Niyaonayo katika utunzi wa gazeti la MTANZANIA la leo
"SHIDA Salum, mama mzazi wa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe." (Sentensi hiyo haina ubishi. Huyo ni mama yake Zitto, hata Zitto mwenyewe amekiri hivyo, ingawa wakati mwingine anajulikana kama Mama Lulu au Mama Salum)
"Amenusurika kuuawa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake na watu wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, wakiwa na silaha za moto." (Kama alivamiwa, inawezekana kweli ni majambazi. Lakini habari inatuambia walikuwa na bastola. Hakuna silaha nyingine iliyotajwa. Lakini ili kutia chumvi, mwandishi anasema walikuwa na "silaha za moto.") Tazama chumvi inayokolezwa. Katika utangulizi wa habari yake, Mtanzania limeandika "watu wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi". Acha tu nikubali inawezekana ni majambazi, lakini gazeti hilo hilo, katika ukurasa huo huo, linatilia mkazo kuwa watu hao ni "wauaji". Linaandika hivi katika blabu yake: "Wauaji wamdai laptop, flash na simu yake." Sasa gazeti hilo hilo linajichanganya. Majambazi wanaweza kuwa wauaji pia, lakini siyo kila muuaji ni jambazi. Sasa hao ni majambazi au wauaji? Chumvi yote ya nini?
Habari zilizolifikia MTANZANIA Jumatano kutoka kwa watu walio karibu na mama huyo zilieleza kuwa, vijana hao walifanikiwa kumfikia akiwa katika sebule ya nyumbani kwake na kumuelekezea bastola kichwani, huku wakimlazimisha awakabidhi baadhi ya vifaa vyake vya kufanyia kazi na simu yake ya kiganjani. (Vijana hao hawakugonga geti wala mlango. Na mama huyo aliwashtukia tu wako sebuleni.)
"Akizungumza na MTANZANIA Jumatano kupitia simu yake ya kiganjani kuhusu tukio hilo, mama yake Zitto alisema ni kweli lilitokea na amekwisharipoti katika kituo cha Polisi cha Buguruni." (Mama huyo ndiye aliyepiga simu kwa mwandishi au mwandishi ndiye aliyempigia mama huyo? Ilivyo ni kwamba mama huyo ndiye aliyepiga simu. Na hii ni baada ya kudai kuwa amesharipoti polisi. Kwanini gazeti la Mtanzania na hakupiga kwenye magazeti mengine? Hakuna chombo kingine chochote cha habari kilichopigiwa simu. Hakuna hata namba ya RB ambayo mama huyo alimpatia mwandishi. Na mwandishi huyu alivyo, wala hakuuliza namba ya RB. Ndio waandishi tulio nao sasa. Mwandishi huyo amekosa hata umakini wa kutuambia tukio hilo lilitukia wapi, ingawa ametaja tarehe na saa. Hapa kinakosekana kiungo muhimu sana cha uandishi kinachojulikana kama WHERE).
Mama Zitto alisema siku kadhaa kabla ya tukio hilo alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kuwa mwanachama wa Chadema wa Tawi la Tabata Relini na kumuomba msaada wa mifuko miwili ya saruji kwa ajili ya kukarabati jengo la ofisi yao. (Potelea mbali. Waliomba msaada wa mifuko miwili ya sementi halafu wanakwenda kuibeba na gari lao. Mafuta ni sh. Ngapi na sementi sh ngapi? wana uwezo wa kuendesha gari lakini hawana uwezo wa sh 30,000? Labda hiyo ni mbinu yao ya mauaji.)
Alisema alikubali kuwasaidia vijana hao kwa kuwataka wafike nyumbani kwake mapema siku ya Ijumaa ya wiki iliyopita, kwa sababu alikuwa na ratiba ngumu na ndefu siku hiyo. (Mhhhhhh).
"Lakini niliposimama kuelekea chumbani kuwachukulia kiasi hicho cha fedha, mmoja wao alitoa bastola na kunielekezea kichwani huku akieleza kuwa hawana shida na pesa, bali wanataka laptop yangu, flash na simu yangu ya mkononi kwa sababu zina mambo muhimu … nikamwita dereva wangu, Mtana, alete simu yangu niliyokuwa nikiichaji chumbani na flash ili niwapatie, wakati akielekea kuvichukua aliwaona walivyokuwa wameniwekea bastola, akakimbia moja kwa moja chumbani akajifungia na kuanza kupiga kelele, wakatoka haraka wakakimbia." (Haya. Dereva ndiye anayeitwa na kutumwa chumbani kwa MWANAMKE huyo? Kwanini wamruhusu azungumze na dereva wakati wangeweza kumburuta hadi chumbani na kumnyang'anya walichotaka?
Alisema anaweza kuwatambua watu hao akiwaona na kwamba mmoja wao si mgeni machoni mwake, kwa sababu aliwahi kumuona mkoani Tanga katika moja shughuli za chama hicho. (Si walimpigia simu. Si anasema hawakufanikiwa kuchukua simu yake. Hiyo namba, au hizo namba, walizotumia kumpigia si zipo? Alizikabidhi polisi? Mbona ni rahisi? Waliwasiliana naye na bado walifika kwake na bastola kama walivyoahidiana. Kwanini namba hizo zisiandikwe gazetini?)
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, naye hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo na hata Mkuu wa Kituo cha Polisi Buguruni, mahali ambako Mama Zitto ameripoti tukio hilo naye hakuweza kupatikana. (Kweli? Ni kweli haya? Kwanini mwandishi aende kwa Kova wakati tukio liko Buguruni?) Hizi ni propaganda za kuwababaisha wananchi waone kuwa kuna matukio yanayopangwa na Chadema. Nachukia siasa na uchafu wake, lakini wanasiasa wachafu wanaotumia vyombo vya habari nawachukia zaidi. Tusubiri Mtanzania Jumapili na Mtanzania Jumatano kuhusu habari nyingine za Chadema. Hizo ndizo habari pekee walizonazo kwa sababu ya njaa. Nasikia hao jamaa wana njaa sana ndiyo maana wakihongwa kidogo tu wanaandika chochote bila kufuata maadili yao ya uandishi.