SEHEMU YA SABA
Siku tatu baadae
KATIBU WA BUNGE alishindwa kuchanganyikiwa baada ya kugundua kuwa nyaraka za mswada wa sakata la Escrow hazionekanai ofisini. Alipekua huku na kule lakini wapi. Niliziweka kwenye droo hii, na nilifunga na funguo nilikuwa nazo mwenyewe, zimepoteaje? Alijiuliza akiwa kaweka mikono yake kiunoni. Kila alipojumlisha moja na moja ilikuja nne na sio mbili. Akashika mkono wa droo na kulivuta kwa kulitikisatikisa lakini halikuwa na kitu ndani yake. Akashusha pumzi ndefu na kuketi kitini huku akihisi macho yake kujaa machozi ya dharula.
Alipoona sasa hana la kufanya, aliinua simu yake na kubofya tarakimu Fulani kisha akaiweka sikioni na kusubiri upande wa pili upokee simu hiyo.
“Hello!”
“Ndiyo mkuu, yaani kabrasha zote za lile sakata hazipo kabisa…”
“Sasa zitakuwa wapi? Au ume-missplace…?”
“Hapana mkuu, naijua kazi yangu, hizi zitakuwa zimeibwa,”
“…Zimeibwa!” ile sauti ya upande wa pili ikahamanika kwa jibu hilo, “…haiwezekani… naomba uje ofisini kwangu mara moja!” ikamwamuru Yule Katibu wa Bunge naye muda huohuo akiwa kajawa na hofu akatoka ofisini. Alipofika nje akasimama kidogo na kisha kama asiyeamini akarudi ndani na kuanza upya kupekua.
Dakika thelathini zilizofuata alikuwa tayari kwa mkuu wake wa kazi, mwili wake ulikuwa umetona kwa jasho ijapokuwa kiyoyozi kilikuwa bize kikifanya kazi ya kupoza hewa.
“Unaniambia zimepoteaje?” Yule mwanamama, mwenye wadhifa mkubwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akamwuliza katibu wake wa bunge mwenye mamlaka ya kutunza na kujua dondoo zote za mhimili huo.
“Yaani hata sijui, tangu kikao cha mwisho, kabla ya msiba wa Msesema niliziweka kwenye loka namba tatu lakini sizioni pale”.
“Ina maana mtu kaingia kaiba ofisini kwako humohumo?” Yule mwanamama akuliza huku akionekana wazi kushikwa na hasira kali.
“Ataingiaje?” Yule kijana akajikuta anauliza.
“kama hajaiba mtu kutoka nje basi ni wewe na wasaidizi wako mtakuwa mmekula njama, na hili lazima lichukuliwe hatua mara moja. Nenda nitafanya utaratibu mwingine juu ya hili kisha nitakuita pamoja na wasaidizi wako, hii ni aibu kwetu, kabrasha linapotea vipi kwenye kitengo nyeti kama hiki? Ajabu!” mkuu akaagana na huyo katibu na kubaki peke yake ofisini, sura yake ilisawajika kwa mawazo.
§§§§
Taarifa za upotevu wa nyaraka hizo ulilitikisa Bunge, kila aliyesikia habari hiyo hakuamini ama kile anachoambiwa au anachozikia. Maswali yasiyo na majibu ndiyo hasa yaliyotawala vichwa vya walio wengi. Jeshi la polisi nalo lilikuwa likajaribu kadiri ya uwezo wao kuona labda hiki au kile lakini yote ya yote hakuna aliyejua kabrasha hizo zimepoteapotea vipi.
Upande mwingine vijana wa Usalama wa taifa ambao daima huendesha shughuli zao katika eneo hilo nao walikuwa wamekutana kwa siri kujadiliana juu ya upotevu wa kabrasha hizo nyeti.
“Hii ni njama, lazima ifanywe na wenyewe,” mmoja alisema.
“Unataka kutuaminisha kuwa wameiba wenyewe?” mwingine akadakia.
“Ndiyo, sasa funguo unatunza wewe, ofisi ni yako, polisi wanasema hakuna mtu yeyote asiyehusika aliyeingia ndani ya wigo huu usiku wa jana. Sasa hii maana yake ni nini? Inabidi tumchunguze Yule katibu si ajabu kala njama,” mwingine akagongelea msumari ambao karibu jopo zime liliunga mkono.
“Itabidi tufanye hilo ijapokuwa vikao vinaisha leo na watakutana hapa miezi miwili ijayo…”
“Sasa huu ndo muda wa kufuatilia kila kona ili wakirudi bungeni kwenye kikao cha arobaini na nane tuwe na jibu na pia tuwe tumewashughulikia wanaohusika,” alidakia Yule aliyeonekana kama ndiyo mkubwa wa kile kikao. Baada ya majadiliano yaliyochukua muda mrefu muafaka ulifikiwa na kila mmoja alipewa jukumu lake katika kipindi hicho.
