Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho anaamini haiwezekani kukimbizana na Manchester City msimu huu katika mbio za ubingwa Ligi Kuu.
City ililaza Everton 3-1 Jumamosi, hiyo ina maana wanahitaji ushindi katika mechi moja tu ili wajitangazie ubingwa kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2013-2014 iwapo watafanikiwa kuifunga Man United kwenye Uwanjani Etihad wikiendi ijayo.
Man United ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 68 baada ya kucheza mechi 31. Wakiwa wameachwa nyuma kwa pointi 16 na City.
Katika ligi nyingine, tungekuwa bado tunapigania taji," alisema Mourinho.
United wamo mbioni kumaliza ligi wakiwa na alama za juu zaidi Ligi Kuu tangu msimu walioshinda ligi 2012-13 wakiwa na Sir Alex Ferguson msimu wake wa mwisho.
Misimu iliyofuata,walimaliza nafasi ya saba, nne, tano na sita.
Baada ya kuondolewa Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya 16 bora na Sevilla, na kisha kutuhumiwa kwa kucheza mchezo usio wa kuvutia, Mourinho amekosolewa sana msimu wake wa pili akiwa kocha wa Man United.
Mreno huyo anatetea sana matokeo ya klabu hiyo, na mapema mwezi huu alitoa hotuba ya dakika 12.
Kabla yao kushinda 2-0 nyumbani dhidi ya Swansea Jumamosi, Mourinho alitumia ujumbe wake kwenye ratiba ya mechi kusisitiza tena kwamba United ni "klabu iliyo kwenye mpito".
Baadaye, alitaja rekodi yao ligi na pia kwamba wanacheza nusu fainali Kombe la FA dhidi ya Tottenham kama ishara kwamba wameimarika msimu huu.
Msimu uliopita, tulishinda vikombe lakini tukamaliza nafasi ya sita katika ligi," alisema Mourinho ambaye alishinda Kombe la Ligi na Europa Ligi msimu uliopita.
"Tunataka kumaliza wa pili msimu huu na tuna alama 10 zaidi ya msimu uliopita, tumefunga mabao mengi, tumefungwa mabao machache, lakini kuna klabu ambayo imeifanya kuwa vigumu sana kuwakimbiza.
"Tumekuwa na msimu mzuri na bado tunacheza Kombe la FA. Tutapigania nafasi yetu huko."