Malezi ~ Elimu juu ya haki na usawa kwa mabinti wa Msalala

Sema Tanzania

JF-Expert Member
May 18, 2016
251
465
Tarehe 1 Disemba 2020 timu yetu ilipokelewa kwa bashasha na mabinti watatu kutoka shule ya Sekondari ya Nyikoboko mkoani Shinyanga. Mabinti hawa kwa majina yao ni Mengi Daudi, Helena Joseph pamoja na Mengi Lucas, wanafunzi wa kidato cha kwanza. Mabinti hawa walikuwa kati ya washindi wa shindano la mbio za baiskeli za #SikuYaBinti 2020 ambapo Helena alikua mshindi wa kwanza, Mengi Lucas akiwa mshindi wa pili na Mengi Daudi akiwa mshindi wa sita.

Katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia tuliongea na wasichana wote kumi ambao walishiriki mashindano hayo namna wanaweza kuwa mabalozi wazuri watakao kuwa kipaumbele katika kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto. Tuliwapatia elimu ya afya ya uzazi na kuwaeleza umuhimu wa kupigania usawa kuanzaia shuleni, mtaani na majumbani mwao. Tulipata faraja sana hasa baada ya kuzungumza na wavulana ambao walionesha kuguswa sana na suala zima la unyanyasaji wa kijinsia wanao pitia dada zao.

"Yaani kama sitaolewa basi nitapata ujauzito na hapo ndio utakuwa mwisho wa ndoto zangu" Mmoja kati ya mabalozi wapya wa kupinga ukatili aliongea kwa uchungu kuwa yeye kama binti kuna mambo mengi ambayo yanaweza kufifisha ndoto zake na kuua kabisa malengo yake. "Bila kusahau umbali mrefu tunaotembea kutoka nyumbani kuelekea shuleni ambapo vyote hivi ni vikwazo tunavyopitia katika kutafuta elimu na maisha bora ya mbeleni. Lakini pia kama mabinti hatuna budi kubaki nyumbani kuwasaidia mama zetu kazi za nyumbani".

Mbali na kuelezea changamoto wanazopitia, mabalozi wetu hawa wapya walikuwa na shauku kubwa ya kuelezea ni namna gani wanaona fahari kuwa kati ya washiriki wa mashindano ya mbio za baiskeli yaliyofanyika mapema mwezi Oktoba katika kilele cha #SikuYaBinti. Lakini pia kunyamazishwa kejeli kutoka kwa wanajamii ambao waliwakebehi kwa kusema wasingeweza shinda maana wao ni watoto wa kike tu na hawawezi kufanya lolote. Ilikua nafasi nzuri kwao kuonesha wazi kuwa mtoto wa kike ni kama mtoto wa kiume na anaweza akipewa nafasi.

Mshindi wa 6 alieleza changamoto iliyomkuta hasa baada ya kuchelewa na washiriki wote wakiwa wameshaondoka shuleni na kuelekea katika viwanja vya mashindano huku yeye akiwa kilometa 22 nyuma wakati alipokuwa akitokea nyumbani kwenda shuleni. Alipiga moyo konde na kuanza safari ya kuelekea shuleni Segese. Alijitahidi kadri ya uwezo wake kushinda maana aliambiwa kuwa asingeweza kushinda maana yuko nyuma sana, lakini alidhamiria kushinda na ndipo alipoibuka mshindi wa sita.

Kwa pamoja mabalozi hawa wapya waliiomba timu yetu kuandaa tena mashindano na semina juu ya kuzuia ukatili dhidi ya wanawake, wasichana na watoto maana wamejifunza mengi na wangependa kuona mabinti wengi wakipata elimu hii.
 
Back
Top Bottom