Mchana wa siku hiyo kikao kingine kiliendelea katika ofisi Fulani huko walikutana watu wasiozidi wanne; Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, mkuu wa Usalama wa Taifa Mkoa wa Dodoma, kiongozi wa askari wa Bunge na Spika. Mjadala uliochukua nafasi ulikuwa ni huo wa kupotea kwa hizo nyaraka nyeti.
Vichwa vilifanya kazi ya kuchambua hiki na kile, lakini jibu la uwazi halikupatikana, polisi walisema kuwa wana uhakika hakuna mtu aliyeingia ndani ya wigo huo kutokana na ulinzi mkali waliokuwa wameuweka kama ilivyo kawaida yao, hata walipohakikisha kwenye kamera za usalama bado hakuna mtu aliyeonekana kuingia ndani ya wigo huo. Baada ya kuchanganua njia zote ambazo kwazo zinaweza kuzaniwa zimetumiwa kuiba nyaraka hizo, bado jibu liligonga kuwa lazima Katibu wa Bunge anahusika kwani nduye ambaye anajua kila kitu jinsi kilivyo na kinavopangwa.
§§§§
Katika kikao cha siku hiyo cha Bunge, Mheshimiwa Kibanio hakuonekana kwenye siti yake, haikuwa kawaida. Kila mmoja alikuwa akimsubiri mtu huyo ambaye alipendwa kwa jinsi anavyojua kujenga hoja ndani ya vikao vya bunge. Mara kwa mara Waheshimiwa walikuwa wakiangalia saa zao lakini hawakumwona kutokea.
Hali hiyo pia ilikuwa kwa Spika wa Bunge, akiwa katika kiti chake alikuwa akitupa jicho mara kwa mara katika kile kiti lakini hakumwona Msesema, huyu leo vipi? Alijiuliza. Kwa siri akaagiza wahudumu wahusika ili kujua kwa nini mtu huyo hajafika bila taarifa na siku hiyo alikuwa na mswada wa kuwasilisha juu ya sakata la Escrow, ilikuwa ni siku aliyoahidi kuwataja wote waliomo kwenye hiyo ‘Orodha ya aibu’.
§§§§
Saa ya ukutani ilipiga muziki wa kuahiria saa kamili imefika, Mheshimiwa Kibanio aliinua uso na kuangalia saa ile, ilikuwa saa tano asubuhi inakimbilia kwenye saa sita huko, akakurupuka lakini alijikuta mwili mzito na kichwa kinamuuma sana. Nini hiki? Alijiuliza pasi na jibu. Akajilazimisha kuamka na harakaharaka akaingia maliwato ili kujiswafi, tayari alikuwa amechelewa kikaoni na ilibaki dakika chache sana kabla hajasimama kulieleza Bunge juu ya wale wote wanaohusika na lile sakata nyeti. Mara akaona simu yake ikiita, alipoinyanyua na kuitazama alimjua anyepiga simu hiyo ni nani.
“Mheshimiwa vipi, tunakungoja kwa hamu!” ile sauti ikamwambia.
“Aaaah! Yaani nashindwa kujielewa asee, ndiyo naamka sijui nini kimetokea,” Mh. Kibanio akajibu huku akivaa shati lake.
“Ok, pole sana, labda jana zilikuwa nyingi sana …”
“Aaaa hapana, jana sijaonja kabisa ila nashangaa nini kimenipata, hata sasa naona kichwa kizito sana na si kawaida,” akaeleza. Alipokwisha kuvaa kila kitu tayari, aliuvuta mkoba wake tayari kuondoka lakini alipounyanyua ukafunguka na kabrasha zote kumwagika, alitupa jicho pale sakafuni zile karatasi zilipozagaa. Hakuamini anachokiona, nani alifungua huu mkoba? Akajiuliza huku akiinama na kuokota yale makabrasha. Badala ya kuyaweka mkobani, akaanza kuyachakura chakura akitazama hili na lile.
“Shiiiit!” akang’aka kwa sauti, akaanza tena kuyachambua yale makabrasha.
“Sasa liko wapi?” akauliza kwa sauti kana kwamba kuna mtu anayeongea naye ndani ya chumba hicho lakini alikuwa peke yake. Akayaacha yale makabrasha na kuanza kupekua kwenye makabati, hakuna kitu. Mheshimiwa Kibanio alijitupa kitandani na kupiga ngolo.
