Makapuku Forum

Makapuku Forum

SEHEMU YA KUMI NA SITA
SEHEMU YA KUMI NA SITA


Mwenye nyumba alilazimika kutushangaa tu asijue nini kinatusibu, ni kama tulikuwa tumechanganyikiwa vile. Mzee yule akiwa na koti lake kubwa aliganda mlangoni akitutazama.
“Mna nini kwani vijana wangu, eeh Jojina ni nini kwani?” hatimaye aliuliza.
Jojina akamtazama kwa jicho linaloashiria kukata tamaa akataka kusema neno lakini akaishia kufungua kinywa tu na lisitoke neno lol.ote lile. Baridi ilikuwa kali na kiza kilikuwa kimetanda. Nilitamani kumweleza mwenye nyumba juu ya hofu yetu lakini nikahamisha na kuuliza swali.
“Kwani wamekuja lini hawa watu!!”
“Le asubuhi tu!! Yaani hata majirani watakuwa hawajasahau, yaani saa nne hivi walikuwa hapa. Mbona wastaarabu sana ndugu zako wale mi sidhani kama wanaweza kuwa wamekufanyia kitu kibaya!!”
“Ndugu zangu wapi mzee, umewahi kuona nimekutambulisha ndugu yangu hata mmoja hapa tangu mzee wangu yule marehemu, sina ndugu ni vibaka tu hao hawana lolote…vibaka kabisa!!” alilalamika Jojina huku akipigapiga mikono katika ardhi na miguu akiirusha huku na kule. Alikuwa amevurugwa sana na jambo lile.
Nikamsogelea na kumnong’oneza, “Hapa si mahali sahihi hata kidogo. Kama walikuja hapa asubuhi basi wanaweza kurudi muda wowote ule nakwambia. Hawa si vibaka watakuwa nd’o hao akina anti Ezekiel.”
Jojina akatumbua macho yake, huenda hakuwahi kuwaza jambo kama lile. Akasimama wima. Wakati anasimama mzee naye alikuwa ameuacha mlanngo na kupiga hatua zaidi mbele.
“Sasa vibaka gani hao wa kuacha makochi, kabati na kila kitu cha thamani na kuchukua sijui picha ganigani hizo Jojina, kweli nd’o vibaka walivyo!!” alizungumza kwa sauti ya chini katika namna ya kusihi.
Suala la vitu walivyoiba likazua mjadala upya na ni hapo ambapo Jojina aliungana nami kuamini kuwa wale hawakuwa vibaka bali ni watu wanaotutambua vyema na kuna kitu walikuwa wanatafuta. Kipi zaidi ya picha za Dulla!!!
La!! Si picha ya Dulla pekee na bahasha!! Bahasha yenye picha na nakala nyingi ambazo bado ni fumbo.
Bahasha yenye ufunguo uliochakaa!!
Nikasimama wima baada ya kukumbuka vitu hivyo, na hapo nikamuuliza yule baba mwenye nyumba.
“Na kitanda wameacha?”
“Hawajachukua kitu zaidi ya hizo picha na makaratasi mengine!!” alinijibu huku akituona kama watu ambao tuna wazimu vichwani mwetu.
Sisi hatukujali, na wakati huo Jojina naye alikuwa amesimama. Akaomba chumba kifunguliwe, baba mwenye nyumba akataka kugoma Jojina akamgeuzia jicho nkatika namna ya kutangaza shari. Akaingia ndani na kurejea na funguo.
Akatukabidhi tukaondoka kuelekea kule chumbani, ni upande ule pia ilikuwepo stoo ambayo alidai kuwa baadhi ya vitu vya Jojina vilihifadhiwa mle.
Jojina akaingia chumbani mimi nikazama stooni, kila mmoja akitafuta bahasha nachochote kile kingine ambacho kitaweza kutusaidia katika kufanikisha azma yetu ya ukombozi.
Giza lilikuwa linatusumbua kuweza kuona vitu barabara, lakini tulilazimika hivyohivyo. Nilivuta makochi huku na kule, nikavuta vyombo na chochote ambacho nilihisi kingeweza kunisaidia mbele ya safari.
Lile giza ambalo tulikuwa tunalichukia mara lilitoweka ghafla, lakini si kwamba ulikuwa ni umeme umewaka la! Hapakuwa na kibatari wala mshumaa na hata taa za kandili hazikuwa jirani.
Nikautafakari ule mwanga!! Nikajivuta hadi dirishani na kutazama miale yake inapoanzia.
Ama!! Zilikuwa ni taa za gari. Tena si gari moja, zilikuwa gari mbili.
Nikajisogeza dirishani zaidi katika nondo niweze kutambua zile gari usiku ule wa manane zinataka kitu gani maeneo yale.
Nani angenieleza? Hakuwepo!!
Vinginevyo nitoke nje na kujisogeza eneo lile. Jambo ambalo sikuwa tayari hata kidogo kulifanya.
Mara nikasikia kishindo nisijue kinatoka wapi. Mhanga wa nyoka akigusana na ujani…….hiyo inajulikana. Nikaanza kuingiwa hofu nisijue ni kitu gani nahofia.
Mara ghafla kiza cha awali lakini cha sasa kikiwa kinene zaidi kwa sababu nilikuwa nimeathirika na ule mwanga.
Nikatamani sana ule mwanga ungeendelea kidogo maana nilikuwa nimeona kitu cha rangi ya kaki. Ni kama bahasha vile.
Nikajiundia matazamio ya wapi nilipokiona, mithili ya mtu asiyeweza kuona nikaanza kupiga hatua moja baada ya nyingi nikipapasa huku na kule huenda ile ingeweza kuwa bahati kuu zaidi kupata kutokea.
Nikapapasa vibaya nikatengua vyombo kutoka katika beseni, zaikazuka fujo!! Nikajikinga, bahati nzuri sikudhurika, nikaendelea mbele, nikapapasa tena huku na kule, wakati huu ikawa safari ya viti kuporomoka, katika kujikinga na kuruka huku na kule nikaparamia kochi na kuanguka chini. Viti kadhaa vikatua juu yangu.
Nikajikaza sikupiga mayowe, nikaanza kufanya jitihada za kujinyofoa kutoka katika hali ile. Lakini haikuwa rahisi, nikiwa nimesahau kabisa juu ya kishindo cha kwanza nikasikia kishindo cha pili, mara cha tau na cha nne. Vishindo vilikuwa vinajongea kuja katika chumba kile.
Mungu wangu!! Nikapagawa na kuanza kujinyofoa kwa pupa. Hali hii haikusaidia.
Nikiwa bado katika sintofahamu, mara nikaona mwanga mdogo kutokea dirishani, na ili kunidhibiti nisitokwe na mayowe nikasikia sauti ya chini kabisa ikinong’ona.
“Wamekuja mabwege, wako wengi kweli wamembana baba mwenye nyuma huko, tokea dirishani usirudi nyuma wanaua wale.” Ilikuwa sauti ya Jojina.
“Joji…Jojina…nimebanwa na makochi nisaidie nipo huku chini.” Nililia kwa uchungu uliochanganyika na uoga, na mara nikakatisha kauli yangu, jicho langu liliiona bahasha ile iliyonipelekea kubanwa na makochi yale.
