SEHEMU YA SITA
“Kijiji chote kimeteketezwa kwa moto!” Waziri wa mambo ya ndani alisikika akiongea kwa kututumka, mbele yake alikuwa Madam S amesimama.
“Huyo ni shetani, na razima utawala wake usambaratishwe na watenda mema,” Madama akajibu.
“Sikiliza Sellina,” Waziri wa Mambo ya Ndani akasimama kwa msisitizo, “Nahitaji uchunguzi wa siri na ikiwezekana huyu mtu akamatwe,” akasisitiza.
“Sikiliza mheshimiwa, usipeleke jeshi kuuuubwa, acha nikafanye kazi, ikifika wakati wa kuhitaji vijana wako nitakwambia, ila kwa sasa waache wale wa Bagamoyo kwa kuwa ni eneo lao, naondoka sasa,” akamaliza Madam S na kutoka mle ofisini.
Akiwa ndani ya gari yake akampigia Amata na Gina wakutane ofisi ndogo, akaitazama saa yake tayari ilitimu saa 4 usiku, ‘kweli kazi za serikali ni za kujitolea, watu wamelala sisi tunahangaika,’ akawaza mwenyewe huku akiicha barabara ya Ohio na kuchukua ile ya Garden kuelekea ofisini kwake.
KITUO CHA POLISI CHA SULENDER BRIDGE
“Bagamoyo, Ba- ba –gamo-yo koh! koh! koh!” Kamba Sebule aliongea mengi baada ya kipigo cha polisi kukolea mwilini mwake.
“Bagamoyo kubwa, sehemu gani?” Kamanda akauliza.
“Si nime-wa-jib…”
Mkanda wa jeshi ukatua mgongoni mwake na kumletea maumivu makali.
“Unafikiri tunacheza hapa? Tuambie ni kijiji au ni sehemu gani?” mmoja wa polisi aliuliza.
“Kisi-wa-wa-ni, Kale-b-be” mwishowe akatamka ijapokuwa kwa tabu kidogo.
Kamanda Amata akatikisa kichwa juu chini huku akimtazama Gina. Simu yake ikaanza kufurukuta mfukoni akaitoa na kutazama ‘Madam S’ ilijiandika juu ya kioo, akaingiza tarakimu fungushi na kuiweka sikioni.
“Tukutane wodini haraka mama anaumwa Tena Sana Aisee,” ilikuwa ni ujumbe wa sauti aliyoutuma. Akageuka na kumtazama Gina, kisha akarudisha macho kwa wale vijana wa polisi.
“Sasa muhifadhini huyu mpaka nitakapowapa amri nyingine, sisi tunatoka,” akawaambia wakati wakiondoka na kuingia garini.
† † †
OFISINI KWA MADAM S
NDANI YA OFISI HIYO Madam S alikutana na vijana wake wote watano, aliwapa ujumbe aliyoupata kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Kwa harakaharaka alionekana hayuko sawa kwani alikuwa akifanya vitu na kuongea kwa harakaharaka.
“Kijiji cha Kitopeni kimevamiwa na kuchomwa moto huku raia wakipigwa vibaya leo jioni hii,” madam aliongea harakaharaka huku akiwa kasimama wima.
“Kitopeni Bagamoyo?” Gina alidaka kwa swali.
“Ndiyo!”
Wakatazamana kisha wakarudisha macho kwa Madam S, hakuna aliyekuwa na swali wala lakuongea ila ndani ya macho yao kulibaki na mshangao wa dhahiri kabisa.
“Kitopeni ndo wapi?” Amata aliuliza.
“Ni usawa ule ambao ndege yenu ilidunguliwa,” akajibiwa na Madam S.
“Bila shaka ni wao, haina kupoteza muda TSA Kazini,” Chiba alisema huku akinyanyuka na kuungwa mkono na wenzake.
“Bila shaka, nimezuia polisi wa huku kufika kule kwanza nataka sisi tuingie kwanza ili tufanye uchunguzi wa awali ambao kwetu ni uchunguzi wa msingi wa kumjua mhalifu,” madam S aliwaambia kisha kila mmoja akaanza kuchukua kinachomfaa katika stoo iliyojengwa ndani humo.