Hakuamini kama kabrasha hizo za muswada muhimu ambao alitakiwa kuuwasilisha mchana huo hazikuwepo, zimekwenda wapi? Lilikuwa ni swali gumu kutegua, akiwa juu ya kile kitanda alijikuta akilia kama mtoto. Akakurupuka na kukusanya yale makaratasi pale chini akayaweka mkobani na kutoka chumbani mle kama mtu aliyechanganyikiwa. Alipoushika mlango akakuta upo wazi, haujafungwa, akasimama na kutazama ndani. Nani kaufungua huu mlango? Nimeibiwa! Akawaza na kujikuta akiishiwa nguvu. Alipokuwa akiuvuta mlango kuufungua akaona karatasi ndogo ikipeperushwa kwa upepo na kuingia sentimeta chache ndani ya chumba hicho. Akaiokota mara moja na kuitazama, ilikuwa na maandishi machache tu.
…Ukitaja hata jina moja tu, yatakukuta yaliyomkuta Msesema…
Kisha mwisho wa maneno hayo kulikuwa na kipicha kidogo cha fuvu la binadamu.
“Shiiit! Ina maana Msesema kauawa? Au ujumbe huu umekosewa?” akajiuliza kwa sauti ndogo. Akiwa anatetemeka, akatoka ndani ya chumba kile na kuteremka ngazi za hoteli hiyo ya Dodoma na kufika chini kabisa kwenye maegesho.
“Mheshimiwa vipi leo? Mbona umekawia sana?” dereva wake akamwuliza.
“Hata sijui kwa kweli nimelala sana, nahisi naumwa maana kichwa chote kizito,” akajibu huku ile gari ikiwa inatoka polepole katika maegesho yale.
§§§§
“Ukimya wetu wa siku tatu umemfanya adui yetu ajitokeze na kufanya mambo yanayoaminika kuwa ni shetani pekee anayeweza,” Madam S alimwambia Amata.
“Ndiyo, ni mbinu nzuri sana uliyotushauri kuitumia, na sasa kama unavyosikia, kabrasha zimeibwa palepale bungeni, inashangaza!” Amata akajibu.
“Yeah, ujue hapa kuna mtu mwenye taaluma kama si ya ujambazi basi sijui tuite ya nini, we kuingia mle ndani ilhali ulinzi mkali na kamera kila kona vyote hivyo vizikubaini. Sasa pale kesi yote inamwangukia Mwambene, katibu wa bunge, lakini hapana, kutokana na wapi tumefikia huyu mtu ni profesheno, lazima tuingie kazini kwa akili zote na nataka apatikane akiwa hai ili tujue nini kipo nyuma ya pazia,” Madam S alimwambia Amata, “Koh! Koh! Koh!” akakohoa kidogo, “Sasa nataka uendelee na kazi, pambana na huyo mtu na umlete mikononi mwangui akiwa na pumzi yake, licha ya hili tu najua atakuwa na mengi sana,” Madam alimalizia kusema, akatoa miwani yake na kuiweka mezani.
“Umesomeka Madam!” Kamanda Amata akajibu huku akinyanyuka, “Nani yuko nyuma yangu?” akauliza.
“Gina, nimeshamuweka tayari”.
“Asante!” Amata akajibu huku akiwa tayari kasimama kwa kuondoka.
“Ofisi yetu imehamia hapa kwa siku chache lakini namnata huyo mtu akiwa hai ili kutoka kwake tujue nani amemtuma,” Madam akasisitiza.
§§§§
Amata akaondoka na kuiacha ofisi hiyo ndogo na kutokomea mjini mpaja hotelini kwake, alipoingia tu jicho lake lilizunguka chumba chote na kugundua kuwa kuna upekuzi wa siri uliofanyika. Wameshajua nilipo, akawaza, kisha kwa hatua za taratibu alikipita kitanda mpaka usawa wa dirisha, alipokaribia kijimeza kidogo kilicho pembeni mwa kitanda ambacho juu yake kuna taa ndogo kwa ajili ya kusomea, saa yake ikapiga ikamfinya na kutoa mlio Fulani mkali. Amata akasimama na kuiinua ile taa akaichunguza na kugundua kuwa kuna kidubwasha kidogo sana kimebandikwa pembeni, alipokiangalia alikijua kidubwasha hicho chenye kazi ya kunasa sauti na kutuma mahala Fulani. Zaidi ya hilo alikitambua kifaa hicho kuwa kina uwezo mdogo wa kurusha mawimbi hayo na si zaidi ya mita 200 za mraba. Adui yangu hayuko mbali kama si yeye basi kibaraka wake, akawaza huku akifungua kabati kubwa la nguo, akachukua kijiredio chake kidogo ambacho hutumia kurekodi sauti mbalimbali, akakibonya na kutafuta sauti aliyoona itamfaa adui yake, akataka kuweka ile ya mtu anakoroma, akaona hiyo sio sawa kwa muda husika, akatafuta nyingine ya kufaa akakiweka katika ile meza kisha akakiwasha, wakati kikiendelea kutoa sauti hizo za mahaba zilizorekodi watu wawili wakifanya mapenzi huku wakiongea maneno ya mahaba, akasogea pembeni na kuvuta meza nyingine akaiweka nyuma ya mlango, akafunga mapazia yote na kuzima taa.
