Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger amesema kuwa hatarajii kama Jose Mourinho atatumia mbinu za kujihami Man United watakaposafiri kwenda Emirates
Mashetani Wekundu wameshindwa kuifunga timu yoyote katika sita kuu kwenye mechi ya ugenini chini ya Mourinho katika matukio saba tangu achukue mikoba kuinoa timu hiyo mwaka jana, akiambulia sare tatu na kupoteza nne.
United pia wamefanikiwa kuweka kimiani goli moja katika mechi waliyofungwa 2-1 na Tottenham Hotspur miezi sita iliyopita - na walikosolwa hivi karibuni kwa mbinu walizotumia kwenye sare isiyo ya magoli dhidi ya Liverpool katika uwanja wa Anfield.
Wenger anaamini kuwa wageni wake watajaribu kutafuta mbinu kuongeza mashambulizi na kukaba pia katika mechi yao ya Jumamosi jioni, hata hivyo, aliwaambia waandishi: "Sitarajii jambo jipya [kiulinzi]. Man United ni timu imara na natarajia tutaweza kuyakabili matatizo watakayotusababishia.
"Watashambulia pia. Hawatakaba tu. Ni mechi baina ya Arsenal na Man United nyumbani kwetu. Nahitaji tu kujidhatiti na kuandaa vema timu yangu, na kuipa timu yangu nafasi nzuri kushinda mechi hiyo. Man United wanafanya vizuri kwa sasa, tunafanya vizuri pia kwa sasa, kwa hiyo inaonekana itakuwa mechi yenye mvuto."
Wenger, ambaye atamkosa mchezaji wake ghali zaidi Alexandre Lacazette dhidi ya United, amefanikiwa kukipandisha kikosi chake nafasi ya nne kufuatia ushindi wa mechi tatu mfululizo.