“Kamanda Amata, una jeraha, halijapona, ni vyema usifanye mikiki mikiki yoyote ile,” Jasmine alimwambia Amata.
“Hapana, wacha niende, kama ni Pancho basi mara hii hatakiwi kuishi, huu ni uhalifu mkubwa sana haijawahi kutokea kwenye historia ya nchi hii,” Amata akaunguruma.
Dakika moja iliyofuata, Land Cruiser V8 ilifuatana na Range Rover zote zikielekea Kitopeni, ndani yake kulikuwamo na hao vijana watano. Gari ya kwanza alikuwapo Amata, Chiba na Gina ambaye aliukamata usukani na ile ya nyuma alikuwamo Jasmine na Scoba pamoja na Madam S. mwendo waliokuwa wakipita nao huku mbele wakitanguliwa na pikipiki la polisi ulikuwa si wa kawaida. Kama wananchi walizoea kuishangaa misafara ya viongozi kwa mwendo kasi basi hii ilikuwa funga kazi. Lile pikipiki liliwaongoza mpaka Tegeta na kuwaacha pale waendelee wenyewe kwani walishapita eneo la msongamano wa magari.
KIJIJI CHA KITOPENI
WANANCHI WA KITOPENI walikuwa wamejikusanya pamoja, wengine wakiomboleza vifo wengine wakiwa hawana makazi na wengine maumivu makali ya majeraha waliyoyapata katika shambulio hilo.
TSA waliteremka kutoka katika magari yao na kuanza kufanya chunguzi zao za hapa na pale kwa kuhoji na kutazama hali halisi ya eneo hilo.
“Mnasema hao watu walikuwa wangapi?” Amata alimuuliza mmoja wa wanakijiji aliyeonekana kujishughulisha sana kuwasaidia wenzake.
“Walikuwa kama kumi au kumi na tano walikuja wakitokea mashambani huku,” Yule kijana alieleza.
“Tuliwaona wanaibuka kule baharini sisi tukakimbia,” mmoja wa watoto aliyekuwa hapo alisema. Kamanda Amata akiwa na Chiba na Madam S walisikiliza maelezo ya wahanga wote walioweza kuongea, kisha wakaitana pembeni.
“Sikia Chiba na Amata hawa bila shaka wamekuja kwa kupiga mbizi,” Madam aliwaambia.
“Kwa maana hiyo hawa jamaa wanaweza kuwa na makazi eneo hilihili,” Chiba akaongeza.
“Kisiwa cha Kalebbe,” Kamanda akawaambia kisha wakamwita tena Yule kijana na kumwomba awatajie majina ya visiwa vilivyo karibu na eneo hilo. Akawatajia kwa majina na kuwaonesha kisiwa hicho cha Kalebbe ambacho kilikuwa katikati ya visiwa vingine.
“Mnafikiri pale atakuwa anaishi mtu? Sio rahisi kisiwa kile kule ndio kuna mtu kajenga nyumba yake ndogo,” Yule jamaa akaonesha kisiwa ambacho kina jingo la kawaida tu.
“Ok,” Madama akaitikia na kumwacha Yule kijana kuondoka.
“Madam, baada ya kumbana Yule Kamba Sebule kule polisi kasema wana maskani yao kisiwa cha Kalebbe, so nafikiri sasa ni kuanza uchunguzi wa kisiwa hicho mara moja. Cha muhimu hapa tuache polisi wafanye kazi na sisi tuondoke tukajipange vyema, wasijue kama tumeingia hapa,” Kamanda akatoa maelekezo.
“Sawa, twendeni tukapige kambi Hoteli ya Ocean Breeze,” Mada akawaambia na wote wakaingia kwenye gari na kuondoka huku wakiacha polisi wakiendelea na itifaki zao.