Giza hafifu lilitawala chumba hicho, ile mashine iliendelea kutumbuiza pale mezani. Amata akaketi, bastola yake akaiweka mezani na kisha kujimiminia pombe kali aina ya GIN na kuinywa taratibu akimsubiri mgeni wake kwani alijuwa kwa vyovyote atakuja.
Kutokana na uchovu aliokuwa nao Amata, kijiusingizi kilikuwa kikimnyemelea kwa mbali, lakini mara kwa mara alikuwa akipambana na hali hiyo. Kama alivyodhani ndivyo ikawa, alihisi kitasa cha mlango kikinyongwa taratibu, akageuza shingo na kuangalia kule mlangoni huku bastola yake iliyofungwa kiwambo ikiwa tayari imekaa kinganjani.
Kabla Amata hajamwona mtu huyo aliona kwanza mlango ukisukumwa taratibu na domo la bastola lililofungwa kifaa cha kuzuia sauti likitangulia na kutema risasi nne mfululizo kuelekea kitandani. Alitamani kucheka lakini akajizuia kwa kuwa haikuwa mahala pake.
“Shiit!” sauti kutoka nje ya mlango ikasikika na mara yule mtu akaingia mzima mzima. Alikuwa ni pande la mtu, mwanaume aliyevalia jeans na fulana nzito, usoni mwake alivaa soksi iliyoficha uso wake na kuacha macho tu.
“Karibu katika mikono ya shetani!” Amata aliongea kwa sauti nzito iliyomfanya yule bwana kushtuka na kusimama ghafla, “nilitaka uje na umekuja mwenyewe, ondoa magazine kwenye silaha yako bila kuigeuka,” akamwamuru.
Yule bwana akataka kuuvuta mkono wake wa kushoto kufanya hilo.
“No! tumia mkono huohuo ulioshika bastola,” akamwambia, naye akafyatua ile magazine ikaanguka chini na risasi zake zikatoka ndani yake na kutawanyika, “weka na bastola yako chini,” akamwambia, naye akafanya hivyo.
“Geuka huku mikono yako ikiwa kichwani, ukiniletea ujinga nakumaliza, sina urafiki na viumbe vibaya kama ninyi, mnaotoa roho za watu bila sababu,” akamwambia na Obobo akafanya hivyo, sasa wakatazamana uso kwa uso.
Akainua glass yake na kupiga funda moja la kinywaji, kabla hajamaliza kinywaji kile. Alijikuta bastola yake ikimtoka mkononi mwake ka teke kali alilopigwa na Obobo. Obobo skstus kando kwa miguu yake miwili na kusimama tayari kwa mapigano. Amata akachukua ile chupa na kumimina kinywaji kwenye glass yake bila wasiwasi wowote, huku Obobo akimtumbulia macho kwa kitendo hicho. Akiwa katika kuzubaa huko chupa ile ya pombe ilitua kichwani kwa Obobo na kuvunjika, Amata aliruka kutoka katika kiti alichokaa na kutu mbele ya huyo jamaa kisha konde moja zito likatua shavuni mwa Obobo na kumpeleka chini bila kipingamizi. Obobo akajibetua na kusimama wima kisha akaruka samasoti na mguu wake wa kwanza ukamkosa Amata ule wa pili ukatua begani mwake. Maumivu nakali yakalipenya bega la Amata, hakujali, konde zito la Obobo likaufuata uso wa Amata naye akaepa, la pili akaepa, la tatu akaepa na kuruka ‘beki’, kwa mtindo huo wa sarakasi akampiga mateke mawili mazito chni ya kidevu, Obobo akajibamiza ukutani.
Amata akatua kitandani na bila kuchelewa, akateremka na kupeleka mapigo matatu ya karate yaliyompata Obobo sawasawa na kumsababishia kizunguzungu, Obobo akajitupa chini na kuiwahi bastola ya Amata lakini Amata alilitambua hilo, akavuta teke moja kali lililotua shavuni mpaka karibu na sikio na kumtupa Obobo upande wa pili, Amata akaiokota ile bastola na sekunde hiyo hiyo, Obobo akona hatari iko upande wake, alijikunja na kujikunjua kama samaki akaruka na kujipiga kwenye kioo cha dirisha, akadondokea nje na kupotelea mtaani.