“JItahidi u..” sikumwacha amalizie.
“Jojina bahasha hii hapa…..hii hapa Jojina.” Nilimsihi wakati huo vishindo vikizidi kusogea na sauti ya baba mwenye nyumba ikisikika ikilia.
Niliukaza mkono wangu nikajitahidi hatimaye nikaishika ile bahasha. Nikaanza kuivuta mara nikawasikia wakiwa wamefika.
Nikajikuta nachagua moja tu!!
Jojina aipate bahasha kama wataniua mimi yeye atausaka ukweli. Nikatumia nguvu zangu za mwisho nikajinyanyua kwa uchungu mkubwa viti vikaparanganyika, nikainyofoa bahasha nikairusha dirishana, niliuona mkono wa Jojina ukiidaka vyema, na hapo kochi kubwa likatua vyema usawa wa paja langu na kunikandamiza vyema.
Hapa sikuweza kujizuia nikatokwa na yowe la uchungu!!
Mara miale mikali ikanimulika machoni, matusi makali makali ya nguoni yakafuata baada ya hapo.
“Huyu ni nani ulisema hajaja mtu kimburu wewe!!” sauti hii iliambatana na kilio kutoka kwa baba mwenye nyumba.
Ulikuwa msala wa aina yake!!
Tochi ziliwashwa na kuzimwa katika macho yangu hivyo kunivuruga nisiweze kuona chochote kile.
“Kill him!!” nikaisikia sauti nyingine ikiamrisha kwa ghadhabu. Nafsi yangu ikakubali kwa shingo upande kuwa sikuwa na namna cha muhimu ni kumwombea Jojina aweze kunitendea haki huku nyuma na hatimaye nizikwe kwa heshima zote kama mpigania ukombozi.
Ukombozi nisioujua hadi nakufa!! Iliniuma sana.
Mara wale watu wakavamia mle ndani, wakaanza kupangua vitu kwa harakaharaka, hata walipofanikiwa kunifikia hakika nilikuwa hoi.
Lakini hawakujali, wakanikwapua na kunirusha nje.
“Samson… Samson!!!” niliisikia sauti ikiniita, nikajaribu kutazama nikakutana nna mwanga wa tochi, sikumtambua ni nani. Lakini alijawa na dharau wakati akilitaja jina langu. Bila shaka alinijua vyema, nikiwa nahaha huku na kule mara kiatu kikatua katika upande wa nyuma wa shingo yangu na uso ukajivuta kwa nguvu kisha ukatua katika ardhi, maumivu yakatambaa mwili mzima nikaishia tu kutoa mguno wa maumivu. Nilipojilamba pembezoni mwa midomo yangu nikaipata ladha ya chumvi, nilitambua kuwa natokwa damu, lakini kabla sijatulia vyema nikasikia kiatu kikiisambaza pua yangu!!
Naam!! Damu zikaanza kuchuruzika na maumivu makali yakanifanya nilie kama mtoto!!
“Jack eeh hebu msake huyu Malaya lazima wapo wote wajinga hawa” aliamrisha na pale wakatoweka wanaume wawili, niliweza kuona miguu yao.” Nilianza kupatwa na mashaka walipoondoka na kuelekea ule usawa ambao Jojina alikuwa. Nikaendelea kuugulia maumivu pale chini. Sasa nilikuwa nikilindwa na wanaume wawili. Hawakusema lolote na mimi, bila shaka walingoja watuunganishe wote pamoja na Jojina waweze kutuadhibu. Adhabu gani nyingine kama si kuuwawa?
Ile hali ya kuamini kuwa baada ya muda mfupi nitakuwa maiti iliniathiri sana, donge la hasira likanikaba na nikahisi machungu ya kuonewa yakilidondosha chozi langu kutoka katika maficho ya macho yangu.
Nauwawa kabla sijaonana na mke wangu na mbaya zaidi kabla sijaonana na Anitha, sijaonana na Eva mwanangu pekee.
Nikalegea na kuikumbatia ardhi nikiisihi iwapo ina uwezo wowote kwa wakati ule na inisaidie niepukane na uonevu ule.
Lakini ardhi haikunisikia vyema, ikazidi kuimeza damu iliyokuwa ikinitoka puani. Mgongo ulikuwa unauma na kiuno vilevile. Niligeuka kumtazama baba mwenye nyumba, mwanga wa zile tochi ukanisaidia kumwona jinsi kinywa chake kilivyosambaratishwa vibaya, taya ilikuwa imelegea na kuangukia upande wa kushoto, udenda uliochanganyikana na damu ulimiminika kutoka katika kinywa chake. Sikumtazama mara mbili licha ya kuonekana kama anayetaka kuniambia neno fulani.
Nilipougeuzia uso wangu upande mwingine nikakutana na kivuli kikubwa chenye umbo kama la mnyama.
Mara kile kivuli kikapiga hatua kubwa mbili na kisha kikapaa.
Kilipotua na jamaa mmoja kati ya wawili waliokuwa wakitulinda akaanguka chini na hapo kile kivuli kikatangaza uhai wake na ubabe uliopitiliza.
Kivuli kikabweka!!!
Lahaula!!! lilikuwa jibwa kubwa mithili wa yale majibwa ya polisi!!!
Nikageuka kumtazama baba mwenye nyumba alikuwa anajilazimisha kutabasamu. Nikastaajabu lakini nikahisi kuwa lazima kuna jambo linaendelea na yeye analijua.
Na hapo nikamsikia akitokwa na sauti kwa kujilazimisha, alijilazimisha kwa sababu kuu moja tu!!!
Sababu alitaka kujiokoa yeye na mimi pia.
“Simbaaa…..umaaa!!!!” alisema kisha akarudi chini na kutulia tuli!!!
Ebwana eeh!! Hivi kumbe mbwa wana hatari kiasi hicho. Yule bwanha aliyekuwa chini alijikuta akishambuliwa kwa kasi ya ajabu, yule mbwa alikuwa anajua nini maana ya kuuma!!
Dakika mbili zilitosha kumnyamazisha yule bwana.
Yule mwenzake aliyekuwa amesimama wima bado alianza kuhaha akiitisha ile mbwa kwa mawe, lakini haikutetereka. Alibahatika kuiponda kwa jiwe moja lakini kwa mara ya pili ilikuwa kazi bure.
Jibwa likajirusha na kung’ata shingo!!! Jamaa akaanguka chini, jibwa likaanza kumrarua kwa fujo.
Lilipohakikisha ametulia tuli likageuka na kutazamana ana kwa ana na mimi!! Hofu ikaanza!!!
Kauli ya kwamba ukilijua jina la mbwa basi hakutishi niliduwaa haikufanya kazi, niliita jina la Simba lakini mbwa yule alionekana kuwa mwenye hasira kali zaidi, aliunguruma kisha akaendelea kunisogelea. Mapigo ya moyo yakazidi kwenda kasi na amani ikatoweka tena.
Mara akaanza kubweka, nikafanya kosa kutishia kuwa naweza kupambana naye kwa kumtisha kama namfukuza. Jibwa likatanua kinywa na bila shaka alitaka kufanya shambulizi!!!
Nikaamini kuwa ng’ombe wa masikini hazai ni usemi sahihi kabisa. Nikakiona kifo tena mbele yangu. Nguvu nazo zilikuwa zimeniishia.

