SEHEMU YA NNE
Walipoingia katika selo zao Pocha akafanya kama alivyoagizwa...
Chopa akawabana watu wale huku akiwaeleza kuwa yeye ni mtu wa usalama wa taifa hivyo ikitokea ameondoka pale ndani wakijifanya kumsumbua Pocha watakiona cha mtema kuni......
Aliwabana katika maana halisi ya kuwatia adabu!!
Ikawa giza na kulipopambazuka alikuwa ni Chopa aliyetolewa gerezani, na hakuna aliyejua wapi amepelekwa!!
Kitendo kile kikamfanya Pocha ajiulize mara mbilimbili juu ya uhusiano wa akili yake na mikono yake.
Na ni vipi atumie uhusiano huu katika kujiweka katika hali nyingine ya kimaisha!!
Akaamua kulishughulikia hilo jambo.
Majuma mawili baadaye akapambana aweze kuonana na mkuu wa gereza!!!
Akafanikiwa kuonana naye akamuelezea alichopanga kumweleza akiamini kuwa kitakuwa na manufaa kwa upande wake............
______
KWANZA ilianza simu ya mkononi, iliita kwa muda mrefu kiasi. Mwenye simu akaitazama katika kijicho cha kuchungulia kana kwamba anaepusha kumtambua ni nani aliyepiga ile simu. Ilikuwa kama alivyodhani mpiga simu alikuwa yuleyule asiyetaka kuipokea simu yake. Haikuwa kwa sababu ya madeni ama ubaya wowote lakini nafsi ilikuwa ina mashaka labda kuna lolote baya limefichuka tayari.
Baada ya simu ya mkononi kuacha kupokelewa simu ya mezani ilianza kuita. Ilikuwa nambari ileile inampigia.
“Prisca!! aliita kwa sauti ya wastani na baada ya sekunde kadhaa mbele yake alikuwa amesimama msichana aliyevalia nadhifu!
“Bee muheshimiwa!! Yule binti aliitikia wito.
“Pokea hii simu mwambie kuwa nipo katika kikao tangu asubuhi sijarejea ofisini....” alitoa maelekezo yale kivivu kabisa.
Yule binti alitii, lakini alipoufikia mkonga ana kutaka kuunyanyua simu ilikuwa imekatika tayari.
“Naona amekata!” alijieleza Prisca.
“Ok! Namba ya dada wa Airport si unayo, mwambie anifanyie utaratibu wa tiketi ya kwenda London baada ya masaa arobaini na nane mwambie azingatie sana na isishindikane!! Nenda ukawasiliane naye sasa hivi, mimi natoka... nitakachochukua kwako ni tiketi na sio maneno” alizungumza kwa ukali kiasi wakati huo anasimama.
“Mh! Bosi wangu huyo safari zaidi ya raisi wake!!” Prisca alisema kiutani huku akitabasamu, hii haikuwa mara yake ya kwanza kumtania bosi wake huyo.
“Whaat! Mpumbavu nini, tangu lini umeanza kazi ya kunipangia safari, nakuuliza we binti nilikuajiri hapa kuanza kunihesabuia mara ngapi au kutimiza yale ninayokuagiza... shwain kabisa....kwa hiyo mi nikisafiri kuliko raisi wangu inakuumiza nini, ul;itaka usafiri wewe au.. haya basi kuwa mbunge mimi niwe sekretari wako... hovyo kabisa... nipishe hebu nipite.. pishaa!! Mambo ya Lucas naomba umuachie Lucas mwenyewe bastard!!” alibwatuka muheshimiwa mbunge akimuacha katibu muhtasi wake akiwa haamini anachokiona mbele yake na kukisikia, hii ilikuwa mara ya kwanza kabisa kwa bosi wake huyo kumfokea na kumtukana namna hii. Bosi huyu alikuwa mtani wake sana.
Muheshimiwa Lucas Kazioba alipiga hatua kubwa kubwa akatoka nje akiwa amebeba koti lake la suti. Alipofikia gari lake akaanza kujipekua huku na kule huku akizungumza peke yake.
Alipekua kila kona, na mara akapata wazo kuwa huenda anachokisaka kwa fujo zote hizo amekisahau ofisinii ile anageuka ili arudi anamuona Prisca akijongea kwa hekima zote na adabu kumuendea akiwa amezishikilia funguo za gari za bosi wake.
Fadhaiko likamuandama muheshimiwa akajisikia vibaya sana kwa maneno aliyomuambia binti yule lakini bado binti hakuweka kinyongo akatambua kuwa amezisahau funguo akampelekea.
“Prisca... nisamehe mama yangu, nimevurugwa kupita maelezo nadhani unanijua si mtu wa kutukana na kufoka kama nilivyofanya nakuomba sana unisamehe....” Lucas aliyasema yale huku aibu zikiyatawala macho yake, lakini pia sauti yake ilikuwa imechoka sana. Bila shaka kuna jambo zito lilikuwa linamkabiri.
“Usijali muheshimiwa Lucas, sisi ni wanadamu na kamwe siku huwa hazilingani...nimelielewa hilo na nimeyasahau yote palepale. As long as hujanipunguza mshahara basi yote yaliyobaki huenda nilistahili...” Prisca alijibu huku akijilazimisha kutabasamu.