“Shenzi kabisa, hiyo nimekuonjesha, kazi bado inakuja!” Amata alijisemea mwenyewe huku akiwa ameshalifikia lile dirisha na kumwona mtu huyo akipotelea mitaani.
Akaiendea ile bastola ya Obobo pale chini na kuiokota kisha akazipachika zile risasi katika magazine na kuiweka mahala pake, kwa mikono yake miwili, kwa kutumia ule wa kushoto akai-slide kwa upande wa juu na kuruhusu risasi ya kwanza kutumbukia chemba. Bastola la kizamani kweli kweli lo! Akawaza huku akiiangalia angalia, ilikuwa ni Smith and Wesson.
§§§§
Hali ya sintofahamu iliwakumba Wabunge baada ya kukosa kusomwa ile ripoti iliyodaiwa kuwa ina majina ya watu waliokwapua pesa za ESCROW. Spika alipotangaza kuwa swala hilo litajadiliwa kikao kijacho wengine wakazomea na wengine wakakosa ustaarabu hata kuamua kutoka nje.
“Kwa nini isisomwe? Haijaibwa wala nini, wameikalia tu kuficha maovu ya wakubwa, hii nchi hii mpaka tutoke hapa tulipo labda aje kuongoza Yesu au Mtume Muhamad” alilalama mmoja wa waheshimiwa huku akiingia kwenye Shangingi lake tayari kwa kuondoka. Ilikuwa ni vikundi vikundi vya watu watatu au wane; hapa na wengine kule, kila mmoja akilaumu kutosomwa kwa taarifa hiyo toka kwa Mheshimiwa Kibanio.
Watu alijawa na shahuku ya kusikia majina hayo yakitajwa hadharani lakini haikuwa hivyo wakati wengi wao wakiamini kuwa faili hilo halikuibwa bali ni mbinu za wakubwa ni wachache tu walioumiza kichwa kuwa kimtokea nini hata faili hizo zipotee katika mazingira ya kutatanisha.
Katika moja ya vyumba vya mikutano nyeti ndani ya jengo hilo la Bunge kulikuwa na kikao kinachoendelea, kikao cha kamati ya usalama ya Bunge. Agenda kuu ya kikao hicho ilikuwa ni kuona juu ya upotevu wa faili hizo.
Mvutano mkubwa ulikighubika kikao hicho baada ya kusikiliza taarifa ya Katibu wa Bunge.
“Wewe si ndio mwenye funguo itakuwaje hilo faili lipotee?” aliuliza mmoja wa wajumbe. Wakati wakiendelea kubishana mara akaingia Spika ambaye muda wote alikuwa akifunga kikao cha Bunge, akakaribishwa na kupewa taarifa ya wapi kikao kimefikia, alipojiridhisha na taarifa hiyo akawasilisha pia taarifa ya upotevu wa nakala kama hizo ambazo zilikuwa mikononi mwa Mheshimiwa Kibanio na wakati huo taarifa za kuvamiwa kwa Mheshimiwa Segeratumbo nazo zikawasilishwa.
“Yote haya tulikuwa hatujayasema kwa sababu za kiusalama, lakini kumbe tumekosea,” akasema Spika.
“Kwa hiyo kuna mtu au watu ambao wanazisaka kwa udi na uvumba? Basi haina haja ya kuumiza kichwa kwa maana watu hao tunao humuhumu,” mjumbe mmoja akatia neno katika kikao hicho.
“Isiwe tunazugana hapa!”
“Tunazugana vipi? Msesema amekufa kwenye ajali ya ajabu tu, na hizi nyingine ndio zinaleta utata mara mia, tumekwisha.”
Kikao kilichukua muda mrefu, majadiliano yalifikia muafaka kuwa uchunguzi ufanyike na ikiwezekana wanaohusika wachukuliwe hatua.
“Mheshimiwa Msesema alipopata ajali alikuwa na mwanamke mle ndani ya gari hivi haiwezi kuwa ni mmoja wapo?” mjumbe mmoja aliogeza.
Kila mtu alishangaa kwa taarifa hiyo hakuna aliyeijua kwanza ijapokuwa wachache wao waliichukulia ni hali ya kawaida. Jopo hilo likaamua kuwa yule mwanamke akamatwe kwa mahojiano kisha baada ya hapo ndio wajue nini chakufanya. Maamuzi yakaandikwa na kuwekwa katika faili.
“Lakini nitaomba msubiri kwanza kabla sijatoa go ahead ya hili,” Spika aliwaambia.
“Aaaah kikao cha kamati kimeamua!” mwenyekiti wa kamati akaunguruma kwa jazba.
