Makapuku Forum

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amehudhuria Mkutano wa kujadili hali ya Usalama wa Mashariki mwa Nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Mkutano huo wa dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Troika na Nchi zinazochangia Vikosi vya Jeshi vya Force Intervention Brigade (FIB) umefanyika leo Mjini Windhoek nchini Namibia.

Aidha mkutano huo umetoa tena wito kwa vikundi vyenye silaha kusitisha uhasama na kujiondoa bila masharti katika maeneo wanayoyashikilia nchini humo.

Mkutano huo pia umewasihi Wanachama wa SADC kuunga mkono Serikali ya DRC na kushughulikia hali ya usalama ya Mashariki mwa nchi hiyo kabla ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Desemba 2023.

Vilevile mkutano huo umesisitiza uungwaji mkono wa DRC katika mapambano dhidi ya makundi ya kijeshi Mashariki mwa chi hiyo ili kuleta amani endelevu, usalama na ustawi kwa wananchi wa Kongo na Jumuiya ya SADC kwa ujumla.

Kwa upande mwingine, mkutano huo umeidhinisha kupeleka Kikosi cha Jeshi la SADC kutoka katika Kikosi cha Kudumu cha Jumuiya hiyo ili kuiunga mkono DRC iweze kurejesha amani na usalama
 
Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Esther Mahawe amesema anashangazwa na Wanaume wanaojiua kwasababu ya mapenzi wakati Sensa inaonesha kuwa Wanawake wako wengi nchini kuliko Wanaume hivyo wanaweza kuoa zaidi ya Mke mmoja.

DC Mahawe amesema hayo leo Jumatatu Mei 8, 2023 wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Francis Michael ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Mbozi.

DC amesema "Mimi nawashangaa Wababa, ujue kwenye Sensa nyinyi ni wachache kuliko Wanawake sasa unamuuaje Mwanamke au na wewe unaanza kujiua wakati Wanawake wengine wanakusubiri kule ukawaoe?"

"Sisi tunataka hata mchukue mbilimbili au tatutatu lakini wewe unamuua Mwanamke halafu na wewe unajiua kwa sababu ya Mwanamke!, sio sawa Wanaume acheni kuuua Wanawake na kujiua kisa mapenziL

DC pia amewataka Wananchi wa Kata ya Nambozi kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi ili kuimarisha ulinzi na usalama kwenye maeneo yao.
 
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso @jumaa_aweso amefanikisha kufanyika kwa mchakato wa maboresho ya mfumo wa ununuzi wa Wakala Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa kushusha shughuli za ununuzi kwenye ngazi ya Mikoa tofauti na ilivyokuwa ambapo ununuzi ulikuwa unafanyika kwenye ngazi ya Makao Makuu pamoja na kwenye Kanda tisa.

Maboresho hayo yaliyofanyika kwenye kikao cha Waziri wa Maji na Menejimenti ya Wizara pamoja na Menejimenti ya RUWASA Jijini Dodoma yamelenga kuongeza tija kwenye shughuli za ununuzi za Wakala, kuongeza kasi ya ununuzi, thamani ya Fedha za Umma na kutoa fursa kwa Wazabuni, Wakandarasi na Watoa huduma waliopo kwenye Mikoa yote ya Tanzania Bara ambalo ndio eneo la kiutendaji la RUWASA.

Katika hatua nyingine Aweso amesisitiza kuwa maboresho haya ni muhimu sana kwani yatarahisisha muda wa kufanyika kwa manunuzi pamoja na kwamba swala hili ni sehemu ya kuzingatia maoni ya waheshimiwa wabunge na wadau mbalimbali katika kuongeza tija kwenye shughuli za ununuzi na ugavi kwa Wakala. Sambamba na maboresho hayo.

Waziri ameiagiza pia Menejimenti ya Wizara kuifanyia kazi changamoto ya Maafisa ununuzi na ugavi ambayo ipo RUWASA kwa kuhakikisha wanaongezwa Watumishi hao ili kuendana na mfumo mpya uliofanyika, Mfumo huo unatarajiwa kuanza kutumika mwanzoni mwa mwaka wa fedha 2023/2024.
 
Rais wa awamu ya pili wa Tanzania, Alhaji Ali Hassan Mwinyi leo anasherehekea kumbukizi ya miaka 98 tangu alipozaliwa May 08,1925 Mkuranga Mkoani Pwani.

Mzee Mwinyi alizaliwa May 08,1925 Mkuranga Mkoani Pwani kabla ya kuhamia Zanzibar akiwa mdogo, amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za Kiuongozi Tanzania ikiwemo kuwa Balozi, Mbunge, Waziri, Rais wa Zanzibar na baadaye alikuwa Rais wa pili wa Tanzania kuanzia mwaka 1985 hadi 1995 baada ya kuachiwa kijiti na Mtangulizi wake Hayati Mwalimu Julius Nyerere, na kisha yeye akamuachia kijiti Hayati Benjamin Mkapa.