HOTELI YA OCEAN BREEZE - BAGAMOYO
KAMANDA AMATA na GINA walikuwa nje kwenye kibaraza cha ghorofa ya nne ya hoteli hiyo ambayo ilitazamana na Bahari ya Hindi katika eneo la Bagamoyo karibu kabisa na bandari ya mji huo mkongwe. Pembeni ya meza yao kulikuwa na darubini kubwa ‘Oberwerk’, yenye nguvu kuliko zote duniani, ilikuwa na urefu wa inchi 24 iliyosimamishwa kwenye stendi madhubuti.
Huku wakiburudika na kinywaji lakini akili zao zilikuwa katika kisiwa cha Kalebbe ambapo ndipo hasa walipoamini adui wao walipo.
“Tutaingiaje pale?” Gina aliuliza.
“Simple, ngoja nuru iondoke tuingie kazini”.
Gina akatazama saa yake ilikuwa tayari saa tisa za mchana, jua linazidi kusogea Magharibi. Simu ya Amata ikaita pale mezani.
“…hello… Madam!” akaipokea.
“…vipi kamanda, kuna lolote huko?”
“…yeah, tunaangalia bado lakini hatujapata ufumbuzi ila taratibu tutapata,”
“…ok, kazi njema, niko na vijana hapa. Tunawaomba mfanye kazi tu na si vinginevyo,” kisha wote wakacheka.
Amata akainuka na kuingia chumbani akachukua simu na kupiga mapokezi akomba kuletewa vinywaji.
Dakika tatu baadae, kijana aliyevalia nadhifu kabisa, nguo za kitamaduni akaleta vinywaji hivyo mpaka pale walipoketi.
“Asante sana,” Kamanda akamshukuru.
“We unaitwa nani?” akamwuliza.
“Naitwa Nassoro,”
“Nassoro unajua kisiwa cha Kalebbe?” Kamanda akauliza. Nassoro akamtazama kwanza kabla ya kujibu swali hilo.
“We cha nini?” akajibu kwa swali.
“A aaaah! Usiwe kama Watanzania kwa kujibu swali kwa swali. Napenda kwenda kukitembele kama utanipa maelezo zaidi juu yake,”
“Kile ni kisiwa cha mashetani, watu huwa hawaendi kule,” Nassoro akajibu kwa kifupi.
“Nahitaji kwenda,” Kamanda akamwambia Nassoro.
“Sawa, karibu sana,” Nassoro akajibu na kuondoka.
Gina na Amata wakatazamana, ‘anajua kitu huyu’ kila mmoja akawaza sawa na mwenzake. Amata akainua mkono na kubofya saa yake hapa na pale kisha akaisogeza karibu na kinywa chake.
“…muweke jichoni, amevaa shati la kitenge na suruali nyeusi na kofia ya kitenge, ni mwenyeji wa hapa tulipo…”
“…copy…” Chiba akajibu kwa njia ileile.
Mara kwa mara Gina alikuwa akisimama na kuiendea ile darubini na kuchungulia ndani yake kuona kama kuna lolote geni, na alipomaliza kuchungulia alibonyeza kidubwasha Fulani na kupiga picha ya hicho anachokiona, na ile taswira ilisafiri mpaka kwa Chiba kwenye mashine ndogo mfano wa simu na wao waliweza kuitazama vizuri na kuangalia kama kuna mabadiliko yoyote.
Mara hiyo saa ya Kamanda Amata ikaanza kumfinya, akaitazama kwenye kioo na kubofya mahala Fulani kisha akapachika kifaa chake sikioni na kusikiliza.
“…yuko jichoni, kaingia mapokezi, anatumia simu ya mezani…” Chiba akamwambia Amata.
“…tegemea ugeni…”
Wakakata mawasiliano, Amata akarudisha macho kwa Gina.
“Vipi?” Gina akauliza.
“Poa,” Amata akajibu na kusimama, akavuta hatua chache kuingia chumbani, akauelekea mkoba wake na kuchomoa bastola moja, akaijaza risasi za kutosha. Nyuma yake akahisi kama kuna mtu kasimama, akahisi mikono ikigusa mabegani, hakugeuka kwani ulaini wa mikono hiyo alishajua ni nani anayemgusa.
