Makosa ya Rushwa na adhabu zake kwa mujibu wa Sheria

Mr George Francis

Senior Member
Jun 27, 2022
186
212
FAHAMU KUHUSU MAKOSA YA RUSHWA NA ADHABU ZAKE KWA MUJIBU WA SHERIA.

SEHEMU YA KWANZA (01)


Mr. George Francis

Mwalimu Nyerere katika hotuba aliyoitoa kwa waandishi wa habari mwaka 1995 alisema,
“Kwa hivyo, tukatengeneza sheria ili tuwafundishe watu hawa kwamba jambo hili hatulipendi. Ikisha kuthibitika mahakamani kwamba kala rushwa hatukumwachia hakimu uamuzi wa adhabu. Tukasema atakwenda ndani muda usiopungua miaka miwili, atapata viboko ishirini na vinne, kumi na mbili siku anayoingia, kumi na mbili siku anayotoka”

Hii inaonesha ni kwa jinsi gani Mwalimu alikuwa mzalendo katika kupambana na rushwa. Taifa letu likewahi kupata viongozi wengi walio na nia ya dhati ya kupambana na rushwa lakini bado hata sasa rushwa imezidi kushamiri katika nchi yetu.

Jamii yetu kwa kiasi kikubwa bado haina elimu juu ya makosa ya rushwa na namna ya kupambana na rushwa. Jukumu hili kwa kiasi kikubwa limeachwa kwa viongozi na maafisa wa mamlaka husika ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa yaani TAKUKURU ambao nao miongoni mwao wapo ambao hawana uadilifu na wamekosa uaminifu.

Vita dhidi ya adui huyu ni kubwa na inapaswa kuwa vita ya jamii yote na sio kuwaachia viongozi au Mamlaka pekeeyake kushughulika na vita hivi.

Hawali ya yote jamii inapaswa kufahamu kuhusu makosa ya rushwa. Yaani lipi ni kosa la rushwa na kipi kifanyike kusudi kuzuia na kutokomeza kabisa vitendo vya rushwa nchini.

Katika makala hii, nakwenda kukuonesha makosa mbalimbali ya rushwa kama yalivyobainishwa katika Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, The Prevention and Combating of Corruption Act
[CAP. 329 R.E. 2022].

Makosa hayo ni haya yafuatayo;

1. Kupokea rushwa, kushawishi au kulazimisha kupewa rushwa, kutoa rushwa au kuahidi kutoa rushwa. Hili ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

✓ ADHABU:
Ukikutwa na hatia ya kutenda kosa hili adhabu yake ni faini isiyopungua shilingi laki tano (500,000/=) na isiyozidi shilingi milioni moja (1,000,000/=) au kifungo kisichopungua miaka mitatu (3) na kisichozidi miaka mitano (5) au faini na kifungo vyote kwa pamoja.
• Pia Mahakama inaweza kufanya yafuatayo.
(a). Kumwamuru mtuhumiwa kulipa kiasi chote au nusu ya pesa au mali alizopewa rushwa.
(b). Kuamuru kutaifisha pesa au mali iliyopokelewa kama rushwa na kuwa mali ya serikali.
Kuongeza maarifa zaidi kuhusu kosa hili na adhabu yake, hunabudi kusoma kifungu cha 15(1),(2)&(3) kwa umakini.

2. Kutoa au kupokea rushwa kwa ajili ya kupata mkataba
wa kutoa huduma kwa idara ya umma au shirika la umma. Hivyo, kutumia ushawishi usio halali kwa afisa wa idara au shirika la umma ili akusaidie kupata mkataba wa kufanya kazi fulani au kutoa huduma fulani katika idara au shirika la umma kwa makubaliano kuwa kuna faida fulani ataipata ni kosa.