“Nina maana yangu kuwaambia hilo…”
Wakakubaliana na kile kikao kikaisha. Kila mtu akatawanyika.
***
“Kwisha habari yao! Bado kumkomesha mmoja, yule anajifanya mjanja,” Mheshimiwa Nnandi aliwaambia wenzake Kagosho na Matata.
“Tumekodi jabali, mtu anyejua kazi yake,” Matata akaongeza kwa sauti ya kilevi.
“Eti leo walikuwa na kikao cha kamati ya usalama kwa lipi? Hawajui kuwa kati yao kuna mwanetu mle! Hii nchi yetu bwana tutakula tunavyotaka, nani wa kutubabaisha?” Kagosho naye alibwabwaja.
Watatu hawa waliendelea kujipongeza kwa kula na kunywa, kila mmoja kichwani mwake akifikiri tu jinsi gani ya kutumbua pesa hizo ambazo si muda zimetolewa kwenye akaunti hiyo na kuwafikia walengwa kwa mbinu tofauti.
MIAKA MIWILI ILIYOPITA
BENKI KUU YA SERIKALI
GAVANA WA BENKI HIYO alikuwa katika kikao kizito katika moja ya ofisi nyeti za serikali, katika kikao hicho agenda kuu ilikuwa ni jinsi gani ya kifunga hiyo akaunti yenye mabilioni ya pesa yaliyoingia kutokana na mradi hewa wa nishati ya umeme.
“Watu tumefanya kazi kubwa kuhakikisha hili linawezekana, sasa ni wakati wetu kula njasho letu,” mmoja wa wajumbe alikiambia kikao.
“Ni sawa usemalo, lakini unajua kuwa hizi fedha ni za umma?” Gavana aliuliza.
“Za umma! Kivipi? Hivi we unajua tumestrago kiasi gani kufanikisha hii akaunti kunona? Watu tumetengeneza mikataba tumekwenda Thailand tukafanya yetu. Tumerisk kazi zetu ujue, si kwamba hatukuwa na plan bali pesa hizi kuja katika akaunti hii ni kosa moja dogo tulilifanya, na hili lilisababishwa na watu kama wewe,” mjumbe mwingine mwenye ushawishi kwa maneno yake alimwambia yule Gavana.
“Sawa, sasa ninachouliza ni kwa nini hizi pesa zikae hapa?” gavana aliendelea kurusha maswali.
“Swala sio kwa nini, swala ni jinsi gani tutagawa hisa za wenye nazo?” mjumbe mwingine akadakia.
“Hisa! Hisa kivipi?” Gavana akashtuka mpaka akasimama.
“Ndiyo, hisa, watu wamewekeza mapesa kibao katika mradi huu, kwa kuwa tulisema itafika wakati wenye hisa zao wapate gawio lao, na wakati huo ndio sasa,” yule mjumbe wa kwanza akasema.
“Sikilizeni, mambo ya mahesabu hasa ya pesa kama hizi hauendi hivi, wala mgawanyo haufanyiki kama mnavyofikiria ninyi. Kwa kuwa pesa hizi nilizipokea kama gavana kwa maandishi kutoka kwa kiongozi mkubwa basi na zitagawiwa mnavyotaka ninyi kwa utaratibu uleule wa kimaandishi…”
“Unamaanisha nini hapo?” mjumbe yule wa kwanza akadakia.
“…Namaanisha wale waliosaini ili ziletwe hapa na kufunguliwa hii akaunti ya Tegeta Escrow ndio hao hao wasaini kuziondoa,” yule Gavana alifafanua kwa lugha rahisi, “Isitoshe Mkaguzi mkuu wa serikali CAG lazima atakuja kufanya ukaguzi wake kwani Bunge la bajeti limekaribia,” akaongeza.
“Kwa hiyo!”
“Kwa hiyo mniache nifanye mawasiliano na hao watu kisha nitawajulisha nini kimeamriwa,” Gavana akamaliza.
MIEZI MITATU ILIYOFUATA
TAARIFA ya maandishi iliyosainiwa na watu kadhaa wenye vye vikubwa vywenye maamuzi ya juu ilifika katika ofisi ya Gavana wa fedha. Ijapokuwa alitumbua macho lakini hakuwa na la kusema au kuamua. Pamoja na taarifa hiyi iliambatanishwa orodha ya majina ya watu na akaunti zao za benki ili pesa hizo zielekezwe kwenye akaunti hizo kwa viwango vilivyopangwa.
“Come on!” alijiseme hukua kijiegemeza kwa nguvu katika kiti chake cha kunesanesa. Alipoona akili yake haifanyi kazi akainuka na kutaka kutoka ofisini aliposhika kitasa cha mlango simu yake ya mezani ikaita, akasimama kwa hofu na kuiangalia. Kwa masikitiko akairudia na kunyakuwa kutoka pale kwenye kikalio chake.
