SEHEMU YA ISHIRINI
RIWAYA: ANTI EZEKIEL
MTUNZI: George Iron Mosenya
SEHEMU YA ISHIRINI
MSAKO
Niliamini nikimshirikisha Jojina juu ya harakati zangu za kwenda kwenye kile kibanda atazidi kuniona wa ajabu na nisiyejua kitu gani ambacho ninafanya.
Kibanda hicho hakuwa akikipa nafasi hata kidogo kuwa kinaweza kuwa na mwqanzo wowote wa kutufumbua macho juu ya siri hii. Hata mimi binafsi sikuwa na imani tele juu ya kibanda kile lakini ningeendelea kulala ndani kila siku? Ningeendelea kumtegemea Jojina kwa kila jambo!
La!! Ni heri mtembea bure kuliko mkaa bure, wengi wamewahi kutembea bure na mwisho wakaokota pesa.
Nikajionya pia kuwa wapo wanaotembea bure na mwisho kujikwaa barabarani huko na kupoteza kucha za vidole vyao!!!
Nikaamua kuwa mtembea bure!!
Saa tatu asubuhi ilinikuta nikiwa natazamana ana kwa ana na kile kibanda kilichoandikwa Michigan, sikujua ni kipi kitafuata baada ya mimi kuwasili pale lakini nilienda nikiamini yawezekana ni harakati za kuusogelea ukweli.
Ukweli ambao utaniweka huru mimi na watu kadhaa wanaonizunguka!!
Hapakuwa na mabadiliko kama tulivyokiona siku ya awali, kwa mbali nilimuona bwana Massawe ambaye ndiye tulimwona siku ya kwanza akiwa amejikita katika kufagia eneo lililopo mbele ya kibanda chake, nikapiga hatua moja baada ya nyingine hadi nikakifikia kibanda kile, nikalitazama vyema lile neno Michigan. Hakika mwandishi alikuwa anatania ama la! Hakulipwa pesa ya kutosha aweze kulisanifu jina lile.
Halikupendeza kulitazama!! Ni kama liliandikwa ilimradi tu limeandikwa
“Karibu aiseee!!” alinikaribisha huku akiutupa fagio kando na kujongea katika kibanda nikiwa nimeduwaa bado. Akafungua mlango wa mbao na kuingia dukani, akatega sikio kunisikiliza.
“Za asubuhi shehe wangu!!” alinisabahi kwa lafudhi yake ya kichaga, nami nikamjibu kwa utulivu!!
“Kuna maziwa fresh!!” nilijikuta nikimuuliza ilihali macho yangu yaliyofanikiwa kupepesa pale ndani hayakuona hata mfano wa maziwa.
“Hamna maziwa bosi wangu, hapa hata friji sina. Unavyoviona n’do vitu pekee humu dukani.” Alinijibu huku akiufungua mlango tena na kutoka nje. Hitaji langu lilikuwa limemkera kiasi fulani.
“Masawe! Njoo unipatie sigara, samahani kwa usumbufu!!”
Hakujibu kitu akajongea kibandani na kunipatia sigara niliyokuwa nimeagizia. Akataka kunipatia kiberiti, nikamweleza kuwa hicho nilikuwanacho!!
“Yaani tumbo limenisumbua jana Masawe. Hapa sijui hata maziwa nt’ayapatia wapi? Lakini licha ya hayo Masawe wewe hunikumbuki nd’o maana hata hujanichangamkia… hata hivyo siku ile giza lilishaanza kutawala…” nikaingiza maongezi ya kulifikia lengo. Akanitazama akijaribu kuitafuta sura yangu bila mafanikio.
“Nilikuja hapa na mke wangu usiku mmoja hivi, tukanunua pipi na vocha…. Ni siku kadhaa nyuma, halafu kigiza kilishaanza kuingia usingeweza kunitambua, halafu siku ile sikiwa na miwani hii….” Nilizidi kumuundia mazingira huku nikiupuliza moshi wa sigara juu.
Kumbe Masawe naye alikuwa mvutaji, akachomoa sigara na kuanza kuivuta.
“Hivi Masawe una uzoefu sana na biashara ya duka kwa huku Iringa hasahasa hapa mjini?” nikamuuliza swali lile huku nikijifanya sitilii maanani sana chochote atakachonijibu.
“Nina miaka minane nauza duka, Moshi huko na hapa pia japo si muda mrefu lakini ninaifahamu vyema Iringa” alinijibu huku tukiendelea kushindana kuvuta sigara.
“Masawe na ujanja wako huo hadi leo unavuta SM shehe wangu…” nilihama nikarejea katika utaniii.
