Mauaji Wanawake wawili Zanzibar. ZAFELA, TAMWA ZNZ wataka wahusika wakamatwe

G-Mdadisi

Senior Member
Feb 15, 2018
157
99
TAARIFA KWA VYOMBO HABARI 28-Mei-2023

Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) zimesikitishwa kwa vitendo vya mauaji ya kikatili dhidi ya wanawake wawili yaliyotokea hivi karibuni Bububu Kijichi na Mbuzini Wilaya ya Maghari “A” Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari pamoja na jeshi la polisi, ni kwamba wanawake hawa wawili, Laura Msemwa (23) na Khairat Juma Bakari (28) wameuwawa kikatili na watu wasiojulikana.

Taarifa zinaeleza kwamba mauaji hayo yaliyobainika tarehe 20/05/2023 yalifanyika karibu ndani ya wiki moja iliyopita na hivyo kuleta wasiwai kwa jamii ya wanawake na wasichana.

ZAFELA na TAMWA, ZNZ zinasikitika kwamba kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la polisi iliyotolewa hivi karibuni kwa waandishi wa habari tarehe 25/5/2023 wauwaji wa wahanga hao bado hawajapatikana.

Hivyo, Asasi hizo za kiraia zinaliomba sana Jeshi la Polisi kutumia raslimali zake zote kuwatafuta na kuharakisha upelelezi ili kuwafikisha watuhumiwa katika vyombo vya sheria mapema iwezekanavyo na hivyo kulipia makosa yao hayo.

Kupatikana kwa haki kutawatisha wahalifu wengine ambao wana nia ya kufanya vitendo hivyo vya kikatili na kuhakikisha kwamba matukio kama haya hayaendelei kutokea Zanzibar.

Pia TAMWA -ZNZ na ZAFELA zinaiasa jamii kuacha kutenda vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambavyo vinakiuka haki za kibinaadamu na kuteteresha ustawi kwa makundi ya wanawake na wasichana.

Kwa mujibu rikodi za taaisi hizo tokea mwaka 2016, matukio 23 ya mauwaji ya wanawake na watoto yameripotiwa ambapo upatikanaji wa haki umekuwa ni mgumu kufikiwa.

Tunaamini kwa nchi ndogo kama Zanzibar kukiwepo na upelelezi na mashirikiano mazuri ya jamii wahalifu wanaweza kupatikana kwa muda muafaka.

Imetolewa na ZAFELA na TAMWA ZNZ.
 

Attachments

  • PRESS RELEASE- Killings 2 women- TAMWA-ZAFELA_page-0001.jpg
    PRESS RELEASE- Killings 2 women- TAMWA-ZAFELA_page-0001.jpg
    702.8 KB · Views: 6
Back
Top Bottom