Mkurugenzi TAMWA ZNZ ataka Vijana, Wanawake kujiamini kugombea nafasi za uongozi

G-Mdadisi

Senior Member
Feb 15, 2018
157
99
DKT MZURI- MKURUGENZI TAMWA ZNZ.jpeg

MKURUGENZI wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ), Dkt. Mzuri Issa, amewashauri wanawake kujiamini na kuondosha woga wakati wa kugombea nafasi za Uongozi ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Dkt. Mzuri ameyasema hayo akifungua mafunzo ya siku mbili ya uongozi kwa vijana wa kike, yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kuungana pamoja na kuleta ushawishi katika maendeleo ya agenda mbalimbali za kitaifa.

Amesema kwa sasa dunia imetambua umuhimu wa mwanamke na imeamini kwamba mwanamke ni Kiongozi kutokana na maendelo tofauti yaliyoletwa na viongozi wanawake duniani.

“Mwanamke ni kiongozi bora, na nyinyi vijana ndio tunawategemea muwe na maono ya mbali katika kuleta uongozi ulio imara na kuibeba nafasi ya mwanamke katika uongozi, mwanamke anaweza kuwa mama, mke, mfanyakazi na kiongozi na wakati huohuo na akaweza kutekeleza majukumu yote hayo na akafanya vizuri katika kila sekta”, Dkt. Mzuri Issa , Mkurugenzi TAMWA ZNZ.

Akitoa mafunzo hayo kwa vijana wa kike 15, Mkufunzi wa masuala ya Uongozi, Imelda Lulu Urrio amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo kujitambua na kutambua nafasi zao ili kufikia ndoto zao katika harakati za Uongozi.

“Nafasi ya wanawake kwa sasa inazidi kuongezeka kwa sababu kuna ukuwaji wa Elimu kwa jamii na hata watoto wa kike wenyewe wameanza kujitambua na kujielewa, tumeona baadhi ya jamii inavyowajenga watoto wa kike kujitambua na kupelekea ongezeko kubwa la viongozi wanawake”, alisema mkufunzi huyo.

Nae Maryam Ame, mratibu wa mradi wa kuwawezesha wanawake kushika nafasi za Uongozi (SWIL) unaotekelezwa na TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway amesema mda mrefu imeonekana wanawake wameachwa nyuma katika ngazi za maamuzi hivyo kwa sasa wanawake watumie fursa na haki yao ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa ili kufikia dhamira ya 50/50 katika masuala ya uongozi.

Aidha washiriki wa mafunzo hayo wamesema wamefarijika kupata mafunzo hayo kwani yanawajenga kuwa viongozi bora na kuahidi kuwatakuwa mabalozi wazuri kwa wanawake na kupambana kugombania nafasi za ngazi za juu ili kuondosha mfumo dume uliotawala katika jamii.

“Matarajio yangu baada ya mafunzo haya ni kuwa Kiongozi mwenye kujiamini, na nitapambana kuwa kiongozi wa ngazi za juu zaidi katika chuo changu,” alieleza Hudhaimat Haji Juma, mwanafunzi wa Shahada ya Pili ya Uhasibu katika Chuo Kikuu cha Taifa, (SUZA).

Mafunzo hayo yameendeshwa ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa mradi wa kuwawezesha wanawake kushika nafasi za uongozi (SWIL), unaotekelezwa kwa pamoja na TAMWA ZNZ, PEGAO NA ZAFELA kwa mashirikiano na Ubalozi wa Norway.
 
Back
Top Bottom