kutumia mishumaa na maji ya visima na mito kwa ajili ya matumizi ya majumbani kutokana na uhaba wa umeme na maji ulioikumba nchi kwa sasa.

Mkazi wa Sabasaba, Hadija Mbika alisema wamekuwa na wakati mgumu wa namna ya kuhudumia familia pindi kunapokuwa na mahitaji ya huduma hiyo muhimu kwa binadamu.

“Kwa mfano mimi ni mwanamke, napaswa huduma zote kutumia nishati ya umeme na maji kama kuoga na kunyoosha nguo, hivyo kukosekana huduma hizo nakosa kuwa mtanashati,” alisema Hadija.

Habari hii imeandikwa na Daniel Mjema, Fina Lyimo (Moshi), Mariam Mbwana, Tuzo Mapunda (Dar es Salaam), Hamida Shariff (Morogoro), Mussa Juma (Arusha) na Hawa Mathias (Mbeya)

Chanzo: Mwananchi
 
Halafu Wachaga wanaona adui yao mkubwa ni Magufuli (RIP) ingawaje hajawahi kuwakatia umeme wala maji (mahitaji makuu ya Binadamu) kwanza hata aliwajengea viwanda na reli, hata kaacha daraja la mto Wami linajengwa ambalo Mbowe wenu alililamikia, sasa hivi madame hata umeme hospitali yenu Kuu anawakatia.
 
Halafu Wachaga wanaona adui yao mkubwa ni Magufuli (RIP) ingawaje hajawahi kuwakatia umeme wala maji (mahitaji makuu ya Binadamu) kwanza hata aliwajengea viwanda na reli, hata kaacha daraja la mto Wami linajengwa ambalo Mbowe wenu alililamikia, sasa hivi madame hata umeme hospitali yenu Kuu anawakatia, …
Umeme sio hitaji kuu la binadamu mkuu
 
Mgao ya mipango, wezi wanaona raha wanavyowatesa watanzania masikini wa nchi hii kwa kuwanyima huduma muhimu za maisha yao ilimradi wao watimize malengo yao, hii laana itawatafuna popote walipo.
 
Watakwambia et miti millioni 4 imekatwa sjui walienda kuihesabu! Kuna watu vilaza sana
Hahahaha! Unanikumbusha wakati tunasoma chuo kwenye group discussion kuna jamaa aliwa kusema ni ubumbavu nchi kuwa "mlokole wa mazingira".
 
Umeme sio hitaji kuu la binadamu mkuu

Inategemea na jinsi unavyoona, kama unatibiwa kwa Mganga wa kienyeji na unaamini uchawi labda ni kweli siyo hitaji kuu, lkn kwa modern World Umeme ni hitaji kuu, bila umeme hauna maji safi, friji za kuhifadhia dawa Hospitalini hazifanyi kazi, daktari hawezi kufanya operation kwa mgonjwa, kuna watu wana dharura wamepata ajali, wameungua moto, mama anajifungua vyote hivi bila umeme haviwezekani …
 
4212D23F-7DC3-417F-AED9-14D6567C09A3.jpeg
 
Back
Top Bottom