**UJUMBE! Kukata tamaa nd’o asili ya mwanadamu, hasahasa akishafanya jitihada zake binafsi pasi na kumshirikisha mtu!! Lakini je? Kukata tamaa ni suluhu ya kujikwamua kimaisha, ama kufanikiwa lolote lile?
Wanadamu wengi hushindwa kutimiza ndoto zao kwa sababu ya pepo hili la kukata tamaa.
Ili ufanikiwe katika maisha ni lazima ulishinde pepo la kukata tamaa lakini vinginevyo katika kila vita ulimwenguni wewe utakuwa wa KUSHINDWA TU!!
Utaishindwa vita ya kuupinga umasikini, utashindwa vita ya kudharauliwa na mwisho kabisa utashindwa vita kuu ya KUSHINDWA KUIONGOZA AKILI YAKO!!!
TAFAKARI!!
 
1468866126255.jpg
 
SEHEMU YA KUMI NA SABA
SEHEMU YA KUMI NA SABA

“Acha simba!!!” ikaamrisha sauti kali. Nikapepesa macho ili nijionee ni nani huyo!!
Na hapo akatokea MAMA LAO akiwa na tabasamu usoni na rungu kubwa mkononi!!
Alikuwa anatokwa damu mdomoni lakini hakuwa na kitu kinachoitwa wasiwasi tena, akaanza kutembea zaidi.
Alikuwa anachechemea!!
“Mama lao…” nikajikuta natokwa na sauti yenye kitetemeshi.
“Tuondoke hapa Sam. Wajinga wana mtandao mpana sana hawa. Simama Sam jikaze simama tupotee hapa.” Alinisihi Mama lao, lile jibwa lilibaki kutikisa mkia, bila shaka lilimjua vyema Jojina na mbwa akojuaye….
Hakuna kilichoharibika.
Nikajikaza nikasimama wima, mbwa huyu hakuwa na madhara tena kwangu ilhali Jojina alikuwa amemkaripia tayari.
Nikajikongoja huku nikiyasikia maumivu ya kiuno bado. Lakini ilikuwa heri maumivu haya kuliko kuuwawa kabla sijatimiza azma yangu.
Sikujua kama mwendo wangu ulikuwa mdogo kiasi cha kumkwaza Jojina, hakusema na hata angesema isingesaidia kuniongezea mwendo mgongo ulikuwa unauma sana, na si hivyo tu hata nilipojaribu kukimbia yale maumivu ya kinywa kilichopasuka yalisababisha kichwa kiwe katika maumivu makali sana. Jojina alinitazama kwa huruma huku akizidi kukaza mwendo.
Mara akasimama ghafla kisha akachuchumaa, nikamfikia nikiwa nashangaa.
“Panda mgongoni Sam… panda upesi” aliniamuru, ni kitu ambacho sikukitarajia hata kidogo lakini hakuwa na masihara hata kidogo, akarudia kauli yake safari hii kwa kuamrisha.
Nikajiweka mgongoni, Jojina akasimama kama kifaru akaanza kutimua mbio mimi nikiwa mgongoni. Usiku wa giza tukielekea anapopajua yeye. Niliyafumba macho yangu kukabiliana na uchungu niliokuwa nikiusikia. Kichwa kilikuwa kinauma haswa!! Lakini haukuwa wakati muafaka wa kulalamika.
Mama lao akaendelea kutimua mbio.
“Taksiii….Taksiiii msaada tafadhali mgonjwaaa!!” aliita kwa nguvu baada ya kuziona taksi kadhaa zikiwa zimeegeshwa.
Dereva moja akawahi upesi akaufungua mlango wa teksi yake. Hapo sasa nilikuwa nimefumbua macho nikishuhudia filamu hii ya aina yake.
“Tupeleke Stendi ya mabasi…” aliamuru Jojina na hapo nilikuwa siti ya nyuma na yeye akiwa pembeni yangu.
Dereva alibaki kuduwaa ni kama hakuwa akiamini kama tulikuwa na pesa ya kumlipa, Jojina akaling’amua hilo, upesi akajipekua na kutona na noti nyekundu akamlipa dereva.
Akatia gari moto tukatoweka…njia haikuwa mbaya sana hivyo wakati huu nilipata fursa ya kutambua kuwa kinywa kilipasuka japo si vibaya sana lakini shingo ilikuwa inauma sana bila shaka yule bwana aliyenipiga mateke.
Stendi haikuwa mbali, tukapewa pesa yetu iliyosalia na kutelemka, wakati huu nikijikongoja mwenyewe. Kila kitu katika suala la maamuzi nikamuachia Jojina maana walau yeye alikuwa na unafuu.
Sikujua alikuwa na maana gani usiku mnene kama ule kuamua safari ya kuja stendi lakini hakuniacha niumie akili kutafakari sana, mara akaita teksi nyingine.
“Tupeleke Gangilonga” akatajiwa bei akalipa.
Ukimya ukatawala kwa takribani dakika kumi na tano. Tukatelemka mahali ambao Jojina aliamua yeye.
Teksi ilipoondoka tukatembea kwa mwendo wa miguu hadi katika nyumba kubwa kiasi iliyozungukwa na majani mengi, bila shaka ni kutokana na watu kutoishi eneo lile kwa muda mrefu.
Jojina alivyofika pale geti lilikuwa limefungwa na hakushtuka ni kama kitu alichokitarajia.
Akachumpa ukutani akatua upande wa pili. Kisha akafungua geti dogo na kuniruhusu niingie ndani.
“Miezi sita sijakanyaga hapa aisee.” Alisema neno la kwanza tangu tufike pale. Sikuchangia chochote.
Akaniongoza hadi ndani, uzuri wa Iringa hakuna vumbi kali sana, badala yake vipindi vya baridi huchukua nafasi kubwa zaidi hivyo hapakuwa na madhara ya vumbi.
“Hapa hakuna umeme wala nini Sam.” Alizungumza tena, nikamuunga mkono kwa kumweleza kuwa hilo si tatizo cha muhimu usalama wetu.
Akapapasa huku na kule akaibuka na mshumaa, kisha akavuta kumbukumbu na kupapasa sehemu nyingine akaibuka na kiberiti na kisha kutengeneza mwanga hatimaye.
Nikaketi naye akaketi katika makochi chakavu yaliyokuwa pale ndani.
“Baba yangu alikufa maskini lakini walau alijenga kibanda hiki kwa taabu.” Akaanzia hapo, hili halikunigusa sana. Nilitamani kusikia juu ya namna tulivyoweza kuokoka.
Nikaamua kumuuliza.
Akatabasamu kidogo kisha akaketi vyema!!
“Sam, yaani japokuwa huwa siendi katika nyumba za ibada hata miezi sita ama mwaka lakini nimeamini kuwa Mungu huwa hamtupi mja wake…. Lakini najiuliza iwapo nami ama sisi ni waja wake. Maana nikiwa katika kile chumba changu nikaisikia sauti ya baba mwenye nyumba ikilalamika, na kuna watu walikuwa wakitoa karipio. Nikasitisha nilichokuwa nafanya, simu yangu nilikuwa nimeweka katika chaji. Nikainyofoa kwanza nikaiweka katika mkoba wangu. Nikatuliza akili, mara nikaona mwanga wa gari. Mwenye nyumba wangu hana gari, nikajishtukia na kuheshimu machale yangu kuwa hapa mambo yanaanza kuharibika, nikapitia dirishani mbiombio nikakimbia hadi nyuma ya nyumba ambapo sauti hizo zilikuwa zinatokea. Nikasikia wakimuuliza juu yangu iwapo nimerudi, kisha wakamuuliza iwapo amewahi kuniona na mgeni. Nikasikia wakimuuliza iwapo anaifahamu sura fulani katika picha ambayo najua tu ni yako hakuna mwingine. Mwenye nyumba akakiri kuwa nilikuwa nimerejea tayari. Lakini hakukubali kiwepesiwepesi badala yake walimpa kipigo kwanza nd’o akalainika.
Alipokubali kuwaongoza kuja upande wa kile chumba changu na stoo pia ndipo nikashtuka na kuja mbiombio upande ule, nikakuita hukuitika, nikawasha tochi nd’o pale ukanipa ile bahasha!!! Wajinga wakavamia pale mimi haraka nikadidimia chini.