Yeyote atakayethibitika kuhusika na vitendo hivi atahesabika kuwa ametenda kosa la rushwa kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

✓ADHABU:
Adhabu yake ni faini isiyopungua milioni moja (1,000,000/=) na isiyozidi Shilingi milioni tatu (3,000,000/=) au Kifungo kisichopungua miaka mitatu (3) na kisichozidi miaka mitano (5) au faini na kifungo vyote kwa pamoja.
•Mbali na adhabu hii, pia mahakama inaweza kuamua yafuatayo.
(i) Kumwamuru mtuhumiwa kumlipa mtu au mwajiri wake kiasi
chote au nusu ya pesa au mali aliyopewa rushwa
au
(ii) Kutaifisha pesa au mali iliyopokelewa kama rushwa na kuwa mali ya serikali.
Kufahamu zaidi juu ya kosa hili hunabudi kusoma kifungu cha 16(1),(2),(3)&(4) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Rushwa ni adui wa haki. Jukumu la Kuzuia na Kupambana na rushwa ni letu sote mimi, wewe na yule.

Ahsante kwa kusoma makala hii, niombe tuwe pamoja katika sehemu inayofuata ili kufahamu zaidi makosa ya rushwa na adhabu zake.

It's me
Mr George Francis
Email: mr.georgefrancis21@gmail.com
 

Attachments

  • FB_IMG_1675433189260.jpg
    FB_IMG_1675433189260.jpg
    21.9 KB · Views: 17
FAHAMU KUHUSU MAKOSA YA RUSHWA NA ADHABU ZAKE KWA MUJIBU WA SHERIA.

SEHEMU YA PILI (2)

mr.georgefrancis21@gmail.com.

Karibu tuendelee kupata elimu kuhusu makosa ya rushwa na adhabu zake kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa. The Prevention and Combating of Corruption Act, [CAP. 329 RE: 2022]

Katika makala iliyopita tuliangalia makosa mawili. Leo tunaendelea na makosa mengine kama ifuatavyo;

3. Vitendo vya rushwa katika ununuzi. Kwa mujibu wa kifungu cha 17(1)(a)&(b) cha sheria ya Kuzuia na Kupambana Rushwa ni kosa kutoa au kupokea rushwa ili kumpendelea mtoa rushwa au kufanikisha kupata tenda katika ununuzi wa mali au huduma katika idara ya serikali, shirika la umma au taasisi binafsi.

✓ADHABU:

Mtu yeyote anayekutwa na hatia ya kutenda kosa hili atawajibika kulipa faini isiyozidi shilingi milioni kumi na tano (15,000,000/=) au kifungo kisichozidi miaka saba (7) au faini na kifungo vyote kwa pamoja kama ilivyo kwa mujibu wa kifungu cha 17(2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
•Pamoja na adhabu hii lakini pia Mahakama kwa mujibu wa kifungu cha 17(3) (a)(i)&(ii) &(b) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, inaweza kuamua yafuatayo.
(a). Kumwamuru mtuhumiwa kumlipa mtu au mwajiri wake kiasi chote au nusu ya pesa au mali iliyopokelewa kama rushwa.
au
(b). Kutaifisha pesa au mali iliyopokelewa kama rushwa na kuwa mali ya serikali.

4. Vitendo vya rushwa katika minada. Kwa mujibu wa kifungu cha 18(1)(a)&(b) cha Sheria tajwa katika mada hii, ni kosa kutoa au kupokea rushwa ili kufanyika kwa upendeleo katika mnada wowote unaoendeshwa na au kwa niaba ya taasisi ya umma (serikali) au taasisi binafsi.

✓ADHABU:

Mtu anayekutwa na hatia ya kutenda kosa hili adhabu yake ni faini isiyozidi shilingi milioni kumi na tano (15,000,000/=) au kifungo kisichozidi miaka saba (7) au faini na kifungo vyote kwa pamoja kama ilivyo kwa mujibu wa kifungu cha 18(2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

•Pamoja na adhabu hii pia Mahakama kwa mujibu wa kifungu cha 18 (3)(a)(i)&(ii) & (b) cha sheria tajwa katika mada hii, inaweza kufanya yafuatayo;

(a). Kumwamuru mtuhumiwa kumlipa mtu au mwajiri wake kiasi chote au nusu ya pesa au mali iliyopokelewa kama rushwa.
au
(b). Kutaifisha pesa au mali iliyopokelewa kama rushwa na kuwa mali ya serikali.