Nikukumbushe tu kwamba Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan January 27 mwaka huu alitimiza miaka 63, Mstaafu Dkt. Kikwete October 07 mwaka huu atatimiza umri wa miaka 73 na kwa upande mwingine endapo Hayati Mwl Nyerere angekuwa hai April 13 mwaka huu angetimiza umri wa miaka 101, Hayati Mzee Mkapa November 12 mwaka huu angetimiza miaka 85 na Hayati Magufuli angekuwa hai October 29 mwaka huu angetimiza miaka 64.
 
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limefafanua kuwa limezifungia Baa za wazi zaidi ya 80 baada kukuta kelele zilizo kinyume cha sheria na na kwamba Baa hizo zinatakiwa kufungwa kabisa na sio kufunguliwa bila kupiga muziki.

Ufafanuzi huo wa NEMC umekuja baada ya baadhi ya Wamiliki wa Baa kusema wamefungiwa kupiga muziki pekee lakini wanaruhusiwa kufungua Baa zao, ambapo @ayotv_ imewatafuta NEMC kupata ufafanuzi zaidi “Sheria inasema maeneo ambayo yanazunguka maeneo ya Watu na kuna biashara kelele zinatakiwa kuwa 60 DBA wakati wa mchana na 40 usiku, wamefungiwa kutokufanya biashara kabisa mpaka watakapotii maelekezo yaliyotolewa, ukishafungiwa huruhusiwi kufanya chochote, ni kama kiwanda kikishafungwa uzalishaji unasimama”

Mapema leo akitangaza uamuzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Samuel Gwamaka amesema “Baadhi yao ni wale sugu ambao tumeshughulika nao tangu mwanzo na mpaka sasa wanaendelea kutusumbua, tumechukua hatua hizo za kufunga kwasababu sio mara ya kwanza kuwaonya tulishapita mara nyingi lakini hawakusikia, baada ya kuwafungia wengi wamefika kuomba msamaha na wengine wameomba wafunguliwe”
 
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ambalo leo limezifungia Baa za wazi zaidi ya 80 limesema ndani ya siku 14 Watu waliofungiwa Baa zao wasipolipa faini walizopigwa watafungiwa kabisa leseni zao za biashara.

Akiongea wakati wa Mkutano na Wadau wa Mazingira Jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Samuel Gwamaka amesema “Haturudi nyuma, lipa faini uliyopigwa ndani ya siku 14 uendelee na biashara, kama haujalipa tunaandika barua kwa wanaohusika ya kufuta leseni ya biashara"

“Wanaotaka wafunguliwe kwanza walipe faini ya Tsh. Milioni 5 ndani ya siku 14 na waandike barua za kukiri kosa na kuahidi kutorudia makosa ya kuwapigia Watu kelele zilizovuka viwango na watoe ahadi ya kujenga miundombinu ya kudhibiti kelele ndani ya siku 30”

“Pia wanapaswa kufuata masharti ya leseni kama vibali vyao vinavyoelekeza, ukitekeleza haya tunakuandikia barua ya kukuruhusu kuendelea na biashara yako lakini pia tutaendelea kukufuatilia”

“Ukishindwa kutekeleza haya tunakufungia leseni ya biashara, tunaamini mmepata fundisho hamtoweza kuzidi DB 40 hasa wakati wa usiku wakati Watu wakiwa wamelala”
 
Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ametoa hotuba kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara hiyo kwa mwaka 2023/2024 Bungeni Dodoma ambapo amesema Kwa kuzingatia takwimu za uzalishaji na mahitaji ya chakula, kwa mwaka 2022/2023 Taifa limejitosheleza kwa chakula kwa asilimia 114.

Bashe amesema “Tathmini ya mwisho ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa mwaka 2021/2022 imebaini kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula umefikia tani 17,148,290 kwa mlinganisho wa nafaka (Grain equivalent) ikilinganishwa na tani 18,665,217 mwaka 2020/2021 ikiwa ni pungufu ya tani 1,516,927.

“Upungufu huo umetokana na mtawanyiko wa mvua usioridhisha, kati ya kiasi kilichozalishwa, nafaka ni tani 9,233,298 na mazao yasiyo nafaka ni tani 7,914,992, aidha uzalishaji wa nafaka ambao unahusisha mahindi, mchele, mtama, uwele, ulezi na ngano ulipungua kwa tani 1,641,127 sawa na asilimia 15.1 ikilinganishwa na uzalishaji wa tani 10,874,425 kwa msimu wa 2020/2021”

“Uzalishaji wa mazao yasiyo nafaka ambayo ni jamii ya mikunde, muhogo, ndizi, viazi vitamu na mviringo uliongezeka kwa tani 124,200 sawa na ongezeko la asilimia 1.6 na kufikia tani 7,914,992 ikilinganishwa na uzalishaji wa tani 7,990,792 msimu wa 2020/2021, mahitaji ya chakula kwa mwaka 2022/2023 ni tani 15,053,299 na ziada ni tani 2,095,256 za chakula”

“Kwa kuzingatia takwimu hizo za uzalishaji na mahitaji ya chakula, kwa mwaka 2022/2023 Taifa limejitosheleza kwa chakula kwa asilimia 114”
 

Similar Discussions

Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…