Sam niliumia sana nilipowashuhudia wakikupa kipigo kiasi kile, bahati nzuri ndani ya chumba changu tofauti na simu nilichukua pia kile kirungu changu cha mgambo si nilikwambia nilipita huko, kiukweli hicho kirungu niliwadhulumu.
Nikajiuliza sasa mimi na kirungu nitakusaidia kitu gani mie. Wakakutukana matusi mazito, nikatamani kukimbia lakini ningeweza vipi kukuacha ufe hivihivi.
Nikatamani kupiga kelele lalini mwenzangu we, sisi wahehe ni waoga sio siri, yaani unaweza kupiga kelele asitokee hata mtu mmoja sasa hapo ni kipi kama si kujitafutia kufa burebure.
Nikataka kuwakabili kwa kirungu lakini kweli wanaume wanne kwa kirungu kimoja, si matusi hayo!!
Nikajikuta naketi chini, na hapo nikakumbuka jambo la muhimu kupita yote na siajui tu niliwaza vipi kuhusu mbwa wa kufugwa wa baba mwenye nyumba. Yule mbwa huwa hana masihara, baba mwenye nyumba alipewa na wazungu fulani hivi rafiki zake. Nikavamia banda nikalifungua, uzuri ananitambua yule mbwa!!
Nikamvuta hadi nyuma ya nyuma, ghafla nakutana na wanaume wawili kati ya wanne nikatambua kuwa kazi sasa imeanza.
Nikamwachia mbwa akala sahani moja na bwana mmoja halafu mimi na kirungu dhidi ya mwanaume asiyekuwa na silaha, Sam nilimrukia, akanipiga teke mbavuni yule bwege, nikajikaza nikafyatuka na rungu nikalituliza hapa (akagusa utosi wake) jamaa akalainika bila kupiga kelele, chini!!. Ile nageuka namkuta mwenzake akitapatapa pale chini damu inamruka, nikammulika nikahisia kuwa uhai ulikuwa unafanya urafiki naye. Nikamrukia kwa ghadhabu, kabla sijamfikia nikajikwaa nikaanguka chini, nilipoamka hasira zote kwa yule bwana, na yeye nikamtandika rungu kwenye paji la uso. Bila shaka kajifia yule we tungoje taarifa ya habari tu. Kuja kusimama wima tena simwoni mbwa. Nikataka kumwita kwa sauti ya juu lakini nikahofia usalama maana nilitambua fika kuwa wale wanaume wawili wapo bado kule mbele. Nikaanza kunyata taratibu gizani ili nitambua kulikoni, nd’o hapo nikaisikia sauti ya baba mwenye nyumba ikimwamrisha mbwa kushambulia!! Walau amani ikarejea japo niliendelea kunyata, hadi wakati nafanikiwa kufika ndipo namuona yule mbwa akitaka kukushambulia nikamzuia…Sam Mungu ametupangia jambo fulani amini!! Hili tukio halikuwa la kuokoka kirahisi namna hiyo hata kidogo.” Jojina alimaliza na kushusha pumzi kwa nguvu, nami nikashusha pia kama tuliambizana kufanya vile kwa pamoja.
“Sam nadhani tunatakiwa kupumzika halafu kesho twende Makanyagio. Lazima tuanzie huko.”
“Makanyagio? Nd’o wapi huko??”
“Kweli wewe mgeni Iringa nimeamini. Huko ni sehemu maarufu sana kuna makaburi kule, kama unakisikia chuo cha Mkwawa basi ndo kuelekea hukohuko.” Alimaliza kisha akasimama, lakini mimi sikuwa na usingizi. Jojina akaleta godoro la pamba ambalo lilikuwa linatoa harufu ya uvundo akalitandika pale sebuleni.
“Tutalala hapa maana huko chumbani hapalaliki kuna harufu sana.”
“Popote tunalala Jojina.” Nilimuunga mkono.
Akajitupa na baada ya muda alikuwa anakoroma, nilijaribu kujilazimisha kulala lakini hata usingizi haukujileta jirani nami.
Nikapata wazo la kujishughulisha na bahasha na yaliyomo.
Maana swali juu ya hawa watu walikuwa wanatafuta nini na mbona wameacha ile bahasha lilikuwa linanisumbua.
Nikaichukua bahasha kutoka katika kiti alichokuwa ameketi Jojina.
Nikashtuka na mapigo yangu ya moyo yakaongeza mwendo kasi. Bahasha ilikuwa nyepesi sana tofauti na ilivyokuwa awali wakati inabeba picha na makorokoro mengineyo.
Nikaanza kutetemeka nikiamini kuwa ule ushahidi nilioupigania kwa muda mrefu umetoweka, nikaingiza kwa uoga mkono ndani ya ile bahasha. Hapakuwa na makaratasi mengi sana.bali karatasi moja tu!!
Nikalichomoa upesi. Lilikuwa karatasi tofauti kabisa na yale ambayo yalikuwa ndani ya bahasha ile awali.
Nilianza kumwamsha Jojina awe shahidi lakini bahati mbaya hakunisikia hata kidogoa alikuwa amezama katika dimbwi la usingizi.
Nilijaribu kuiweka akili sawa labda si bahasha ninayoitazamia, lakini ilikuwa ni ile na sasa haikuwa na kitu ndani yake.
Nikafungua ile karatasi kwa makini nitambue kama nayo ni moja kati ya zile za awali lakini hapana hii ilikuwa tofauti.
Nikajongea katika mshumaa, nikaanza kuisoma.
Hofu ikatanda maradufu, ulikuwa mwandiko wa kike.
“Sam kama huu ujumbe utakufikia sam, fanya kila uwezalo uniokoe Sam. Nimefanya kila jitihada nijitoe katika mikono ya watu hawa lakini jitihada zimegonga mwamba. Nakuandikia ujumbe huu nikiwa nimekata tamaa kabisa ya maisha na sina uhakika kama utaupata ujumbe huu, Sam yanayotokea huku hayasimuliki hata kidogo kwa maandishi, ninayoyashuhudia huku nilipo ni mazito mimi na wewe hatuyawezi bila msaada wa watu wengine, lakini hao watu wengine ambao nawasema wote wapo katika upande wa watu hawa. Sam kama ukiona ni ngumu sana kuniokoa, amini kuwa nimeridhia kufa. Wewe funga safari ondoka katika nchi hii, nenda mbali Sam maana ukiingia huku hautatoka Sam. Jiondokee uende mbali labda utapata msaada kutoka kwa watu wengine huko wasiokuwa wenyeji wa ardhi hii.
Natamani sana walau ningejua huku nilipo ni wapi lakini bahati mbaya sina hata kitu kimoja cha kufananisha ene3o hili. Na bora ningekuwa natulia sehemu moja, hawa jamaa wananihamisha kila leo. Nimeuza utu wangu Sam na nimeshiriki penzi na huyu bwana ambaye kama ni mkweli atakufikishia ujumbe huu, ameshindwa kabisa kunivujishia siri za humu lakini amesema kuwa hapendezwi na mambo ya humo na atakushirikisha. Nimeamua kumwamini kwa sababu sina namna na hata nisipomwamini mimi ni wa kufa tu Sam wangu!!! Sama kama itakuwa sawa naomba umsikilize huyu bwana, macho yake hayadanganyi hata kidogo, na laiti kama pasingekuwa na vifaa vya kurekodia humu ndani angeweza kunieleza jambo nami nikakuandikia.
Samahani kwa mwandiko huu mbaya, nimeyaandika haya nikiwa katika giza, narudia tena kama huyu bwana ni mkweli basi alifanya hila ya kuzima taa na kuzuia kamera kuweza kunirekodi, nikafanikiwa kukuandikia haya.
Sam, kama sitafanikiwa kupona nifikishie salamu hizi kwa mama yangu mwambie nampenda sana, pia mwambie mzee Matata katika maisha yake ajifunze kumsikiliztu kabla hyajaamua kumuhukumu. Hii itasaidia kuokoa wengi.
Akupendaye!!!
 
