The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
617
1,801
DIGITALI KATIKA HUDUMA ZA SERIKALI.jpg

Katika dunia ya leo, si tu biashara zinazopeleka huduma zao mtandaoni, pia kuna mabadiliko ya kidigitali kwa serikali. Serikali zimekuwa zikilazimika kupitia mabadiliko mbalimbali kadiri mahitaji na matakwa ya raia yanavyobadilika. Mabadiliko haya ya kidigitali ya serikali ni matumizi endelevu ya teknolojia za kisasa zinazoboresha utendaji kazi wa serikali na ni muhimu ili kukidhi matarajio ya raia wa leo.

Ingawa wananchi ndio lengo kuu la mabadiliko haya ya kidigitali katika huduma za serikali, pia kuna mwelekeo wa mahusiano ya serikali na biashara, lakini pia baina ya serikali na serikali.

Huduma ambazo serikali sasa zinaweza kutoa kwa njia ya kidigitali ni bora zaidi na ni wazi kwa pande zote zinazohusika. Mabadiliko ya kidigitali ya serikali yameruhusu huduma nyingi kutotegemea tena mafaili ya karatasi na uhitaji wa uwepo wa wananchi katika ofisi za umma ili kupata huduma fulani, jambo ambalo linawapa muda wafanyakazi wa umma na wananchi kuendelea na shughuli nyingine.

Huduma za kidigitali zinaweza pia kumaanisha watu kutosimama tena kwenye foleni kwani wanaweza kupata huduma wanazohitaji kwa haraka mtandaoni na kwa urahisi. Huduma hizi zinaweza kuwa ni maombi ya leseni za uvuvi au uwindaji, kusasisha leseni za udereva, pasi za kusafiria, ulipaji kodi, na mengine mengi.

Hata hivyo, mabadiliko haya yanahitaji ubora kuliko kuweka tu huduma kwa haraka mtandaoni bila kujali ubora au urahisi wa matumizi.

Serikali zinapaswa kutambua mahitaji ya raia wake ili huduma za kidigitali wanazotoa ziwe ndizo ambazo wananchi wanazihitaji na kuzitumia zaidi. Mkakati wa kidigitali wa serikali ni muhimu ili kuongeza matokeo chanya ya huduma za kidigitali.

Kando na kuokoa muda, manufaa mengine ya matumizi ya teknolojia ya digitali yanaweza kujumuisha masuala kama vile uchakataji wa haraka, kupunguza uingizaji wa data wenye makosa, na kupunguza gharama za kuhifadhi na kuchapisha. Matumizi ya digitali pia huzipa serikali taarifa zinazohitaji ili kufanya maamuzi ambayo yananufaisha wananchi.

Ni muhimu kukumbuka kuwa mabadiliko ya kidigitali ni safari. Haifanyiki kwa wakati mmoja au kwa usiku mmoja. Hufanyika kwa hatua na awamu kwani teknolojia inaboreshwa kila mara, huku wafanyakazi wakiendelea kufunzwa kutumia mifumo mipya inayobuniwa kila uchao.

Serikali zinahitaji kufikiria upya jinsi digitali inavyoweza kutumika kuboresha uzoefu (experience) wa raia katika kufikia huduma za umma. Hili linahitaji kupitishwa kwa kuzingatia dhana ya ‘raia-kwanza’ katika kubuni sera na kutoa huduma. Lengo kuu ni kuboresha utoaji wa huduma, kukuza mwingiliano wa uwazi na ufanisi, kuongeza kiwango cha imani ya umma kwa serikali, na kuendeleza matokeo bora.

Mitandao ya kijamii, kwa mfano, inachukua nafasi ya njia za kawaida kama namna ya kuingiliana na serikali, kuripoti matatizo na kutoa maoni.

Matumizi sahihi ya digitali pia yanaweza kuboresha usimamizi wa rasilimali za umma kwa kuweka namna ambazo wananchi wanaweza kufuatilia jinsi pesa za umma zinavyotumika na kulinganisha na matokeo, na hivyo kuongeza uwajibikaji na uaminifu.

Hata hivyo, ili kufikia viwango vya juu vya matumizi bora ya digitali, Serikali zinapaswa kuweka mkazo katika kustawisha uchumi wa kidijitali. Hii inahusisha kufanya kazi na mashirika binafsi ili kukuza ujuzi wa kidigitali kwa umma na kuongeza upatikanaji wa intaneti bora na ya gharama zilizo rafiki kwa wananchi wake, pamoja na kukuza ujumuishaji wa kidijitali (digital inclusion).
 
Back
Top Bottom