“Hello…”
“Umepata barua elekezi juu ya zile fedha ulizoziita za umma?” ile sauti ikamwuliza.
“..Ndi-ndi-yo nime-pa-pata!”
“Ok, sasa fanya kama ilivyokuagiza,” ile sauti kaendelea kusema.
“…La-la-ki-n…”
“DO IT NOW, THERE IS NO LAKINI HAPA!” ile sauti ikafoka. Yule Gavana akakaa juu ya kiti chake huku mwili ukitiririkwa na jasho la kutosha, ingawaje kiyoyozi kilikuwa kikijitahidi kuifanya hewa ya humo ndani kuwa tulivu lakini sasa ilikuwa ni mithiri ya tanuru la kuokea mikate. Kila alichokishika kilikuwa cha moto kwake. Akaikamata ile barua kwa mara nyingine, akairudia kuisoma kwa makini na baadae akitafsiri kwa kiingereza ili aone kama maana zinafanana. Mwili wake ulikuwa ukikumbwa na hali mbili mara baridi na mara joto, kipindi Fulani alijipepea kwa gazeti na wakati mwingine akafunga vizuri tai yake, ilikuwa ni sintofahamu ndani ya kichwa chake. Muhuri wa moto uliogongwa na mtu aliyeonekana kuwa na nguvu ulionekana bila shida mwisho wa ile barua na nembo yake tukufu ilikuwa pale.
‘Sina cha kufanya lakini huu ni msala huu!’ akawaza na kuwazua kisha akainua simu yake na kupiga kwenda kwa mtu mwingine. Dakika moja tu alikuja kijana mmoja nadhifu na kupewa maagizo yale, naye bila ajizi maadam ‘mkubwa kasema’ akaenda zake na kufanya uhamisho wa fedha hizo.
Gavana alihisi kichwa kikimuuma, alihisi joto kali kwa mbali aliona kama mwili wake unapoteza nguvu, aliamua kutoka ofisini na kumwomba dereva wake kumfikisha hospitalini haraka kwa uchunguzi.
***
Baada ya zoezi hilo kukamilika watu wengi wakaingiziwa pesa mamilioni kwa mabilioni wakiwamo wafanyabiashara wakubwa, viongozi wa dini, wananchi wa kawaida, viongozi wa serikali na hata watoto wa vigogo waliyakwaa mapesa hayo. Taarifa hiyo iliastua wananchi na wabunge wanaopenda haki na hatima ya Taifa lao.
“Huu ni ufisadi mkubwa, haiwezekani,” mmoja alijisemea hilo.
“Yaani wamegawana!” mwingine alijikuta akitamka.
“Hii nchi inatisha, inabidi tufike wakati tumwogope Mungu!” huyu naye alijikuta akitamka baada ya kusoma habari hiyo gazetini.
“Mamaaaaa we! Hata huyu yumo, mijitu haina aibu,” mwingine alijikuta anapiga kelele.
SEHEMU FULANI FULANI – Siku nyingi tu zilizopita
“Sikiliza! We usiogope, nitatumia akaunti yako ile ya P.O.T Bank, nitaingiza kama Bilioni 19.99 hivi, wewe pale kuna kamisheni yako umesikia kijana!” Mzee Fulani alimwambia kijana mmoja katika ofisi yake mchana huo. Siku hiyo aliwaita watu kama saba hivi ambao alikuwa akiwaamini kuliko anavyojiamini mwenyewe.
“Lakini mzee…”
“Sikiliza wewe: Unataka pesa?”
“Pe-pe-pe-sssa? Ndi-yo, the, kwani kuna asiyependa pesa?” yyle kijana alijibu kwa kuweweseka.
“Sasa katika hizo pesa nitakupa shilingi Milioni mbili na nusu,”
“Hapo sawa! Hamna shida, akaunti yangu ndiyo hiyo hiyo mzee,”
Kila mmoja alijua ni jinsi gani atasafirisha pesa zake kutoka kwenye akaunti hiyo na kufikia akaunti yake binafsi. Hali hiyo wapenda uzalendo hawakuweza kuvumilia, walipigia kelele, wakatangaza maredioni, wakaandika magazetini, wananchi wakakasirika, wakapaza sauti zao dhidi ya dhukuma hiyo ya haki.
Kati ya watu walioibuka katika sakata hilo kama wapenda uzalendo alikuwa Mheshimiwa Msesema, Segeratumbo na Kibanio.