SEHEMU YA KUMI NA NANE
SEHEMU YA KUMI NA NANE

Barua ilimalizika nisijue kama imemaridhika, maneno yaliyoandikwa ndani ya barua ile yalikuwa mazito sana. Nikamkumbuka yule bwana aliyekuwa akinibinyia macho kila mara nilipofanikiwa kutazamana naye, sikuweza kupata jibu la moja kwa moja iwapo ni yeye aliyeagizwa na Anitha kunifiikishia ujumbe ule.
Nikakumbuka pia jinsi yule mbwa alivyomng’ata shingoni na labda kuondoka na uhai wake.
Labda alikuwa mtu mwema!!! Macho yake yalijawa na huruma yule mtu!!!
“Jojina….” Sasa nikamkanyaga kwa nguvu, akaamka. Nikamshirikisha juu ya nilichokutana nacho katika bahasha tuliyosadiki kuwa ina nyaraka zetu za kutuongoza.
Kama nilivyoduwaa na yeye akaduwaa vilevile. Akaisoma barua na kuimaliza.
“Sam, hawajatuchezea akili hawa tujiingize mkenge!!!”
“Hapo n’do pagumu pa kuamini na pagumu zaidi kukataa.” Niliishia kujibu kwa sauti ya chini.
“Inawezekana kumbe Anitha yupo hapahapa Iringa eti!” akaniuliza swali la kizembe kabisa. Sikumjibu badala yake nikabetua midomo.
Hakuna aliyelala tena!!!
Bahasha iliyokuwa na zile takwimu nyingine za muhimu ikawa imepotea katika namna ile ya kustaajabisha.

****

SAA MBILI asubuhi tulikuwa maeneo ya Makanyagio, Jojina alikuwa kiongozi kama kawaida. Kwa mtazamo alionekana kuipoteza kumbukumbu ya nyumba ambayo alikuwa anataka twende, mbaya zaidi alilisahau hata jina la mzee wa makamo ambaye alihitaji twende kuonana naye.
“Ujue nimekuja huku mara ya mwisho mwaka juzi ule, sasa watu wamejenga majumba yao huku, siikumbuki nyumba hata kidogo. Na jina nd’o limenitoka sasa.” Alilalamika, tayari ilikuwa saa saba.
Hadi majira ya saa kumi na mbili hatukuwa tumefanikiwa kwa lolote.
Tukarejea Gangilonga kisirisiri usiku mnene.
Jojina alijituliza peke yake akivuta kumbukumbu hii mara ajaribu kubinyabinya kichwa chake. Nilimsikitikia sana maana macho yake makubwa yalikuwa mekundu, akachukua kipande cha mkaa na kuandika chini herufi A hadi Z akidhani kwa kuiona herufi fulani atakumbuka jina la mzee huyo ambaye sikujua alihitaji nini kutoka kwake.
Bado hakulikumbuka jina!!
Angeweweza kukumbuka hata majina ya watoto wake lakini bahati mbaya hakuwahi kuwa na mtoto wa kumzaa.
“Sam…Sam….. “ Ghafla Jojina aliniita, nikiwa nimeduwaa akanishika mkono na kunivuta kuelekea chumbani.
“Baba alikuwa anaandika namba za simu katika kitabu fulani hivi…..” alizungumza huku akianza kupekuea maboksi kadha wa kadha na mimi nikamsaidia. Haikuwa kazi nyepesi kulikuwa na harufu kali sana isiyostahimilika. Lakini tulilazimika kujikaza.
Saa nane usiku na dakika kadhaa nikafanikiwa kupata kijitabu kidogo rangi ya kijani. Jojina akapiga kelele kushangilia. Kilikuwa chenyewe, upesiupesi akapekua majina.
“Mzee Madati huyu hapa!!!” akakutana na jina ambalo alilihitaji.
Tukalala tukiwa na jina hilo vichwani mwetu!!!
Mzee Madati!!!


