Mawaziri, wabunge na wakuu wa mikoa feki watajwa
Monday, October 19, 2009 2:18 PM
ZAIDI ya mawaziri wanne wa serikali ya awamu ya nne ambao wameghushi vyeti kujinyakulia madaraka na vyeo hivyo wameorodheshwa.Majina hayo yanayozidi 15 yamekabidhiwa kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Samuel Sitta, wakiwemo mawaziri, wakuu wa mikoa na wabunge, wanaodaiwa kughushi vyeti vya taaluma zao.
Hatua ya kukabidhiwa kwa orodha hiyo imekuja baada ya Utafiti huru uliofanywa na Mwanaharakati, Kainerugaba Msemakweli kwa msaada wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU), katika kipindi cha mwaka mmoja.
Katika utafiti huo umebaini kuwa wanasiasa hao wametumia vyeti vya kughushi na kuwasilisha katika ofisi za umma kwamba wana elimu hiyo kitu ambacho si kweli na kujinyakulia mamlaka hayo isivyo halali.
Utafiti huo ulianza kufanyika tangu Juni 25, mwaka jana hadi na kukamilika Oktoba 9, mwaka huu, katika nchi za Marekani, India na Uingereza, ambako vigogo hao wanadaiwa kuwa walisoma na kupata shahada hizo.
Utafiti huo Baada ya kubaini kwamba hawana sifa za elimu wanazodai kwenye wasifu wa elimu zai, ripoti hiyo imekabidhiwa kwa Ofisi ya Spika wa Bunge.
Miongoni mwa vigogo waliotajwa katika orodha hiyo ni wale waliowahi kutajwa kusoma katika vyuo vya elimu ya juu nje ya nchi ambavyo havitambuliki.
Katika orodha hiyo, wamo mawaziri watatu akiwemo Waziri mmoja mwanamke kutoka mikoa ya Kanda ya Kaskazini na manaibu waziri watatu wa wizara nyeti nchini ambao wana hadhi ya udaktari na waziri mmoja anayeongoza wizara muhimu sana nchini.
Pia yumo mkuu wa mkoa ambaye ni mbunge wa jimbo moja kutoka mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Katika orodha hiyo, wamo pia wabunge watatu machachari wenye hadhi ya udaktari kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kaskazini.
Viongozi waliotajwa kwenye orodha hiyo, walikabidhi taarifa za uongo na za kughushi kuhusu taaluma zao, kitendo ambacho ni ufisadi wa elimu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo viongozi walioghushi vyeti vya elimu yao wanapaswa kuchukuliwa hatua ili kurejesha taifa katika maadili yanayotakiwa.
Alitaja adhabu ambazo watuhumiwa hao wanaweza kupata kama wanatiwa hatiani kuwa ni pamoja na kuhukumiwa kifungo kisichozidi miezi sita au kulipa faini ya sh 1,500,000 au vyote kwa pamoja.
Katika siku za hivi karibu, kumekuwa na mjadala wa kuhoji viwango vya elimu vya baadhi ya watendaji wa serikali ambapo baadhi yao wamefika hatua ya kulazimishwa waitwe kwa hadhi ya viwango vyao vya elimu wakati hawana sifa hizo.
Hata hivyo hii ni mara ya kwanza kwa wanaotuhumiwa kughushi viwango vya taalamu yao kutajwa hadharani na kupekelewa ushahidi katika ofisi ya spika.
Spika wa Bunge Sitta, jana hakuweza kupatikana kwa njia ya simu kuzungumzia jambo hilo ambalo ni dhahiri sasa litaibua upya mjadala wa viwango vya taaluma kwa baadhi ya watendaji nchini.