“Vipi ushaanza kufikiri kuua!”
“Akili yangu tayari ishaanza kuzunguka, nahisi kutokea hatari ndani ya muda mfupi ujao, jiweke tayari nawe pia,” akamwambia Gina na kumgeukia. Gina akaweka mikono yake kiunoni mwa Amata.
“Nimemiss!” akamwambia.
“Sio wakati wake,” kamanda akajibu na kujitoa katika himaya ya Gina. Akaipachika bastola yake kiunoni na kuiendea ile darubini, akaweka macho yake pale na kutazama tena. Mara hii kitu kipya kikaonekana, kwa mbali aliona kitu cheupe katikati ya bahari, ‘Nini kile?’ akajiuliza na kukiweka vizuri katika muonekano sawa.
Boti, ilikuwa ni boti iliyoonekana kuja kwa kasi na kutimua maji hayo kuyafanya kuwa meupe, akabonyeza kile kitufe na kupiga ile picha. Akaendelea kuangalia ile boti iliyokuwa ikisogea kwa kasi, sasa aliweza kuiona vizuri, ndani yake kulikuwa na watu watatu, wanaume wawili, waliovaa nguo nyeupe za kisasa, mmoja alikuwa akiongoza boti hiyo na mwingine alikuwa nyuma kabisa. Katikati yao kulikuwa na mwanadada mrembo sana aliyeketi kwenye kiti na bilauri iliyojaa kinywaji fulani, akabonyeza tena kile kitufe na kuisafirisha ile picha.
† † †
“Ugeni kama ulivyotabiriwa,” Chiba akamwambia Madam S huku akimpa kile kimashine ambacho kilimwezesha kuona zile picha vizuri. Muda huohuo akamwona Yule kijana akitoka katika chumba Fulani na kuelekea nje, Madam S akamwita kwa mruzi, Yule kijana akageuka na kusogea pale mezani.
“Nahitaji vinywaji kijana,” akamwambia.
“Oh! Samahani kuna mgeni nampokea hapo gatini naomba nikuitie mhudumu mwingine,” Nassoro akajibu.
Madam S akamshika mkono kwa nguvu na kumkazia macho.
“Kwa nini unataka kupoteza bahati kijana,” akamwangalia juu mpaka chini.
Nassoro akajikuta njia panda, akashindwa kuamua, alijuwa wazi kuwa kumkatalia huyu mama kama mteja haiwezekani na kutokwenda kumpokea huyo mgeni nako ni jambo lingine.
“Ok, niitie mtu mwingine,” Madam akamwambia na kumwacha. Nassoro akaenda na kumwita mwhudumu mwingine wa kike ili amsikilize Madam. Yule mwanadada akaifikia meza waliyoketi Madam S na Chiba.
“Samahani, huyo anayekuja nhuko ni mgeni gani?” akamwuliza Yule mhudumu badala ya kumuagiza vinywaji.
“Malkia, Malkia wa Kalebbe!”
“Malkia?” Madam akauliza na wakati huohuo Yule mwanadada aliyejulikana kama malkia akaingia akiwa anafuatana na Nassoro na moja kwa moja akaenda kuketi kwenye meza iliyopambwa maua mazuri kabisa. Kulikuwa na siti mbili moja ikabakia wazi. Vazi alilovaa mwanadada huyo ndiyo kilikuwa kivutio kingine, alivaa bikini nyeupe na juu yake akavaa vazi linguine jeupe lakini lililokuwa wazi sehemu ya mbele na kuruhusu mwili wake kuonekana.
Nassoro akasogeza vinywaji pamoja na kibweta cha kuwekea jivu la sigara, Yule malkia mwenye mwili wa kisichana zaidi aliketi na kukunja nne huku akiwashiwa sigara na kijana huyo na kuanza kuvuta taratibu.