UTATA MPYA WA ANTI EZEKIELI

KAMA ilivyokuwa siku iliyopita maeneo ya Makanyagio, tulihangaika kuuliza huku na huku hatimaye tukaipata nyuma iliyojificha sana tukaelezwa kuwa hapondipo anapatikana mzee Madati. Ajabu sasa kila ambaye alituelekeza alitutazama kwa mashaka, wakati mimi nilikuwa na kofia ya pama na miwani kichwani na Jojina naye alijifunika vyema na wigi lake asiweze kuonekana.
Tuliwakuta akinamama watatu wakiwa wanatwanga majani ambayo mimi sikuyafahamu. Nikawasalimia kwa Kiswahili lakini hawakunijibu.
Jojina akawasalimia kikabila, mimi nikabaki kimya nisiambulie neno hata moja.
Hata yeye hawakumjibu vilevile.
“Tunahitaji kuonana na mzee Madati….” Alizungumza Kiswahili hatimaye. Bado wale wanawake hawakujibu kitu. Mmoja wao akaingia ndani, na baada ya hapo akatoka kijana moja mrefu mwenye macho mekundu.
“Samahani tunahitaji kuonana na mzee Madati!!” alisema kwa unyenyekevu Jojina lakini yule kijana hakuguswa na unyenyekevu huo.
Akatutazama na kutuuliza ni ipi shida yetu.
Jojina alishindwa aanze vipi kujielezea shida yake kwa mtu baki kiholela namna ile, nikamwona akianza kukunja ndita nikatambua anataka kuzua zogo. Nikamkanyaga mguu, akatambua dhima yangu. Akatulia
“Kaka tuna shida kubwa sana ambayo ni yeye tu wa kuisikiliza.” Alisema Jojina kwa sauti ya chini kabisa.
“Mnatoka wapi.”
“Gangilonga!!”
“Mbona unajibu wewe tu mwenzako yupo kimya, we jamaa unatoka wapi?” alikoroma yule kijana. Mara nikamwona Jojina akitokwa na tabasamu na hapo akatokwa na kauli iliyoleta urafiki.
“We Geza wewe yaani ujue nilikuwa nimekusahau kabisa, mwone mtoto mdogo unakoroma hivyo!!!”
Yule kijana akashtuka kuitwa jina lile.
“Ndema mie!!” Jojina akajitambulisha kwa jina jipya. Kumbe lilikuwa jina lake la ukoo.
Sura ya yule kijana ikajawa na tabasamu si yeye tu na wale akinamama wakaanza kuzungumza, wakamsemesha Jojina kikabila naye akawajibu. Wakakiri kuwa alikuwa amebadilika sana.
Tukakaribishwa ndani!!
Mzee Madati alikuwa mahututi kitandani!!!
Ilisikitisha kumtazama, lakini nd’o ilikuwa hali yake haswa.
Jojina akazungumza kwa muda mrefu sana na ile familia kwa kikabila. Baadaye akaninong’oneza.
“Ile homa ya Ezekiel inamwondoa mzee Madati.” Kauli fupi lakini nzito sana.
Nikatamani kuuliza lakini hatukuwa huru kiasi kile.
Jioni hiyo tukapata fursa ya kuzungumza na mzee Madati alipokuwa ameamshwa kwa ajili ya kunywa uji pamoja na dawa.
Alichukua muda sana kumkumbuka Jojina, lakini alipomkumbuka ilikuwa shangwe tele. Alizungumza naye juu ya baba yake ambaye alikuwa marehemu tayari.
Akatuelezea namna alivyochukuliwa na watu asiowafahamu wakamlaghai kuwa wanataka kununua shamba lake hivyo aende kuzungumza na bosi wao.
“Nilipofika wakaniuliza iwapo nafahamiana na mzee wako Ndema, mimi nikakubali upesi tu na hapo ili kufanya biashara iende haraka nikawaeleza kuwa nauza kipande changu kwa sababu ya kusimamia kesi ya mzee wako. Wakanipongeza sana kwa utu wangu kisha wakaniuliza matumaini ya kushinda kesi. Ndema unajua jinsi gani mimi na baba yako….(akasita akakohoa sana) kisha akaendelea… mimi na baba yako tangu utoto ni chanda na pete. Kwanini nimwombee mabaya, nikawaeleza ukweli kuwa naamini kuwa ile kesi kuna watu wenye fitina wameitengeneza.
Ndema, awali nilikuwa nimekataa kata kata kunywa kahawa yao, niliikataa kata kata lakini baada ya sote kuchangamka na kuonekana kufahamiana. Nikanywa ile kahawa yao ya moto nyeusi.
Nd’o nikajipa tiketi ya maswaibu haya, nakufa najiona na mzee wako wakamuua wajinga wale….. Ndema na wewe kijana kaa mbali kabisa na Anti Eze naninani sijui, Anti nani yule…msijihusihe kabisa na hao…mi wameniua na ninyi watawaua ”
“Baba usiseme hivyo!! Hautakufa hata tafadhali, kwani wenyewe wanapatikana wapi ili tuangalie uwezekano wa kuwachukulia hatua.” Jojina aliuliza kwa upole kabisa.
“Akina nani tena jamani?” mara mzee Madati aliuliza kwa sauti ya kukoroma.
“Si hao watu wabaya waliokuwekea hiyo kahawa. Na huyo Ezekiel ni nani tena maana…” Aliuliza Jojina huku akimpoozea uji mzee Madati.
“Kahawa gani tena?” alihoji huku akiwa katika kubung’aa.
Na hapo wale wanawake wakatueleza kuwa mzee Madati ana tatizo la kusahau na hapo hawezi kukaa sawa tena ilikuwa bahati kubwa sana kwetu amesema nasi kwa muda mrefu.
Hawakuwa katika utani!!
Tulijaribu zaidi ya mara kumi lakini mzee Madati alikuwa haonyeshi ushirikiano, na baadaye akasinzia.
Akaondokea kuwa katika hali ile hata siku iliyofuata na nyingine tena, hakuonyesha ushirikiano nasi tukabaki katika utata mtupu.
Mzee Madati naye anamtambua huyo Ezekiel.
Kulikoni? Ama ni mzimu huu unatuzunguka kwa ajili ya kuja kuyavuruga maisha yetu? Niliwahi kujiuliza.
Lakini kuna kitu mzee Madati anajua kuhusu Anti Ezekiel.

Siku ya nne hatukwenda tulibaki mafichoni. Lakini tukifanikiwa kununua gazeti mjini.
Hapakuwa na habari yoyote ile mpya. Sikuzungumziwa hata kidogo katika kurasa za mbele, bila shaka walitaka kuwaaminisha watu kuwa nimeuwawa.
Wakati najiaminisha hivyo, mara nikakutana na habari ambayo bila shaka katika siku kadhaa nyuma ilikuwa ikiunda vichwa vya habari lakini sasa ilibakia kuwa habari ya kawaida.
“Mama aliyefukua kaburi la mwanae na kuutoa mwili kisha kuuchoma amegundulika kuwa na matatizo ya akili……..” habari ile ilitaja jina la mama yangu mzazi!!
Nilichoka!!
Mama yangu amefukua kaburi langu akautoa mwili na kuuchoma?? Haya yalikuwa maigizo kabisa tena yaliyokosa waigizaji wazuri.
Hawa watu walikuwa wanatumia pesa!!
Waligundua kuwa Dulla aliuwawa mjini Morogoro. Wakajiaminisha kuwa mama lao hawezi kuwa muhusika.
Wakati huo wakijua fika kuwa mimi bado nipo hai. Kile kifo wakakihusisha na uwepo wangu, bila shaka walimbana mama awaambie kama tuliwasiliana, mama akagoma.
Wakatumia pesa kumuuzia kesi nzito, kisha wakatumia pesa tena kumhonga daktari ampime mama akili na kisha wakayanunua majibu kwa pesa zao.
Daktari akalipa fadhila kwa kuandika kuwa mama yangu mimi ana matatizo ya akili.
Akatolewa rumande na kutupwa hospitali ya vichaa Mirembe.
Hakika ilistaajabisha.
Machozi yakanitoka!!!
Jojina akasogea karibu yangu na kuanza kunibembeleza!!!
“Jojina, wamemchukua Mama Eva, wamemchukua mama Eva, Anitha ndo huyu anatoka kutuandikia barua hajui kama atapona ama atakufa, wametaka kukuua Jojina, sasa wamemchukua mama yangu, walimuua baba yako, wamemchukua mtoto wako.. ni kipi sasa wanataka. Mi siwezi kuishi hivi kwakweli siwezi kabisa.si bora nife sasa eeh bora nife” nilijikuta nakaribia kufanya kufuru. Jojina akaingilia kati.
 