“Hapana hataaa ‘sports huwa navuta sema leo nabadilisha ladha” jibu lake likaleta matabasamu na vicheko hatimaye!!!
Urafiki ulianza kujengeka!!
“Masawe mimi ni mgeni huku Iringa, na kitu kikubwa kilichonileta huku ni kufanya biashara ya duka katika mtaa fulani huko karibu na chuo sijui wanakiitaje. Mwanzoni nilitarajia kumweka mke wangu asimamie lakini bahati mbaya ameugua na hali ya huku imemkataa kabisa, sasa natafuta mtu mwingine wa kumweka pale. Wewe nakuona ni mzoefu sana, waweza kunisaidia mawazo kidogo.” Nikatupa karata yangu kubwa zaidi niliyokuwa nimeiandaa.
Masawe akatabasamu kidogo kisha akaingiza utani.
“Mbona mimi nipo waweza kuniajiri tu shehe wangu!! Ilimradi masilahi tu” tukacheka pamoja lakini nikausimamia ule utani wake ili uniongoze zaidi.
“Aaah Masawe mtu mzito kama wewe nitakulipa bei gani, maana utalazimika kuiacha ofisi yako. Sasa ndugu si utanifilisi wewe….. yaani mtaji ukiongezea na mshahara wako n’do nafilisika kabisa.” Nilifanya utani kimalalmiko. Masawe akacheka kabla ya kuleta jibu langu la kwanza kabisa.
“Bora hata kingekuwa kibanda changu asee. Cha wenyewe hiki bwana, kila nikilalamika bidhaa ziongezwe bosi anadai ningoje kidogo, hiyo kidogo huu mwezi wa sita tangu nianze malalamiko!!. Tazama sasa mfano tangu umefika wewe hapa bado hajafika mteja mwingine tena. Eneo lenyewe hili halijakaa kibiashara kabisa na bosi hashauriki hata kidogo!”
“Aah Masawe yaani unataka kuniambia wewe umetoka Arusha na kuja kuajiriwa huku kwenye hiki kibanda kikiwa hivi hivi ama amehamishia bidhaa nyingine mahali. Mbona unanitisha bwana ama huku Iringa maduka hayalipi, niweke wazi bwana Masawe.” Nilifanya udadisi, wakati huu sigara ilikuwa imemalizika.
“Ni stori ndefu shehe wangu, ila bosi wangu aliponitoa Moshi kunileta huku yalikuwa makubaliano mengine kabisa. Alinileta kufanya kazi mahali lakini mwisho wa siku nikaishia hapa dukani. Sema ninachoshukuru nikiwa na shida ananisaidia..” alijibu kwa ufupi lakini nikatambua kuwa kuna mengi sana anayo na si wa kumwendea kwa pupa.
“Aisee Masawe pole ndugu yangu, basi ngoja niingie hapo stendi Masawe nikitoka nitakuja tubadilishane mawazo bwana Masawe. Maana mimi shemeji yako bwana, nimeoa hukohuko kwenu!!” nilijenga undugu wa kilazima huku nikiamua kuonyesha kuwa sihitaji sana kujua kuhusu hicho kibanda.
Laiti kama Masawe angejua kila neno lake lilivyo la muhimu kwangu asingethubutu kuzungumza nami!!
Niliondoka pale na kujizungusha mjini, nikanunua nguo nyingine mpya, kisha nikatafuta nyumba ya kulala wageni nikalipia, nikaoga na kubadili nguo.
Nikatoka na kurejea kwa Masawe tena, kama kawaida kofia kichwani na miwani usoni. Sikutaka Masawe anitambue maana angejua tu kuwa ni mimi yule ninayetafutwa basi mambo yangeharibika. Na nilichoshukuru zaidi magazeti hayakuwa na habari na mimi tena baada ya kuthibitishiwa kuwa nimekufa.
Masawe alinichangamkia baada ya kuniona tena kwa mara nyingine, sasa nilikuwa nadhifu kabisa tofauti na awali. Shida yangu kucheza na akili ya Masawe, nilitambua ni kiasi gani watu kutoka Moshi na Arusha walivyo makini linapokuja suala la kutumia nafasi.
“Haya sasa tazama tangu wewe uondoke wamekuja wateja wawili tu mmoja kununua kibiriti na mwingine mtoto amekuja kununua pipi kifua. Unaweza kuiita hii biashara shehe wangu!! Mimi nataka kuchakarika yaani.” Alianza kujivutia upande wake. Nikaipenda hali hii.
“Kwa makadirio mfano, samahani lakini. Wanakulipa milioni ngapi hapa ili nijipange na mimi nikitaka kukunyofoa.”