USIKU FULANI
“Pesa tumepata tena nyingi mno ambazo tutakula milele amina, lakini kuna vijitu viko vitatu vinataka kuleta tabu, hivi wanajua tumetoa jasho kiasi gani kutengeneza hii hela?” Mheshimiwa Matata akawauliza wenzake.
“Wajue wapi? Wanataka wapate sifa tu wale,”
“Dawa yao iko jikoni, tena haina haja ya kuwafanyia mbaya ila tuwashawishi tu nao wenyewe wataingia mtegoni,”
“Kwa ngapi?”
“Milioni mia mbili tu kila mmoja akamalize shida zake,” Matata akamaliza huku Nnandi na swahiba wao wakikata kilaji.
***
“Ngriiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiii! Ngriiiiiiiiiiiiiiiiiiii!...” Msesema alishtuliwa na simu iliyo katika kijimeza chake pembeni tu mwa kitanda, akamruka mkewe na kushuka upande wa pilia akinua simu hiyo.
“Unaongea na Mheshimiwa mkubwa sana, Bwana Matata!”
“Ndiyo Comrade!”
“Najua una njaa kama walivyo wanaojiita Wazalendo wenzio, yeyo anayejiita mzalendo huyo ana njaa tu. Najua mbinu zako na wenzio Kibanio pamoja na Segeratumbo. Sasa kuna Milioni mia tisa; tatu kwa kila mmoja, kesho asubuhi kijana wangu atakuletea hundi…”
“Hapana! Siwezi kabisa, hiyo ni rushwa, na rushwa ni adui wa haki, mimi ni Mzalendo hata kama wazalendo ni wenye njaa basi ninyi mabwanyenye mistake wazalendo tufe njaa, tunazitaka pesa za umma zirudi zinufaishe wananchi. Tazama watoto wetu hawana vitabu vya ziada wala kiada, madawati ni shida, madawa hospitalini ni kitendawili, huduma za afya ni dhoofu, vifo vya akinja mama na watoto vinaongezeka ilhali ninyi mnahubiri kupungua kwa asilimia zake. Kuweni na huruma jamani, hizo ni pesa za umma na tutapigana mpaka mwisho. Kumbuka kwamba Mzalendo akichoka damu itaongea…” akakata simu.
“Pumbav sana, limekata simu, linajifanya linajua kumbe linaungua na jua, wacha wafe masikini,” Mheshimiwa Matata akawaambia wenzake.
Ushawishi kwa watu hao watatu ili wakubali kutoufuatilia mpango huo viligonga mwamba. Ndiyo kwanza wakawachochea na wao wakauwasha moto bungeni, mpaka ikapelekea Katibu wa Bunge na Katibu wa Wizara ya Nishati na Madini kumuomba Mkaguzi Mkuu wa Serikali kufanya ukaguzi wa akaunti hiyo. Ukaguzi huo ulilenga kufanya uchunguzi wa kina ambao ungetoa taarifa kamili yenye kuonesha hali halisi kuhusu miamala (transactions) kwenye akaunti maalum ya Tegeta Escrow kisha kutoa taarifa kuhusiana na ukaguzi huo.
MIEZI SITA BAADAE
Ofisi ya Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ikauomba umma uvumilivu kwa kuwa ukaguzi huo ulichukua muda mrefu kutokana na hadidu zilizotolewa kuridhiwa na ofisi ya Bunge pamoja na ile ya Wizara ya Nishati na Madini.
Taarifa hiyo kwa umma ilielezea na kufafanua kuwa…
‘ Kwa kuwa Hadidu za Rejea pekee haziwezi kuonesha ukubwa wa kazi bali utekelezaji wa kazi yenyewe ndio unaoweza kutoa taswira halisi, ni vyema umma wa watanzania ukatambua kuwa Ukaguzi huu haujaweza kukamilika kwa kipindi kilichokadiriwa awali hivyo ukaguzi unaendelea kwa kuzingatia Hadidu za Rejea na kifungu cha 29 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya mwaka 2008.’
Kwa kuwa wahenga walisema mvumilivu siku zote hula mbivu ndipo ilipofika wakati ambapo ukaguzi huo ulikamilika na hekaheka za huku na huko zikaanza. Watu matumbo yakawa moto, miguu haifanyi kazi wengine mahospitalini. Taarifa hiyo ya ukaguzi ilianisha majina ya watu waliojichotea mifedha hiyo na akaunti zote ziliainishwa wazi wazi.
Waheshimiwa; Msesema, Segeratumbo na Kibanio walizipata taarifa hizo kutokana na vyanzo vyao na kuahidi kutaja majina ambayo hayajaorodheshwa katika orodha hiyo.
“He! Kumbe kuna wengine hapa hawajorodheshwa, tobaaaah!”