SEHEMU YA KUMI NA TISA
SIMULIZI: ANTI EZEKIEL
MTUNZI: George Iron Mosenya
SIMU: 0655 727325

SEHEMU YA KUMI NA TISA

“Ufe wewe ili mama ateseke huko bila kuwa na msaada wowote, kufa kwako ni kumkimbia Eva mtoto wako, aibu ilioje Sam. Unawaza kufa, basi sikuwa na haja mimi ya kumuua yule askari kule porini, sikuwa na haja yoyote ya kujiingiza katika utata huu, ni heri ungeniacha nikiwa nauza bajia na sambusa zangu kuliko huku uliponileta. Ungeniacha sasa. Haya si unataka kufa!!!
Naomba unirudishe uliponitoa, nirejeshe stendi na kapu langu la bajia na sambusa lakini usisahau kitu kikubwa kabisa. Naitaka amanmi yangu ambayo umeipoteza!!!” Mama lao Jojina alikuwa amekasirika haswa. Lakini sio hasira zilizozungumza, aliyoyasema yote yalikuwa kweli tena kweli tupu. Nikakumbwa na aibu nikatamani kuomba msamaha lakini Jojina hakuwa tena pembeni yangu!!! Alikuwa ameelekea chumbani.
Nililazimika kumfuata, ikawa zamu yangu kumbembeleza kutoka katika kilio chake.
Nilimsihi sana, hatimaye akanikumbatia miili yetu ikagusana na kila mmoja kujikuta akivuta pumzi ya mwenzake. Baridi kali la Iringa likatusababisha tutamani kuendelea kukumbatiana.
Kilichotokea baada ya hapo hakuna aliyekitazamia kuwa kitatokea.
Tulikurupuka asubuhi kila mmoja akiwa utupu!!!
Hakuna aliyeanzisha mazungumzo juu ya ajali iliyotokea usiku.

****


SIKU yetu ilianzia nyumbani kwa mzee Madati, tulikuwa tunajaribu bahati yetu kama akili zake zitakuwa zimekaa mkao aweze kutueleza ni kitu gani anafahamu kumuhusu huyo Ezekiel.
Utulivu pale nyumbani uliniweka katika wasiwasi, kitu cha kwanza kuhisi ni kwamba mzee Madati anauwezekano mkubwa wa kuwa marehemu ama mahututi zaidi ya awali.
Majirani wakatueleza kuwa familia nzima imealikwa katika kituo kimoja cha redio pale Iringa mjini kwa ajili ya mahojiano juu ya utata wa afya ya mzee wao. Wakatutajia na jina la kituo hicho cha redio. Jojina alikuwa anakifahamu, tukataka kwenda huko lakini wazo la kujiingiza matatani likatuingia.
Tukafikia maamuzi ya kurejea kule Gangilonga mafichoni, kama kawaida tukiwa na tahadhari kubwa kabisa. Tukanunua magazeti mbalimbali kwa ajili ya kujipatia taarifa zozote kuhusiana na mkasa wetu ili tujue adui amejipanga vipi kutuangamiza ili tuzidi kujihadhari.
Majira ya saa moja usiku, tukiwa na amani kabisa tukarejea tena nyumbani kwa mzee Madati ili tuweze kujua ni kitu gani wamehojiwa redioni, na pia kama hali ya mzee ni njema tuweze kuzungumza naye.
Umati wa watu ukatuvutia na kutuweka katika umakini mwingine.
Askari!! Ndo kitu cha kwanza nilichowaza na kumshirikisha Jojina, tukaishi kimashaka eneo lile. Taratibu kwa kupitia upande usiokuwa na watu wengi tukafanikiwa kufika jirani na umati.
Kweli tulikuwa sahihi, walikuwa ni maaskari lukuki wameizunguka ile nyumba. Umati wa watu ukifanya minong’ono mingi kila mmoja na lake.
Mnong’onaji mmoja akanivutia zaidi kumsikiliza.
Akawa anamtuhumu mama Sadiki, mama nisiyemfahamu kuwa ni yeye ameyafanya haya. Lakini mwenzake akampinga na kusema kuwa mama Sadiki amesafiri kwenda Mbeya hiyo ikiwa siku ya nne.
“Kwani kila sumu lazima ikuue hapohapo wewe jamaa yangu vipi wewe.” Alizidi kusimamia msimamo wake.
Akili ikafyatuka kusikia kauli ya huyo bwana ambayo ilionekana kuwa tatanishi lakini yenye kuaminika katika kichwa chake.
“Sikieni jamani, kama kuna anayemjua muuaji askari wale pale akawaeleze sio kutusumbua huku sisi tusiokuwa na msaada wowote.” Mzee mmoja wa makamo akatoa karipio, yule mnong’onaji akatulia kimya asiseme kitu lakini akirusha mikono huku na kule kama anayenyimwa haki zake za msingi.
Jojina alikuwa kama hasikilizi lolote lakini ghafla akamvuta yule bwana aliyekuwa akirusha mikono huku na kule.
Kisha akanivuta na mimi. Tukawa tumejitenga!!
Jojina akajifanya na yeye anaamini kuwa mama Sadiki anaweza kuwa nyuma ya haya, yule bwana akafurahi kupata wanaomuunga mkono.
“Yaani mimi nimewasikiliza redioni wote wakiwa na afya tele hata huyu mzee Madati aliweza kuongea, sawa alikuwa haeleweki na maneno yake hayo ya Ezekiel sijui kitu gani lakini alikuwa mzima wa afya, sasa wanafika nyumbani mzee anafia kitandani, mke wa kwanza anafia bafuni, mwingine akaanguka ghafla tu uani. Mama Sadiki hayupo!! Na hao wanaodai amesafiri, safari gani ya ghafla hivyo kama sio kujitafutia sababu za kuonekana hausiki?
Tangu mwanzo mimi nilisema kuwa huyu mama kisa ana mtoto wa kiume anataka arithi mali za mzee Madati kinguvu. Mtoto mwenyewe sio wa Madati wala nini!!! Ameiteketeza familia ya watu jamani!!!” alilalama bwana yule kwa uchungu. Hakujua kama anatupa faida kubwa sana kujua ni kitu gani kinaendelea.
Kulisikia jina Ezekiel hapohapo nikaikumbuka kauli ya siku ya kwanza kabisa aliponiambia.
UKIMJUA EZEKIEL NA WEWE UNAPOTEA.
Mzee Madati na familia yake ikawa imepotea kwa kumtaja Ezekiel.
Huyu mtu ni nani hadi awe amesambaa kila mahali, na kwani yeye ni nani hadi asitajwe?
Sura yake ipoje kama si yule aliyejifia kitandani Dar es salaam.
Swali gumu kupita yote kati ya yale tuliyowahi kujiuliza.
Miili mitatu ikaondolewa usiku ule na kupelekwa katika hospitali ya wilaya.
Tukajiondokea mapema sana ili kukwepa kuanza kuhojiwa iwapo kuna lolote tunalojua, maana kuna baadhi ya watu walianza kututambua kama ndugu wa karibu wa familia ile.
Ndani ya chumba chetu cha kule mafichoni kila kitu kilionekana kuwa shaghalabaghala. Jojina alikuwa amechoka na mimi nikiwa hoi vilevile. Adui yetu alikuwa ametupiga mapigo makali mfululizo bila sisi kujibu lolote.
Mbaya zaidi ni kwamba hata sisi tuliojua kiasi juu ya Ezekiel tulitakiwa kuuwawa kama ni kweli kila anayetaka kumjua lazima apotee.
Jojina alijaribu kuweka mezani mikakati kadhaa ya kujaribu kukabiliana na huyo bwana wa kujiita Ezekiel ma lolote lile kuhusu Michigani. Tukaamua kujisahaulisha juu ya Anti Ezekiel ambaye niliamini kuwa alikuwa mtu mwenye utata zaidi kupata kuonekana machoni pangu na kisha kutoweka ghafla.
Akiwa mzima, akiwa kitandani maiti na kisha akiwa muuaji Iringa!!
Muuaji asiyeonekana.