5. Vitendo vya rushwa katika utoaji wa ajira.
Kwa mujibu wa kifungu cha 20(1)&(2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, kitendo cha kutoa au kupokea rushwa ili kufanyika kwa katika suala lolote linalohusu mtu kupata ajira, kupandishwa cheo au jambo lolote linalohusiana na ajira atakuwa ametenda kosa la rushwa.

✓ADHABU:
Mtu yeyote anayekutwa na hatia ya kutenda kosa hili adhabu yake ni faini isiyozidi shilingi milioni tano (5,000,000/=) au kifungo kisichozidi miaka mitatu au vyote kwa pamoja.

6. Vitendo vya rushwa na maafisa wa mashirika ya kigeni. Kwa mujibu wa kifungu cha 21(1) &(2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, kutoa au kupokea rushwa ili kufanya upendeleo kwa maafisa wa mashirika ya kigeni ili kufanikisha kutenda au kuacha kutimiza majukumu yao vile isivyo halali ni kosa kwa mujibu wa sheria.

✓ADHABU:
Yeyote anayekutwa na hatia ya kutenda kosa hili adhabu yake ni faini isiyozidi shilingi milioni kumi (10,000,000/=) au kifungo kisichozidi miaka saba (7) au vyote kwa pamoja.

7. Kutumia nyaraka kwa lengo la kufanya udanganyifu. Kwa mujibu wa kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, ni kosa la rushwa kutumia nyaraka kwa lengo la kudanganya na kujipatia fedha, mali au faida fulani vile isivyo halali.

✓ADHABU:
Ukikutwa na hatia ya kutenda kosa hili adhabu yake ni faini isiyozidi shilingi milioni saba (7,000,000/=) au kifungo kisichozidi miaka mitano (5) au vyote kwa pamoja.

NB: Kataa kutoa au kupokea rushwa ushwa ili kupata au kutoa upendeleo wowote kwa mtu yeyote. Rushwa ni adui wa maendeleo.

Tukutane kuendelea na mada hii katika sehemu inayofuata.

NAME: Mr George Francis
EMAIL: mr.georgefrancis21@gmail.com
 

Attachments

  • FB_IMG_1675433189260.jpg
    FB_IMG_1675433189260.jpg
    21.9 KB · Views: 11
FAHAMU KUHUSU MAKOSA YA RUSHWA NA ADHABU ZAKE KWA MUJIBU WA SHERIA.

SEHEMU YA TATU (3)

mr.georgefrancis21@gmail.com

Sehemu iliyopita tuliishia katika kosa la kutumia nyaraka kwa lengo la kufanya udanganyifu. Leo tunaendelea na makosa mengine ya rushwa na adhabu zake kwa mujibu wa sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Nayo ni kama haya yafuatayo;
8. Kujipatia faida au kumpatia faida mtu mwingine vile isivyo halali huku mpokeaji wa faida hiyo akijua fika kwamba atatoa maamuzi fulani katika jambo linalomhusu mtoaji wa faida hiyo. Jambo ambalo lina uhusiano na majukumu yake ya kiofisi au afisa mwingine wa chini yake.

✓ADHABU:
Mtu yeyote anayekutwa na hatia ya kutenda kosa hili adhabu yake ni faini isiyozidi shilingi milioni kumi (10,000,000/=) au kifungo kisichozidi miaka saba (7) au vyote kwa pamoja.
•Pamoja na adhabu hii lakini pia Mahakama inaweza kuamua kuwa fedha au vitu vilivyopokelewa na mtuhumiwa kuwa mali ya serikali.

Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 23(1)(a)(b) &(2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.

