Sitta azungumzia digrii za vigogo zenye mushkeli
Na Muhibu Said
21st October 2009
Spika wa Bunge, Samuel Sitta.
Spika wa Bunge, Samuel Sitta (pichani), amesema tuhuma dhidi ya mawaziri sita na wabunge wanne waliotajwa kuwamo katika orodha ya watuhumiwa 19 wenye vyeti vya elimu vyenye mushkeli, zinafanyiwa kazi.
Tuhuma hizo zinadaiwa kuwasilishwa kwa Spika wa Bunge na Mwanaharakati, Kainerugaba Msemakweli, kwa njia ya barua na viambatanisho, Septemba 15 na 16, mwaka huu.
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, Spika Sitta alisema kwa sasa yuko nje ya nchi na kusema kwamba: "Nadhani wataalamu watakuwa wanazifanyia kazi."
Awali, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, jana alisema kuwa juzi aliwauliza vijana wake kama barua ya Msemakweli imewasilishwa katika Ofisi za Bunge na kusema kwamba: "Wakaangalia kwenye kitabu cha register (usajili), wakasema hawajaiona."
Hata hivyo, akizungumza na Nipashe jana, Msemakweli ambaye kitaaluma ni Mwanasheria, alisema barua aliipeleka Septemba 15, mwaka huu na kuikabidhi kwa kiongozi wa Masijala ya Ofisi za Bunge kama utaratibu unavyotaka na kugongwa muhuri wa Ofisi ya Bunge.
Alisema siku iliyofuatia (Septemba 16, mwaka huu), alipeleka viambatanisho vyake, pia wakamgongea muhuri wa Ofisi ya Bunge.
Nipashe inayo nakala ya barua na viambatanisho hivyo, ambavyo vyote vinaonyesha kugongwa muhuri wa Ofisi ya Bunge.
Mawaziri na wabunge hao walihusishwa na kashfa hiyo kufuatia utafiti huru uliofanywa na Msemakweli kwa msaada wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU), katika kipindi cha mwaka mmoja na kubaini kwamba wanasiasa hao walitumia vyeti vyenye mushkeli na kuviwasilisha katika ofisi za umma kwamba wana elimu hiyo, kitu ambacho si kweli.
Kwa mujibu wa Msemakweli, utafiti huo ulianza kufanyika Juni 25, mwaka jana hadi Oktoba 9, mwaka huu katika nchi za Marekani, India na Uingereza, ambako vigogo hao wanadaiwa kuwa walisoma na kupata shahada hizo.
Baada ya kubainika kwamba, hawana sifa za elimu wanazodai kwenye wasifu wa elimu zao, Msemakweli alisema ripoti hiyo ilikabidhiwa kwa Ofisi ya Spika wa Bunge.
Alisema kitendo cha kuwasilisha nyaraka zenye mushkeli katika ofisi ya umma ni kinyume cha Ibara ya 68 na 56 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia, ni kuvunja sheria ya Vyuo Vikuu ya mwaka 2005 (5 na sheria ya makosa ya jinai sura ya 16 (333).
Msemakweli alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Jumapili iliyopita na kusema kwamba, alilazimika kufanya utafiti huo baada ya kuingiwa na wasiwasi kuhusu elimu ya vigogo hao.
Alidai vigogo hao wanajiwasilisha kuwa wana shahada za masuala ya kimataifa na diplomasia, biashara na utawala, wengine shahada za uzamili, udaktari wa falsafa, na wengine shahada za ualimu nakadhalika, wakati si kweli.
Msemakweli alisema katika taarifa aliyowasilisha kwa Ofisi ya Spika wa Bunge, aliomba iwawajibishe vigogo hao kwa kashfa hiyo na kwamba, anaendelea na utafiti kwa vigogo wengine tisa na kwamba, atauarifu umma mara tu atakapokamilisha.
Msemakweli alidai ana ushahidi wa kutosha juu ya madai anayoyatoa dhidi ya vigogo hao kwani amefanya utafiti wa uhakika na kwamba, kigogo yeyote atakayehisi kuwa ameonewa aende kwenye vyombo vya sheria na yuko tayari kwenda kuthibitisha madai yake.