SALAMU KUTOKA DAR ES SALAAM

MAAMUZI aliyoyapitisha Jojina ni kugawana majukumu, kujificha Iringa tu haina maana yoyote ile. Kwa sababu mimi nilikuwa nasakwa sana jijini Dar es salaam na yeye akiwa anajulikana Iringa, akaamua kuniacha mimi Iringa na yeye akimbilie Dar es salaam kuangalia iwapo mpango aliokuwa ameupanga utaweza kuleta mafanikio yoyote.
Niliibariki safari yake, kama kawaida akajiweka katika mavazi ambayo yataubadilisha muonekano wake.
Akajihifadhi katika baibui jeusi!!
“Sam, ishi kwa tahadhari, usikae hapa kila siku, watakusoma na mwisho watakudaka kama kuku. Nadhani sina haja ya kukukumbusha juu ya hatari inayotukabili mbele yetu, usilemae. Pesa unayo lala hotelini, ikibidi wakati mwingine nenda Mbeya huko, kimbia Morogoro kidogo.
Wewe na mimi ni wakimbizi. Tusikae kama watu huru kiasi hicho!!” alinisihi mama lao, Jojina alfajiri wakati akiondoka kuelekea Dar es saalam kujaribu kutimiza mipango aliyoiita mipango makini.
Jojina akaniacha mpweke katika ardhi ya Iringa, ardhi inayosadikika kuwa ina mahali panaitwa Michigani ambapo nd’o kuna utata unaotakiwa kutatuliwa.

****

MAJIRA ya saa nne usiku nikapokea simu ya kwanza kutoka kwa Jojina, akanielezea kuwa amefika salama na muda ule naongea naye tayari alikuwa hotelini.
Wakati nataka kumpa pole juu ya safari yake, akanicheka kidogo kisha akaniambia nimpe pole ya mizunguko maana tangu saa kumi na moja jioni alikuwa jijini Dar.
Mizunguko ipi tena huyu mwanamke ama kwa mahawara zake tena.
“Sam, nilikuja Dar es salaam kufanya kazi na sio kulala. Niliposhuka Ubungo kitu cha kwanza kama ulivyonielekeza kuwa mzee Matata anaishi Shekilango, niliamua kuitafuta nyumba yake muda uleule. Bahati nzuri kama ulivyonielekeza kuwa huyo mzee ni maarufu sikuhangaika sana kuipata nyumba anayoishi. Nadhani umaarufu wake umekuwa maradufu!! Kisa kilichokuza jina lake zaidi ni kuchanganyikiwa na kuwa anaongea peke yake barabarani baada ya mtoto wake wa kike anayempenda kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Wamemtafuta kwa kila namna lakini hawajampata!! Kesho nitaenda kuitembelea familia hiyo ili niweze kuanza ule mkakati ambao nilikwambia…..” Anitha alimaliza kuongea, nilishangazwa sana na uchapaji kazi wake mkubwa kiasi kile. Wakati mtu mwingine angefika na kupumzika yeye alikuwa ameingia moja kwa moja katika jambo lililompeleka huko.
“Jojina, naogopa kukupoteza tena naogopa sanma. Ujue ni wewe uliyebaki katika maisha yangu ambaye naweza kukuamini. Niite muoga niite mdhaifu lakini nasema ukweli kuwa naogopa sana kusikia jina Matata. Asije kukuingiza matatani Jojina, yaani usiporudi huku nikwambie kitu kimoja tu. Sitajali kama umekufa ama nini. Mimi ni heri nijiue Jojina. Sitakuwa na nguvu tena za kupambana….” Kabla sijamaliza akanikatisha, “Sam, ukinitia uoga basi yatakuwa kama usemavyo, acha niende na ule mkakati. Kumbuka ni mkakati ambao nimetumia masaa manne kukuelezea na ukakiri kuwa umenielewa Sam. Kama hukunielewa ulimaanisha nini kunibariki nikaondoka huko.
Sasa Sam ni hivi kitu kimoja naomba nikwambie, mkakati huu sitaachana nao, na kama nikishindwa na kuingia matatani, tambua kuwa ni wewe upo nyuma ya haya yote. Wakiniua jua kuwa na wewe kwa maneno ya mdomo wako umechangia, wakinitesa na kuninyima uhuru basi upo pia katika shutuma hizi.
Na pia kama simulizi hiyo ya mwanangu Justin kuwa yu hai mafichoni pia ni kweli basi baya lolote watakalomtenda ni juu yako wewe na si mimi Sam….
Kitu unachotakiwa kufanya kwa sasa ni kuniombea tu yasitokee hayo yote…..nadhani umenielewa vyema kabisa Sam… na usinipigie simu tena kuniambia mambo yako ya kipuuzi puuzi….hujui thamani ya mama yako, mkeo na mtoto wako wa kumzaa Sam… hivi umerukwa akili Sam eeeh!!” Jojina alizungumza haya kwa hisia kali na baada ya hapo akakata simu.
Nilibaki katika zizimo nisijielewe ni mkasa gani huu unaoendelea kunikabili katika maisha yangu. Nikabaki kuumia nisitambue kama siku moja maumivu haya yataisha ama la!! Maana sikuwa naupata unafuu badala yake nilikuwa mtu wa janga hili likiondoka linaibuka jingine!!
Sasa nikaziona dalili zote za kumpoteza Jojina.
Jojina alikuwa katika mlango wa kutokea na kisha kukaribisha maumivu makali katika moyo wangu!!
Jojina alikaribia kabisa kuufunga ukurasa wa mwisho wa maumivu yangu huku nikiamini kuwa bila yeye basi tena sitakuwa na thamani zaidi.
Wakati huu ni moyo tu ulibaki kuuma, machozi yalikuwa mbali nami.
Nikasimama imara tena na kuilazimisha akili yangu kuwa machozi si tiba ya mkasa huu ninaopitia, ni lazima nichakarike ili niweze kuupata mwanga. Kumtegemea Jojina kwa asilimia mia ni kujitafutia msongo wa mawazo pale mambo yatakaposhindikana.
Nikazikumbuka harakati za Anitha punde tu baada ya kuwasili Iringa kisha nikayakumbuka na maneno yake. Na mwisho nikajionya kuwa nikilemaa nitapoteza kila kitu.
Nikalala nikiwa na wazo moja tu!! Jojina anapiga hatua Dar es salaam nami napiga hatua Iringa!!
Haba na haba hujaza kibaba!!

****
**JIFUNZE… Kutojiwekea matumaini ya asilimia mia moja katika jambo, naam! Ni vyema sana kuamini lakini si kuamini kupita kiasi maana jambo ulilolitarajia kwa asilimia mia moja likishindikana waweza kujihisi wewe ni mtu mwenye mikosi kupita wote duniani.
Matumaini ya asilimia hamsini kwa hamsini ni bora zaidi kuliko asilimia mia isiyo na uhakika…..
George Iron, 2012
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom