MAMA YANGU ADUI YANGU - 15-
ILIPOISHIA;
Kwa vile taarifa niliipata siku tatu kabla, nilijiandaa kwa kutafuta nguo itakayoendana na maeneo yale, japokuwa siku zote sikupenda kuvaa nguo fupi kwani zilininyima uhuru na kujiona nakuwa mtupu.
Siku ya Jumatatu niliamka alfajiri nikajiandaa na kuelekea kwenye kazi hiyo. Saa moja kasoro bwana wa dada Sauda alifika na gari lake na kunichukua kunipeleka kwenye hiyo super market.
Tulikwenda mpaka kwenye super market iliyokuwa katikati ya jiji. Tulipofika alipiga simu na kumsikia akizungumza.
Haloo...eeh...nimefika...haya nakuja.
Baada ya kukata simu aliniambia.
Twende.
SASA ENDELEA...
Sikumjibu nilimfuata, tuliingia naye ndani na kwenda moja kwa moja mpaka kwenye ofisi moja iliyokuwa ya vioo vitupu na kuingia ndani.
Ndani tulimkuta kaka mmoja mtanashati, baada ya kuingia nilikaribishwa kwenye kiti. Nilikaa na kutulia huku bwana wa dada akisalimiana na yule kaka kisha alisema:
Sasa bibie mi acha niwahi, kila kitu atamalizia huyu mwenyeji wako.
Hakuna tatizo.
Bwana wa dada alitoka na kuniacha na yule kaka ambaye aliniomba radhi na kutoka. Baada ya muda alirudi na fomu ambazo zilikuwa za kuajiriwa. Baada ya kukaa aliniuliza maswali mawili matatu kisha alinipeleka sehemu, nikapigwa picha.
Baada ya zoezi lile nilirudi ofisini kwa yule kaka aliyekuwa meneja wa duka lile kubwa sana. Alinyanyua simu na kuagiza chai, baada ya muda ililetwa na kunywa kisha alimwita dada mmoja.
Alipofika alimweleza:
Suzy huyu ni mfanyakazi mpya, naomba umpe ushirikiano wa hali ya juu.
Hakuna tatizo bosi.
Kampatie sare na aanze kazi.
Hakuna tatizo, atakuwa sehemu gani bosi?
Mweke kwa keshia.
Hakuna tatizo, kitambulisho?
Muone Sam nina imani kitakuwa tayari.
Haya shem, nina imani Suzy atakusaidia, kazi njema.
Asante.
Nilitoka na Suzy mpaka kwenye chumba kimoja kilichokuwa na sare na kunichagulia inayonitosha kisha tuliongozana mpaka kwenye chumba kingine na kukuta kitambulisho changu kipo tayari.
Nilipewa na kukivaa kisha nilipelekwa sehemu na kuelekezwa kama mtu akishalipia bidhaa aliyonunua namuwekea kwenye mfuko na kuwakaribisha tena.
Haikuwa kazi kubwa sana lakini nilichoka sana kwa vile sikuwa nimezoea kusimama muda mrefu. Jioni bwana wa dada alinipitia. Kabla ya kuondoka da Suzy niliyekuwa nimemzoea kwa haraka, alinieleza muda wa kuingia kazini na umuhimu wa kuwahi.
Nilimshukuru na kumuahidi kuwahi siku ya pili. Niliingia ndani ya gari la shemeji na kurudishwa nyumbani. Njiani shemeji aliniuliza mambo mengi kuhusiana na kazi.
Sikusita kumshukuru kwa msaada wake ambao ulikuwa muhimu kuliko kitu chochote kwa wakati ule.
Tokea siku ile nilianza kazi ya kuuza kwenye super makert na jioni shemeji alinipitia kama kawaida. Siku zote nilirudi nimechoka baada ya kuoga na kula muda mwingi niliutumia kitandani kwangu kupumzika.
Taratibu nilianza kumsahau mtalaka wangu Beka na kuamini kuna maisha mengine baada yake kwa kujua kila linalomtokea mwanadamu lina makusudio yake.