Maneno ya Prisca yakamchoma Mh. Lucas, na sasa hakutaka kuomba tena msamaha kwa maneno, akamsihi Prisca asubiri kidogo. Akafungua gari lake na kunyofoa bahasha moja ya rangi ya dhahabu!!
“Pokea hii.... haina maana yoyote mbaya nimejisikia tu. Hii itakusaidia kuwa maikini wakati unazungumza na dada wa airport kuhusu tiketi yangu, si unajua wanavyokera watu wa airport... sasa hii ni kinga ya kutokwazika. Basi baadaye!!” akapanda kwenye gari bila kusubiri asante ya prisca!!
Lucas alipoondoka upesi Prisca akaifungua ile bahasha, akahesabu zile pesa kana kwamba anahakikisha wakati hakutajiwa kiasi sahihi ni ngapi.....
Ilikuwa mshahara wake wa miezi miwili, shilingi laki tisa!!
Prisca alisahau kabisa kama alitukanwa na bosi wake.
Amakweli pesa sabuni ya roho!!
Lakini Prisca alikuwa wa tofauti kidogo, licha ya pesa zile kumsahaulisha matusi ya bosi, lakini kile kitendo cha bosi kuitaka safari ile ya haraka huku akiwa amepagawa hakukipuuzia hata kidogo alihisi kuna jambo zito linamkabili bosi wake.
Umbea ni kama rangi ya ngozi jama unaweza kujifanya umeuacha lakini likitokea tukio la kuhusu umbe utajikurta umeshiriki tu!!!
Prisca hakuiacha asili yake!!
Akairejea fani yake!!!
Laiti kama angeikumbuka ile kauli ya umbea hauna posho abadani asingejihusisha tena na umbea.... lakini hakuukumbuka usemi ule.
Ni kawaida ya vijana wa kisasa kuwapuuzia wahenga!!!
Prisca naye alikuwa kijana.
_______
Desemba, 2013
Mara, Mugumu Serengeti
__MTU HURU__
Lango la gereza lilifunguliwa, takribani mwaka mzima uliopita lango lile lilipofunguliwa yeye na wenzake walikuwa wameveshwa bangili zisizopendeza machoni kuzitazama na usiombee kuzivaa.
Walikuwa wameunganishwa kwa pingu, na kama si pingu basi walikuwa wamewekwa katika karandinga huku ulinzi ukiwa mkubwa sana.
Lakini siku hii alikuwa huru kabisa, alisindikizwa hadi getini, hapo alikuwa amekabidhiwa pesa kiasi sawa na ujira wake kwa kulitumikia gereza. Akapewa na ziada ya usafiri kwa sababu hapo awali alihamishwa kutoka gereza la Ukonga Dar es salaama kabla ya kupelekwa Kiomboi Singida na hatimaye gereza la mahabusu la Mugumu Serengeti!!
Gereza pekee katika wilaya ile.
Alipiga hatua kama sita kisha akapiga goti chini akainama akainyanyua mikono yake juu akaanza kumshukuru Mungu huku akilia kilio kikuu kwa sauti ya chini kiasi lakini machozi yakibubujika kwa kasi.
“Mungu! Mimi si mtiifu sana kwako, sikumbuki kama nimekutumikia kwa muda mrefu lakini kwa uweza wako wewe nipo hai na huru leo... ninayo mengi ya kukushukuru lakini naomba nikukabidhi kwako wenzako waliobaki katika gereza hili moja kati ya magereza mabovu niliyowahi kuyashuhudia katika mapito yangu, Baba iamshe serikali ifike huku na kuuimarisha ukuta wa gereza hili kabla haujawaangukia waja wako, waamshe wabunge waje kutazama huu mrundikano katika gereza, waamshe wanasheria waje kuwatetea waliofungwa kimakosa ama kwa kuonewa.... na kuu la msingi baba nipunguzie hii hasira ama la kam,a hii hasira haitafutika katika moyo wangu, naomba unisamehe baba kwa sababu sitatulia kabla ya kumtafuta yeyote yule aliyehusika katika mpango huu.... mpango wa kunipotezea dira ya maisha yangu.....”
Alikaa kimya akiwa ametulia pale chini kwa muda akiamini kuna wapiti njia kadhaa wanamshangaa lakini hilo halikumuumiza kichwa.
Akasimama hatimaye hakujihangaisha kujifuta vumbi!!
Akageuka kulitazama lango la gereza ambalo lilikuwa limefungwa tayari. Akatikisa kichwa na kulazimisha tabasamu, alipopiga hatua nyingine mbele akajisemea.
“Asante raisi kwa msamaha huu kabla ya kukimaliza kifungo changu, najua sikustahili wapo waliostahili kusamehewa..... ila asante”
Akamaliza na kujifuta machozi kisha akapiga hatua kuelekea popote anapoweza kuelekea.
“Babaa... baba!” alisikia sauti ya mwanamke ikimuita.