Akacheka sana kabla ya kunijibu, “Yaani uuze pipi na sigara ulipwe milioni!! Hata laki mbili haifiki sema nina sehemu ya kulala ya bure.”
Nikatikisa kichwa kisha nikawalaumu mabosi wake ambao sijawahi kuwaona, kuwa ni wanyonyaji sana. Nikalaani na mwisho nikajisemea.
“Mimi siwezi kumlipa mfanyakazi wangu chini ya laki tatu na nusu. Nimesota katika maisha na ninaujua ugumu wa hizi kazi na maisha yako juu pia Masawe.”
Masawe akafanya tabasamu kisha akacheka kibwege huku akiona aibu. Bila shaka lile dau langu lilimkamata akili. Nikaamua kuendelea kumkamata.
“Ujue wakati mwingine unapompa mfanyakazi mshahara kidogo ndo mwanzo wa kuanza kukuibia, mara leo hiki kesho kile. Anakuwa hawezi kujikimu, lakini ukimlipa mtu vizuri akikuibia huyu ni mwizi wa tabia tu!!”
Masawe akatikisa kichwa kuunga mkono hoja!!
“Sasa kwa hii biashara bosi wako anaweza vipi kukulipa mshahara kama leo umeuza pipi na sigara na kibiriti?”
“Inashangaza sana, ananilipa hivyo hivyo, tena anaendesha magari yule ya kifahari. Kuna kipindi zinapita hata wiki mbili sifungui duka, yaani ana maamuzi ya ajabu sana anaamka tu Masawe leo hakuna kwenda dukani mpaka nitakapokwambia. Zinapita hata siku kumi nd’o nafungua tena…. Sijui ana wazimu?” alijiuliza Masawe, mimi nikapata faida nyingine.
Kumbe Masawe hata yeye hajui kwanini bosi wake analing’ang’ania hilo duka. Nikayakumbuka maneno ya Anitha aliponisisitiza kuwa huyu aliyepo dukani si lolote si chochote yupo mwingine mdosi zaidi.
“Looh!! Kwa hiyo ukifunga nd’o hakuna kinachoendelea tena dukani, kumbe nd’o maana mnafukuza wateja.”
“Aaah!! Bosi wangu wa ajabu mno, kuna kipindi alikuja ghafla mimi nikaambiwa kutoka nje, walikuwa wawili. Nilipokuja kuchungulia ndani sikuwaona hata. Baadaye kabisa wakatoka, hata sikuuliza lakini nilipowashirikisha watu kadhaa wakaniambia kuwa hayo ni mambo ya ushirikina tu hakuna la ziada.. nikapuuzia na kusahau.”
“Dah!! Inasikitisha sana!!” nilimaliza maongezi hayo, lakini moyo ukinienda mbio, ni kama kulikuwa kuna kitu cha ziada nilitakiwa kukitambua kutoka katika himaya ile. Kitu cha msingi zaidi!!
Siku hiyo maongezi yakaishia pale nikaaga!! Kwa makubaliano ya kufika tena siku nyingine.
“Bosi wangu wewe ukiwa tayari niambie tu mimi nafanya kazi kama kawaida.” Alinisihi, nikaondoka!!
****
USIKU huo nikiwa nyumba ya kulala wageni nilikuwa nikiunganisha mambo kadha wa kadha, kubwa zaidi kuhusiana na utata wa kile kibanda kilichoitwa Michigani. Nilitaka kujua kiundani zaidi kuhusu mmiliki na mengine ya ziada. Nikajipanga kikamilifu kwa ajili ya kumkabili tena Masawe kwa lugha nyingine ili niambulie mengi zaidi.
Nikaamua kujipa siku tatu mbele zaidi ili niweze kumtembelea tena yule bwana muuza duka.
Wakati huo niliendelea kupokea jumbe kadha wa kadha kutoka kwa Jojina akinijulia hali huku akidai kuwa anaendelea na harakati kwa kasi kabisa. Jambo ambalo lilinitia nguvu na mimi kuendelea
CHEUPE DAWA.
BAADA ya siku tatu kama nilivyojipangia majira ya saa nne asubuhi nilifunga safari kwenda kuonana tena na bwana Masawe. Siku hii nilijipanga kumchukua tukae mahali tuzungumze kwa kina, maswali niliyoyaandaa kutokana na taaluma yangu ya uandishi wa habari niliamini kuwa hata awe mjanja vipi bwana Masawe hawezi kuchomoka!!
Maswali yale nilikuwa nikiyatumia katika matukio magumumagumu hasa hasa kujua ukweli juu ya jambo fulani kutoka kwa mtu mbishi na mjanja mjanja!!
