MAMA YANGU ADUI YANGU - 13............
ILIPOISHIA
BABA mkwe alirudi kunisikiliza, baada ya kukaa alinisuburi mimi nieleze kilichonipeleka pale. Kwanza nilianza kwa kuwaomba msamaha.
Samahani wazazi wangu.
Bila samahani mama, alijibu mama mkwe.
Nina imani mnajua kilichotokea hivi karibuni kuhusu mimi na mwenzangu.
Ndiyo.
Kauli yao ilinishtua kidogo kuonesha wanajua kila kitu lakini waliamua kukaa kimya. Ile ilinifanya niamini nitaweza kujua sababu ya mimi kupewa talaka.
Wazazi wangu mpaka sasa nipo njia panda, ni kweli nimeachika talaka moja. Lakini mpaka sasa sijajua sababu ya kuachwa.
SASA ENDELEA...
Hujui sababu ya kuachwa! Unamaanisha nini kwani ilikuwaje?
Amekuja na kunipa talaka bila maelezo.
Mmh! Sasa mwanangu amekupa talaka bila maelezo inakuja kweli, au kuna kosa ulilolifanya mwenzio kagundua?
Wazazi wangu, Mungu ndiye anajua lakini toka mume wangu ameondoka nimekuwa mtulivu na mvumilivu kumsubiri yeye huku nikimuombea kwa Mungu afanikiwe.
Lakini amerudi mume wangu kapendeza, furaha yangu ya kumuona ikageuka shubiri.
Wee mwana, unataka kutuambia mume wako amefika tu na kukupa talaka? mama mkwe alionesha kushtuka.
Ndiyo wazazi wangu.
Kakwambia tatizo nini?
Wazazi wangu kila nikimuuliza aniambie tatizo la kunipa talaka haniambii zaidi ya kusema nimuulize mama yangu ndiye anajua, mama naye kumuuliza kanijia juu kuwa mume wangu hana adabu, talaka atoe yeye sababu atoe mama.
Mmh! Makubwa, ina maana hakuna tatizo lolote kabla ya kuondoka mumeo?
Hakuna wazazi wangu.
Amekuja na kukupa talaka bila kosa?
Ndiyo mama, nimemuuliza sababu ya kunipa talaka haniambii. Hata kama alikuwa na nia ya kuniacha angeniambia nikajua moja. Inauma mtu kumsubiri siku zote hizo halafu faida ya uvumilivu wangu kwake ni talaka? Inauma...Inauma sana, nilianza kulia kwani moyo ulikuwa ukiniuma.
Basi mwanangu nyamaza kulia.
Mama inauma, jinsi tulivyopendana na Beka si wa kunipa talaka kama ameniokota baa.
Kwa hiyo hakukueleza sababu? walirudia swali la awali.
Ndiyo wazazi wangu ndiyo maana nimekuja hapa mnieleze sababu ya mimi kupewa talaka ili nijue kosa langu huenda kweli nilimkosea mwenzangu bila kujua.
Eti mama Beka mwanao alikueleza sababu ya kumpa talaka mkewe? baba mkwe alimgeukia mkewe.
Hajaniambia.
Wazazi wangu nakuombeni nipo chini ya miguu yenu niambieni sababu ya Beka kunipa talaka.
Uongo mbaya mi sijui, labda mama yako, baba mkwe alimtupia mpira mkewe.
Mume wangu, Beka aliporudi alitueleza amempa talaka mkewe. Nina imani wote tulishtuka kwa sifa alizokuwa akikumwagia kabla ya kuondoka na aliporudi siku ile hata bila kupumzika alikuja kwako.
Aliporudi alitushtua kwa kutuambia kuwa amekupa talaka. Tuliingia wasiwasi labda amekuja huko kwa vile ni muda mrefu uko peke yako basi kakukuta na mwanaume.
Hapana wazazi wangu, amekuja ametukuta tupo sebuleni, alipofika alitusalimia na kuniomba tuzungumze, tukaingia chumbani kwetu, amesema ananipenda sana na hata pata mwanamke kama mimi lakini hana jinsi ameamua kunipa talaka.
Nimembembeleza anieleze sababu ya kuniacha amekataa zaidi ya kuniambia kila kitu mama anajua. Basi niliamini wazazi wangu lazima aliwaambia.
Kama mama yake hakumwambia sijui nani anajua sababu ya talaka, tulitegemea mzazi wako kuja lakini amekaa kimya basi tumejua sababu mnaijua wenyewe.
