Utata wa kupoteza sifa ya kugombea
Hukumu hiyo iliibua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii juu ya uwezekano wa kumzuia Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni kuwania tena ubunge au urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Hata hivyo, Mwanasheria, Alex Mgongolwa akinukuu Katiba ya Tanzania Ibara ya 67 (1)(c); 67(2) (c na d) alisema hukumu hiyo haiwezi kumzuia kugombea ubunge kwa sababu hakwenda jela na kosa lake halihusu kukosa utovu wa uaminifu, kukwepa kodi wala kuvunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Suala hilo linafanana na lililotokea katika mchakato wa uteuzi wa wagombea urais mwaka 2005 wakati aliyekuwa mgombea urais wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila na mgombea mwenza wake, Saidi Soud Said walipowekewa pingamizi kutokana na kutumikia kifungo jela, Mtikila akitumikia mwaka mmoja kwa kosa la uchochezi, Said akitumikia chuo cha mafunzo kwa kosa la biashara ya vitambaa. Hata hivyo, pingamizi hilo lilitupwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Lewis Makame (marehemu) baada ya kusikiliza utetezi wa Mtikila na Said, kuwa makosa waliyofungwa kwayo hayakuwa ya kukwepa kodi, kukosa uaminifu wala kukiuka maadili ya viongozi wa umma.
Mashtaka
Mbowe alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya kumfanyia shambulio la kawaida, mwangalizi wa ndani wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 31, 2010, Nassir Yamin katika kituo cha kupigia kura kilichokuwa katika Zahanati ya Lambo.
Yamin alikuwa ni mwangalizi wa kutoka Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mpelembwa ambaye amehamishiwa Bukoba, alisema kitendo kilichofanywa na Mbowe hakikubaliki na kinapaswa kukemewa.
Kitendo alichokifanya mshtakiwa akiwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema na Mbunge wa Jimbo la Hai ambaye alipaswa kuwa kioo cha jamii hakikubaliki na lazima kikemewe, alisema
Source.Mwananchi.