Kazi niliizoea na kuwa maarufu kutokana na ucheshi wangu. Lakini nilikuwa na wakati mgumu kazini kutokana na wanaume wengi wakware kunitaka kimapenzi.
Pamoja na ahadi nyingi nilizopewa kama nitakubali kujitoa kwao kimapenzi, sikuwa tayari kujiingiza katika dunia iliyoniumiza na kufikia hatua ya kuwachukia wanaume, japokuwa sikutakiwa kumhukumu mtu kwa kosa la mwingine.
Moyoni nilipanga baada ya miaka miwili ndipo niufungue moyo wangu. Najua unaweza kushangaa uamuzi wangu lakini kila aliyekumbwa na mkasa wa mapenzi hawezi kunishangaa kwa vile mapenzi yanaumiza sana hasa uachwe na mtu unayempenda tena bila kujua kosa lako.
Siku zilikatika huku nikizidi kuifurahia kazi yangu na maisha yangu mapya ya kuishi kama mdudu wa sikio bila kuwa na mshirika. Mwanzo niliamini maisha yale yangekuwa magumu ya kuishi bila mwanaume, lakini kila kitu ukiamua unaweza nami niliweza kabisa.
Nakumbuka siku moja wakati natoka kazini nikiwa ndani ya gari la shemeji bwana wa dada. Baada ya kutoka kazini tulikwenda mwendo wa dakika tano, alinigeukia na kuniuliza:
Mwaija una mpango gani?
Kuhusu nini shemeji?
Si nilisikia umeachana na mumeo?
Ndiyo.
Sasa una mpango gani baada ya kuachana naye?
Mmh! Bado sina mpango wowote nimeamua kupumzika kwanza.
Mwaija wewe bado msichana mdogo kwa nini ujifuje?
Sijifuji bali nimeamua kupumzika, kilichonikuta Mungu anajua.
Mwaija siyo Mungu anajua, mwanaume uliyekuwa naye hakuwa sahihi kwako.
Ukisema hivyo sikubaliani na wewe, Beka namjua vizuri kuliko mtu yeyote, kuna kitu tu ambacho kimesababisha aniache.
Kitu gani?
Wee shemu, tuyaache tu yalishapita hayo, kwa kweli sikupenda kuzikumbuka habari za mtalaka wangu.
Kama anatokea leo na kutaka kukurudia utakubali?
Naweza kukubali kama atanieleza sababu ya kuniacha na mimi kuikubali.
Sasa Mwaija tuachane na hayo kuna kitu nataka kukuambia japokuwa ninacho muda mrefu, lakini naamini leo ni siku muafaka.
Kitu gani hicho shemeji yangu?
Kuhusu wewe.
Mimi! Nimefanya nini?
Siyo kwamba umefanya kitu ila kuna jambo nimejifunza kwako kwa muda mrefu.
Kipi?
Mwaija unatabia tofauti na dada zako.
Kivipi?
Unajiheshimu pia unajifahamu.
Nashukuru kwa kulifahamu hilo.
Baada ya kuligundua hilo nilikuwa na ombi moja ambalo nina imani litakuwa na faida kubwa kwako.
Ombi gani?
Nataka nitabadili maisha yako uweze kumiliki nyumba na gari.
Kivipi?
Nafikiri unajue mimi na dada yako tukoje?
Ndiyo najua.
Basi nimeishamfumania na wanaume zaidi ya watatu.
Shemeji alitulia kuzungumza akasimamisha gari kuwaruhusu watu waliokuwa wakivuka barabara eneo la Changombe Maduka Mawili wavuke. Baada ya watu kuvuka alibadili gea na kukanyaga mafuta kisha alinigeukia na kusema:
Unajua nilikuwa nina mipango mikubwa na dada yako.
Mipango gani?
Nimjengee nyumba na kumnunulia gari.
Tatizo nini?
Hataki nimuoe zaidi ya kupenda maisha anayoishi, wewe ni mdogo lakini una akili sana.
Shem, si nasikia umeoa?
Ndiyo, lakini angekuwa nyumba yangu ndogo.
Mmhu, na mimi unataka kuyabadilisha maisha yangu kivipi?
Nini kitaendelea? Tukutane tena jumamosi....