“Tacho hano mona wane.. tacho ulaghere! Weii mona wane....” mwanamke yule alizungumza kikabila.... yule mtu huru hakuelewa anachomaanisha lakini ishara ya mkono ni kama alikuiwa akimuita.
“Wewe ni wa huku kwetu...” yule mama alimuuliza huku akionyesgha huruma ya hali ya juu.
“Hapana mama..shkamoo, mimi si wa huku..”
“Aaah! Nilidhani ni mkurya, nilikuita uje ule chakula mtoto wangu, aaah! Ona walivyokuchubua chubua....aaah! gereza hili gerezaaa lilimmeza mtoto wangu wakampiga akafia huko eti kisa alimtukana balozi... aaargh!” mama akashindwa kuzungumza akaanza kutokwa machozi.
Na wakati huohuo akaifungua chupa ya maziwa ambayo alikuwa anauza kama biashara akammiminia mtu huru. Yule bwana akapokea na kunywa, maziwa yale yalimchangamsha na kumtia nguvu.
“Unaitwa nani?” alimuuliza wakati anamalizia kunywa yale maziwa.
“Naitwa Manfred Gregory!!”
“Mnifureti!!” alijari8bu kutaja jina lile yule mama... lafudhi ya kikurya ilikuwa ikimsumbua.
“Niite CHOPA!!” mtu huru akabadilisha jina ili kumrahisishia yule mama.
“Chopa.. eeh! Pore mwanangu, sasa usiangarie nyuma usitazame sijui nani alikuweka ndani sijui nani alikudhurumu haki yako we kapambane na maisha tu. Yariyotokea uyasahau sawa mwanangu!!” mama alimsihi Chopa.
Chopa akakubaliana na yule mama ambaye ‘R’ na ‘L’ zilikuwa tatizo kwake.
Akamshukuru kwa maziwa kisha akaondoka, akatembea hadi alipoipata nyumba ya kulala wageni!!
Akaipata ya bei ya kawaida akaingia humo. Akaoga tena kwa mara nyingine, hapo awali alioga gerezani kabla ya kutoka rasmi!!
Wakati anaoga akawa anakumbuka juu ya siku yake ya mwisho uraiani!
Siku aliyokamatwa na kisha kutupwa gerezani akisomewa shtaka la kughushi vyeti feki na kujipatia kazi asiyostahili hivyo alikuwa anashtakiwa na jamuhuri ya muungano wa Tanzania.
Kesi hii ilimfanya asite kidogo kuoga, akaanza kuzungumza peke yake.
“Yaani mimi nimeishia kidato cha nne, nikapata daraja la pili, halafu anatokea mtu anasema nimeghushi vyeti?? Kazi yenyewe bora ingekuwa inaingiza milioni nyingi, yaani kazi ya mshahara laki na nusu chakula na usafiri juu yangu, anakuja mtu ananipeleka gerezani... hivi hii ni haki?? Eeh! Ni haki hii?” alijiuliza mwenyewe.
Alipomaliza kuoga akakiendea kioo kikubwa kilichokuwa kimebandikwa ukutani.
Hapa ndipo Chopa alilia kama mtoto tena..
Mwili wake ulikuwa na mabakamabaka, ngozi yake ilikuwa hovyo kabisa, akageuka na kujitazama mgongoni.
Ilitisha sana hali aliyokuwanayo, mfanowe ngozi yqa punda aliyebebeshwa mzigo kwa muda mrefu akachubuka na kuacha jeraha na mwenye punda asijali hayo akaendelea kumbebesha mizigo.
Chopa alilia sana na hii hali aliyoitazama kwa macho yake mwenyewe ikamfanya azidi kuifikiria kesi yake.
Na hapo akazikumbuka tena zile jumbe alizotumiwa kabla ya kuingia gerezani.
Akaukumbuka ujumbe wa kwanza.
“SIKU ZAKO ZINAHESABIKA SI UNAJIFANYA MJUAJI! TUTAONA MJUAJI NANI KATI YA MTU HURU NA ANAYEENDA KUUPOTEZA UHURU.”
Huu ulikuwa ujumbe wa kwanza siku ile asubuhi, ujumbe alioupuuzia kwa kuamini kuwa umekosea njia.
Chopa alihangaisha sana kichwa chake, akawafikiria ndugu zake. Eti hakuna hata mmoja aliyefika gerezani kumjulia hali.....
Akamfikiria Caro mchumba wake, eti na yeye kwa miaka hiyo miwili hakuwahi kwenda japo kumsalimia!!
Kichwa kilimuuma sana alipoyafikiria haya, kujiepusha na haya akajirusha kitandani. Godoro laini lisilokuwa na hiyana likampokea, akalivuta shuka na kujifunika.
Nadhani haitakiwi kuendelea kusimulia kilichotokea!
Miaika miwili hujalalia godoro lililo katika mazingira mazuri halafu unajikuta eneo kama hilo......
Zilihitajika kelele za milio ya risasi kumwamsha mtu huru huyu, Chopa!
Wakati Chopa analala usingizi wa samaki aitwaye Pono....
Mahali pengine nchini Tanzania kulikuwa na majadiliano mazito!
Kuna mtu huru mwingine alikuwa anaongezeka!
______