Niliamua kutumia usafiri wa taksi ili niweze kuidhihirisha hadhi ambayo tayari nilianza kuijenga kwa Masawe, tena safari hii nilitaka niendeshe mwenyewe hadi mahali ambapo Masawe ataniona vizuri kabisa.
Nikajivuta hadi katika kijiwe cha taksi nikazungumza na ‘shanta’ juu ya shida yangu!! Yeye hakuwa na kikwazo baadaye akamuita mmiliki halali.
Wakadai nilipe zaidi ya kawaida nikakubaliana nao.
Nikaingia katika usukani, shanta (deiwaka) akawa ameketi kiti cha nyuma!! Nikaanza kunyonga kuelekea kwa Masawe huku Shanta akiniongoza kila nilipotaka kupotea njia.
Ni wakati nataka kukata kona ili gari iweze kutazamana moja kwa moja na duka la Masawe ndipo nikaona gari nyingine ya kifahari ikiwa katika harakati aidha za kuegesha ama kuondoka kutoka eneo lile. Akili ya haraka ikajirusha katika kichwa changu!!
Sikukata kona badala yake nikanyoosha moja kwa moja!
Shanta akadhani nimekosea njia, nikamsisitiza kuwa nilikuwa sahihi kabisa. Nikaegesha gari kwa mbele kabisa, tukakubaliana na Shanta kuwa ataningojea palepale. Akatoa pakiti ya sigara na kuchomoa moja!!
Nikaondoka na funguo za gari huku nikitembea kimadaha, katika namna ya kuridhika sana kana kwamba ni mdosi kutoka nje ya nchi!! Kwa nje ningeweza kuonekana nimeridhika sana lakini macho yangu yalijikita katika kuitazama Nissan Patrol ilivyokuwa inajaribu aidha kuondoka ama kuendelea kuwa eneo lile. Na hapo nikagundua kuwa ile gari haikuwa ikiondoka bali ilikuwa imewasili.
Akili ikanicheza upesi!! Kwa mbali kabisa nikaangaza sikufanikiwa kuiona sura ya Masawe wala dalili yoyote ya uwepo wake!! Upesi nikatoa simu yangu mfukoni, nikaitazama kana kwamba ilikuwa inaita nikapokea wakati si kweli kuwa ilikuwa inaita.
Nikajizungusha huku na kule kama ninayetafuta mtandao.
Nia yangu ikiwa kutazama kama naweza kuona chochote kitu kinachoendelea!!
Mlango wa duka ukafungwa!! Upesi nikaikumbuka kauli ya Masawe kuwa aliwahi kuchungulia ndani baada ya kutolewa nje! Nami nikajitia jeuri tena nisiyekuwa na hatia nikajisogeza mbele kwa kujiamini funguo zangu zikiruka hewani huku na kule.
Nikakifikia kile kibanda.
“Masaweee!!” nikaita kwa sauti ya chini!!
Kimya! Nikaita tena kwa sauti ya chini bado hapakuwa na jibu. Nikalisogelea lile gari niweze kuangaza kulikoni, nikajifanya natazama kama kuna mtu ndani yake niweze kumuulizia kulikoni mbona Masawe hajafungua duka.
Nilipolikaribia gari nikakutana na vioo vilivyovikwa utando mweusi ‘Tinted’ nikatamani kujua ni nini kinaendelea ndani!!
Nikachungulia!!
Nikaona kitu mfanowe bahasha, bahasha kama ile yangu iliyokuwa na nyaraka zangu kutoka kwa yule bwana wa kuitwa Ezekiel. Nikazidi kukisogelea kioo ili nijihakikishie zaidi juu ya ile bahasha katika kile kiti.
Lahaula!! Pua yangu ikagusana na kile kioo. Ving’ora vya dharula vikaanza kulia, ile gari ikawa inapiga makelele kwa fujo, hofu ikanitanda. Nikapagawa na kuamini kuwa wakati wa kuumbuka na kukamatwa ulikuwa umewadia, nikataka kukimbia lakini nikagundua kuwa ni upuuzi uliopitiliza. Sijaiba cha mtu, nimevaa kofia na miwani machoni, nikimbie nini. Lakini nafsi nyingine ilikuwa inanisihi nikimbie, maana kama ni kweli hiyo bahasha ni ile nilikuwa naisaka basi hao watu lazima watakuwa watu wabaya.
Na hivyo watakuwa wananifahamu fika!!!
Maswali mawilimawili, nikimbie ama nisikimbie!!
Nikakosa maamuzi na kubaki kama zezeta nikingoja kuumbuliwa!!
**HAYA SAM ameingia rasmi katika harakati…….. king’ora kinapiga kelele na hajui ni nani mmiliki wa gari lile…..
Nini kitajiri