Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya, Sophia Mwakagenda, ametangaza kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM), akisema uamuzi huo unalenga kuendeleza jitihada zake za kuwatumikia wananchi kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza mbele ya mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Bulyaga iliyopo Tukuyu, mkoani Mbeya, ametumia nafasi yake kuwaaga wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akikipongeza kwa kumlea na kumjenga kisiasa tangu aanze safari yake ya uongozi.
“Ninashukuru CHADEMA kwa malezi na mafunzo ya kisiasa niliyoyapata, kuanzia saa tano asubuhi ya Juni 28, 2025, nitajiunga rasmi na CCM ili kuendelea kuhudumia wananchi,” amesema Sophia.
Kupata matukio na taarifa zote kwa kila mkoa kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025 ingia hapa: Special Thread: Mijadala na Matukio ya Uchaguzi Mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025
Hata hivyo, Mwakagenda bado hajafichua kama atawania Ubunge wa Jimbo la Rungwe katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Mwakagenda ni miongoni mwa wabunge 19 wa Viti Maalum waliovuliwa uanachama na CHADEMA. Katika uchaguzi wa mwaka 2020, aliwania Ubunge wa Jimbo la Rungwe kupitia tiketi ya CHADEMA, akichuana na mbunge wa sasa, Antony Mwantona wa Chama cha Mapinduzi (CCM)