Mama haki ya Mungu sijui lolote, niliamini ninyi mnajua.
Mwanetu tumembembeleza, lakini amesema wewe unajua.
Mimi? nilisema nikijishika kifuani kushangaa kauli ya mume wangu.
Ndiyo.
Jamani Beka mbona ananionea, mi nijue sababu halafu nije niulize?
Ndiyo maana hata sisi tunashangaa wewe kusema hujui.
Wazazi wangu kama Beka kapata mwanamke mwingine angeniambia kuliko kunikosanisha na mama yangu. Japo nampenda lakini suala la kuachwa siwezi kulipinga japokuwa linaniuma sana.
Mmh! Sasa huu mtihani, mama mkwe alisema.
Kwani mama, Beka yupo wapi?
Beka aliondoka siku ya pili baada ya kutoka kwenu bila kutupa jibu lolote.
Amekwenda wapi?
Kwa kweli, kama yeye mwenyewe hakukuambia sisi itakuwa vigumu.
Sawa wazazi wangu, kama mmekataa kuniambia alipokwenda Beka nina imani hata sababu za kuniacha mnazijua.
Hilo hatujui.
Nashukuru wazazi wangu kwa kunificha, lakini siwezi kuwalaumu, ila siku zote nitamlaumu Beka kwa kunitendea unyama.
Baada ya kusema vile nilinyanyuka na kuondoka bila kuaga. Baada ya kutoka nilisikia nyuma wakiniita lakini sikugeuka baada ya kuona napoteza muda wangu bure.
Nilikwenda kwa mwendo wa haraka hadi Buguruni nilipochukua daladala mpaka Mikoroshini kisha nilielekea nyumbani. Nilipofika niliingia chumbani kwangu na kujifungia, nikajilaza kitandani.
Nilijikuta moyo ukiniuma kwa kuonewa bila kosa, nilijiuliza kosa langu nini, kwa nini nimekosa ushirikiano na kuwa peke yangu kama nimerogwa. Machozi yalizidi kunitoka kama maji.
Sauti nisiyoielewa niliisikia ikisema: Machozi siyo dawa ya maumivu wala ufumbuzi wa matatizo. Dawa ni kupambana, acha kulia futa machozi songa mbele.
Nilishtuka na kujikuta nipo peke yangu chumbani, niligundua nipo kwenye mawazo makali yaliyonifanya nizisikie sauti za watu. Lakini niliikumbuka kauli ile tulielezwa na mwana harakati mmoja aliyekuja shule wakati nipo kidato cha nne na kutupa moyo wasichana tunapotokewa na matatizo ya kukatisha tamaa. Nilinyamaza na kufuta machozi na kujikuta nikirudia mlolongo mzima wa maisha yangu mpaka kupewa talaka na yote niliyokutanana nayo baada ya kupewa talaka.
Nilijikuta nikikubaliana na kauli ya mama kuwa Beka alipokwenda alipata mwanamke na aliporudi aliamua kunipa talaka akisingizia mama anajua ili kunikosanisha na mama yangu.
Nilinyanyuka na kwenda kuoga huku nikiapiza kusahau yote yaliyopita. Baada ya kuoga nilitoka hadi nje nilipowakuta dada zangu wakiendelea kunywa pombe.
Nilisimama kwa muda nikiwaangalia jinsi walivyokuwa wakiyafurahia maisha. Hawakuwa na wanaume lakini kila siku mioyo yao ilijaa furaha tofauti na mimi niliyekuwa nimeolewa kila kukicha maumivu yaliutawala moyo wangu.
Nilijikuta nikijilaumu kuchelewa kutoa uamuzi wa kutafuta mwanaume kwa mtu aliyenitenda. Moyoni niliamini unaweza kuishi bila mwanaume na maisha yako yakasonga. Nilikumbuka maisha ya mama toka baba afariki ambaye sikubahatika kumuona. Aliweza kuishi maisha ya furaha japokuwa niliamini kwa umri wake baada ya kifo cha baba alikuwa na uwezo wa kuolewa.
Lakini mama hakutaka kuolewa alikuwa akiishi maisha yake mwenyewe. Japokuwa mwanzo tabia yake ya kuwa na mwanaume zaidi ya mmoja na wote wakiwa waume za watu sikuipenda.
Baada ya maumivu niliyopewa na Beka nilikubaliana na mama anaona hakukuwa na faida ya kuishi maisha ya ndoa au kuwa muaminifu kwa mwanaume asiyekuwa muaminifu.
Je, nini kitaendelea fuatilia Jumapili inayokuja .........