✓Lakini pia fedha au mali ikipokelewa kwa niaba ya mtuhumiwa, na mtuhumiwa akawa anajua kuwa kuna mtu amechukua fedha au mali kwa niaba yake inatosha kabisa kwa mtuhumiwa huyo kuwa na hatia ya kutenda kosa la rushwa.

Mahakama ikijiridhisha kuwepo kwa uhusiano au vinginevyo kulingana na majukumu yao ya kazi kati ya aliyepokea kwa niaba na huyo aliyepokelewa kwa niaba, faida hiyo itachukuliwa kuwa imepokelewa kwa niaba ya mtuhumiwa huyo hivyo kuwa na hatia ya kutenda kosa hilo la rushwa. Hii ni Kwa mujibu wa kifungu cha 24 cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

9. Rushwa ya ngono. Mtu yeyote aliye na mamlaka au madaraka akitumia mamlaka hayo kwa kumlazimisha au kumshawishi mtu mwingine kufanya naye tendo la ngono kwa ahadi ya kumpatia ajira, kumpandisha cheo, haki au upendeleo wa aina yoyote atakuwa anatenda kosa la rushwa.

✓ADHABU:
Mtu yeyote anayekutwa na hatia ya kutenda kosa hili adhabu yake ni faini isiyozidi shilingi milioni tano (5,000,000/=) au kifungo kisichozidi miaka mitatu (3) au vyote kwa pamoja. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

NB. Aina hii ya rushwa imekuwa ikipigiwa kelele malakwamala lakini bado watu wenye mamlaka hasa vyuoni au makazini wamekuwa wakiitumia sana kama fimbo ya kukidhi haja au matamanio ya miili yao.
Hali inayopelekea kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya UKIMWI na mimba zisizotarajiwa. Usikubali kuweka afya yako hatarini ama kushusha thamani au utu wako kwaajili tu ya kupata au kutoa upendeleo. NI HATARI.

10. Kukataa kutoa taarifa au Kutoa taarifa za uongo

Mtumishi wa umma ambaye amekataa kutoa maelezo au ametoa maelezo ya uongo kwa afisa wa TAKUKURU aliyekuja kufanya uchunguzi kuhusiana na mali au kiwango cha pesa alizonazo na namna alivyozipata mali au pesa hizo atakuwa ametenda kosa. Kwa mujibu wa kifungu hiki, hii inahusisha mali anazomiliki mtumishi wa umma mwenyewe au zile zinazomilikiwa na mtu wa familia yake kama vile mume, mke au mtoto wake.

✓ADHABU:
Mtumishi wa umma atakayekutwa na hatia ya kutenda kosa hili adhabu yake ni faini isiyozidi shilingi milioni tano (5,000,000/=) au kifungo kisichozidi miaka mitatu (3) au vyote kwa pamoja. Soma kifungu cha 26(1)(2)(3)(4)& (5) kuongeza maarifa zaidi kuhusiana na kosa hili.

Ahsante kwa kuendelea kufuatilia mada hii. Tukutane kuendelea na sehemu inayofuata ya mada hii.

Rushwa ni adui wa haki, rushwa ni adui wa maendeleo.

NAME: Mr George Francis
EMAIL: mr.georgefrancis21@gmail.com
 
Mwalimu Nyerere katika hotuba aliyoitoa kwa waandishi wa habari mwaka 1995 alisema,
“Kwa hivyo, tukatengeneza sheria ili tuwafundishe watu hawa kwamba jambo hili hatulipendi. Ikisha kuthibitika mahakamani kwamba kala rushwa hatukumwachia hakimu uamuzi wa adhabu. Tukasema atakwenda ndani muda usiopungua miaka miwili, atapata viboko ishirini na vinne, kumi na mbili siku anayoingia, kumi na mbili siku anayotoka”
Wakati wenzenu wanawaua na kuwanyonga wala rushwa nyie mnawafunga miaka miwili? Serious mnataka kutokomeza rushwa?
Big no kwa adhabu hizi
 
Back
Top Bottom