Madam S akamtumia ujumbe Kamanda Amata juu ya huo ugeni. Haikupita dakika moja, Kamanda Amata akajitokeza kutoka katika ngazi na kuvuta hatua fupifupi kuielekea ile meza. Akiwa ndani ya suti nadhifu nyeupe.
† † †
“Bila shaka hautajiuliza mengi kwa mimi kuketi mbele ya msichana mrembo kama wewe, malkia wa kalebbe, hakika Mungu anajua kuumba kwa maana jinsi ulivyo hakuna mwanaume rijali atakayepita mbele yako bila kujikwaa hata kama sakafu ni ya marumaru,” Amata akaanza swagga na kuketi huku akichukua matunda madogo ya strawberry na kuyatia kinywani.
Malkia huyo alijikuta akiangua kicheko cha mwaka kwa maneno hayo matamu nay a kufurahisha.
“Hakika kuna wanaume wameumbwa kufurahisha wanawake, lo, ulifikiri nini kuzungumza yote hayo?” akauliza huku bado akiendelea kucheka. Nassoro mhudumu wa Malkia huyo akawasili pale mezani na kumtaka radhi Amata kuicha meza ile.
“Oh, asante Nassoro, lakini mwache, mwache kanifurahisha sana huyu, mpe kinywaji tafadhali,” malkia akamwambia Nassoro naye akafanya hivyo. Ingawa juu ya meza ile kulikuwa na kinywaji ambacho bado kilijaa pomoni, lakini Amata aliletewa kinywaji kingine kabisa, kikawekwa mezani na kumiminwa kwenye bilauri safi, akaiinua na kuipunga juu kisha Yule malkia naye akafanya hivyo wakagonga cheers kwa afya.
“Nitasikia raha sana nikikunywesha japo kidogo,” Amata aliendelea na ubembe wake.
“Oh! No! kinywaji ni kwa ajili yako, enjoy” akamwambia, Amata akakiinua na kukinywa chote kisha akaishusha ile bilauri mezani.
“Waoh, you are so strong man,” (wewe ni jasiri)
“Yes I am,” (ndiyo) Amata akajibu. Mazungumzo yakaendelea ikiwa ni pamoja na kujishana kila mmoja anapoishi, Yule mwanadada aliyejitambulisha sasa kwa jina kamili la Zulekha alimwambia mengi sana juu ya kisiwa cha Kalebbe.
Nusu saa ikapita katika mazungumzo yao Amata hakuendelea kunywa kile kinywaji ila sasa alikuwa ni mzungumzaji zaidi kila Zulekha alipomhamasisha kunywa zaidi yeye aliishia kumimina tu, akimwambia ‘usijali nitakunywa’.
“Utapenda kunitembelea?” Zulekha akauliza.
“Yeah, hata sasa,” kamanda akajibu na mara hiyo, Zulekha akainuka na kumpa mkono kamanda Amata, wakatembea kwa hatua za madaha kuelekea gatini ambako ile boti bado ilikuwa ikimsubiri. Wakaagana na Nassoro na kuondoka zao.
† † †
Gina aliinuka kitini na kuiendea ile darubini, akaanza kuchungulia na kuiona ile boti ikipotelea majini.
“Shit! Janaume linapenda wanawake hili..” akajikuta akiongea peke yake alipomuona Amata akiwa na Zulekha katika ile boti, akasonya na kuiacha ile darubini huku akiondoka, alipofika mlangoni, akakumnbana na Chiba na Madam S.
“Rudi ndani,” madam akamwambia huku Chiba tayari akiwa kwenye ile darubi akitazama ile boti.
“Jiandaeni kwa kazi ya kumkamata Yule mwanaharamu, Amata atatuletea taarifa kama mtu huyo yupo au la,” Madam aliwaambia huku akibofyabofya simu yake hapa na pale, akaiweka sikioni.
“Hey Scoba na Jasmine, stand by, tukutane Ocean Breeze ndani ya nusu saa, chambo tumeshatupa mtoni bado kuvua samaki,” akamaliza.
“…copy…” akajibiwa na ile simu ikakatika.