Minza Maduhu (92) Mkazi wa Mtaa wa Mwakibolo, Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu, ameuawa na kisha kunyofolewa macho na watu wasiojulikana.
Tukio hilo limegunduliwa jana Julai 31, 2023; ambapo mwili wa kikongwe huyo ambaye alikuwa akiishi peke yake, ulipokutwa na mjukuu wake ambaye alikuwa akienda kumhudumia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Edith Swebe, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuahidi kulingumzia zaidi baada ya kupokea taarifa kamili kutoka kwa wasaidizi wake.
"Jeshi la Polisi linaandaa taarifa kamili itakayotolewa kwa vyombo vya habari baadaye," amesema Kamanda Swebe alipoulizwa kuhusu mauaji hayo.
Akisimulia tukio hilo, Anna Maduhu, ambaye ni mjukuu wa kikongwe huyo, amesema alimkuta bibi yake akiwa amelala kitandani huku damu zikiwa zimegandana kichwani.
"Tulikubaliana niwahi kuja asubuhi ili nikasage mahindi, huwa nina kawaida ya kuja, kisha ninamuita dirishani, na yeye ananifungulia mlango alafu ninaendelea na kazi, lakini siku hiyo hakufungua nilipotazama mlangoni ulikuwa umefungwa kwa nje," amesimulia Anna.
Ameongeza kuwa baada ya kufungua mlango aliingia chumbani na kumkuta bibi yake akiwa amelala, aliendelea kumuita bila mafanikio, ndipo alipotumia mwanga wa simu kumulika na kumuona akiwa ameinamisha kichwa uvunguni na damu zikiwa zimeganda kitandani.
Kijana mkubwa wa familia hiyo Gulinja Mahangila amesema baada ya kupata taarifa ya tukio hilo alifika nyumbani kwao na kukuta mwili ukiwa umelala kichwa kikiwa kimeinamia uvunguni.
"Nilipofika nilichungulia mahala kichwa kilipokuwa kimeinamia, ndipo nilipoona damu zimeganda na tundu kwenye eneo la jicho hivyo nikatoa taarifa kwa mwenyekiti wa mtaa," amesema Gulinja.
Akizungumza baada ya kufanya uchunguzi wa mwili Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Bunamhala, Praygod Charles, amesema chanzo cha kifo cha bibi huyo ni kuvuja damu nyingi.
"Mwili wake ulikuwa na jeraha karibu na sikio na macho yote mawili hayakuwepo, baada ya vipimo; mwili umekabidhiwa kwa familia kwa ajili ya taratibu nyingine za maziko," amesema.