MAMA YANGU ADUI YANGU - 18-
ILIPOISHIA:
Da Suzy alitulia kwa muda akiwa ameinama kuonesha jinsi gani mapenzi yalivyomuumiza kumpenda mtu asiye muaminifu. Baada ya muda alinyanyua uso wake na kuchukua glasi ya juisi na kunywa kidogo, akanitazama kisha akasema:
Mdogo wangu una mtihani mzito ambao ni sawa na kuitumia turufu moja iliyokuwa mkononi, ikutoe mrithi au ikutoe kapa.
SASA ENDELEA...
Una maana gani da Suzy?
Mpaka mzee anakueleza jambo kama hilo ujue basi kakufuatilia muda mrefu. Malengo yake ni makubwa sana kwako.
Lakini kumbuka tayari ameshatembea na dada yangu.
Ni kweli lakini kwa tabia ya dada yako ya kutokuwa na bwana mmoja. Hiyo ni nafasi ambayo naamini unaweza usiipate mpaka unakufa.
Mtu akujengee nyumba na kukununulia gari kwa ajili ya mapenzi? Ni wachache katika dunia ya leo ambayo wanaume wengi ni matapeli.
Kama huwezi kukubali kuwa nyumba ndogo basi mbebee ujauzito ili upate hayo mamilioni. Naamini mzee Sambi alivyo na hamu ya mtoto lazima ahadi zote tatu atatimiza ukimzalia mtoto.
Mmh! Dada unanipa mtihani.
Hakuna mtihani, yupo wapi Beka uliyempenda kuliko kitu chochote chini ya jua? Mdogo wangu, Waswahili wanasema bahati haiji mara mbili na mchuzi wa mbwa unywe ungali wamoto, ukipoa haunyweki.
Kwa hiyo unanishauri nimkubalie?
Mwaija mkubalie, nafasi kama hiyo mdogo wangu wenzako tunaiendea kwa waganga wewe inakujia miguuni unataka kuipiga teke?
Lakini naogopa kugombana na dada.
Fanyeni hata penzi la siri nina imani litakusaidia katika maisha yako.
Mmh! Nitajaribu kwa vile umeivunja ngome ya moyo wangu sina budi kukubaliana na wewe, nilijikuta nikilegeza msimamo.
Tena nakuomba mdogo wangu usiipoteze bahati hii. Hebu angalia jinsi Mungu alivyosikia kilio chako baada ya kukimbiwa na Beka.
Tena amekwambia humpi mwili wako mpaka akamilishe alichokuahidi, Mungu akupe nini? Waache dada zako watakuja kuuanika wakati jua limekuchwa na kuutwanga mbichi.
Nilikuwa nawaza kumshirikisha mama suala hili, nilimweleza wazo langu la awali.
Mwaija utaharibu kila kitu, kama una wasiwasi wa kugombana na ndugu zako mbebee mimba ule maisha. Tena mtoto anazaliwa akiwa na uhakika wa maisha yake tayari.
Mwaija mizee kama hii ndiyo inatafutwa mjini, hela zao hazina chenji. Mdogo wangu kwangu mimi hata angekuwa mpenzi wa mama yangu mzazi, kama angenitangazia bingo kama hiyo nisingelaza damu.
Naweza kumkubalia lakini sijui kama yupo sawa?
Kivipi?
Kiafya, si unajua dada yangu mwingi wa habari, tusije chuma janga tulile wenyewe.
Mmh! Kweli hilo umenena mdogo wangu.
Kwa hilo utanisaidiaje?
Usimpe mwili wako labda mtumie kondomu.
Tukitumia kondomu mtoto tutampaje?
Sikiliza mdogo wangu, hilo kwa sasa achana nalo, akishatimizia kila kitu kwa jina lako, sharti lako kubwa ili umpe mwili wako ni kwenda kupima kwanza.
Mmh! Dada nimekueleza itabidi nifanye hivyo.
Na majibu yake usiyacheleweshe ili asibadili uamuzi, si unajua wanawake tupo wengi wote tunataka hichohicho!
Nashukuru dada yangu kwa ushauri wako.
Baada ya mazungumzo nilimpigia simu bwana wa dada kuwa nimemaliza kilichonichelewesha naye alinieleza atafika muda si mrefu. Baada ya robo saa alifika kunichukua, kwa vile da Suzy alikuwa akikaa njiani kwenda kwetu, tuliondoka naye na kumteremshia njiani.
Baada ya kumteremsha da Suzy, tulibakia wawili kwenye gari, tulikwenda mwendo mfupi, bwana wa dada akaanza kunisemesha akiwa ameangalia mbele.
Mwaija za kazi?
Nzuri shemeji, shikamoo.
Marahaba, sasa wewe wasiwasi wako nini? aliniuliza swali bila kunitazama.
Wasiwasi! Wa nini?
Naona umeshaanza kuniogopa, nimekueleza lile ni ombi wala haliingiliani na mambo mengine.
Nikuogope kivipi? sikumuelewa.
Najua huniamini na kuona natumia turufu ya kukusaidia ili niweze kufanikisha mambo yangu. Lakini siyo hivyo, sina nia mbaya na wewe. Ningeweza kumpa mtu yeyote fedha niliyonayo lakini naamini kwako haitapotea.
Uliyosema nimekuelewa lakini sikuwa na maana hiyo. Nilikuwa na mazungumzo kidogo na da Suzy, nikaona nitakuchelewesha.
Niliyeamua kukuleta kazini na kukurudisha ni mimi wala sikulazimishwa na mtu.
Sawa, lakini kunipitia si adhabu, kama kuna dharura lazima tuambiane.
Nimekuelewa, ila nilipata wasiwasi, jana kuzungumza leo upatwe na dharura.
Walaa, wasiwasi wako siku zote wanadamu si wapangaji bali kila kitu hupanga wenyewe.
Ni kweli, vipi mzigo uliuona?
Ooh! Samahani kwa kuchelewa kushukuru, asante sana shemeji yangu, nilijikuta nikiona aibu ya kuchelewa kutanguliza shukurani mapema.
Usihofu ni kawaida, nia yangu siku moja, uishi maisha kulingana na heshima yako.
Itaendelea katika Alkhamisi ijayo.....